Jumatano, 22 Rajab 1446 | 2025/01/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Uchaguzi wa Agosti 9: Zoezi Lisilokuwa na Maana

Habari:

Wakenya watashiriki uchaguzi mnamo 9 Agosti, 2022. Majirani wa Kenya wanafuatilia uchaguzi huu kwa umakini, kwa kuwa Kenya ndio kitovu cha kiuchumi cha Afrika Mashariki na Kati. Huu unatarajiwa kuwa uchaguzi wenye ushindani mkubwa baina ya muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Ruto na muungano wa Azimio unaoongozwa na Raila.

Maoni:

Kikatiba Kenya inatambuliwa kama nchi huru yenye ubwana, lakini kiuhalisia imebakia kuwa ni shamba la kikoloni. Kwa hiyo, walioko madarakani nchini Kenya wapo kwa ajili ya kudumisha na kuimarisha mahusiano ya kikoloni. Hivyo basi, siasa za kidemokrasia zina sifa ya kutoa ahadi nyingi na manifesto zinazovutia kama ngazi za kuwahadaa watu kwamba mustakbali wao ni mzuri. Hata hivyo, punde tu uongozi mpya unapoingia mamlakani, hutekeleza yale ambayo yanawafaidi wao, washirika wao na hususan maslahi ya mabwana zao wakoloni.

Kwa mara nyingine Wakenya wapo njia panda hawajui ima wapigie kura mgombea urais kutoka muungano wa Kenya Kwanza au Azimio. Kuwa njia panda huko kumetokana na kuwa wamemeza chambo hadaifu ambacho msingi wake ni siasa za kidemokrasia. Chambo hicho kinahusisha kushiriki uchaguzi kila baada ya muhula wa miaka mitano kwa msingi wa kuwa na matumaini juu ya sarabi ‘wanasiasa’ kwamba watatatua matatizo yao. Alas! Hakuna kinachotatuliwa na uchaguzi, badala yake ni kuwa mambo yanazidi kuwa magumu kila muda unaposonga licha ya kuwepo uongozi mpya.

Tangu uhuru bandia wa bendera mnamo 1963, Wakenya wanaendelea kutaabika kutokana na changamoto za kupindukia za kisiasa, kijamii na kiuchumi kama vile ukiritimba wa rasilimali za umma kwa kampuni za kigeni, umasikini na kipote cha wanasiasa waliochini ya ushawishi wa kimagharibi. Hakuna utawala tangu wakati huo umeweza kutatua changamoto zilizotajwa kwa sababu wao ni sehemu ya tatizo linalohitaji kutatuliwa kimsingi.

Suluhisho lipo katika kuondosha nidhamu ya uongozi wa kidemokrasia ambayo imelazimishwa juu ya shingo zetu na wakoloni wamagharibi. Nidhamu ambayo inatanua kwa kuendeleza mapengo na uchafu katika nyanja zote za maisha. Ni nidhamu ambayo imejikita na kupigia debe mchakato wa bahati nasibu katika usimamizi wa mambo ya watu. Ni kupitia kuiondosha PEKEE ndipo kutapatikana fursa kwa Wakenya, Afrika na ulimwengu hatimaye kuweza kupumua kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Kuiondosha na sehemu yake kuchukuliwa na nidhamu ya utawala wa Kiislamu ya Khilafah. Khilafah itapeana kipaumbele katika kusahilisha maisha ya watu na SIO kukazanisha vitanzi vya kisiasa, kijamii na kiuchumi, kama inavyofanyika hivi sasa nchini Kenya na ulimwenguni kote. Haishangazi kuona utawala unatumia uwezo wote ilio nao ili kuhakikisha kwamba masanduku ya kutilia karatasi za kupigia kura na karatasi zinafikishwa sehemu za ndani ndani kabisa. Lakini, tawala hizo hizo zinafeli katika kufikisha huduma msingi sehemu hizo hizo za ndani ndani!

Wasiwasi na hofu za kisiasa ziko juu kwa sababu nidhamu yenyewe ni natija ya vurugu za kisiasa baina ya watu wa kawaida na wanafikra wakiwa upande mmoja dhidi ya watawala ‘wafalme’ na makasisi huko Ulaya. Ama nchini Kenya siasa za kidemokrasia zimejikita katika idadi na mirengo ya kikabila.  Hivyo basi, Wakenya wanafuatilia kwa makini yale matamshi na maelekezo yanayotolewa na viongozi wao wa kisiasa.

Kushiriki katika uchaguzi kunadaiwa kuwa ni kutekeleza haki ya kidemokrasia, lakini kiukweli ni kuwa una halalisha ufisadi unaotekelezwa juu ya ardhi. Msingi wa ufisadi ni kuwatawala watu kwa kutumia tungo za akili na sio wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu (swt). ﴾إِنِ ٱلۡحُكۡمُ إِلَّا لِلَّهِ﴿ “Hapana hukumu ila ya Mwenyezi Mungu tu.” [12. Yusuf: 40]. Hivyo basi, kila mzunguko wa uchaguzi tunawaona wanaojiita viongozi walewale wakitoa ahadi tupu lakini hakuna chochote kiuhalisia. Kwa kuongezea, lau watachangamkia mradi, lengo sio kuboresha maisha ya raia. Bali, lengo lao kuu ni kushiriki ili waweze kupata hongo kupitia miradi hewa na ubinafsishaji wa rasilimali za umma.

Kiuhakika, uchaguzi wa Agosti 9 sio chochote bali ni zoezi lisilokuwa na maana ambalo litaleta fujo na machungu zaidi kwa walioshiriki na ambao hawakushiriki. Historia ya uchaguzi wa kidemkorasia duniani inatoa taswira ya tawala zilizo sambaratika na wanadamu waliokata tamaa na waliozama katika simanzi. Mfano mzuri ni uchaguzi wa hivi majuzi wa Amerika ambao ulithibitisha kwa watu wote kwamba uchaguzi wa kidemokrasia ni mazoezi yasiyokuwa na maana na kwamba hakuna matumaini ya utulivu na ustawi kupitia kwayo. Amerika inayojiita kuwa ndio ngome ya demokrasia imethibitisha rasmi kwamba mungu wa demokrasia amefeli kabisa!

Kwa kutamatisha, hatutakiwi kupoteza muda katika bahati nasibu, badala yake tunatakiwa kuanza kufanyakazi kwa ajili ya kurudisha tena maisha ya Kiislamu kupitia kusimamisha Khilafah kwa njia ya Utume. ﴾وَيَوۡمَٮِٕذٍ۬ يَفۡرَحُ ٱلۡمُؤۡمِنُونَ﴿ “Na siku hiyo Waumini watafurahi.” [30. Ar-Rum: 4].

Imeandikwa kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu