Jumatano, 22 Rajab 1446 | 2025/01/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Barua ya Wazi kwa Waislamu nchini Denmark Kuhusiana na Uchaguzi wa Mabaraza ya Manispaa:

Enyi Waislamu: Hamtakuwa na Uzito wala Athari katika Maisha ya Kisiasa Isipokuwa kwa Msingi wa Uislamu.
(Imetafsiriwa)

Uchaguzi wa mabaraza ya manispaa unafanyika mwezi huu, kampeni za uchaguzi ziko katika makali zaidi. Mjadala kuhusu uchaguzi unazunguka miongoni mwa Waislamu pia, na baadhi ya manispaa zimeanzisha baadhi ya mipango ya kuwataka Waislamu kushiriki katika uchaguzi huo. Kwa mfano, Manispaa ya Aarhus ilifanya kampeni iliyoelekezwa kuhusu elimu ya kidemokrasia, kwa umbo la kozi ya mafunzo, ili kuongeza kiwango cha ushiriki katika uchaguzi miongoni mwa wageni kutoka asili zisizo za Ulaya.

Ndugu Waislamu: Kama ilivyo katika masuala yetu yote ya maisha, ni muhimu sana katika suala hili pia, kwamba tuwe na nia ya dhati kwa yale ambayo hukmu za Uislamu zinasema na sio kitu kingine chochote, na hatuwezi kujadili suala la kushiriki katika uchaguzi kwa msingi kwamba sisi ni wachache tunaotaka kutambuliwa na jamii, lakini kinyume chake, ni lazima tulishughulikie kama kundi la Kiislamu, ambalo jukumu lake ni kuhifadhi kitambulisho chake cha Kiislamu na kujikinga na mawazo batili ya Kimagharibi.

Ndugu Waislamu: Sharti la kushiriki katika uchaguzi katika Uislamu ni rahisi na liko wazi: Inajuzu tu kumpigia mtu kura ya kutekeleza kazi ambayo haijakatazwa katika Uislamu. Mwenyezi Mungu Mtukufu asema:

 [وَتَعَاوَنُواْ عَلَى الْبَرِّ وَالتَّقْوَى وَلاَ تَعَاوَنُواْ عَلَى الإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ]

“Na saidianeni katika wema na uchamngu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui.” [Al-Ma’ida: 2].

Ukweli kuhusu chaguzi katika tawala za kisekula ni kwamba zinawapa wanasiasa mamlaka ya kutabikisha hukmu zinazokinzana na Uislamu.

Ingawa mabaraza ya manispaa si mamlaka za kutunga sheria, kuna tatizo la msingi kushiriki katika kazi ya kisiasa katika manispaa hizi katika mifumo hii kwa sisi Waislamu, ambao tunaamini kwamba sheria ya Mwenyezi Mungu iko juu ya sheria au kanuni yoyote katika sheria zilizotungwa na mwanadamu.

Mabaraza ya manispaa katika miji ya Denmark kwa kweli ni mamlaka za kiidara zinazofurahia baadhi ya uhuru maamuzi, na kazi yake haikufungika tu katika masuala ya idara pekee. Ni sehemu ya utawala wa kisekula wa kikafiri, na hii ni haram kwa Muislamu kushiriki ndani yake yeye mwenyewe binafsi au kwa kumchagua mwakilishi wake kufanya kazi humo. Wajumbe wa mabaraza ya manispaa ndio wanaoteua mameya, na ni washirika wao kimajukumu kwa sera zao na matendo yao.

Kwa upande mwingine, mabaraza hayo yanatekeleza sheria na mipango ya kisiasa inayoelekezwa dhidi ya Waislamu nchini, ambayo inatungwa Bungeni, kwa mfano, vita dhidi ya maadili ya Kiislamu kwa kisingizio cha kile kinachoitwa “udhibiti wa kijamii”.

Pia, mabaraza ya manispaa yana kazi nyingi ambazo ni kinyume na kanuni za Uislamu, ikiwa ni pamoja na, lakini sio hizo tu, kupitishwa kwa bajeti, ambapo riba ndio msingi katika bajeti hizo, pamoja na mikataba ya riba, ambayo ni moja ya madhambi makubwa katika Uislamu, pamoja na mikataba ya ndoa za mashoga, kutoa leseni za vileo, udhibiti wa kasino na vitendo vyengine ambavyo haviendani na hukmu za Uislamu. Hapana shaka kuwa kura kwa mtu anayefanya vitendo vilivyokatazwa ni haramu, kwani kumpa kura mtu au chama ni kumpa uwakilishi mtu au chama hicho kufanya kazi hiyo. Na kwa vile haiwezi kuhakikishwa kuwa kazi hiyo haipingani na Uislamu, hairuhusiwi kumpa mamlaka mtu yeyote kuifanya.

Enyi Waislamu: Ni lazima tutambue hapa kwamba kuunga mkono chama chochote cha kisekula ni haramu katika Uislamu, Usekula unagongana kikamilifu na Uislamu katika misingi na katika matagaa, na kuunga mkono vyama hivi ni kusaidia katika uenezaji na utekelezaji wa mawazo ya kikafiri. Vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi nchini Denmark, ni vyama vya kisekula. Mtu anapomchagua mwanachama wa chama kimojawapo kati ya hivi anakipa chama kura, kwani mwanachama wa chama chochote anakuwa amejitolea kwa maamuzi yanayotolewa na uongozi wa chama hicho, na anakubaliana na mpango wa chama hicho.

Machaguo yaliyo mbele ya Waislamu katika nchi hii, yamefungwa kwa wagombea na vyama vya kisekula, na vyama hivi ndio vile vile ambavyo haviachi kuushambulia Uislamu na kanuni zake. Vinashambulia hijab na kukadiria kuwa ni dalili ya ukandamizaji wa wanawake, na wanaufanya mtazamo wa Uislamu katika uzazi kuwa ni tatizo, na masuala mengineo.

Ama kusema kuwa kusitasita kwa Waislamu kushiriki katika uchaguzi kunapelekea Waislamu kutengwa na kuwafanya waishi katika jamii sambamba, usemi huu si chochote zaidi ya propaganda ya kupotosha. Ushiriki wa Waislamu katika jamii hauwezi kupunguzwa hadi kwenye suala la kushiriki katika uchaguzi, sisi Waislamu tumepewa jukumu la kushiriki katika jamii kwa njia chanya, lakini kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na Uislamu kwa hilo, tupende tusipende, kwani kushiriki katika chaguzi ni tangazo la kuwa na imani katika mfumo wa kisekula. Ni kielelezo cha kukubali wazo la ukafiri, yaani kutenganisha dini na siasa, na hili haliruhusiwi kwa Muislamu kulikubali au kuliunga mkono. Na hii ndiyo sababu haswa inayopelekea shinikizo kwa Waislamu kuzidisha ushiriki wao katika uchaguzi, kama sehemu ya mpango wa ushirikiano wa kisiasa.

Ndugu Waislamu: Mnaziamini sheria za Mwenyezi Mungu, huku mataifa ya Magharibi, wakiwemo watu wa Denmark wanazidi kupoteza imani yao kwa mfumo wa kidemokrasia, na hilo linadhihirishwa na tafiti mbalimbali zinazoonyesha watu wa Denmark wanapoteza imani yao kwa wanasiasa na demokrasia yao kwa jumla, kwa hivyo msipande mashua iliyozama, lakini jiulizeni: Je, ni jukumu letu ni lipi ambao lazima lifikishwe kwa jamii inayotuzunguka? Je, ni tamko la kuuamini usekula au kuiepusha kutokana nayo?

Hivyo, msiwe njia ya uokozi kwa mfumo unaoelekea kuzama, pamoja na kuwa ni mfumo unaokinzana kimsingi na yale mnayoyaamini, bali unapiga vita imani yenu, mchana na usiku. Nyinyi ndio mnaoubeba Uislamu na mtazamo wake sahihi wa maisha na hukmu zake zilizowekwa na Mola wenu, mmefungamanishwa na ulinganizi wa Uislamu na mfumo wake, sio ulinganizi wa kujihusisha na mifumo na fikra nyengine batili!

Ndugu Waislamu: Badala ya kukimbilia nyuma ya wagombea na vyama vya kisekula, ni lazima tuwe mwili mmoja mbali nao ili kulinda kitambulisho cha Waislamu, kwa kuzingatia kanuni za Kiislamu ambazo pekee ndizo zinazotumikia maslahi ya kweli ya Waislamu, badala ya kuweka imani yetu katika nidhamu za kisiasa za kisekula. Tunapaswa kufanya kazi ili kupata imani kwamba mfumo wa Kiislamu ndio mbadala, na kutoa ujumbe wa Uislamu kwa jamii za Magharibi, ambazo zinateseka vibaya kwa sababu ya mifumo hii ya kisekula, ambayo ndiyo sababu ya matatizo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Ndugu na Dada Wapendwa wa Kiislamu: Manufaa makubwa kabisa katika maisha haya ya dunia hii na Akhera ni utumwa kamili kwa Muumba wetu, Mwenye nguvu na Mtukufu, Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa hiyo, sisi katika Hizb ut Tahrir, kwa ukweli na ikhlasi tunakulinganieni kujiepushe na demokrasia ya kisekula, inayogongana na Uislamu wenu, na mshirikiane nasi kisiasa na kifikra kuulingania Uislamu kwa ujumla wake, na kwa pamoja kukilinda kitambulisho chetu cha Kiislamu kwa kushiriki katika kufanya kazi nasi kurudisha mfumo wa Uislamu na kurudisha mfumo wa maisha kamili ya Kiislamu katika nchi za Waislamu na kisha kueneza kheri hii kwa ulimwengu mzima.

[يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ]

“Enyi mlio amini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapo kuitieni jambo la kukupeni uzima wa milele.” [Al-Anfal: 24].

H. 7 Muharram 1443
M. : Ijumaa, 05 Novemba 2021

Hizb-ut-Tahrir
Denmark

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu