Ijumaa, 20 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Uingereza Yaishinda Ujanja Amerika kwa Mara Nyengine Tena kwa Kuthibitisha Mamlaka yake Barani Afrika

Habari:

      Ukoloni mkongwe wa kinyang'anyiro cha Bara la Afrika umepita mipaka baina ya Amerika inayo lingania kukumbatiwa kwa demokrasia na vyama vingi na upande wa pili Uingereza bwana mkoloni mkuu anayelingania kudumishwa kwa hali halisi kwa kufanya mabadiliko machache ya kisanii kuhadaa watu walio na kiu ya mabadiliko ya kihakika.

Maoni:

       Serikali za kiafrika ni serikali zenye uhuru bandia, ambazo huchukua sera zake za ndani na kigeni kutoka kwa mabwana zao wakoloni. Kiasi cha kuwa watawala wa kiafrika ni vibaraka wa kisiasa wa moja kwa moja, wanao wakilisha mabwana zao wa kikoloni kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Mabwana wote wa kikoloni wa kimagharibi ikiwemo Uingereza, wameazimia kulitawa bara la Afrika kwa njia isiyo ya moja kwa moja kupitia vibaraka wao watiifu kwa sababu mbili kuu:

       Kwanza, kupunguza shinikizo la ongezeko la matumizi yao ya kigeni baada ya matokeo ya Vita vya Pili vya Dunia vilivyo wagharimu sana.

       Pili, kujihifadhi kutokana na mahusiano hasimu yatokanayo na hamasa za kulingania uhuru kutoka kwa wakoloni wa kimagharibi.

        Huku Uingereza ikifanya marekebisho ya sera yake juu ya bara la Afrika, Amerika upande wa pili ilitumia fursa ya matukio ya kiulimwengu baada ya Vita vya Pili vya Dunia, na kusonga mbele kuanzisha sera yake ya bara la Afrika kupambana na athari ya utawala wa Uingereza barani humu. Amerika ililingania demokrasia na vyama vingi katika nchi zilizokuwa chini ya mkono wa Uingereza na dola za Ulaya kwa ujumla. Hili lilipekea matukio ya mashambulizi ya kujibizana ya kisiasa huku Uingereza ikijizatiti kudumisha athari yake ya kiulimwengu kwa kukazanisha mashiko yake kwa koloni zake, na Amerika ikitumia mbinu za kisiasa, kijamii na kiuchumi kujaribu kuwavunja moyo vibaraka wa Uingereza barani katika tabaka la kijeshi na kisiasa. Katika matukio mapya ya mwaka 2017 yaliyo naswa pasi na shaka yoyote ni kuwa kwa hakika Uingereza bado haija poteza werevu wake katika siasa za Afrika na kuishinda Amerika kwa ujanja katika nchi zifuatazo za Afrika:   

          Kwanza, Kenya; koloni imara ya Uingereza ambayo kwa sasa inaongozwa na Uhuru Muigai Kenyatta mwana wa kibaraka wa kwanza wa Uingereza Jomo Kenyatta. Huku miito ya mabadiliko nchini Kenya ikipamba moto na uwezekano wa kutokea kwa ghasia baada ya uchaguzi wa Agosti 8, hili lingeipoteza mwelekeo mipango ya Uingereza nchini Kenya. Zaidi ya hayo, matokeo ya ghasia hizo yangempa Raila Odinga kibaraka wa Amerika mkono wa juu dhidi ya kibaraka wa Uingereza Uhuru Kenyatta katika meza ya majadiliano. Hivyo basi, Uingereza ikaunda njama iliyolenga kuionyesha Kenya kuwa mfano kwa Afrika pamoja na Ulimwengu kwa kukomaa kwake kidemokrasia na kuheshimu taasisi zake. Njama hii ilikuwa ni kubatilisha uchaguzi wa uraisi wa Agosti 8, 2017. Wakati huo huo kumfanya kibaraka wake kuheshimu uhuru wa mahakama ingawa ilimpa mwanya wa kuonyesha kutoridhika kibinafsi na uamuzi huo lakini kama wadhifa wa uraisi unaheshimu uhuru wa mahakama. Yote haya yalifanyika kwa manufaa ya Uhuru Kenyatta. Sifa zilimiminika kwa Kenya kama mwenge wa Afrika na Kenyatta akaonyeshwa kama kiigizo kwa maraisi wa kiafrika ambaye licha ya kuchaguliwa kwake tena kubatilishwa hakuzua rabsha kwa kutumia zana za serikali zilizo mikononi mwake. Huku upande mwengine Amerika ikishindwa kwa ujanja sawia na kibaraka wao Raila Odinga aliye nyimwa ufadhili wa kifedha na hivyo basi kushindwa kuanzisha kampeni nyengine kali ikilinganishwa na mpinzani wake mkuu aliyekuwa na zana za serikali mikononi mwake. Hili lilimpelekea Raila badala ya kufanya kampeni kwa marudio ya uchaguzi, badala yake; akapinduka na kuitisha mabadiliko katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC). Mwishowe akaishia kujiondoa katika marudio ya uchaguzi wa uraisi wa Oktoba 26, 2017, uliofanyika na Uhuru Kenyatta kuibuka mshindi na kisha kuapishwa mnamo 28 Novemba 2017. Hivyo basi, kilicho salia kwa Raila Odinga ni mbwembwe za hapa na pale tu na kujikusanya upya kwa uchaguzi wa 2022, ambao ni miaka mitano ijayo!   

            Pili, Zimbabwe; vile vile koloni imara ya Uingereza inayoongozwa na Emerson Mnangagwa rafiki wa raisi aliye tawala kwa muda mrefu zaidi Robert Mugabe ambao wote wawili ni vibaraka wa Uingereza. Huku miito ya mabadiliko ikipamba moto nchini Zimbabwe kutokana na kuzorota kwa hali ya kiuchumi kwa kuteremka kwa asilimia 40% kwa uzalishaji jumla wa nchi, kushuka kwa asilimia 51% kwa mazao ya ukulima na kuanguka kwa asilimia 47% kwa uzalishaji wa viwanda. Uingereza kwa ujanja ilikuza mfarakano wa kimakusudi ndani ya chama tawala cha Zimbabwe African National Union – Patriotic Front (ZANU-PF). Mfarakano huu ulikusidiwa kugurisha hamasa kutoka kwa mabadiliko msingi halisi na badala yake kuzitumia kukaribisha mabadiliko ya kisanii. Njama hii ilikuwa ni kumtumia Grace Mugabe kama mwanamke mwenye uchu wa uongozi anayetaka kukwea mamlakani kwa kudandia fursa ya afya duni na uzee wa mumewe Robert Mugabe. Kisha kutumia jeshi ambalo liko imara chini ya mshahara wa Uingereza kutekeleza mapinduzi mepesi yasiyo na umwagikaji damu. Hili lilipelekea Emerson Mnangagwa kupewa hatamu za uongozi kwa lengo pekee la kudumisha hali halisi kama raisi watatu wa Zimbabwe. Huku watu wakisherehekea na kukaribisha mabadiliko na kudekezwa kwa maneno hadaifu ya hotuba ya kutawazwa ya Emerson Mnangagwa mnamo 24 Novemba 2017 katika uga uliojaa pomoni katika jiji kuu, Harare. Amerika kupitia kibaraka wake Morgan Tsvangirai walirudi upya katika mchoro wa mikakati yao huku wakikuna vichwa vyao baada ya kushindwa ujanja na Uingereza.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Hizb ut Tahrir Kenya

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumapili, 09 Agosti 2020 07:12

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu