Jumatatu, 27 Shawwal 1445 | 2024/05/06
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Jibu la Swali

Uchaguzi wa Bunge la Congress la Marekani

(Imetafsiriwa)

Swali:

Chama cha Republican kilipata udhibiti, kwa wingi mdogo, juu ya Baraza la Wawakilishi la Marekani ambalo lina viti 435. [“Kilishinda angalau viti 218, kulingana na makadirio ya CBS News, mshirika wa BBC nchini Marekani.” (BBC, Novemba 17, 2022)]. Kuhusu Wanademokrasia, walisherehekea [“Jumapili kwamba chama kilibakisha wingi wa watu wengi katika Seneti ya Marekani,” (Al-Jazeera, Novemba 14, 2022)]. Vyombo vya habari vya ndani katika nchi nyingi za dunia vilikuwa vikitangaza habari za uchaguzi wa Bunge la Marekani (Baraza la Wawakilishi na Seneti). Tungewezaje kuelewa kwamba tukio la ndani huko Amerika - ambalo halizingatiwi sana na wenzao katika nchi zingine - limekuwa tukio kuu ulimwenguni kote? Au ni Amerika inayotaka vibaraka wake na wategemezi wake wazingatie matukio yake ya ndani ili kulifanya kuwa suala la kimataifa sawa na Uingereza, ambayo vyombo vya habari vya vibaraka wake vinatangaza habari zisizo na maana kuhusu wafalme wake, ndoa zao, watoto wao, na kadhalika? Au ni kwamba chaguzi hizi zina athari ya kweli kote ulimwenguni?

Jibu:

Ndiyo, Uingereza inatoa wito kwa vibaraka wake na wategemezi wake wazingatie mambo madogo madogo nchini Uingereza kutokana na maana kubwa na ya kina ya ukuu wa Waingereza, kana kwamba ile iliyoitwa hapo zamani, milki ambayo jua halitui bado iko hadi leo. Kwa upande wa Uingereza, hili ni suala la kuhuisha hisia zake za kale za ukuu, lakini kuhusu Amerika, suala hilo ni tofauti kabisa. Ili kufafanua hili, tunasema yafuatayo:

1- Ili kuelewa athari za matukio ya ndani ya Marekani katika uga wa kimataifa, tunaregelea kile Rais Biden wa Marekani alisema kwamba ikumbukwe kwamba Urusi ilisubiri matokeo ya uchaguzi wa bunge la Marekani kabla ya kuanza kujiondoa kutoka Kherson (Al-Jazeera, Novemba 11, 2022). Pia tunaregelea uamuzi wa Saudi Arabia kupitia OPEC+ kupunguza uzalishaji wa mafuta kwa mapipa milioni mbili kwa siku na matokeo yake bei hiyo ilipanda duniani kote na raia wa Marekani amekerwa na bei ya mafuta ndani ya nchi, hivyo raia wa Marekani aligoma kuwachagua Wanademokrasia na badala yake akachagua Wanarepublican. Bado haijawezekana kuthibitisha ikiwa kufungwa kwa China kwa kisingizio cha virusi vya Korona ni kwa sababu za kweli au kama suala la kuunga mkono uchaguzi kwa chama cha Rais Biden, na hivi ndivyo siku zijazo zitafichua. Kwa mukhtasari, uchaguzi wa katikati ya muhula wa tarehe 8 Novemba 2022 uliwakilisha tukio kuu la kimataifa. Inatosha hata kusema kwamba tetemeko lolote linalotokea ndani ya Amerika linaweza kujirudia katika maeneo mengine duniani kote. Kwa hivyo, umuhimu wa chaguzi hizi za kimataifa za Marekani hazipaswi kupuuzwa, na kinachofanya hili kuwa muhimu ni kwamba muda wa utawala wa Raisi wa zamani Trump ulifichua mgawanyiko mkali sana ndani ya Amerika, kati ya watu, serikali, vyama, na makampuni ya kifedha. Kwa haya yote, ulimwengu ulikuwa ukiangalia nini kinaweza kutokea kutokana na uchaguzi wa bunge la Marekani.

2- Katika nchi maarufu na kubwa zaidi ya kirasilimali duniani, Marekani, mfumo wa kisiasa umefanya ushindani baina ya vyama viwili pekee, ambavyo kila kimoja kinategemea makampuni ya kirasilimali kushinda chaguzi! Dalili ya wazi kwamba anayeamua ni makampuni makubwa ya kirasilimali na sio watu, ni kwamba matumizi ya makampuni katika kuunga mkono wagombea wa uchaguzi wa bunge la Marekani katika nyumba zote mbili. Mwaka huu ilikuwa takriban dolari bilioni 17 katika matumizi ya uchaguzi. [Marekani inaonekana kila wakati kuwasilisha mfano wa kitendawili. Wakati ambapo nchi inakabiliwa na mfumko wa bei wa kihistoria, matumizi ya propaganda ya uchaguzi wa katikati ya muhula yalifikia rekodi ya juu. Shirika moja la Marekani lilifichua rekodi ya gharama ya uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani kwa mwaka wa 2022, ambayo ilizidi dolari bilioni 16.7. (Sky News Arabia, Novemba 13, 2022)] Ambayo ni sawa na bajeti ya baadhi ya nchi za Afrika na nyenginezo. Ni wazi kwamba warasilimali wa Marekani, wamiliki wa makampuni makubwa, ndio wanaoelekeza watu wa Marekani kumchagua mmoja na sio kumchagua mwengine, kwa uchaguzi wa Marekani kwa nje, ni kwamba mamlaka ni ya watu, lakini ndani yake ni kwamba mamlaka ni ya makampuni makubwa ambayo yanaweza kutumia mamia ya mamilioni ya dolari kumuunga mkono mgombea fulani, hadi ikasemekana kwamba wanasiasa wa Amerika wanachagua wapiga kura wao, si vyenginevyo. Ushahidi wa hili ni kwamba yeyote anayeibua kauli mbiu ya uhuru wa kutoa mimba anataka hadhira ya wanawake ili wamchague, na anayeibua kauli mbiu ya kutetea uhamiaji anawalenga walio wachache kumchagua yeye, na anayeibua kauli mbiu za kibaguzi anawalenga Wamarekani weupe kumchagua, na kadhalika.

3- Udhibiti wa fedha na makampuni umekuwa hivyo kila mara nchini Marekani, lakini muda wa utawala wa Raisi wa zamani Trump umefichua mabadiliko makali yanayotokea ndani ya Marekani, na mabadiliko haya yalipewa jina la kwamba ushindani mkubwa kati ya makampuni makubwa sio ushindani wa kiriadha kama ulivyokuwa hapo awali, lakini unazidi kupamba moto. Na joto lake liliongezeka hadi kufikia au kukaribia kuchemka pale ulafi wa warasilimali haukuruhusu kuishi pamoja kwa amani kwa kuzingatia maslahi yanayokinzana ya warasilimali hawa. Ushindani mkubwa wa kirasilimali kati ya makampuni ulihamia katika hali ya kuvunjika mfupa miongoni mwa wanasiasa wanaowakilisha maslahi ya makampuni hayo, na kwa ujumla, warasilimali wamegawanywa katika makundi mawili hadi sasa: Sehemu inayotawaliwa na makampuni ya teknolojia na kuwakilishwa na Chama cha Demokrasia cha Marekani, na sehemu nyingine inayotawaliwa na makampuni ya mafuta na nishati na kuwakilishwa na Chama cha Republican cha Marekani. Sehemu hizi mbili zinatarajiwa kugawanyika zaidi, kulingana na maslahi ya makampuni makubwa ambayo yanasimama nyuma ya huyu au yule, na kulingana na hali ya Marekani ambayo maslahi ya makampuni hayo yanategemea. Ikumbukwe kwamba makampuni ya mafuta na nishati ya Marekani yaliwakilisha kwa miongo kadhaa kama kito cha uraslimali wa Marekani ambapo yalikuwa na ushawishi mkubwa ndani ya Amerika na nje ya nchi. Vita vya mafuta na sera za kupanua mabomba kati ya nchi na kujenga meli kubwa za mafuta zililetea makampuni haya ushawishi mkubwa na faida kubwa. Hata hivyo katika miongo miwili iliyopita, makampuni ya teknolojia yaliibuka, mitaji yao ilipanda hadi mtaji wa baadhi yao ukapita, chini ya miongo miwili, mtaji mkuu wa baadhi ya makampuni ya mafuta na nishati ambao ulikuwa umejikusanya kwa karibu karne moja. Na kwa kuongezeka kwa ukali wa tatizo hili, ambalo liliongezeka kwa kasi wakati wa kipindi cha virusi vya Korona, kwani sera ya kusitishwa kwa shughuli za kawaida kulinyima kampuni za mafuta faida kubwa, na bei ya mafuta wakati mwingine ilifikia hasi, huku ukuaji wa kampuni za teknolojia uliongezeka wakati watu walibaki majumbani mwao, kuwasiliana na kila mmoja na kufanya kazi zao kupitia mawasiliano na vifaa vya kompyuta. Miamala ya kibiashara na kifedha iliongezeka kupitia kampuni hizi, kama vile kampuni ya Amerika ya Amazon ambayo ilidhibiti sekta nyingi za biashara na kuigeuza kuwa biashara ya kielektroniki na ugawaji wa bidhaa nyumbani. Hatua hizi kubwa ziliendana na ujio wa utawala wa Trump, na hapa moto wa migogoro kati ya makampuni haya makubwa yenye hasara na faida ulipamba moto hadi ukali ukafikia majaribio ya kuvunja mifupa ya kila mmoja wao. Na kwa sababu makampuni haya yanatekeleza yale wanayotaka kupitia wanasiasa, wanasiasa hawa wamegawanyika vikali.

4- Mgawanyiko huo umeongezeka nchini Marekani, ambapo majimbo yanayodhibitiwa na chama cha Democrats yalitunga sheria dhidi ya makampuni ya mafuta, kama vile California ilitoa sera ya kutotoa hewa chafu na kuegemea kabisa kwa magari yanayotumia umeme kufikia 2035. Wakati majimbo kama vile Texas, ambayo yanadhibitiwa na Republican na inayoungwa mkono na makampuni ya mafuta ambayo yanadhibiti serikali, yalijumuisha makampuni ya viwanda ya kijani kibichi yaani yale yanayopitisha sera ya kupunguza utoaji wa hewa chafu, kwenye orodha yao isiyoruhusiwa. Uhalali wa mgawanyiko huo uliongezeka wakati majimbo yanayodhibitiwa na Republican yalipoanza kugawanya wilaya za uchaguzi na kutoa sheria ili kuhakikisha udhibiti wao juu ya jimbo hilo katika chaguzi zozote zijazo, kama vile sheria zinazozuia upigaji kura kwa barua, ambayo inapendelewa na wafuasi wa Democrat. Wakati majimbo yanayodhibitiwa na Wanademokrasia yalianza kugawanya wilaya za uchaguzi na kutoa sheria kama vile kurahisisha upigaji kura kwa njia ya barua ili kuhakikisha kuwa Wanajamhuri hawaingii katika majimbo haya, bila kusahau mgawanyiko wa kitamaduni kama vile kujumuishwa kwa utamaduni wa "nadharia ya mbari" katika mitaala ya shule katika majimbo yanayodhibitiwa na Republicans na kuenea kwa utamaduni dhidi ya uhamiaji na wahamiaji. Kwa upande mwingine, utamaduni wa uhuru wa kuavya mimba unaenezwa katika majimbo yanayodhibitiwa na Democrats, kwani ni kinyume na mtazamo wa kihafidhina wa Republican, pamoja na utamaduni wa kukaribisha wahamiaji. Kwa hiyo, Marekani iligawanywa katika majimbo mekundu yaliyokuwa yakidhibitiwa na Wanajamhuri, yaliyokuwa yanatawaliwa na Wamarekani weupe, na majimbo ya samawati yaliyokuwa yakidhibitiwa na Wanademokrasia, ambao walileta pamoja jumuiya nyingi za wahamiaji pamoja nao. Wakati mgawanyiko ulihamia kuchukua sura ya kikabila, na mgawanyiko huu ukawa wa kudumu kwa kiwango kinachoongezeka, na wanasiasa katika majimbo waliegemea katika kuongeza masuala ya utata!

5- Amerika, pamoja na serikali za ulimwengu, ziliangalia matokeo ya uchaguzi wa katikati ya muhula wa bunge  la Amerika, kulingana na masilahi yake. Kwa upande mmoja, Urusi ilikuwa ikingojea "kundi la Trump" kuzuia, baada ya ushindi wao katika chaguzi hizi, uungwaji mkono mkubwa wa Marekani uliotolewa na utawala wa Biden kwa Ukraine. Na Ulaya, hasa Ujerumani, inahofia ushawishi wa kundi la Trump juu ya msimamo wa Marekani na Ulaya ili kuzima mielekeo ya Urusi ya kujitanua. Labda China pia iliogopa athari za uzembe wa Amerika dhidi ya China au silaha za nyuklia za Korea Kusini na Japan. Kadhalika, vibaraka wa Amerika katika eneo la Kiislamu, ambao baadhi yao, kama Saudi Arabia, wanaona kwamba kundi la Trump ni bora kwao kuliko "kundi la Biden," wakati wengine wanaona kinyume chake. Ni kweli kwamba hizi si chaguzi za urais lakini zilielezwa kuwa za urais, bila kusahau kuwa ni kiashirio kikubwa cha uchaguzi ujao wa urais mwaka 2024. Kutokana na mfumko wa bei nchini Marekani, ikiwa ni pamoja na kupanda kwa bei ya mafuta, hali nzuri ilienea kwa Chama cha Republican kushinda. Hivi ndivyo kura za maoni zilitabiri na kukuzwa na vyombo vya habari kwa kiwango ambacho kiliwatia hofu Wanademokrasia kutoka kwa kile kilichoitwa "wimbi jekundu linalojitokeza", ikimaanisha kuwa hali ya uchaguzi kwa ujumla ilikuwa inawapendelea Wanajamhuri. Hata hivyo, matokeo ambayo yameibuka hadi sasa yanajumuisha mgomo wa kura za maoni na vyombo vya habari, na baadhi ya njia hizo ziliunga mkono Democrats, ambayo ilitarajia "wimbi jekundu". Rais wa zamani Trump alisafiri kati ya majimbo kuwaunga mkono wagombea wa Republican kana kwamba ni kampeni ya uchaguzi wa urais, na kwa upande wake, Democrats walitumia kampeni zilizofanywa na Rais wa sasa Biden, na Marais wa zamani kama vile Obama na Clinton kwa matumaini ya "kuzuia wimbi jekundu” ambalo alifikiri lilikuwa karibu. Hata hivyo, wimbi hili halikutokea badala yake matokeo ya uchaguzi yanaonyesha kwamba Chama cha Republican kimepata udhibiti wa Baraza la Wawakilishi la Marekani kwa wingi wa kura katika Baraza la Wawakilishi lenye wajumbe 435. [kilishinda angalau viti 218, kulingana na makadirio ya CBS News, mshirika wa BBC nchini Marekani. (BBC, Novemba 17, 2022)]. Kuhusu Wanademokrasia, [walisherehekea Jumapili kwamba chama kilibakisha wingi wa watu wengi katika Seneti ya Marekani. Chama cha Democrat kwa sasa kina viti 50, mbali na kura ya Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris, anayeongoza Seneti, ikilinganishwa na 49 vya Republican, na kiti kimoja bado hakijaamuliwa katika uchaguzi wa Seneti. Inasubiri duru ya pili katika jimbo la Georgia iliyopangwa kufanyika tarehe sita Disemba, ambapo chama cha Democrats kinaweza pia kuimarisha wingi wao. (Al Jazeera, Novemba 14, 2022)], na matokeo haya ni kinyume na matarajio na kura zote!

6- Kupitia uchunguzi, tunagundua kuwa majimbo yanayodhibitiwa na Republican, ambayo ndani yake kuna gavana wa Republican na idadi kubwa ya wawakilishi wa mitaa na maseneta katika jimbo hilo, ni Republican, yamebaki Republican bila Chama cha Kidemokrasia kuwa na ushawishi wowote mkubwa ndani yao, isipokuwa kidogo, kama vile ongezeko la wahamiaji, hasa kutoka Amerika ya Kusini, kwa mfano Texas imetoa baadhi ya wawakilishi wake, ni Democrats wachache wakati udhibiti mdogo unabaki kwa Republican, na kinyume chake ni kweli kwa yale majimbo ambayo yanadhibitiwa na Democrats. Mgawanyiko huu ulionekana kuwa wa kina na ulioimarishwa vyema, wakati baadhi ya majimbo yalisalia chini ya mzozo kati ya pande hizo mbili, ambazo huitwa majimbo ya bembea, kama vile Georgia, Arizona, Nevada, na Pennsylvania. Pengine matokeo ya uchaguzi huo, ambayo yalipingana na matarajio yote ya kijadi na tofauti na kura za maoni na usomaji wa kawaida wa mchakato wa uchaguzi, yanaashiria kuwa majimbo ya Marekani yakiwemo Washington DC sio majimbo yaliyoungana tena kama ilivyokuwa huko nyuma, bali sifa ya utengano kati yao inachukua njia kuelekea kudumu. Kwa upande mwingine, mapambano ya vyama viwili kuhusu utawala na maslahi yanayokinzana ya makampuni makubwa ambayo yanasimama nyuma ya vyama viwili yanaweza kupamba moto katika majimbo yanayozunguka, kwa sababu udhibiti wa chama kimoja juu ya yeyote kati yao katika chaguzi hizi na utunzi wa sheria zake mpya dhidi ya upande mwingine na usambazaji wa utamaduni dhidi yake ni kuivuta serikali mbali na upande mwingine, ambayo haitakubaliwa na upande uliopoteza. Kwa hivyo, inawezekana kwamba majimbo haya ya bembea yataibua cheche za vurugu, jambo ambalo litapelekea nchi kwenye ghasia zaidi, hivyo kukanganya sera ya mambo ya nje ya nchi.

Hakika, imechanganyikiwa tangu leo, na mshikamano wa Saudi Arabia na kundi la Trump kuhusu kupunguzwa kwa mafuta ilikuwa dalili hatari ya mwenendo huu. Mgawanyiko huu wa kina ni moja wapo ya mambo muhimu ambayo yalifichuliwa na chaguzi hizi, kwani pande hizo mbili zinakaribia usawa kwa nguvu, na hali mpya kama vile kupanda kwa bei hazikuathiri nguvu zao ambazo ziliimarisha sana maoni ya washiriki wa neva, na hili ni jambo hatari na matokeo yasiyotarajiwa. Mvutano huu wa vyama ulionekana wazi katika uchaguzi, kwani baadhi ya wagombea katika kundi la Trump, hata wanawake, walikuwa wakifanya kampeni wakiwa na bunduki mabegani mwao. Labda siku zijazo zitadhihirisha tofauti zaidi na uhalali wa tofauti hiyo kati ya majimbo na kuongezeka kwa uhamiaji wa watu wasio wazungu kutoka maeneo yanayodhibitiwa na Chama cha Republican ambamo nadharia ya ukuu wa wazungu inakuzwa.

7-Kulingana na kile kilichotokea katika uchaguzi huo, baadhi ya taa zinaweza kuangaziwa kuhusu yatakayofuata matokeo ya uchaguzi wa katikati ya muhula wa Bunge kama ifuatavyo:

a. Huku Marekani ikionekana kutokuwa na watu wenye akili timamu wanaoweza kuziba pengo kati ya pande mbili zinazozozana juu ya madaraka huko Washington, na wakati Wamarekani wakionyesha mvutano zaidi katika uaminifu na misimamo ya kisiasa, utawala wa Rais Biden, katika miaka miwili ijayo, uko ukingoni. Vikwazo zaidi vilivyowekwa na majimbo "mekundu" ya Republican, pamoja na Baraza la Wawakilishi. Haya yote yatapelekea nchi kuwa makini zaidi na kujishughulisha zaidi na hali yake ya ndani kwa gharama ya kuzingatia sera za mambo ya nje. Kwa upande wa Trump, ilionekana kuwa Donald Trump kabla ya uchaguzi alikuwa ameweka mamlaka yake kwa chama kizima cha Republican, lakini baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa, ilionekana baadhi ya wagombea wanaoungwa mkono na Trump wameanguka, lakini baadhi yao walifanikiwa, na hii inaweza kuleta ugumu kwa Trump katika uchaguzi ambapo aliwania urais wa pili nchini Marekani kwa niaba ya Chama cha Republican.

b. Hivyo kutokana na makampuni makubwa ya Marekani ambayo yanasimama nyuma ya Chama cha Republican kuwa na ushawishi mkubwa wa kimataifa, jambo ambalo lilifichuliwa na uamuzi wa Saudi Arabia wa kupunguza uzalishaji wa mafuta, dalili za mgawanyiko wa ushawishi wa kimataifa wa Marekani huenda zikaongezeka, jambo ambalo linaidhoofisha Amerika kimataifa, na hili ni jambo ambalo haliwezi kudharauliwa. Ilionekana mapema wakati mawasiliano ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje John Kerry, Mwanademocrat, yalipodhoofisha sera za shinikizo kubwa za utawala wa Trump na Iran, na Wanarepublican waliitikia wakati wa utawala wa Kidemokrasia wa Biden kwa kuichochea Saudi Arabia kupunguza uzalishaji wa mafuta, ambayo ilidhoofisha shinikizo la utawala wa Biden kwa Urusi... Hii inafanya ushawishi wa kimataifa wa Marekani kuwa na athari mbili, na kugawanya baadhi ya maslahi yake ya kimataifa katika maslahi ya Republican na yale ya Democrats, wakati mzunguko wa maslahi ya pamoja ya kimkakati bado, kama vile kupambana na Urusi na China, lakini wanaweza kutofautiana katika mbinu na sera ndogo za kufikia hili.

c. Utawala wa Biden bado una miaka miwili kamili ya kuweka shinikizo kwa Urusi kuhusu Ukraine, na hata ikiwa Amerika itafungua mlango wa mazungumzo kati ya Ukraine na Urusi, Amerika itaendelea kuweka shinikizo kwa Urusi kuacha faida zake zote za Ukraine katika muda mfupi, na kubaki chini ya vikwazo vikubwa vilivyowekwa juu yake hadi Amerika ipate mafanikio mengine nje ya uwanja wa Ukraine, kama vile kuhakikisha kuwa silaha za nyuklia za Urusi hazileti tishio kwa Amerika. Inaonekana kwamba hii ndio sera wakati wa kipindi cha Biden, na bila Biden kufikia mafanikio haya, Urusi itabaki kutengwa na ulimwengu wa Magharibi na matawi yake, na uchumi utabaki kuwa wa shida na hauwezi kusimama.

d. Kwa kutishia China kuunga mkono Urusi, utawala wa Biden ulifaulu kuitenga China kivitendo kutoka kwa Urusi, bila kujali taarifa tupu zilizotolewa na Wachina na Warusi juu ya nguvu ya uhusiano wao. Kauli hizi ambazo hazibadili ukweli. Mchakato huu wa kuwafukuza bado haujakamilika, ingawa Urusi inahisi kwa nguvu kwamba China imeiangusha na kuiacha peke yake mbele ya Amerika na nchi za NATO ambazo hutoa msaada mkubwa wa kijeshi kwa Ukraine na kuiwekea Urusi vikwazo vizito vya kiuchumi ambapo China haikutoa msaada wowote kwa mshirika ambaye alielezea muungano wao kabla ya kuzuka kwa vita nchini Ukraine kama "usio na kikomo."

e. Nchi za Ulaya Magharibi zilikuwa na hofu ya aina yoyote ya kuregea madarakani kwa Trump, iwe kwa kuregea tena kwenye kiti cha urais au kupitia udhibiti wa kundi lake kwenye Bunge la Amerika kwa sababu anapitisha sera inayosema kuwa NATO ni muungano uliopitwa na wakati, na kwamba nguvu za kijeshi za Ulaya  zilikuwa dhaifu na hazikuweza kukabiliana na sera ya upanuzi ya Urusi, ilifurahishwa na kuregea kwa utawala wa Biden barani Ulaya. Pia, makampuni ya gesi ya Marekani yaliaibisha utawala wa Biden ulipotoa gesi ya Marekani kama mbadala wa gesi ya Urusi kwenda Ulaya kwa bei ya juu mara nne kuliko bei zao za Marekani, na nchi za Ulaya zilipinga. Kadhalika, Rais Biden mwenyewe alizikosoa kampuni hizo, ambapo alisema zimepata faida za juu kupita kiasi wakati wa vita vya Ukraine, na kutishia kutoza ushuru wa ziada kwa faida yao.

Bila shaka, Biden alikuwa akikosoa kupanda kwa bei ya mafuta ndani ya nchi, kwa sababu kupanda kwa bei barani Ulaya hakumhusu sana. Badala yake, sera ya Amerika ambayo Biden anaongoza kwenye mhimili wa Ujerumani inaongoza kwa kusambaratika kwa Ulaya, na ni sawa na sera ya Rais wa zamani Trump juu ya mhimili wa "Brexit Britain" kugonga umoja wa Wazungu.

8- Kwa kumalizia, imeonyeshwa jinsi uchaguzi wa katikati ya muhula wa Bunge la Marekani ulivyo na mwelekeo na athari nyingi za ndani na nje, na jinsi utawala wa Marekani ulivyofanya kuwa tukio la kimataifa ambalo nchi nyingi za dunia zinajali kama suala la athari zake juu ya sera ya nje ya Amerika.

Hivi ndivyo dola zinazoitwa dola kubwa zilivyo, na hivi ndivyo umuhimu wa matukio yao ya ndani unavyoonekana, na pale Mwenyezi Mungu atakaporuhusu kusimamishwa dola ya Kiislamu na Umma wa Kiislamu uchukue njia yake kuuathiri ulimwengu, ukiwaletea uongofu, basi tukio lolote lile, dogo au kubwa miongoni mwa Waislamu, litakuwa na thamani kubwa ya kisiasa na vyombo vya habari kwa nchi za kikafiri, ambazo zitachunguzwa na kuchambuliwa ili kujua athari zake kwao. Nchi kubwa za Kikafiri hivi leo zinaonyesha kupendezwa na kila tukio dogo na kubwa katika ulimwengu wa Kiislamu, na zinaonyesha kupendezwa na harakati za Kiislamu, na vyombo vyao vya habari vina angazia baadhi ya harakati hizi, ambazo wanaziita "za wastani," na kujaribu kuuweka mbali Ummah na harakati nyengine za dhati. Nchi hizi za kikafiri huzingatia mara elfu ya mienendo ya kweli ya Waislamu, hivyo wanaifuatilia na kuwaita vibaraka wao kuizuia. Hii ni kabla ya kuasisiwa Dola ya Kiislamu, Dola ya Khilafah, basi makafiri watakuwaje ikiwa Ummah wa Kiislamu na nguvu zake kuu utakuja chini ya uongozi wa ikhlasi na makini unaofanya kazi ya kumridhisha Mwenyezi Mungu na kutumikia maslahi ya Ummah wake? Kisha Ummah utaregea katika utukufu wake na udhaifu wa zile zinazoitwa nchi kubwa utadhihirika.

(وَسَيَعْلَمُ الَّذِينَ ظَلَمُوا أَيَّ مُنْقَلَبٍ يَنْقَلِبُون)

“Na wanao dhulumu watakuja jua mgeuko gani watakao geuka.” [Ash-Shu’ara 26:227]

25 Rabii’ al-Akhir 1444 H

19 Novemba 2022 M

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu