- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Habari na Maoni
Uache Ubaguzi wa Rangi kwani Unachukiza
Habari:
Mtoto wa miaka 9 wa Syria kwa jina Wael al-Saud, aliyekuwa anaishi katika wilayah ya Kocaeli’s Kartepe, alijitoa uhai kwa kujinyonga katika mlango wa makaburi. Imeripotiwa kwamba mtoto huyo mdogo alikuwa amelikejeliwa na mwalimu siku hiyo na kuzomewa kwa ujumla na wanafunzi wengi kwa kuwa alikuwa ni Msyria. (http://www.haber7.com)
Maoni:
Moja katika desturi za ujahiliya ambazo zilikuwa zimetawala maisha ya watu wakati wa utawala wa Rasulullah (saw) alipokuwa ametumilizwa kama nabii, ilikuwa ni ubaguzi wa rangi na utaifa. Uislamu ukaondosha chuki hizo wakati wa ujahiliya ambazo zilijitokeza kutokana na tofauti za makabila, “kwa kuwafanya Waislamu ni ndugu” na kuharamisha kudai ubora kwa misingi ya ukabila na kuufunga tu kwa Uchajimungu pekee.
Uislamu ukayeyusha tofauti za ukabila na kuwa umoja mmoja katika chungu cha “Aqeedah ya Kiislamu” na kufundisha udugu. Mwamko wa udugu chini ya Khilafah ukapelekea Waislamu kufaulu kwa miaka. Na makafiri walipogundua kwamba hawawezi kuwashinda Waislamu katika vita wakabuni mipango yao miovu na wakakatikiwa kuwa njia pekee ya kuwashinda Waislamu ni kuivunja Dola ya Kiislamu ya Khilafah ambayo ilikuwa ni kiunganishi cha Waislamu, kwa kupanda mbegu za mizozo na kupenyeza sumu za utaifa na hivyo wakafaulu. Lakusikitisha walifaulu katika mipango yao michafu. Natija yake ilikuwa ni kuvunjika kwa umoja wa Ummah kwa kuigawanya dola moja ya Waislamu na kuwa zaidi ya vijidola 50 vilivyokuwa na mipaka ghushi ya Sykes-Picot. Hili likafuatiwa na uvamizi na uporaji wa ardhi zetu kwa kuongezea mauaji kwani ngao ya kuwalinda Waislamu na imani yao ilikuwa imevunjwa.
Kujitoa uhai kwa mtoto wa miaka 9 wa Syria kwa jina Wael al-Saud ni natija ya mchakato wa historia ya uhamiaji ambayo ilianza kwa uhamiaji miaka tisa iliyopita na kuishia kwa kifo. Mapinduzi ya Syria yalianza takribani miaka 9 iliyopita. Wakati wa mapinduzi, ndugu zetu walijipata katika ulengwaji wa risasi na mabomu kwa nyumba zao na unyama mwingi. Familia nyingi zimesambaratishwa kabisa. Idadi ya watoto wasiokuwa na wazazi na wanawake wajane wamezidi.
Matatizo haya yamepelekea uhamiaji wa ndugu zetu ili kutafuta mazingira yenye ustawi zaidi. Hivyo basi milioni kadhaa ya ndugu zetu Wasyria wakapata makaazi ndani ya Uturuki. Ndugu zetu Wasyria wamelazimishwa kuwacha nyuma nyumba zao na miili iliyokufa ya wenzao ambazo ni mali zetu kama zilivyo mali zao kwa kuwa ni za Uislamu ili kupata hifadhi kutoka kwetu. Lakini kumekuwa na wakati ambapo walichomwa kwani nyumba zao zilipoporwa na wakati mwengine walikuwa waathiriwa wa mauaji. Ukandamizaji walioukimbia ndio unaoendelea kuwakumba ndani ya bandari ya salama waliyokuwa wakiitafuta.
Hivyo basi, nani anaweka msingi huu wa rai amma dhidi ya ndugu zetu Wasyria? Kwa maana nyingine ni nini sababu ya uadui dhidi ya Wasyria? Ni wazi kuwa dola ya Uturuki iliyobeba siasa za utaifa za uhamiaji ndio wanaoulingania.
Ndiyo, yanayojiri kutokana na siasa mbaya za utaifa, hatua ya ukandamizaji kutoka kwa serikali tawala na vyombo vyake vya habari wamejidhihirisha ndani ya mujtama kwa muda mfupi. Ujenzi wa rai amma dhidi ya Wasyria imeandaa mazingira ya ufurushaji wa ndugu zetu wahamiaji Wasyria. Hisia za chuki dhidi ya Wasyria miongoni mwa umma, mtazamo wa kejeli unaoashiria “nenda zako!” na kufanyiwa maudhi kumezidi. Vitendo vya kinyama vimechipuza ambavyo vimewalenga wanawake na watoto, Wasyria wanalaumiwa pasina shutuma zilizo na msingi wakifuatiwa na kuvamiwa kupitia kuporwa na kuchomewa nyumba zao Wasyria.
Kujitoa uhai kwa mtoto wa miaka 9 wa Syria kwa jina Wael al-Saud ni mfano wa hivi karibuni. Kwani ripoti zinasema kwamba Wael al-Saud alifanyiwa kejeli na wanafunzi wenziwe na mwalimu siku hiyo ya kujiua. Lau hilo ni kweli, basi kujiua kwa mtoto huyu sio tu tukio la kujiua bali ninapendekeza lizingatiwe kuwa mauaji na watekelezaji wake wanajulikana. Watekelezaji hawa waliompelekea mtoto wa miaka 9 kujiua ndio walinganizi wa utaifa wabaguzi wa rangi ambao wanachukia uwepo wa Muislamu wa rangi nyingine na wanasiasa walinganizi wa utaifa ambao kila mara wanachochea uadui na chuki kwa matamshi yao dhidi ya Wasyria na uhamiaji na baadhi ya mashirika ya habari ambayo hayajui mipaka wakati wa kushambulia Uislamu.
Haya ni madhambi na ni madhambi ya wale wanaochochea ubaguzi wa rangi. Ni madhambi ya wale wanaopanda hisia za uadui badala ya kuwa Ansar. Ni madhambi ya wale wanaotaka kuendeleza dhati ya Sykes-Picot badala ya dhati ya Ummah. Kwa ufupi haya ni madhambi ya wale ambao nafsi zinawataka Wasyria kuondoka.
Sasa ndio wakati wa kuwa Ansar wa karne hii kwa ajili ya Waislamu Wasyria ambao wametafuta hifadhi kwetu – ndugu zao – ili kukimbia maangamivu na ukandamizaji walimokuwa wakiishi. Leo ndio siku ya kuwa Ansar ambao walimkubali Rasulullah (saw) wakati wake wa shida na kumnusuru yeye (saw) na Dini yake kwa kumpa nguvu na utukufu.
Katika hadith ndani ya Al-Bukhari, Rasulullah (saw) asema:
«الْمُسْلِمُ أَخُو الْمُسْلِمِ لَا يَظْلِمُهُ وَلَا يُسْلِمُهُ وَمَنْ كَانَ فِي حَاجَةِ أَخِيهِ كَانَ اللَّهُ فِي حَاجَتِهِ» “Muislamu ni ndugu ya Muislamu mwengine, kwa hiyo hatakiwi kumkandamiza, wala hatakiwi kumsalimisha kwa mkandamizaji. Yeyote atakayekidhi haja za nduguye, Mwenyezi Mungu atamkidhia haja zake.”
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Abdullah İmamoğlu