- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Silsila ya Majibu ya Mwanachuoni Mkubwa Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah Amiri wa Hizb ut Tahrir "Juu ya Maswali ya Wanaozuru Ukurasa Wake wa Facebook wa "Kifiqhi"
Jibu la Swali
Maandamano na Hadith ya Waislamu Kutoka Wakiwa Safu Mbili
(Imetafsiriwa)
Swali:
Kwa: Moadh Seif Elmi
Sheikh wetu Assalamu Alaikum. Je, ile hadith ya Waislamu kutoka wakiwa safu mbili, akiwa katika uongozi wa safu moja ni Umar na safu nyengine ikiongozwa na Hamza, je hiyo hadith ni dhaifu?
Na
Assalamu Alaikum Sheikh Wetu Mtukufu.
Katika jibu lenu la swali kuhusu maandamano mlitumia dalili ya hadith iliyopokewa na Abu Nuaim Ahmad bin Abdillah… Al-Asbahaani (aliyekufa 430H) kwenye kitabu chake kiitwacho “Hilyatul Awliyaa” kutoka kwa Ibn Abbas, amesama: nilimuuliza Umar (ra) kwa nini uliitwa Al-Faaruq? Akajibu: Hamza alisilimu kabla yangu kwa siku 3, kisha Mwenyezi Mungu (swt) akakikunjua kifua changu nikasilimu pia… nikasema: yuko wapi mjumbe wa Mwenyezi Mungu? Akasema dadangu: yuko nyumbani kwa Arqam huko Swafaa… nikapiga Shahada (ash-hadu an laa ilaaha illaah…) asema (Umar): watu wa hapo nyumbani (kwa Arqam) wakapiga takbir (Allahu Akbar) kwa sauti ambayo waliyoko msikitini (Al-Kaaba) waliiskia. Asema (Umar): nikasema ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu hivi si tuko katika haki, tukifa ama tukiwa hai? Akajibu: "Ndio! Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mikononi mwake hakika nyinyi muko katika haki. Mkifa ama mkiwa hai!" nikasema: basi kwa nini tunajificha? naapa kwa aliyekutuma kwa haki tutoke. Basi, tukatoka safu mbili, Hamza akiwa katika safu moja, na mimi nikiwa katika safu nyengine. Zikitoa sauti kama sauti ya jiwe la kusagia. Mpaka tukaingia msikitini. Maquraish wakaniangalia mimi na Hamza, wakapatwa na dhiki ambayo hawajawahi kupata mfano wake. Basi, siku hiyo ndio mtume wa Mwenyezi Mungu akaniita Al-Faaruq, na Mwenyezi Mungu akatenganisha kati ya haki na batil”. Mwisho.
Na tukifuatilia hadith hii, Albani amesema ni Munkar, na imedhoofishwa na wanahadith wengi. Sasa, maswali yangu ni mawili:
1. Je, yafaa kutumia hadith dhaifu kama dalili? Kama jibu ni ndio, basi ni wakati gani? Na vipi tutaihukumu?
2. Na kama jibu ni hapana, je mna matokeo mengine kinyume na hiyo iliyotajwa katika swali?
Mwenyezi Mungu akubariki na akufungulie.
Jibu:
Wa Alaikum Salaam wa Rahmatullahi wa Barakaatuh.
Maudhui ya maswali yote mawili ni moja, kwa hiyo jibu ni hili:
Enyi ndugu wakarimu, sio kila mkisoma kwamba kuna mtu amedhoofisha mapokezi basi lazima iwe ni dhaifu moja kwa moja. Kwa mfano, kuna baadhi ya masheikh ambao walizidhoofisha baadhi ya hadith katika Sahih Bukhari na Muslim! Yaani, wamedhoofisha hadith zilizo kwenye vitabu ambavyo Ummah umevikubali kwa utulivu kabisa. Na hakika Bukhari na Muslim walikuwa wakichunga vipimo vikubwa na vya hali ya juu ili kusahihisha mapokezi “Sanad na Matni”. Lakini pamoja na hilo, wametokea watu na kudhoofisha hadith walizopokea!
Ndio, ikithubutu kuwa hadith ni dhaifu, basi haifai kutumiwa kuwa dalili. Lakini, hutokea baadhi ya wanahadithi wakaihukumu hadith kuwa ni dhaifu, na wengine wakaihukumu kuwa ni “hasan” inayofaa kutolea dalili. Na yeyote anayejua elimu ya hadith na misingi yake basi atafahamu haya mambo ambayo ni mashuhuri kwa wanazuoni wa hadith na kwa wenye “ijtihaad”. Utaona huyu atumia hadith kuwa dalili, na yule haitumii hiyo hadith kama dalili… na haya tumeyafafanua kiupana katika kitabu chetu cha “Shakhsiyyah” juzuu ya kwanza, mlango wa “hadith zinazokubalika na zisizokubalika”, na pia katika mlango wa “kuzingatiwa hadith kuwa ni dalili ya hukmu za kisheria”.
Na sasa, tutakujibu kuhusu Maswahaba kutoka wakiwa Makkah baada ya kusilimu Umar (ra):
1. Hakika, mapokezi yaliyo katika jibu la swali yamepokewa na Abu Nuaim Ahmad bin Ahmad bin Abdillah… Al-Aswbahani (aliyekufa 430H) katika kitabu chake “Hilyatul Awliyaa”. Na Abu Nuaim ni hafidh, muaminiwa. Amesema Zarkaliy kumhusu, katika kitabu “Alamun Nubalaa”: Abu Nuaim (336-430H) Ahmad bin Abdillah bin Ahmad Al-Aswbahaniy, Abu Nuaim: ni hafidh, mwanahistoria, ni kati ya waaminifu katika kuhifadhi na mapokezi pia. Alizaliwa huko Aswbahan. Kati ya vitabu vyake ni Hilyatul-Awliyaa juzuu 10, na Maarifat Al-Swahabah, kikubwa, kimebakia kwa maandishi ya mkono kikiwa juzuu mbili, juu kukiwa na maandishi “mwaka 551” kipo kwenye maktaba ya Ahmad 3 Istanbul, na. 497… na kitabu chake kingine ni Twabaqat ul-Muhaddithin wa Ruwaat, pia Dalaailun Al-Nubuwah, na Dhikr Al-Akhbaari Aswbahaan, na kitabu cha Ash-uaraa”. Mwisho.
Kwa hiyo, yamkinika kutegemea mapokezi yake kuhusu Waislamu kutoka wakiwa safu mbili baada ya Umar kusilimu.
2. Pamoja na hilo, hayo sio mapokezi pekee. Bali pia kuna mapokezi mengine sahihi:
- Imekuja katika kitabu cha Al-Mustadrak ala As-Swahihain cha imam Hakim: "kutoka kwa Uthman bin Abdillah bin Arqam, kutoka kwa babu yake ambaye ni Arqam, aliyehudhuria vita vya Badr, ambaye pia Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa akijihifadhi nyumbani kwake Swafaa: hadi Waislamu kukamilika 40, wa mwisho wao kusilimu akiwa ni Umar bin Khatwab (ra) basi, walipotimia arubaini walitoka kwa washirikina…”. asema Hakim: “hii ni hadith iliyo na Sanad Sahih, na hawakuipokea” (yaani Bukhari na Muslim) na imam Al-Dhahabiy ameafikiana naye.
- Na katika kitabu “Al-Twabaqat ul-Kubra” cha ibn Saad asema: "kutoka kwa Yahya bin Imran bin Uthman bin Arqam, asema: nIlimsikia babu yangu Uthman bin Arqam akisema: “nikiwa na miaka saba katika Uislamu, alisilimu babangu akiwa mtu wa saba na ilikuwa nyumba yake Makkah iko Swafaa nayo ndiyo ilikuwa nyumba ambayo Mtume (saw) alikuwemo humo mwanzoni mwa Uislamu. Humo akiwalingania watu, na wakasililimu humo watu wengi. Akasema (mtume) humo katika usiku wa Jumatatu:
((اللهم أعز الإسلام بأحب الرجلين إليك: عمر بن الخطاب أو عمرو بن هشام))
"Ewe Mola! Utie nguvu Uislamu kupitia unayempenda zaidi kati ya wanaume wawili: Umar ibn Khatwab, au Amr ibn Hisham”. Basi, akaja Umar kesho yake asubuhi, na akasilimu kwenye nyumba ya Arqam, halafu wakatoka, wakapiga takbir, wakaizunguka Al-Kaaba waziwazi. Na nyumba ya Arqam ikaitwa Dar ul-Islam (nyumba ya Uislamu)…”.
- Amesema ibn Is'haq katika Assirat Al-Nabawiyah: "...Akasema Umar wakati huo: Wallahi! Sisi tuna haki zaidi kwa Uislamu kunadi… na idhihiri dini ya Mwenyezi Mungu Makkah. Na watu wetu wakitaka ushari na sisi tutapambana nao. Na wakitaka uadilifu, basi tutawakubalia". Basi, Umar na wenzake wakatoka, wakaketi msikitini na Maquraish walipoona Umar amesilimu, walijuta”.
- Na vilevile, maudhui ya safu mbili imetajwa na Taqiyyud din al-Maqriziy katika Imtaa ul-Asma`a. Pia Husain bin Muhammad Diyaar Bakriy katika “Taarikh ul-Khamis”. Na Muhammad Abu Shuhba katika “Assirat un-Nabawiya”, imetajwa pia na Safiyyu Rahman katika “Arrahiq ul-Makhtum” na wengineo.
3. Ukishafahamu hayo, nitanabahishe pia kwamba, kusema yafaa kufanya maandamano, sio kwa mapokezi haya tu. Kwa sababu, maandamano ni mbinu tu ya kutoa rai na kufikisha fikra, sawa na matoleo, mihadhara, sinema, video, na nyenginezo katika mbinu tofauti. Na kimsingi, mbinu na muundo ni mubaah (zaruhusiwa) maadamu haijakuja dalili ya kuharamisha baadhi yake, hapo tu ndipo huzuiliwa. Na hizi mbinu na miundo huwachangamsha watu kuubeba Uislamu na kujifunga, na kujihusisha nao pia. Na Hizb hutumia matendo haya kulingana na inavyowezekana kwa sharti yasimamiwe na kuendeshwa na Hizb, kikitumia bendera zake, kauli mbiu zake, na kikusanye watu chini ya uongozi wake… wala sio kwa mchanganyiko na wengine ikawa kila mmoja atoa mwito wake na bendera yake… Hizb haifanywi matendo kama hayo bali, tuwezalo kufanya kwa uwezo na uongozi wetu tutafanya. Na yaweza kupita mda tukawa hatuwezi kufanya matendo haya, na wakati mwengine tukaweza… ni kama mbinu ya Afisi za Habari, ilikuwa ngumu wakati wa Abu Ibrahim Mwenyezi Mungu amrehemu, na ikawa afadhali kiasi wakati wa Abu Yusuf Mwenyezi Mungu amrehemu. Akanikalifisha niwe msemaji rasmi nchini Jordan. Na leo kama unavyoona, Afisi zetu za Habari ni ziko nyingi.
4. Mwisho: enyi ndugu watukufu, kila kitendo tunachokifanya, na kila hatua tunayopiga, huwa tunafikiria na kuzingatia. Sio tu ili tuepuke haraam, bali tunaepuka hata vumbi dogo la vumbi la jambo haramu; huku tukimtegemea Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa siri na dhahiri, katika dogo na kubwa… hakika, sisi twabeba jukumu kubwa linalolemea hata majabali!. Basi, hivi mwadhani tutaweza kuenda mbele kweli lau sio kwa kujifunga na hukmu za kisheria katika nyoyo zetu, na katika ndimi zetu, na katika viungo vyetu vyote kiujumla?!. Twamuomba Mwenyezi Mungu atusaidie, na atuongoze kwenye mazuri zaidi. kwani yeye ndiye msimamizi wa walio wema.
Ndugu Yenu,
Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
Link ya jibu hili kutoka ukurasa wa Amiri wa Facebook