Jumapili, 26 Shawwal 1445 | 2024/05/05
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

Afisi ya Habari
Tanzania

H.  10 Sha'aban 1445 Na: 1445 / 03
M.  Jumanne, 20 Februari 2024

Taarifa kwa Vyombo vya Habari

Ujumbe wa Hizb ut Tahrir Tanzania Wapeleka Risala Maalumu kwa Mufti Mkuu na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA)

(Imetafsiriwa)

Jana tarehe 19 Februari 2024 Sheikh Mussa Kileo, Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Mawasiliano ya Hizb ut Tahrir Tanzania aliongoza ujumbe wa watu watatu akiwemo Masoud Msellem, Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari wa Hizb ut Tahrir Tanzania uliokwenda Afisi ya Mufti kumfikishia risala ya nasaha ya kimaandishi iliyopokewa na afisi ya Katibu wake kwa niaba yake.

Risala hiyo ni kuhusu namna jamii ya Kiislamu isivyoridhishwa na ukimya wa Mufti na BAKWATA au kutoa kwao kauli zisizostahiki kuhusiana na kadhia mbalimbali za Waislamu za kitaifa na kimataifa.

Risala ya Ujumbe huo ilihusu kadhia zifuatazo:

  1. Mauaji Yanayoendelea ya Halaiki yanayotendwa na kijidola bandia cha Mayahudi kwa Waislamu wa Palestina:

Licha ya kuwepo upazaji sauti juu kilimwengu kutoka kwa Waislamu na wasiokuwa Waislamu katika kulaani na kufedhehi ukatili, dhulma na mauaji ya maelfu, wengi wakiwa wanawake na watoto kutoka kwa kijidola bandia cha Israel, bado Mufti na BAKWATA wamekuwa kimya.

  1. Kufungwa kwa Kituo cha Al-Habash, Madrasa ya Wanawake ndani ya Dodoma:

Mnamo tarehe 02/02/ 2024 serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliamua kukifungia chuo cha wanawake cha Al-Habash kilichokuwa maeneo ya Songambele na Nkuhungu mkoani Dodoma, katikati mwa Tanzania kwa madai kwamba kinaendeshwa katika mazingira hatarishi. Madrasa hiyo ina jumla ya wanafunzi wa kike 132 kuanzia umri wa 13-20. Kwa bahati mbaya BAKWATA ilitoa kauli isiyo muwafaka kufuatia kadhia hii kuiunga mkono hatua ya serikali, ikipuuza ukweli kwamba kadhia ya msongamano wa wanafunzi wengi na usalama duni wa kiafya imeenea hata katika shule za Umma. Hata hivyo hatujaona serikali kuifungia shule yoyote.

  1. Kuvunjwa Msikiti wa wanafunzi, Bagamoyo:

Mnamo tarehe 06/02/2024 serikali iliuvunja msikiti wa wanafunzi uliopo Shule ya Sekondari ya Tawalanda, Chalinze, Bagamoyo, mkoa wa Pwani.  Msikiti huo ulijengwa mwaka jana ambao uliwapa wanafunzi fursa ya kufanya ibada katika mazingira ya hapo hapo shuleni badala ya wanafunzi kwenda msikiti wa kando kidogo. Uongozi wa Shule ulipata baraka kutoka kwa serikali ya eneo kufanya ujenzi huo. Wakati ujenzi ukiendelea, ghafla wafadhili wakaitwa na mamlaka ya Chalinze na kusimamishwa.

Hatujamsikia Mufti wala BAKWATA kutoa kauli za kupinga hatua ya kuvunjwa msikiti huo.

  1. Wanafunzi wa Kiislamu kuzuiliwa kufanya ibada / swalah

Malalamiko juu ya jambo hilo yamekuwepo kwa muda mrefu, na wazazi na walezi wa wamekuwa wakionesha kutoridhishwa na jambo hilo kwa watoto wao. Video fupi iliyosambaa karibuni ikimuonesha mzazi akilaumu hatua ya kuzuiliwa watoto wake kufanya ibada katika wilaya ya Manyoni, mkoani Singida ni moja ya mifano mingi ya uwepo wa jambo hilo. Kwa bahati mbaya na kwa masikitiko makubwa mmoja wa maafisa wa BAKWATA ndani ya wilaya ya Manyoni alijaribu kukanusha lisilokanushika akimpachika mzazi aliyepaza sauti juu ya kadhia hiyo ya kuzuiliwa na kunyimwa watoto kufanya ibada kwamba ni muongo.

Ujumbe wa (Hizb ut Tahrir) ulimtaka Mufti na BAKWATA kuchukua hatua za haraka na stahiki kuyakabili mambo hayo (yanayowasibu Waislamu) kwa kuwa wao wamekubali kuchukua dhamana ya Uislamu na Waislamu wa Tanzania na kwamba kwa jambo hilo watakuwa wenye kuwajibishwa (mas’ul) Siku ya Kiyama. Hivyo wanapaswa kuhakikisha yafuatayo:

  1. Kadhia za ndani na nje kama suala la Gaza zizungumziwe kwa upana na kwa mtazamo sahihi wa Kiislamu, na pia Waislamu wahamasishwe kufanya hivyo kupitia majukwaa yao mbalimbali kama khutba za Ijumaa nk.
  2. Kushinikiza ili chuo cha wanawake cha Al-Habash kifunguliwe na kupewa walau muda fulani kuweza kuboresha hali na mazingira ya usalama wa kiafya, kupunguza msongamano mkubwa wa wanafunzi nk. Visingizio vilivyotolewa na serikali vya kukifungia kituo hicho vinagongana na uhalisia wa vituo vingi vya kielimu zikiwemo shule nyingi za Umma, na hatujaona vituo hivyo kufungiwa na wanafunzi wake kurejeshwa majumbani kama ilivyofanywa kwa kituo hiki cha Madrasa ya Al-Habash.
  3. Msikiti wa Shule ya Sekondari ya Talawanda, Chalinze, Bagamoyo uendelee kujengwa, na wanafunzi wapewe fursa huria ya kuutumia kufanyia ibada bila ya pingamizi.

Kuhusiana na wanafunzi kuzuiliwa kufanya ibada ya swalah, tunamtaka Mufti na BAKWATA yafuatayo:

Kushinikiza kwamba suala la wanafunzi kubakia shule baada ya muda uliopangwa na serikali liwe jambo la khiyari. Pia wanafunzi waruhusiwe kuswali kila siku na sio siku ya Ijumaa pekee. Mitihani ya majaribio kwa wanafunzi ifanywe siku za kawaida za masomo na sio siku za Jumamosi, ambapo wanafunzi hunyimwa fursa ya kujumuika na familia na kushiriki madrasa za masomo ya kidini.

Masoud Msellem
Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari

Hizb ut Tahrir Tanzania

Hizb-ut Tahrir: Afisi ya Habari
Tanzania
Address & Website
Tel: +255778 870609
E-Mail: mediarep@hizb.or.tz

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu