Ijumaa, 20 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Silsila ya Maswali Yaliyowasilishwa kwa

Amiri wa Hizb ut Tahrir

Sheikh Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah katika Ukurasa Wake wa Facebook

Jibu la Swali
Kumtegemea Dhalimu
Kanuni (Qaida) ya la Hafifu katika Maovu Mawili
Kwa: Osama Alshanab
(Imetafsiriwa)

Swali:

Assalam Alaikum Wa Rahmatullah Wa Barakatuh

Awali ya yote napenda kukushukuru na kukusifu kwa juhudi zako zilizobarikiwa, na namuomba Mwenyezi Mungu (swt) akunusuru kwa ushindi wake, na aandae kwa ajili ya ulinganizi huu wenye kuunusuru kama Saad bin Muadh, na tunamuomba kwa hilo uuondolee ugumu Ummah, na kuurudisha katika zama zake za awali.

Nina maswali mawili muhimu, na natumai kuwa jibu litakuwa la kina kadiri inavyowezekana, nikijua kuwa majibu yanayochapishwa ni ya kina kila wakati, lakini ningependa dalili nyingi za Shariah zenye maelezo ya kina ili ufahamu wa maswala haya uwe wa kina. Ama kuhusu swali langu:

La kwanza, kwa nini hairuhusiwi kumtegemea dhalimu (au mtu yeyote ambaye ana mamlaka na ushawishi na ana uwezo wenye manufaa, awe ni mnafiki, mtenda dhambi au hata kafiri) kwa kumuomba pesa au msaada ili Muislamu anaweza kupigana jihad, au hata kuinusuru Dini?

La Pili, ikiwa uko katika nchi, watu wake wengi ni Waislamu, na kuna uchaguzi wa urais. Wagombea wote hawataki kutawala kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu isipokuwa mmoja anayetaka kutawala kwa baadhi ya yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, huku ukijua kwamba mgombea huyu atahifadhi baadhi ya madhihirisho ya Kiislamu. Wagombea wengine wanaweza kuwahamisha baadhi ya wakaazi wa nchi hiyo na kuharibu madhihirisho mengi ya Uislamu, na wataeneza maovu na maadili machafu. Basi je, inajuzu kwangu kwa mujibu wa Shariah kumchagua muovu mdogo miongoni mwao, kama msemo maarufu unavyosema: (msiba ni mdogo kuliko msiba) na wakati huo huo Waislamu hawana uwezo wa kusimamisha udhalilifu huu na ni uhalisia uliolazimishwa. Kwa hiyo, nikimruhusu muovu (kiongozi) atawale, atawafanya watu wahamishwe na anaweza kuwachinja ndugu zangu Waislamu, na lau nitampa kura yangu yule muovu mdogo, basi nitakuwa nimekubali kutawaliwa na mtu asiyetaka kutawala kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu.

Jibu:

Wa Alaikum Assalam Wa Rahmatullah Wa Barakatuh,

Kwanza: Kuhusu swali lako la kwanza, jibu liko katika swali hilo:

1- Unauliza [Kwa nini hairuhusiwi kumtegemea dhalimu (au mtu yeyote ambaye ana mamlaka na ushawishi na ana uwezo wenye manufaa, awe ni mnafiki, au mtenda dhambi, au hata Kafiri), kwa kumuomba pesa au msaada ili Muislamu apigane jihad, au hata kuinusuru Dini?], kana kwamba unakusudia kwa kauli yako (kumtegemea dhalimu) kauli yake Mtukufu:

[وَلَا تَرْكَنُوا إِلَى الَّذِينَ ظَلَمُوا فَتَمَسَّكُمُ النَّارُ وَمَا لَكُمْ مِنْ دُونِ اللهِ مِنْ أَوْلِيَاءَ ثُمَّ لَا تُنْصَرُونَ]

“Wala msiwategemee wanao dhulumu, usije ukakuguseni Moto. Wala nyinyi hamna walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, wala tena hamtasaidiwa.” [Hud: 113] Imebainika kutokana na Aya hii kwamba uregee kwenye uharamu wa kuwategemea wale waliodhulumu, basi vipi unauliza juu ya kujuzu kwake?

2- Yafuatayo yameelezwa katika tafsiri ya Al-Qurtubi ya Aya hii:

[...Ina maswala manne: la kwanza – Kauli yake: (Wala msiwategemee) uhalisia wa kuegemea ni kutegemea, kuegemea, kujiliwaza na jambo na kutosheka nalo. Qatada akasema: Maana yake usiwe na urafiki nao na usiwatii. Ibn Jurayj (alisema): Usiegemee kwao. Abu Al-Aaliya (alisema): Msitosheke na matendo yao, na wote wanakaribiana...

Tatu - kauli ya Mwenyezi Mungu:

[إِلَى الَّذِينَ ظَلَمُوا]

“wanao dhulumu” ikasemwa: watu wa shirki. Na ikasemwa: Ni jumla kuhusu wao na kuwaasi kwao, kama katika kauli ya Mwenyezi Mungu:

[وَإِذا رَأَيْتَ الَّذِينَ يَخُوضُونَ فِي آياتِنا]

“Na unapo waona wanao ziingilia Aya zetu” [Al-An’am: 68] Hili lilielezwa hapo awali. Na hili ni sahihi katika maana ya Aya. Inaashiria kuachana na makafiri na kutowatii watu wa bid’a na wengineo. Kusuhubiana nao ni Ukafiri au uasi, kwa sababu usuhuba hupatikana tu kutokana na mapenzi.

Nne - kauli yake Mwenyezi Mungu:

[فَتَمَسَّكُمُ النَّارُ]

“ukakuguseni Moto” yaani itakuunguzeni; kwa kuchanganyika nao, kusuhubiana nao, kufuata pingamizi zao, na kuafikiana nao katika mambo yao...] Mwisho.

Imebainika kutokana na tafsiri ya Aya hii kwamba kumtegemea dhalimu ni haramu kabisa, na hakuna shaka juu yake, iwapo dhalimu ni kafiri au Muislamu muasi. Kwa hivyo, kumtegemea dhalimu kupitia mapenzi yake, utiifu, mwelekeo kwake, kumtegemea, kumsifu, na kukaa kimya juu ya udhalimu wake ... nk, yote yanakuja chini ya kutegemea, ambako ni haramu kutokana na andiko la ayah tukufu.

3- Pia kwa mujibu wa swali lako, dhalimu anaweza kuwa mtawala kafiri, na anaweza kuwa mtawala muasi au mnafiki anayetawala kwa yasiyokuwa Uislamu, kama ilivyo kwa watawala wa Waislamu leo.

a- Iwapo mtawala ni kafiri, basi kuomba msaada kwake haijuzu kwa mujibu wa Shariah, hata ikiwa ni kwa kuchukua pesa kutoka kwake kufanya jihad kwa sababu kuchukua pesa kutoka kwake bila shaka kunapelekea kumpa mamlaka juu ya upande uliochukua pesa kutoka kwake, ambayo ni mandhari yakuhisika, haswa linapokuja suala la makundi yanayopigana na wanamgambo. Wanakuwa ni mateka wa nchi zinazowafadhili, na maamuzi yao hayana thamani yoyote, kwa sababu yeyote aliye na ufahamu mdogo wa ukweli wa mambo anatambua kuwa nchi hazitoi msaada wa hisani, hivyo pesa zote ambazo nchi yoyote duniani inatoa upande mwengine usiokuwa wananchi wake ni kufikia malengo fulani kwa ajili yake, na haijali maslahi ya upande inayotoa misaada. Pindi watu binafsi, makundi na mapote yanapochukua pesa kutoka kwa nchi za kigeni, za makafiri kwa ajili ya jihad na kupigana na mvamizi, kwa yakini huo ni ushirikiano na mgeni na kujiua kisiasa, na huwapa makafiri mamlaka juu ya Waislamu, na Mwenyezi Mungu (swt) asema:

[وَلَنْ يَجْعَلَ اللهُ لِلْكَافِرِينَ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ سَبِيلاً]

“…wala Mwenyezi Mungu hatawapa makafiri njia ya kuwashinda Waumini.” [An-Nisa: 141]

b- Lakini ikiwa mtawala ni muasi, kama hali halisi ya watawala wa sasa katika nchi za Kiislamu, yeye pia haitoi pesa kwa upande wowote wa nje isipokuwa kufikia malengo fulani, na mara nyingi malengo haya ni ndani ya mipango inayotolewa na nchi za makafiri kwa sababu watawala wa Waislamu ni vibaraka wa nchi za kikoloni za makafiri. Kwa hiyo, upande ambao inafungamana na mtawala yeyote katika nchi za Kiislamu na kupata usaidizi na uungwaji mkono kutoka kwake huwa ni chombo mikononi mwa mtawala huyo anayekielekeza apendavyo. Tuliyoyaona huko Ash-Sham hayako mbali na sisi, katika suala la utegemezi wa makundi na mashirika mengi juu ya pesa chafu za kisiasa ambazo nchi za eneo hilo zinawapa, bila kusahau sifa zinazoelekezwa na pande zinazohusishwa na watawala madhalimu na utiifu wao, kung'arisha sura zao na kutozikataa... n.k hayo yote bila shaka yameharamishwa vile vile kwa sababu yanapelekea kupuuza haki na malengo ya Waislamu na kumfanya mchukuaji pesa kuwa mtumishi wa dhalimu na msaliti kwa Ummah wake na Dini yake.

4- Zaidi ya hayo, jihad katika njia ya Mwenyezi Mungu (swt) na kuinusuru Dini sio kwa kutafuta msaada wa makafiri au watawala madhalimu, kwa sababu makafiri ni maadui wa Waislamu na wao ndio ambao Ummah lazima unapaswa uwapige vita na kukabiliana nao. Haiingii akilini kwamba jihad yao ni kwa kuchukua misaada na pesa kutoka kwao, kwani huu ni mgongano wa wazi. Bali jihad na kunusuru Dini ni kwa kuutegemea Ummah na kuufanya kuwa ndio chanzo cha nguvu na utoaji.

Zaidi ya hayo, watawala madhalimu katika nchi za Kiislamu ni zana mikononi mwa makafiri, basi vipi itadhaniwa kuwa Muislamu atachukua misaada na pesa kutoka kwao ili kuwapiga vita makafiri na kuinusuru Dini, maadamu wao ni zana duni mikononi mwa makafiri, maadui wa Ummah, na wanausibu Ummah kwa adhabu kali kabisa, na kupigana na mujahidina wakweli na wabebaji Dawah wakweli?!

Pili: Ama kuhusu swali lako la pili:

Tayari tulishajibu kwa kina mnamo tarehe 29/8/2010, kuhusu kanuni ya la hafifu katika maovu mawili (au kama unavyosema katika swali lako: (msiba ni mdogo kuliko msiba), na haya ndio maandishi yake:

[Kanuni: “La Hafifu katika Maovu Mawili au La Hafifu katika Madhara Mawili” Hii ni kanuni ya Shariah iliyotabanniwa na wanazuoni wa fiqhi wengi. Na kwa mujibu wa wanavyuoni wanaoitabanni, ina maana moja ambayo ni kuruhusiwa kufanya mojawapo ya matendo mawili yaliyoharamishwa, ni kipi katika vitendo viwili chenye uharamu mdogo endapo mtu aliyekalifishwa na Mwenyezi Mungu (Al-Mukalaf) hana budi ila kufanya moja kati ya mawili yaliyoharamishwa na hawezi kujiepusha nayo, kwa sababu ni nje ya uwezo wake kwa kila njia. Mwenyezi Mungu (swt) asema:

[لَا يُكَلِّفُ اللَّهُ نَفْساً إِلَّا وُسْعَهَا]

“Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya iwezavyo.” [Al-Baqara: 286]. Mwenyezi Mungu (swt) asema:

[فَاتَّقُوا اللَّهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ]

“Basi mcheni Mwenyezi Mungu kama mwezavyo” [At-Taghabun: 16].

Yaani, kanuni hii kwa mujibu wa walioitabanni inatumika tu ikiwa hakuna njia ya kuepuka kufanya mojawapo ya makatazo mawili, wakati huwezi kuachana na matendo yote mawili yaliyoharamishwa isipokuwa kufanya kitendo kikubwa zaidi kilichoharamishwa, basi dogo la maovu mawili linachukuliwa. Wanachuoni hawa pia hawafafanui la hafifu katika  maovu mawili kwa mujibu wa matamanio, bali kwa mujibu wa hukmu za Shariah. Kwa mfano, ulinzi wa nafsi mbili unatangulizwa kuliko kuhifadhi nafsi moja, na kuhifadhi nafsi tatu ni bora zaidi, na kadhalika. Kuhifadhi nafsi kunakuja kabla ya kuhifadhi mali. Kuihifadhi Dar ul Islam kunakuja chini ya kuhifadhi Dini ambayo ni muhimu zaidi kuliko kuhifadhi roho na mali. Kadhalika, Jihad na utawala (Imamah) mtukufu yako chini ya kuhifadhi Dini ambayo ni ya juu na muhimu zaidi ya mahitaji. Mwanachuoni Ash-Shatibi amesema katika Al-Muwafaqat: “Nafsi zinaheshimiwa na kuhifadhiwa na lazima ziokolewe, ikiwa kuna chaguo kati ya kuiruhusu nafsi kuishi au kupoteza mali juu yake, au kuiua nafsi na kuhifadhi mali, basi kuiweka nafsi hai kunatangulizwa.”

Mifano iliyotajwa na wanazuoni hawa katika matumizi ya kanuni hii ni pamoja na:

1- Iwapo mwanamke anakabiliwa na hatari katika uchungu wa uzazi na ikawa vigumu kuwaokoa mama na mtoto na uamuzi wa haraka unahitajika: ima kumwokoa mama ambayo inapelekea kifo cha mtoto, au kumuokoa mtoto ambaye ni kifo cha mama, na ikiwa hali hiyo itaachwa na mmoja wa hao wawili akatolewa muhanga ili kuokoa mwingine au mmoja kuokolewa na kifo cha mwingine, hii inaweza kusababisha kifo cha wote wawili. Katika hali hii tunaweza kutumia “la hafifu katika maovu mawili, haramu mbili, au madhara mawili, ambayo ni kutekeleza kitendo cha kumwokoa yule anayetakiwa katika kesi hii, ambaye ni mama, hata kama kitendo hiki hiki kitamuua wa pili.

2- Kwamba mtu anazama maji au kuuwawa na mtu mwingine, au kudhuriwa sana mwilini na viungo vyake, au mwanamke kunajisiwa, mbele ya mtu aliyekalifishwa na Mwenyezi Mungu (Mukalaf) ambaye anaweza kuzuia maovu haya na ana swala ya faradhi ambayo huenda ikampita wakati wake; ima azuie kitendo hicho kilichoharamishwa na akose kutekeleza wajibu, au akiwa atatekeleza wajibu kwa wakati, basi kitendo hicho kilichoharamishwa kitatendeka, na muda hautoshi wa kufanya mambo yote mawili kwa pamoja. Hapa yanakuja matumizi ya kanuni hii, na mizani pia inaamuliwa na Shariah, ambayo ilifanya kuondolewa kwa makatazo haya yaliyotajwa hapo juu kuwa ya kutangulizwa kuliko kutekeleza jukumu lililotajwa hapo awali, lakini ikiwa inawezekana kutekeleza majukumu yote mawili kwa pamoja, basi hilo linakuwa wajibu.

3- Hii ni mifano mengine iliyotajwa na Imam al-Ghazali na Izz al-Din ibn Abd al-Salam, Mwenyezi Mungu awarehemu, inayoonyesha matumizi ya kanuni ya “la hafifu katika maovu mawili”, kwa mujibu wao, na pia kuonyesha mizani kati ya hukmu. Al-Ezz amesema katika kitabu chake “Qawa’id Al-Ahkam Fi Masalih Al-Anam”: “Ikiwa uovu mtupu utaungana, endapo inawezekana kuuzuia, tutauzuia. Ikiwa ni vigumu kuzuia maovu yote, tunazuia lenye kudhuru zaidi na kufuatiwa na lenye kudhuru zaidi na baya na baya zaidi,” kwamba mtu analazimishwa kumuua Muislamu, na akikataa maana yake ni kwamba atauawa, hivyo basi ni lazima aepuke madhara ya kumuua (Muislamu) kwa kuwa na subira ya kuuwawa, kwa sababu subira yake ya kuuwawa haina madhara kuliko kumuua (Muislamu) ...” Huu ni mfano wa wazi kwamba ni chaguo kwa la hafifu katika madhara mawili au haramu mbili, kwa sababu hawezi kuepuka yote mawili, na ikiwa anaweza kuzuia madhara mawili, ni lazima afanye hivyo.

Na amesema katika mfano mwingine: “Kadhalika, akilazimishwa kumuua mtu kwa kutoa ushahidi wa uongo au hukmu ya uongo (dhidi ya Muislamu), au atauwawa. Ikiwa yule anayelazimishwa kutoa ushahidi au kutoa hukmu inayopelekea kuuwawa mtu, au kumkatakata, au kufanya Zina, ushahidi au hukmu hiyo haijuzu, kwa sababu kujisalimisha kwa kuuwawa kunatangulizwa kuliko kusababisha kuuwawa Muislamu asiye na dhambi, au kumkatakata bila kosa, au kutenda Zina...", yaani ikiwa atauwawa au kutoa ushahidi wa uongo dhidi ya mwingine ambao unapelekea kumuua au kumkatakata, au kumshambulia heshima yake, basi haijuzu kwake kushuhudia bali awe na subira ya kuuwawa, kwa sababu kusalimu amri kwa kuuwawa kwake kunatangulizwa kuliko kumuua Muislamu mwingine.

Kwa maana nyengine, hali ya mtu anapokimbilia kutekeleza la hafifi ya makatazo mawili au madhara mawili ni pale mtu anaposhindwa kuepuka au kuzuia mambo yote mawili yaliyoharamishwa.

Hii ni mifano ya matumizi ya kanuni ya "la hafifu katika maovu mawili", kulingana na wale wanachuoni wanaoitabanni. Hata hivyo, yale ambayo ‘wanazuoni wa serikali’ wanayapigia debe au wale wanaotaka Muislamu kuzipa mgongo hukmu za Shariah kwa kupotosha na batili hayatoki katika mifano ya kanuni hii.

Wale wanaotumia kanuni hii kufanya kitendo hiki kilichoharamishwa badala ya kitendo kile kilichoharamishwa, wakihalalisha matendo yao kwa kuogopa kufungwa au kufutwa kazi, huu sio mfano wa kanuni hii.

Kadhalika wale wanaosema tunashiriki katika utawala wa kikafiri ijapokuwa imeharamishwa, ili tusiwaachie wapotovu vyeo vyote vya kutawala kwani kuwaachia ni haramu zaidi... hili sio miongoni mwa matumizi ya kanuni hiyo, badala yake ni kama mtu anayesema tunafungua baa (kwa ajili ya pombe) na kupata pesa kutoka kwayo badala ya kumwacha kafiri aifungue na kupata pesa.

Sio miongoni mwa matumizi ya kanuni kwamba mtu anawasilishwa na mambo mawili yaliyoharamishwa na anachagua dogo wakati ana uwezo wa kujiepusha na yote mawili, kama vile kusema wale wanaosema mchague fulani, hata kama yeye ni kafiri mkisekula au fasiki, au muunge mkono fulani na wala usimuunge mkono mwengine, kwa sababu wa kwanza anatusaidia na wa pili hautusaidii, au mithili kitu kama hicho, bali yale yanayosemwa hapa: masuala haya mawili yaliyowasilishwa mbele yetu yameharamishwa, kwa hivyo haijuzu kumchagua mtu wa kisekula na haijuzu kumteua kuwa mjumbe kumwakilisha Muislamu katika rai, kwa sababu hashikamani na Uislamu, na kwa sababu anafanya vitendo vilivyoharamishwa ambavyo haviruhusiwi kwa mjumbe kutekeleza kama kutunga sheria na kuidhinisha miradi iliyoharamishwa, na kulingania vitu vilivyo haramishwa, kuvikubali na kuvifuata, yaani anakataza mema na kuamrisha maovu. Kwa hiyo, hakuna hata mmoja wao anayepaswa kuchaguliwa; kwa sababu kumchagua yeyote kati yao ni haramu. Na kujiepusha na uchaguzi wa yeyote kati yao iko ndani ya uwezo wa mtu.

Sio mojawapo ya matumizi ya "la hafifu katika maovu mawili" kwamba Muislamu anakabiliana na vitendo viwili vilivyoharamishwa, na anaweza kujiepusha na vyote viwili, lakini anachagua lililo jepesi zaidi kulingana na matamanio yake, na analitekeleza kwa madai kuwa ni vigumu kuzuia haramu zote mbili…! Bali ni lazima ajiepushe na makatazo yote maadamu hilo linawezekana kwake kwa mujibu wa hukmu za Shariah.

Hii ni picha fupi ya "la hafifu katika ya maovu mawili" au "la hafifu katika madhara mawili"] Mwisho wa kunukuu jibu la swali lililotangulia.

Natumai hili linatosheleza, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Zaidi na Mwenye Hekima.

Ndugu Yenu,
Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

23 Dhul Hijjah 1444 H
11/7/2023 M

Link ya jibu hili kutoka ukurasa wa Amiri wa Facebook

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu