- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Ukoloni Mamboleo ndio Unaopelekea Ukosefu wa Umeme Nchini Zambia
(Imetafsiriwa)
Habari:
Tarehe 1 Februari 2025, Bodi ya Udhibiti wa Nishati ya Zambia (ERB) iliongeza muda wa tozo za umeme za dharura za Shirika la Ugavi wa Umeme la Zambia (ZESCO) kwa miezi mitatu ya ziada, ambayo ni kuanzia Februari 1 hadi Aprili 30, 2025, huku nchi ikiendelea kukabiliwa na tatizo kubwa la upungufu wa umeme. (Lusaka Time 2/02/2025)
Maoni:
Bodi ya Udhibiti wa Nishati Zambia iliidhinisha tozo za dharura za Shirika la Ugavi wa Umeme Zambia (ZESCO) ili kusaidia shirika hilo kuzalisha takriban dolari milioni 15 kila mwezi kutoka kwa wateja wa reja reja ili kuchangia kuagiza kutoka nje ya nchi takriban kiasi cha megawati 788 za umeme. Licha ya uwepo wa tozo hizo Shirika la Ugavi wa Umeme Zambia, bado halikufikia lengo la kuyapata mapato hayo, bali lilichoweza kupata ni dolari milioni 10 pekee katika miezi miwili ya Novemba na Disemba.
Kufuatia tozo hizo mpya, bei ya umeme kwa wateja wanaotumia nyuzi (units) 200 hadi 300 imeongezwa kwa Ngwee 53 (0.0019$) kwa nyuzi, wanaotumia nyuzi 300 hadi nyuzi 400 kwa takriban Ngwee 85 (0.0036$) kwa nyuzi na wanaotumia nyuzi 400 mpaka nyuzi 500 kwa Kwacha 1 na ngwee 27(0.0133$) kwa kila nyuzi. Ongezeko hilo lililopendekezwa linafika 50% mpaka 156% na wastani wake ni 82.75% katika makundi yote ya wateja.
Hii si mara ya kwanza kwa Shirika la Ugavi wa Umeme nchini Zambia kupandisha bei ya umeme kwa kisingizio cha tozo za dharura. Mwaka 2019 lilifanya ongezeko la wastani wa 113%, lakini hadi sasa hakuna chochote kikubwa ambacho kimefanywa kuboresha hali hiyo ya upungufu wa umeme unaojitokeza mara kwa mara.
Inasikitisha sana kwamba Zambia ambayo inazalisha umeme wake mwingi kutoka katika bwawa la Kariba, bwawa kubwa zaidi duniani lililotengenezwa na binadamu lililojengwa kati ya 1955 na 1959 na mkoloni wa Uingereza kwa lengo la unyonyaji wake wa madini katika eneo la makoloni yake lililokuwa likijulikana kama Shirikisho la nchi za Rhodesia na Nyasaland ambalo linajumuisha Zambia, Zimbambwe na Malawi, bado hata baada ya uhuru wa bendera Zambia bado inaandama mwenendo ule ule wa zama za ukoloni (kutumika nishati ya umeme kwa ajili ya malengo ya unyonyaji).
Mfano wa hilo ni Kampuni ya Kimagharibi ya Copperbelt Energy Corporation inayomilikiwa na watu binafsi, ndio inayonunua asilimia 55 ya umeme unaozalishwa na Shirika la Ugavi Umeme Zambia na kusambaza umeme huo migodini, huku ni 25% tu ya Wazambia kiujumla ndio wanaopata huduma hii muhimu ya umeme, ilhali vijijini hali ni mbaya zaidi ambapo ni chini ya 5%.
Nakisi ambayo ililazimu kuibuka kwa tozo ya dharura ni 700MW mpaka 1300MW pekee, wakati nchi ya Zambia ina uwezo wa kuzalisha 2,300 MW kutoka katika nishati ya jua na 3,000 MW kupitia upepo. Kwa vyanzo hivi viwili pekee ingeweza kumaliza kabisa shida yake ya umeme.
Athari za tozo hizi ni kuwa zinaishia kuwa mzigo usiobebeka kwa watu hasa maskini na kuwa kizuizi zaidi cha upatikanaji wa nishati ya umeme kwa jamii ya watu wa kipato cha chini.
Hali hii ni zao la ukoloni mamboleo ambapo mataifa ya kibepari yanaifanya dunia hususan mataifa yanayoendelea kuamini kuwa kodi ndio njia pekee ya kuzalisha mapato ya serikali.
Afrika licha ya rasilimali nyingi haitaweza kamwe kuwa huru na kuweza kutatua ipasavyo matatizo yake chini ya mfumo wa kibepari wa kikoloni wa Magharibi. Mabadiliko ya msingi yanahitajika ya kubeba itikadi ya haki ya Uislamu ambayo ina uwezo wa kuleta suluhu kwa matatizo yote ya binadamu na kuzalisha viongozi wenye uwezo wa kusimamia masuluhisho hayo.
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Said Bitomwa
Mwanachama wa Afisi ya Habari Hizb ut Tahrir Tanzania