Afisi ya Habari
Malaysia
H. 17 Rabi' I 1446 | Na: HTM 1446 / 08 |
M. Ijumaa, 20 Septemba 2024 |
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Ewe Waziri Mkuu wa Malaysia! Kumfuata Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) si kwa Maneno tu, bali ni kwa Moyo na Vitendo
(Imetafsiriwa)
Wakati wa sherehe za Kitaifa za Maulid ur Rasul 2024/1446H katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Putrajaya (PICC), Waziri Mkuu wa Malaysia, Datuk Seri Anwar Ibrahim, alisambaza ujumbe kwenye ukurasa wake wa Facebook akiwataka Waislamu kumchukulia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kama kiigizo—sio tu kwa ajili ya shakhsiya yake bali pia kama kiongozi wa dola, jamii, na familia, hasa katika muktadha wa muundo wa Madina. Anwar alisema, “Katika kutafuta kiigizo, inafaa kwetu mara kwa mara kumwangalia Mtume mtukufu na mheshimiwa zaidi wa Mwenyezi Mungu (saw) kama Uswatun Hasanah.” Je, isingefaa zaidi kwa Anwar kutumia neno ‘faradhi’ badala ya ‘kustahiki’ anapomuelezea Mtume (saw) kama ni kiigizo? Anwar alifafanua zaidi kwamba matamanio ya dola ya Madani hayatenganiki na uchukuaji mafunzo na mifano kutoka kwa Hati ya Madinah (Sahifah Madinah) iliyoanzishwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), kwa kuzingatia kanuni ya utofauti wa watu ndani ya muundo wa umoja, unaosimamiwa na uadilifu (Adl) na Ihsan.
Inatia moyo kumsikia Anwar akieleza nia yake ya kuchukua mafunzo kutoka kwa Hati ya Madina kama kielelezo katika kutawala nchi hii. Hata hivyo, swali linazuka: Je, Anwar ana nia ya kweli kufuata hukmu za Mtume (saw) mjini Madina kama kigezo cha “Dola yake ya Madani” aliyoitunga, au hii ni domo kaya tu wakati wa sherehe za kitaifa za kuzaliwa Mtume (saw)? Je, Anwar hajui kwamba Madina (zamani ya Yathrib) hapo mwanzo ilikuwa ni Dar ul Kufr (Dola ya Kikafiri), ambayo kisha ikageuzwa kuwa Daulah Islamiyyah (Dola ya Kiislamu) na Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), kwa kuzingatia Wahy (Ufunuo wa Mwenyezi Mungu)! Je, Anwar atajitahidi kuigeuza Malaysia kuwa Dola ya Kiislamu yenye msingi wa Wahyi wa Mwenyezi Mungu? Fauka ya hayo, je, Anwar hajui kwamba Hati hiyo na sheria zote zilizotekelezwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) mjini Madina pia ziliegemezwa kwenye Wahyi wa Mwenyezi Mungu? Je, Anwar basi atabadilisha katiba na sheria zilizotolewa na wakoloni makafiri wa Kiingereza kuwa katiba ya Kiislamu na sheria zinazoegemezwa kwenye Wahyi wa Mwenyezi Mungu?
Kama kweli Anwar anatamani kuichukua Hati ya Madina kama kiigizo, ni wakati mwafaka kwake kuitupilia mbali hati ya Lord Reid (katiba), ambayo imekuwa kama msingi utawala katika nchi hii hadi sasa. Tungependa kumkumbusha Anwar kwamba Hati ya Madina inafanya kazi kama makubaliano pamoja na sheria ya kimsingi inayosimamia mahusiano miongoni mwa Waislamu na kati ya Waislamu na wasio Waislamu, hususan Mayahudi, kama raia. Hati ya Madina inaeleza kwa uwazi kwamba maingiliano kati ya wananchi yanapaswa kuegemezwa kwenye Uislamu, huku raia wote wakiwa chini ya sheria za Kiislamu. Zaidi ya hayo, maandiko ya makubaliano hayo yanabainisha kwa uwazi wajibu wa Mayahudi kujisalimisha kwa sheria za Kiislamu na kushirikiana na Waislamu kwa ajili ya maslahi ya Dola ya Kiislamu. Miongoni mwa masharti mengi ndani ya Hati hiyo, inatosheleza kwetu kuangazia sharti moja ambalo linadhihirisha wazi kwamba masuala yote ya Dola ni lazima yatatuliwe kwa Qur'an Tukufu na Sunnah: «وَإِنّهُ مَا كَانَ بَيْنَ أَهْلِ هَذِهِ الصّحِيفَةِ مِنْ حَدَثٍ أَوْ اشْتِجَارٍ يُخَافُ فَسَادُهُ فَإِنّ مَرَدّهُ إإلَى اللهِ عَزّ وَجَلّ وَإِلَى مُحَمّدٍ رَسُولِ الله» “Kunapotokea baina ya pande za Hati hii mzozo au kesi, inayohofiwa madhara yake, iregeshwe kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na Muhammad Mtume wa Mwenyezi Mungu.”
Uchunguzi wa Hati ya Madina unadhihirisha kwa uwazi kwamba dola iliyoanzishwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ilikuwa ni Dola ya Kiislamu, inayohukumu kwa yale yote aliyoyaamrisha Mwenyezi Mungu (swt). Kinyume chake, dola inayoongozwa kwa sasa na Anwar ni dola ya kitaifa ya kidemokrasia ya kisekula, inayotawaliwa na matamanio ya watu. Iwapo Anwar anataka kweli kuifuata Madina kama kigezo, lazima aonyeshe dhamira hii kwa kuigeuza nchi hii kuwa Dola ya Kiislamu (Khilafah), kama alivyousia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kwa Ummah wake, na hivyo kuibadilisha dola ya sasa ya kidemokrasia iliyoundwa na wakoloni kwa raia wao. Tunapenda kumkumbusha Anwar kwamba maneno yake kuhusu kumfuata Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) na Dola ya Madina kama vielelezo vya kuigwa, yasipopatikana kwa matendo yanayoonekana, yatasababisha ghadhabu ya Mwenyezi Mungu (swt).
[يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا لِمَ تَقُولُونَ مَا لَا تَفْعَلُونَ * كَبُرَ مَقْتًا عِندَ اللَّهِ أَن تَقُولُوا مَا لَا تَفْعَلُونَ]
“Enyi mlio amini! Kwa nini mnasema msiyo yatenda? Yanachukiza vikubwa mno kwa Mwenyezi Mungu kuwa mnasema msiyo yatenda.” [As-Saff (61): 2-3].
Kumbuka kwamba kumtambua Mtume (saw) kama Uswatun Hasanah (kiigizo chema) haipaswi tu kupitia maneno ya mdomo au maandishi bali lazima pia kukumbatiwa kikweli ndani ya moyo wa mtu na kudhihirishwa kupitia vitendo. Anwar anapaswa kutafakari na kujiuliza, tangu alipokuwa Waziri Mkuu, ni kwa kiasi gani amejitahidi kuitawala Malaysia kwa Qur'an na As-Sunnah, sambamba na hamu yake ya kuifuata Daulah Madina kama kiigizo. Iwapo Anwar atashindwa kudhihirisha maneno yake, basi kauli zake si chochote zaidi ya maneno matupu, yanayodhihirisha sura yake halisi tangu ashike madaraka. Ikiwa Anwar angekuwa na hisia yoyote ya aibu, angegundua kuwa amevua mara kwa mara barakoa yake usoni, na kusababisha watu zaidi na zaidi, wakiwemo wafuasi wake mwenyewe, kuiona sura yake halisi.
Ni wajibu kwa yeyote anayetamani Madina kuwa kama nchi kigezo cha kuigwa kufanya kazi kwa umakini kwa ajili ya kusimamisha tena Dola ya Kiislamu (Khilafah). Dola hii ya kupigiwa mfano mwanzoni iliasisiwa na Mtume (saw), baadaye ilishikiliwa na Khulafa'ar-Rashidin, Umawiyya, Abbasiyya, na Uthmaniyya, na kisha ikavunjwa rasmi mnamo tarehe 28 Rajab 1342 H (sawia na tarehe 3 Machi 1924 M). Muundo huu hautahuishwa tena kupitia matamshi ya viongozi au maneno tu; bali inahitaji imani, na juhudi za kujitolea na za dhati kutoka kwa wale wote wanaoitetea. Mwenyezi Mungu (swt) amewaahidi walio amini na wakatenda mema kwamba atawapa mamlaka (Khilafah), kupitia Maneno yake:
[وَعَدَ اللَّهُ الَّذِينَ ءَامَنُوا مِنْكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِنْ قَبْلِهِمْ]
“Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walio amini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyo wafanya makhalifa wa kabla yao” [An-Nur (24): 55].
Abdul Hakim Othman
Msemaji Rasmi wa Hizb ut Tahrir
Malaysia
Hizb-ut Tahrir: Afisi ya Habari Malaysia |
Address & Website Khilafah Centre, 47-1, Jalan 7/7A, Seksyen 7, 43650 Bandar Baru Bangi, Selangor Tel: 03-8920 1614 www.mykhilafah.com |
Fax: 03-8920 1614 E-Mail: htm@mykhilafah.com |