Jumamosi, 30 Rabi' al-thani 1446 | 2024/11/02
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Jibu la Swali
Uhakika wa Misimamo ya Kimataifa na ya Kieneo Juu ya Vita vya Idlib
(Imetafsiriwa)

Swali:

Serikali ya Syria imepeleka majeshi yake kusini mwa mkoa wa Idlib, na Urusi imetangaza kuwa tayari kupigana vita vya Idlib, “vita vikuu vya mwisho!” nchini Syria, na imefanya mazoezi ya kijeshi; makubwa zaidi kufanya katika historia yake ya hivi karibuni mashariki mwa bahari ya Mediterrania. Wengi walikuwa wanasubiri kuanza kwa vita baada ya kongamano kati ya Urusi, Uturuki na Iran kufanywa jijini Tehran mnamo 7/9/2018. Raisi wa Uturuki Erdogan alionyesha upinzani wake kwa kampeni hiyo ya kijeshi juu ya Idlib, na kwa hivyo shambulizi juu ya Idlib lilibadilishwa kupitia makubaliano ya kuwepo eneo lisilo na athari ya kijeshi yaliyofanyika baina ya Erdogan na Putin mnamo 17/9/2018. Ni ipi sababu ya mabadiliko haya? Amerika pia ilitishia kwa majibu yake makali endapo silaha za kemikali zitatumika, na baadhi ya nchi za Ulaya zilifuata sauti hii … Ni upi uhakika wa misimamo ya kimataifa na ya kieneo juu ya vita vya Idlib?    

Jibu:

Ili kuelewa misimamo ya Kimataifa juu ya vita vya Idlib ni sharti tuangalie ukweli ufuatao:

1- Mwanzo, twasema kuwa Amerika haina ikhlasi katika uhadaifu wake wa kuusaidia upinzani. Inasimama nyuma ya serikali za Uturuki na Saudi kuyahadaa makundi ya Syria kwa sera ya “karoti na kigongo” na kuyasukuma katika maridhiano na mikataba ya kusitisha vita na serikali na kuyasalimisha maeneo kwake. Hakika, risala ya Amerika kwa upinzani wa Syria eneo la kusini ilikuwa dhahiri na wazi, kuwa wasitarajie usaidizi wa Amerika kuzuia mashambulizi ya jeshi la Syria. Kuhusu Idlib, balozi wa Amerika katika Umoja wa Mataifa Haley aliuambia mkutano wa waandishi habari: “Hii ni hali mbaya, na ikiwa wanataka kufuata njia hiyo ya kuichukua Syria, wanaweza kufanya hivyo,” akimaanisha serikali ya Syria ya Bashar al-Assad pamoja na washirika wake Urusi na Iran… Aliongeza: “Lakini hawawezi kufanya hivyo kwa silaha za kemikali.” (Reuters, 4/9/2018).

Upinzani uliotangazwa na Amerika ni katika utumiaji wa silaha za kemikali na sio katika udhibiti wa serikali juu ya Syria. Hii inajumuisha yale aliyotoa wito mwenyekiti wa muungano wa wakuu wa kijeshi wa Amerika, Jenerali Joseph Dunford, ‘Majadilano zaidi baina ya Waturuki, Wasyria na Warusi juu ya oparesheni halisi za kupambana na ugaidi, ndiyo yatakayokuwa mwelekeo sahihi, kinyume na oparesheni kubwa za kawaida,’ alisema: “Napendekeza kuwa oparesheni za kupambana na ugaidi zifanyike katika njia itakayoondoa tishio la kupoteza maisha ya wasiokuwa na hatia” (Reuters, 4/9/2018). Amerika huitumia kadhia ya kemikali kila inapotaka, na kuitisha hatua kutoka kwa serikali ili iwe kisingizio chake cha kutekeleza sera zake. Serikali hiyo imehakikishiwa kwa kukaririwa usaidizi mkubwa wa Amerika kwake. Pasi kwayo, Iran na Urusi hazingekuja. Pasi kwayo, Uturuki na Saudi Arabia hazingetia shinikizo juu ya makundi ya kisilaha kutia saini makubaliano ya kusitisha vita na kujiondoa kutoka maeneo yao ili yanyakuliwe na serikali ya Syria. Na pasi kwayo, serikali ya kikatili haingerudi kwa jamii ya kimataifa na majadiliano ya Geneva na kupata uhalali ilioupoteza katika miaka ya mwanzo ya mapinduzi. 

2- Amerika imeliruhusu jeshi la Urusi kuingilia kati na kuisaidia serikali. Urusi na Iran na wanamgambo walikamilisha kazi kubwa na serikali imechukua udhibiti wa maeneo mingi ya Syria. Eneo kuu na lenye umuhimu zaidi ya ardhi zote lililosalia ni Idlib … Urusi inateseka ndani ya janga la Syria na inataka kuvunja ngome na kuingia Idlib ili kumaliza kizungumkuti cha kijeshi na kuangazia kazi ya kisiasa, na Amerika inataka kupanga suluhisho la kisiasa kabla ya kumalizika Idlib na kuitumia kadhia ya Idlib kuikamua Urusi, kupitia kurefusha kizungumkuti cha kijeshi au kukifupisha, kwa mujibu wa uidhinishaji wa Urusi kwa mpango huo wa suluhisho la Amerika kwa Syria, linalohusisha kuondolewa kwa kambi za kijeshi za Urusi kama sharti la suluhisho hilo la kisiasa lililoundwa na Amerika na kuufanya upinzani kusisitiza juu ya kuondolewa kwa kambi hizo kama sharti, yaani Urusi itaridhika kuondoka bila ya uharibifu zaidi! Hivyo basi, kupelekea upinzani wa Uturuki kwa hatua ya kijeshi ya Urusi, ulioundwa kushambulia Idlib kwa ushajiisho wa Amerika…

3- Urusi imeendelea kutekeleza misheni yake ya kijeshi nchini Syria, pasi na kazi yoyote ya kisiasa katika eneo hilo baada ya kuingia kwa utawala wa Trump, kwa hivyo kunyakuliwa kwa Ghouta kulifanyika kwa ushirikiano wa Uturuki, yaani kwa ridhaa ya Amerika, na kwa muktadha huo huo kunyakuliwa kwa eneo la kusini kukafanyika … Wakati huo huo, Amerika inakataa kujadiliana pamoja na Urusi juu ya Syria, kwa mtazamo kuwa utawala wa Trump hauoni dori yoyote ya kisiasa ya Urusi angaa kabla ya kukamilisha misheni yake ya kijeshi. Pindi mapinduzi ya kisilaha ya Syria yatakapo malizwa mjini Idlib, Urusi inataka iendelee na oparesheni zake za kijeshi, ndio maana ikapeleka majeshi yake, na kufanya mazoezi ya kijeshi katika bahari ya Mediterrania, kwa manuari kubwa, zana za kurusha makombora hewani na kuifunga anga katika eneo la mashariki mwa Mediterrania kwa mara ya kwanza katika historia yake. Imejipata katika tatizo kubwa; Urusi iligundua mambo ambayo haikuyapangia, ikiwemo:

A- Upinzani wa Uturuki kwa operesheni kubwa mjini Idlib: Uturuki haikukubali vita vipana mjini Idlib. (Waziri wa Uturuki alikadiria kuwa “magaidi” watambuliwe na kupigwa vita, na si sahihi kuanzisha vita kamili juu ya Idlib na kuipiga mabomu bila ya kuchagua) I’nab Baladi 14/8/2018. Upinzani wa Uturuki kwa vita hivi ulionyeshwa waziwazi wakati wa kongamano la Tehran kati ya maraisi wa Urusi, Uturuki na Iran. Uturuki, kwa njia ya kuishangaza Urusi, iliangazia hofu yake ya vita dhidi ya Idlib na kufurika kwa wakimbizi ndani yake. Iliifedhehesha Urusi, kwa kuvizingatia vita hivi kama chombo cha kuliondoa suluhisho la kisiasa nchini Syria. (Recep Tayyip Erdogan, Raisi wa Uturuki alisema mnamo Ijumaa kwamba kuendelea na mashambulizi katika mkoa wa Idlib, yakidhibitiwa na upinzani, itapelekea kuporomoka kwa mchakato wa kisiasa nchini Syria… (Al-Youm As-Sabi’ 7/9/2018). Na kisha kupitia kunyanyuka kwa sauti ya Amerika dhidi ya juhudi za Urusi kwa vita vya Idlib, Uturuki imejaza silaha katika vituo vya udhibiti mjini Idlib, vituo hivyo vilibuniwa ndani ya makubaliano ya kupunguza kasi ya Urusi na Iran, (duru za viwanjani na mashahidi waliiambia runinga ya “Sky News Arabia”, Jumapili, msafara wa kijeshi wa Uturuki ulielekea mji wa Idlib, karibu na mpaka wa Uturuki, unaodhibitiwa na makundi ya upinzani ya Syria na makundi mengineo. Duru hizo zilisema kuwa msafara huo wa kijeshi wa Uturuki uliingia eneo la Syria kutokea Kafr Lusin ukivuka kuelekea Idlib na viungani mwake, kaskazini mwa Syria, ukiwa na vifaru, zana za kijeshi na ulikuwa umebeba silaha … (Sky News Arabia 09/09/2018).    

Hivyo basi, Uturuki imekuwa ni kizingiti kwa matarajio ya Urusi ya kuyafagia makundi ya kijeshi mjini Idlib. Kutokana na hili, ilifanya mkutano wa pili baina ya Erdogan na Putin mnamo 16/9/2018 mjini Sochi, yaani siku tisa tu baada ya mkutano wao jijini Tehran.

B- Viashiria vya mabadiliko katika msimamo wa Iran: Iran imeonyesha ubaguzi usio wa kawaida katika kongamano la Tehran, mnamo 7/9/2018 baina ya makundi ya kisilaha ya kati na kati na ya “kigaidi” mjini Idlib, kana kwamba inaunga mkono msimamo wa Raisi Erdogan wa Uturuki ikipinga vita ambao ni kinyume na msimamo wa Urusi, kisha uchukuaji misimamo ya Iran ukawa wazi zaidi: (Waziri wa Kigeni wa Iran Mohammad Javad Zarif, mnamo Jumamosi, katika taarifa kwa vyombo vya habari alielezea kukinai kwa nchi yake kuwa suluhisho nchini Syria ni la kisiasa kuliko kuwa la kijeshi, na Zarif alisema katika mahojiano na gazeti la Ujerumani (Der Spiegel) kuwa Iran inajaribu kuepuka kile alichokiita “Umwagaji damu”, akikusudia upinzani wa nchi yake kwa shambulizi lolote la kijeshi eneo hilo … (gazeti la Uturuki la Zaman 15/9/2018). Ikiwa hii ndio hali ya upinzani wa Iran, Urusi huenda ikajipata peke yake katika vita vya Idlib endapo itasisitiza juu yake, na haiwezi kupigana nayo peke yake. 

C- La hatari zaidi ya yote pengine ni msimamo wa Amerika, ambayo ilitoa ilani kwa haraka ya shambulizi la kijeshi endapo silaha za kemikali zitatumika mjini Idlib. Urusi inajua kwamba Amerika kupitia serikali yake ndiyo inayo shikilia udhibiti wa mashambulizi ya kemikali. Hii ndio sababu Urusi ilifanya haraka kutuhumu upinzani wa kisilaha wa maandalizi ya shambulizi la kemikali dhidi yake ili kuhalalisha shambulizi la Amerika. Hata iliituhumu Uingereza pia kwa kujihusisha katika kile ilicho kiita “njama ya kemikali”, na mashambulizi ya Amerika kwa jumla nchini Syria yanaifedhehesha Urusi sana, lakini shambulizi la Amerika la wakati huu litakuwa kali na kubwa zaidi! “Tumejaribu kufikisha ujumbe siku za hivi karibuni kuwa endapo kutakuwa na utumizi wa silaha za kemikali kwa mara ya tatu, majibu yatakuwa mazito zaidi,” Bolton alisema katika hotuba juu ya sera. “Naweza kusema tumekuweko katika mashauriano pamoja na Uingereza na Ufaransa ambazo zilijiunga nasi katika shambulizi la pili na pia zinakubali kuwa matumizi mengine ya silaha za kemikali yatasababisha majibu mazito zaidi.” (Arabi 21, 10/9/2018) Urusi haihofii tu shambulizi la Amerika la Kimagharibi linaloifedhehesha nchini Syria bali pia shambulizi juu ya vikosi vyake huko.

D- Vile vile, shambulizi la kijeshi la umbile la Kiyahudi mnamo 4/9/2018 juu ya kijiji cha Wadi al-Uyun, karibu na mji wa Masyaf, magharibi mwa Hama na Banias, viungani mwa Tartus, maeneo yote yakiwa karibu na kambi za kijeshi za Urusi (50 km kutoka kambi ya Urusi ya  Hmeimim) na juu ya kambi ya Urusi mjini Tartus na wakati wa mazoezi makubwa yaliyo anzishwa na Urusi katika bahari ya Mediterrania kuanzia mnamo tarehe 1 hadi 8 Septemba 2018 pamoja na kushiriki kundi kubwa la majeshi ya wanamaji na wanaanga, mazoezi hayo yaliyoidhinishwa na Urusi kama mazoezi makubwa zaidi ya Urusi katika historia ya hivi karibuni katika bahari ya Mediterrania. Shambulizi hili la umbile la Kiyahudi lilibeba changamoto ya kipekee kwa Urusi. “shirika la habari la serikali ya Syria, SANA, liliripoti kuwa nidhamu za ulinzi wa angani za serikali ya Assad zilijibu makombora kadhaa yaliyo rushwa kutoka kwa ndege za (Israel) juu ya Wadi al-Uyun katika viunga vya Hama. (SANA) iliripoti kuwa nidhamu za ulinzi wa angani zililijibu shambulizi la “Israel” kupitia ndege iliyopenya kwa upeo wa chini kutokea magharibi mwa Beirut na kuelekea kaskazini zikiyalenga maeneo ya kijeshi katika mikoa ya Tartus na Hama. Roketi hizo zilikabiliwa kwa “baadhi yazo kuangushwa na ndege hizo zenye kushambulia zikalazimika kukimbia.” (Al-Arabiya.net 4/9/2018). Shambulizi kama hili la kijeshi karibu na kambi za Urusi, umbile la Kiyahudi halitasubutu tena kulifanya pasi na mawasiliano na Amerika, pengine wanabeba baadhi ya jumbe ambazo teknolojia ya Amerika haipingwi na majeshi ya angani ya Urusi (S-500), ili Urusi hatimaye itishike kutokana na ubwagaji mabomu wa Kimagharibi kuwa huenda ukazishambulia kambi zake au ndege zake nchini Syria.

E- Hilo ndilo lililotokea, ndege ya Urusi iliangushwa viungani mwa Idlib, ikiifanya Urusi kuwa matatizoni: “Msemaji wa Jeshi la Anga la Urusi Meja Jenerali Igor Konashnekov alisema kuwa marubani (wa Israel) waliiangazia ndege hiyo ya Urusi na kuifanya kuwa hatarini kwa shambulizi nchini Syria iliyo sababisha kuanguka kwake. Aliongeza kuwa: “Haimkiniki kwa waendeshaji wa ndege hiyo (ya Israel) na marubani wa “F-16” kukosa kuiona ndege hiyo ya Urusi, kwa kuwa ilikuwa imeshuka hadi kina cha kilomita 5, huku ikifanya uchokozi huo wa kimakusudi.” Ndege aina ya EI-20 iliyobeba wanajeshi 15, iliangushwa, ilikuwa ikirudi katika kambi ya wanahewa ya Hmeimim karibu na mji wa pwani wa Lattakia, ambao ulikuwa chini ya mashambulizi ya “makombora hasimu” mnamo Jumatatu jioni. Msemaji wa “Israel” alisema kuwa “Israel” haikuyaonya mapema majeshi ya Urusi nchini Syria, na walipokea ripoti ya oparesheni kupitia laini za simu za dharura chini ya dakika moja kabla ya shambulizi hilo, wakiongeza: “Ambapo tulishindwa kuipeleka ndege hiyo ya Urusi katika eneo salama” … (Sky News Arabia, mnamo Jumanne mchana, 18/9/2018).

(Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi Igor Konashnekov alisema mnamo Jumanne 18/9/2018 kuwa (Israel) haikuwaonya vinara wa majeshi ya Urusi nchini Syria kuhusu oparesheni zake karibu na Lattakia. Konashnekov alisema: “Israel haikuuarifu uongozi wa majeshi ya Urusi nchini Syria kuhusu oparesheni iliyopanga. Ripoti hiyo ilikuja kupitia “laini za dharura za simu” chini ya dakika moja kabla ya shambulizi hilo, ambayo haikuiwezesha ndege hiyo ya Urusi kurudi katika eneo salama.” Msemaji huyo alisema kuwa ndege (ya Israel) iliweza kuiangazia ndege hiyo ya Urusi, hivyo basi ndege hiyo ya Urusi ikapokea shambulizi kutoka kwa nidhamu ya ulinzi ya angani ya Syria, akiongeza kuwa ndege (ya Israel) iliunda mazingira ya hatari kimakusudi katika eneo la Lattakia mnamo 17/9/2018. Shambulizi hilo lilifanywa kutokea upeo wa chini. Konashnekov alisema kuwa hatua hizo za kizembe zilipelekea vifo vya wanajeshi 15 wa Urusi, ambapo hili linakhalifu ushirika kati ya Urusi na Israel. (Arabic Sputnik News 18/9/2018) 

Dalili zote hizi zimeifanya Urusi kushindwa kuitatua Idlib kijeshi ili kuitoa katika jinamizi, na haiwezi kuhimili uchokozi wa umbile la Kiyahudi unaoshajiishwa na Amerika!

4- Hivyo basi, Amerika inataka Urusi kubakia imekwama nchini Syria, ikishindwa kujitoa humo hadi Amerika ikamilishe utekelezaji wa suluhisho la kisiasa kwa mujibu wa mipango yake. Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Amerika John Bolton alisema mnamo Jumatano katika mahojiano ya kipekee na waandishi habari wa shirika la Reuters: (“Urusi “imekwama nchini Syria na kuwatazama wengine kufadhili ujenzi mpya wa Syria baada ya vita,”) ikiashiria kuwa hii inaipa Washington ala za majadiliano pamoja na Moscow. Bolton alisema kuwa Washington ina mkono katika majadiliano pamoja na Moscow kwa sababu “Kwa sasa hivi Urusi imekwama kule.” Aliongeza: “Sidhani kama wanataka kukwama kule…” (Arabic. Sputnik News 22 / 8/2018)  

Urusi sasa imeifahamu sera hii ya Amerika, na pengine kutambua athari ya kuhusishwa kwake na Amerika nchini Syria. Imekwama kikweli kweli ndani yake na haiwezi kutoka isipokuwa kwa ruhusa ya Amerika, ambayo ina ala zote za ushawishi nchini Syria, hii ndiyo sababu haikuweza kukamilisha shambulizi ililoliandaa ili kumaliza mgogoro mkoani Idlib kwa njia yake kwa sababu Uturuki ilipinga (kwa kusukumwa na Amerika) na Iran ikanyamaza kimya … Hivyo basi, mkutano wa Iran mnamo 7/9/2018 ulifeli kuidhinisha mpango wa Urusi wa kuishambulia Idlib na kumaliza mgogoro huo kwa njia ya Urusi. Ni siku chache tu sasa tangu mkutano kati ya Erdogan na Putin na shambulizi hilo lilibadilishwa kwa kubuniwa eneo lisilo na athari ya kijeshi! Hili lilifanyika kwa baraka za Amerika, shirika la habari la Novosti lilimnukuu afisa wa Amerika mnamo 18/9/2018 akiliambia shirika hilo: “Tunazikaribisha na kuzishajiisha Urusi na Uturuki kuchukua hatua za kivitendo ili kukinga shambulizi la kijeshi kutoka katika serikali ya Assad na washirika wake katika mkoa wa Idlib…” Mnamo Jumatatu, Raisi wa Urusi Vladimir Putin alitangaza makubaliano hayo pamoja na mwenzake wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan,

“Kubuniwa kwa “eneo lisilo na athari ya kijeshi” katika mkoa kaskazini magharibi mwa Idlib kufikia Oktoba 15, ambalo litakuwa chini ya udhibiti wa nchi zao mtawalia. Raisi wa Urusi alisema kwa kutamatisha mkutano wake na mwenzake wa Uturuki katika hoteli ya Kirusi ya Sochi: “Tumekubaliana kubuniwa kwa “eneo lisilo na athari ya kijeshi” lenye kina cha kilomita 15 na 20 katika mpaka wa mawasiliano, kuanzia mnamo Oktoba 15 mwaka huu.” Putin alisema kuwa makubalinao haya yanawakilisha “suluhisho muhimu” kufaulisha “maendeleo katika kutatua tatizo hili”. Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei Shweigo aliyaambia mashirika ya Urusi kuwa makubaliano haya yatazuia mashambulizi yaliyotarajiwa kwa siku kadhaa katika ngome ya mwisho ya makundi ya wapiganaji nchini Syria. Katika jibu la swali juu ya kama makubaliano haya yanamaanisha kuwa hakutakuweko na shambulizi la kijeshi juu ya Idlib, waziri huyo alijibu “ndio”, kwa mujibu wa mashirika ya Interfax na Tass … Kinyume chake, Erdogan alisema katika mkutano wa waandishi habari baada ya mkutano kati ya maraisi hao wawili: “Urusi itachukua hatua zinazo hitajika kuhakikisha kuwa hakuna shambulizi juu ya eneo lililobuniwa la kutuliza joto la kivita mkoani Idlib.” (France 24 / AFP 17/09/2018).

Hivyo basi, Urusi ilikomesha ubwagaji wake mabomu kwa Idlib na kurudisha manuari zake, zilizofanya mazoezi ya kijeshi katika bahari ya Mediterrania, na ingali inaiomba Amerika moja kwa moja au kupitia Uturuki kutatua kadhia hii ya Idlib kijeshi kabla ya suluhisho la kisiasa. Lakini Amerika inataka suluhisho la kisiasa kabla ya suluhisho lolote la kijeshi mkoani Idlib, ili kulitumia kama karata ya shinikizo ili kuihadaa Urusi katika kambi zake za kijeshi nchini Syria na kisha kuufanya upinzani kuibua kadhia kuhusu kambi hizo katika suluhisho la kisiasa … Yaani, maslahi ya Uturuki na Amerika nyuma yake kusitisha shambulizi la Urusi juu ya Idlib kimsingi ilikuwa kwa manufaa ya Amerika na wala si kuizuia serikali kutokana na kuifikia Idlib au kulinda raia, bali katika wakati ambao Amerika itatekeleza suluhisho hilo inalolitaka na kuishinikiza Urusi kwalo. Kisha hawatajali damu ya Idlib, ya raia au ya wasiokuwa raia, kuondoa athari ya kijeshi au kutoondoa athari ya kijeshi … na historia yao inaelezea hili katika maeneo tofauti tofauti ya Syria, na uhalifu wao ni maarufu mno …

5- Huu ndio uhakika wa misimamo yenye ushawishi juu ya kadhia ya vita vya Idlib, kimataifa na kieneo … Lakini kuna kitu ambacho, kwa mapenzi ya Allah, kitabadilisha sura ya misimamo ya kimataifa na ya kieneo, ambayo ni kwa kutekelezwa dori ya makundi mkoani Idlib kisahihi na kwa ukweli na ikhlasi kwa Allah (swt). Makundi haya yako aina mbili:

Ya kwanza: ni makundi ya kijeshi yanayo nasibishwa na Uturuki, yaliyotekeleza kujiondoa na khiana katika maeneo tofauti tofauti. Na kueneza kifkra za maridhiano na makubaliano ya kusitisha mapigano kutokana na shinikizo zito la Uturuki, lililofuatwa na ununuzi wa maadili ya viongozi wa makundi haya na kuyasheheni kwa pesa za Saudi. Haya ndiyo makundi ambayo Uturuki iliyaburuza katika majadiliano ya Astana, ikipelekea kuweko kwa maeneo yaliyo pungua joto la kivita. Yaani kuiruhusu serikali kuyadhibiti na kuyasalimisha kwake. Makundi haya leo yanasimama mbele ya haki, nayo yalikuwa ni chombo kilicho yadhoofisha mapinduzi ya Syria na kupotea kwa maeneo mengi kutokana na ahadi za Uturuki ambazo zimeonyesha urongo wao … Kwa kuwa vyeo vya makundi haya havikukosa watu mukhlisina, mnong’ono wa waziwazi ambao unasikika na karibu kila mmoja unaenea miongoni mwa makundi kuhusu uhadaifu wa Uturuki kwao, Erdogan aligundua hili, kama alivyo dhihirisha katika kongamano la Tehran pamoja na maraisi wa Urusi, Putin na wa Iran Rohani, pindi aliposema “upinzani unahisi kuhadaiwa na yanayojiri baada ya kubuniwa kwa maeneo hayo,” maeneo yasiyo na athari ya kijeshi” (mtandao wa Al Jazeera.net 7/9/2018). Erdogan anaungama kuwa mipango yake ya kuyahadaa makundi ya Syria imefichuka kwao, ambalo ndilo analohofia Erdogan, makundi haya hadi sasa hayajakimbilia kupigana na makundi yanayopinga suluhisho la amani kwa mujibu wa mpango wa Uturuki … na kufichuka kwa uhadaifu wa Uturuki huenda kukatumiwa kuyafanya makundi haya kukimbilia na kupigana vikali endapo yatashambuliwa …  

Ya pili: ni makundi mengine aghalabu yanayojulikana na vyombo vya habari kama “magaidi.” Nguvu hii imeongeza kupelekwa uhamishoni kwa wanamapinduzi wengi kutoka maeneo tofauti tofauti nchini Syria, mithili ya Ghouta, kusini, Homs, mji wa mashariki wa Aleppo na mengineo. Nguvu hii inadhibiti sehemu nyingi za eneo hilo. Na licha ya tofauti ya idadi yake na kiwango cha silaha zake, lakini hofu yao kwayo yaweza kufupishwa kama ilivyo ripotiwa nyuma katika ripoti za Amerika juu ya Syria, zinazo sema kuwa nguvu za “misimamo mikali” katika upinzani wa Syria, ingawa sio nyingi sana, lakini zinahusika katika vita vikuu katika uwanja wa Syria. Yaani, ni nguvu imara ambazo si rahisi kuzishinda … hususan kwa kuwa eneo la Idlib linakadiriwa kuwa eneo la mwisho la wanamapinduzi, wanaopigana ndani yake, kwa ujumla zitakuwa kali kutokana na kuwa wanamapinduzi hao wamekwama ndani yake na hakuna njia nyengine ya kutokea. Kwa yote haya, vita vya kijeshi kimsingi haviko kupendelea upande wa serikali licha ya kukusanyika kwa jeshi kubwa lililoandaliwa na Urusi kwa hili. Bali urefu wa vita hivi mkoani Idlib na kumakinisha kwa serikali majeshi yake na ya wafuasi wake huko huenda kukafungua mlango kwa maeneo mengine yaliyo dhibitiwa na serikali mwanzoni, kuwa nje ya udhibiti wake.

Hivyo basi, makundi haya kwa aina zake zote ikiwa yana ikhlasi kwa Allah, na kutumia kizungumkuti cha Urusi kutokana na shinikizo la Amerika ili kuihadaa, na kutotii uhadaifu wa Uturuki na pesa za Saudi Arabia … na kabla ya hili na kwamba daima yakumbuke maneno ya Allah (swt):﴾ كَمْ مِنْ فِئَةٍ قَلِيلَةٍ غَلَبَتْ فِئَةً كَثِيرَةً بِإِذْنِ اللَّهِ﴿ “Ni makundi mangapi madogo yameyashinda makundi makubwa kwa idhini ya Allah” [Al-Baqarah: 249].

Na hayatajisalimisha na kumuunga mkono Allah kwa ikhlasi basi kwa uwezo wa Allah, yataivunja mipango ya maadui wa Uislamu na Waislamu na yatawashinda mkoani Idlib.

وَلَيَنْصُرَنَّ اللَّهُ مَنْ يَنْصُرُهُ إِنَّ اللَّهَ لَقَوِيٌّ عَزِيزٌ﴿

“Na kwa yakini Allah atawanusuru wale wanaomnusuru Yeye. Hakika Allah ni Mwenye nguvu Mtukufu.” [Al-Hajj: 40]

12 Muharram Al-Haram 1440 H

Jumamosi, 22/9/2018 M

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoAlhamisi, 02 Aprili 2020 21:11

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu