Jumatatu, 21 Jumada al-thani 1446 | 2024/12/23
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Silsila ya Maswali Yaliyowasilishwa kwa

Amiri wa Hizb ut Tahrir

Sheikh Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah Katika Ukurasa Wake wa Facebook

Jibu la Swali:

Zaka juu ya Bidhaa za Biashara
Kwa: Yasser Khudair
(Imetafsiriwa)

Swali:

Namaanisha, zaka ya bidhaa za biashara ni thamani ya bidhaa inayotolewa kwa ajili ya kuuzwa, thamani ya kuiuza kutoka kwa mlipaji zaka kwa wateja wake, sio thamani ambayo mlipaji zaka anainunulia kwayo!

Ikiwa nilinunua simu za rununu 10,000 na kuziuza kwa 15,000. Zaka itakuwa kutokana na 15,000.

Je, hii ni sahihi?!

Jibu:

Katika Kitabu ya Al-Amwaal: [Zaka juu ya Bidhaa za Biashara

Bidhaa za biashara ni kila kitu isipokuwa sarafu inayotumika kufanya biashara, kununua na kuuza, kwa ajili ya faida k.m. vyakula, nguo, samani, bidhaa za viwandani, wanyama, madini, ardhi, majengo na bidhaa nyinginezo zinazonunuliwa na kuuzwa.

Zaka inawajibika kwa bidhaa zinazochukuliwa kwa ajili ya biashara kwa makubaliano ya wanachuoni wa awali na wa baadaye. Kutoka kwa Samura b. Jundub ambaye alisema:

«أَمَّا بَعْدُ، فَإِنَّ رَسُولَ اللَّهِ ﷺ كَانَ يَأْمُرُنَا أَنْ نُخْرِجَ الصَّدَقَةَ مِنَ الَّذِي نُعِدُّ لِلْبَيْعِ»

“Ama baada ya swala na salamu! Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa akituamrisha kutoa Zaka kwa vile tulivyovitayarisha kwa ajili ya kuviuza” (Imepokewa na Abu Dawud). Imepokewa kutoka kwa Abu Dharr kutoka kwa Mtume ambaye amesema: «وَفِي الْبَزِّ صَدَقَتُهُ» “Kuna Zaka katika Bazz.” Imesimuliwa na Al-Daraqutni na Al-Bayhaqi. Al-Bazz ni nguo na vitambaa vya kusuka zinazotumika kwa biashara. Abu ‘Amra b. Hamas amepokea kutoka kwa babake ambaye alisema: “‘Umar ibn Al-Khattab alipita na akasema: ‘Ewe Hamas, toa Zaka katika mali yako’. Nikasema: ‘Sina mali yoyote isipokuwa Ji’b (podo za mishale) na ngozi’. Akasema: ‘Zikadirie, kisha toa Zaka zao.’” AbdurRahman b. Abdul-Qari alisema: “Niliteuliwa juu ya Bait ul-Mal katika zama za ‘Umar ibn Al-Khattab. Zawadi zilipotolewa, mali ya wafanyibiashara ilikusanywa na kuhesabiwa, kwa kile kilichopo au kisichokuwepo.” Kisha Zaka ikachukuliwa kutoka katika mali ya sasa kwa ile iliyokuwepo na isiyokuwepo.” Kutoka kwa ibn ‘Umar ambaye amesema: “Kuna Zaka ya Raqiiq (watumwa) na suti za Bazz ambazo zinakusudiwa kufanyiwa biashara.” Faradhi ya Zaka katika biashara imesimuliwa kutoka kwa Umar na mwanawe, ibn Abbas, mafaqihi saba, Al-Hassan, Jabir, Tawus, Al-Nakhai, Ath-Thawri, Al-Awzai, Ashl-Shafii, Ahmad, Abu Ubaid, watu wa rai (As’hab ar-Rai), Abu Hanifah na wengineo.

Zaka ya bidhaa za biashara ni wajibu inapofikia thamani ya Nisab ya dhahabu na fedha, na kuzungukiwa na mwaka.

Ikiwa mfanyibiashara ataanza biashara yake kwa mali iliyo chini ya Nisab kisha ikafika Nisab mwishoni mwa mwaka, hakuna Zaka juu yake kwa sababu mwaka haujapita juu yake. Zaka italazimika katika Nisab yake baada ya kupita mwaka mzima juu yake.

Iwapo mfanyibiashara ataanza biashara yake na mali iliyo juu ya Nisab kiasi kwamba anaanza biashara yake kwa Dinari 1,000 kisha biashara yake ikakua na kupata faida ifikapo mwisho wa mwaka na thamani yake ikawa Dinari 3,000, ni wajibu kwake kulipa Zaka juu ya 3,000 Dinari sio Dinari 1,000 alizoanza nazo. Hii ni kwa sababu faida yake inafuatana nayo yaani asili, na kipindi cha mwaka mmoja wa faida inayozalishwa ni sawa na kipindi cha mwaka mmoja wa asili. Hii ni kama watoto wa mbuzi (Sikhal) na wa kondoo (Baham), wanaohesabiwa pamoja nao, kwa sababu muda wao wa mwaka mmoja (Hawl) ni wa mama zao. Sawia na hii ni faida kwenye mali hivyo wakati wake (Hawl) ni kipindi cha mwaka mmoja wa asili ambayo faida ilipatikana. Pindi mwaka unapokwisha mfanyibiashara hukadiria bidhaa ya biashara yake iwe Zaka ni wajibu juu yake kwa sababu ya aina ya bidhaa yenyewe kama ngamia, ng'ombe na kondoo, au la, kama nguo, bidhaa za viwandani, ardhi na majengo. Anazikadiria zote kwa pamoja kwa vipimo vya dhahabu au fedha. Kisha anatoa zaka ya robo ya ushuri ikiwa itafikia thamani ya Nisab ya dhahabu au fedha, akitoa Zaka ya faradhi kwa sarafu inayotumika.

Inaruhusiwa kwake kutoa Zaka yake kwa bidhaa yenyewe ikiwa hilo ni rahisi kwake, k.m. pale anapofanya biashara ya kondoo/mbuzi, ng’ombe au nguo na thamani ya Zakat anayolazimika kukadiriwa kuwa ni kondoo, ng’ombe au nguo, anaweza kutoa Zaka yake kwa fedha au kutoa kwa kondoo, ng’ombe au nguo yaani anaweza kutoa chochote anachotaka.

Zaka ya bidhaa za biashara, ambayo mali yake inatozwa kama ngamia, ng'ombe na kondoo / mbuzi, inatolewa kama Zaka ya biashara, sio Zaka ya mifugo. Hii ni kwa sababu biashara ndiyo inayokusudiwa katika umiliki wao, sio umiliki tu...]. MWISHO.

Kwa hivyo biashara inakadiriwa mwanzoni, na ikiwa imefikia nisab au zaidi, hii inahesabiwa kuwa ni mwanzo wa mwaka na mwisho wa mwaka inafanywa tena, basi zaka yake hutolewa kulingana na makadirio wakati zaka inapostahiki, na kama ilivyotajwa hapo juu, faida inajumuishwa wakati wa kuhesabu thamani ya biashara hata kama mwaka mmoja haujapita, kwa sababu faida inahusiana na mtaji.

Yaani, makadirio ya biashara ni mwanzoni mwa nisab, kisha baada ya mwisho wa mwaka kutoka mwanzo wa nisab, yaani, wakati zaka inapostahiki.

Natumai hii inatosheleza, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Zaidi na Mwingi wa hekima.

Ndugu Yenu,

Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

28 Sha’aban 1444 H

Sawia na 20/03/2023 M

Link ya jibu hili kutoka kwa ukurasa wa Amiri wa Facebook

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu