- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Jibu la Swali
Zaka juu ya Pesa Shirika
Kwa: Ahmad Saleh Ajoli
(Imetafsiriwa)
Swali:
Assalamu Alaikum wa Rahmatullah wa Barakatuhu,
Mada: Je, Zaka ni ibada ya kipeke yake?
Amiri wetu mheshimiwa, na sheikh mtukufu...
Mwenyezi Mungu akupe nusra, akuruzuku mafanikio, na akusaidie kwa Maanswari (wenye kunusuru) mithili ya Aws na Khazraj…
Kwa kuregelea mada ya juu ningependa kuuliza:
Je, Zaka ni ibada ya kibinafsi iliyo faradhishwa juu ya kila mtu binafsi pekee au imefaradhishwa kwa kampuni vilevile?
Ili kufafanua swali langu, nitatoa mfano:
Khalil na Zaid wana kampuni kwa hisa ya asilimia 50 kila mmoja, na mtaji wa kampuni hii ulikuwa ni dinar za Jordan 3000, Khalil hakuwa na kitu chengine chochote kinachostahili kutolewa Zaka, na alikuwa na deni la kibinafsi la dinar 1000, na Zaid alikuwa na dinar 4000 nyumbani kwake na zilikuwa zimezungukiwa na mwaka…
Je, ni vipi Khalil na Zaidi watakavyo tathmini Zaka zao? Je, kila mmoja atatathmini asilimia yake katika kampuni kando na ya mwenzake, au Zaka italipwa juu ya hesabu jumla ya mtaji wa kampuni?
Jibu:
Wa Alaikum Assalam wa Rahmatullah wa Barakatuhu,
Mwenyezi Mungu akulipe kheri kwa dua hii karimu, na namuomba Mwenyezi Mungu (swt) aijibu dua hii na kukulipa kheri…
Zaka ya mali ya pamoja:
Kuhusu zaka juu ya mali katika dhahabu na fedha, na pesa za sasa ambazo zinachukua mahali pake, zaka juu yake ni wajib kwa kila mtu binafsi katika pesa zake anapofikia nisaab (kiwango) na kuzungukiwa na mwaka mmoja…
Ama kuhusu mfano ulioutaja ndani ya swali, jibu lake ni kama ifuatavyo:
1. Ama Khalil, hisa yake ya mtaji wa kampuni ni "dinar 1500", na anadaiwa deni la "dinar 1000," ikimaanisha kuwa kilicho bakia ili kutathminiwa zaka ni "dinar 500" kwa sababu deni analodaiwa hupunguzwa kutoka kwa pesa zake na zaka huwa juu ya pesa zinazosalia baada ya kulipa deni, na tumefafanua dalili ya hilo katika kitabu kilichotabanniwa – Al Amwal fii Dawlatil Khilafah – Mali katika Dola ya Khilafah chini ya mada ya Zaka juu ya deni, ukurasa 165, ambapo kinasema:
(Ikiwa mtu anapesa zilizofikia nisaab, na zimezungukiwa na mwaka, na anadaiwa deni linalofikia nisaab, au pesa zinazosalia baada ya deni hilo kulipwa, ni kidogo kuliko nisaab, basi hatalipa zaka, na mithili yake ni kama mtu anaye miliki dinar elfu moja, na anadaiwa deni la dinar elfu moja, au ikiwa anamiliki dinar za dhahabu arubaini, na anadaiwa dinar za dhahabu thalathini, basi katika hali hizi mbili zaka sio wajib juu yake, kwa sababu hamiliki nisaab. Imesimuliwa na Nafi', na ibn 'Umar aliyesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:
«إذا كان لرجل ألف درهم، وعليه ألف درهم، فلا زكاة عليه»
“Pindi mtu anapokuwa na dirham elfu moja, na juu yake ni deni la dirham elfu moja, basi hakuna zaka juu yake” imetajwa na ibn Qudamah katika Al-Mughni.
Lakini ikiwa pesa zilizobakia kutokana na deni zinafikia nisaab, hapo ni lazima alipe zaka juu yake…) Mwisho.
Tathmini ambayo tumeitaja kabla ya nukuu zimetokana na makisio kuwa hakuna faida za mtaji wa kampuni hiyo, lakini ikiwa kuna faida kwa kampuni, huzingatiwa kama ukuaji wa mtaji na hivyo kuchukua hukmu yake, yaani huongezwa katika mtaji wa kila mshirika kwa kiwango cha hisa yake ya faida na huzingatiwa wakati wa kutathmini zaka…
Kwa hayo, ikiwa kiwango kinacho bakia na Khalil kwa mujibu wa hesabu za juu ni "dinar 500", endapo kiwango hiki kitapita nisaab, na kitazungukiwa na mwaka mmoja, basi zaka itatathminiwa kwake kwa kiwango cha asilimia 2.5, ambayo Khalil atalipa kutokana na pesa zake… na endapo kiwango kilicho tangulia kutajwa hakiko juu sana au bado hakijazungukiwa na mwaka mmoja, basi hawajibiki kulipa zaka hadi kifikie nisaab na kizungukiwe na mwaka mmoja… Kama ilivyo tajwa juu, endapo kuna faida, basi zitaongezwa katika mtaji.
2. Kuhusu Zaid, hisa yake ya mtaji wa kampuni ni "dinar 1500", na ana "dinar 4000" nyumbani kwake na hana deni juu yake, ikimaanisha anamiliki idadi jumla ya "dinar 5500", na hesabu hii bila shaka ni kutokana na makisio kuwa kampuni haina faida za mtaji, endapo kuna faida kwa kampuni, huzingatiwa kuwa ni ukuaji wa mtaji na hivyo kuchukua hukmu yake, yaani huongezwa katika mtaji wa kila mshirika kwa kiwango cha hisa yake ya faida na huzingatiwa wakati wa kutathmini zaka…
Na ni wazi kwa Zaid kwamba pesa alizo nazo zimefikia nisaab kwa sababu ni kiwango kikubwa cha "dinar 5500." Endapo kitakuwa kimezungukiwa na mwaka, basi zaka ni wajib juu yake katika kiwango cha asilimia 2.5 juu ya pesa jumla, yaani, juu ya "dinar 5500", na mwaka huanzia pale zinapofikia nisaab.
Nataraji jibu hili linatosheleza, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Zaidi Mwingi wa Hekima.
Ndugu yenu,
Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
19 Dhul Hijjah 1441 H
Sawia na 09/08/2020 M
Link ya jibu hili kutoka kwa Ukurasa wa Amiri wa Facebook