Jumatano, 22 Rajab 1446 | 2025/01/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Demokrasia iko Hatarini: Je, Wamarekani Wamepoteza Imani katika Chaguzi?

(Imetafsiriwa)

Kufikia tamati ya uchaguzi wa katikati ya muhula wa 2022, maswali yameibuka kuhusu mazingira ya kisiasa na hadhi ya demokrasia nchini. Utafiti wa hivi majuzi wa New York Times na Chuo cha Siena ulifichua kuwa 71% ya wapiga kura wote walisema demokrasia iko hatarini. Wengi wa waliohojiwa katika utafiti huo waliona kuwa tishio kubwa zaidi kwa demokrasia lilitokana na ufisadi wa serikali. Inashangaza, wale waliohojiwa waliripoti wasiwasi wa muda mrefu kuhusu utendakazi wa kimsingi wa demokrasia, kama gazeti la New York Times lilivyosema, "Kama [hata] serikali inafanya kazi kwa niaba ya watu." Kura ya maoni pia ilionyesha kuwa wapiga kura wengi katika pande zote mbili walitambua chama pinzani kama "tishio kubwa kwa demokrasia." Vile vile, kura nyengine ya maoni iliyofanywa na NPR/Ipsos mnamo Januari 2022 ilipata 64% ya Wamarekani waliamini demokrasia ya Amerika ilikuwa "katika mgogoro na iko katika hatari ya kufeli," huku 70% wakihisi Amerika yenyewe inafeli.

Yeyote ambaye amefuatilia siasa za Kiamerika katika miongo michache iliyopita ataona kwamba maoni yaliyotolewa katika tafiti hizi ni ukweli halisi. Kuna wasiwasi mkubwa kati ya Wamarekani wastani kuhusu siasa nchini. Mazingira ya kisiasa nchini yamekuwa tete sana, huku matukio ya vurugu za kisiasa yakiibuka katika miaka michache iliyopita, ikiwa ni pamoja na wakati wa uchaguzi wa sasa wa katikati ya muhula. Mifano ya vurugu hizo za kisiasa ni pamoja na 'uasi' wa Capitol Hill mnamo Januari 6, 2021, shambulizi dhidi ya mume wa Nancy Pelosi, na vitisho dhidi ya wajumbe wa Congress. Nchi imegawanyika sana katika misingi ya kisiasa—juu ya masuala kama vile uavyaji mimba, sera ya kumiliki bunduki, uhalifu, na uhamiaji—na utiifu kwa vyama vyao vya kisiasa kiasi kwamba hata wanandoa wanaotaka kuoana huona tofauti za kisiasa kuwa suala lisiloweza kusuluhishwa.

Bila kujali matamshi ya kichama, imani katika taasisi za serikali iko chini mno. Kutoaminiana kwa taasisi za serikali, uadilifu wa mchakato wa uchaguzi, ukandamizaji wa wapiga kura, na uteuzi wa kisiasa unapitia tofauti za kivyama. Hii inaonyeshwa zaidi katika kura ya maoni ya Gallup ambayo ilifichua kuwa ni 27% tu ya Wamarekani walikuwa na imani kubwa katika taasisi kuu za Amerika. Kura hiyo hiyo ya maoni ya Gallup pia ilionyesha kupungua kwa uaminifu kwa matawi matatu ya Serikali ya Kifederali: Afisi ya rais, Mahakama ya Upeo na Bunge la Congress. Jambo la kushangaza ni kwamba tumeona mielekeo hiyo katika mataifa mengine ya Magharibi pia. Maswali ya demokrasia kufanya kazi kwa ajili ya watu, imani katika taasisi, na mfumo unaofanya kazi kwa maadili yake yanajadiliwa katika nchi za magharibi. Kuongezeka kwa umashuhuri, utaifa na watu hodari waliochaguliwa kidemokrasia kama Bolsonaro na Trump kunaonyesha zaidi kuchanganyikiwa kwa watu na hali halisi ilivyo na kupoteza imani katika mfumo wa demokrasia.

Zaidi ya hapo awali, vita vya kithaqafa vya Amerika vilivyogawanyika kuhusu masuala kama vile uavyaji mimba, CRT, LGBT na haki za Wanabadili jinsia, hadi uteuzi wa kisiasa kwenye Mahakama ya Upeo ni dalili ya watu waliogawanyika na jamii isiyo na maelewano. Tashwishi, ubaguzi, hasira na kutoaminiana huku kunaenea zaidi katika taasisi za Marekani, mwelekeo ambao umekuwa ukiongezeka kwa miongo michache iliyopita, hasa kuhusu Congress. Mazungumzo nchini yamepita zaidi ya siasa za upendeleo na sasa yanahoji kiini hasa cha demokrasia—ikiwa mchakato wa uchaguzi ni huru, wa haki, na wenye kuwakilisha watu.

Haya yanasisitizwa zaidi katika kauli ya hivi majuzi ya Rais Biden aliposema kuhusu suala la "wagombea wanaogombea kila ngazi ya afisi Amerika...ambao hawajitolei kukubali matokeo ya uchaguzi wanaoshiriki. ..[kwamba] Hii ndiyo njia ya machafuko nchini Amerika. Haijawahi kutokea. Ni kinyume cha sheria. Na si Kimarekani."

Ukweli ni kwamba kufeli kwa mfumo wa demokrasia kudumisha madai yake ya kuwa mwakilishi wa watu ni hadithi ya zamani-kama ilivyobainishwa, kwa mfano, na utafiti wa Chuo Kikuu cha Princeton wa 2014 uitwao "Kujaribu Nadharia za Siasa za Amerika," ambao ulihitimisha kwamba Marekani kimsingi ni serikali ambayo utawala umo mikononi mwa kipote cha wachache (oligarchy). Utafiti ulionyesha kuwa watu hawakuwa na athari kidogo kwa sera ya umma, iwe ya nje au ya ndani. Utafiti huo ulisema, "Uchambuzi wa aina nyingi unaonyesha kuwa kipote cha wanauchumi na makundi yaliyopangwa yanayowakilisha maslahi ya biashara yana athari kubwa huru kwa sera ya serikali ya Marekani, huku wananchi wa kawaida na makundi ya watu wengi yenye maslahi yana ushawishi mdogo au hawana ushawishi huru." Wakati wa uchaguzi huu wa katikati ya muhula, takriban dolari bilioni 17 zilitumika katika kampeni za uchaguzi huku nchi ikikabiliwa na mfumko wa bei wa kihistoria. Kutokana na hayo, hofu ya kweli katika takwimu za hali halisi kama ilivyo kwa Rais Biden ni kuchanganyikiwa na watu kutouamini mfumo wenyewe, badala ya kuondoka kinadharia au kimfumo katika Demokrasia ya Marekani ambayo kamwe haijawahi kuwepo.

Leo, demokrasia—mbali na ukweli wa kiulimwengu wote na mfumo mkuu wa utawala na haki unaopigiwa debe na Magharibi—inaporomoka kindani, huku watu wake wakipoteza imani katika uadilifu wake wa uchaguzi na uwezo wa Mfumo wa Kidemokrasia kutatua matatizo halisi.

Kinyume chake, nyoyo na akili za Waislamu kote duniani zinaendelea kutamani Uislamu na Mfumo wa Kiislamu utawale na kutatua mambo yao kivitendo. Uislamu unaongezeka na unaleta changamoto kubwa kwa mfumo wa kiliberali wa kisekula unaofeli. Uislamu una serikali yake na mfumo wake wa uadilifu unaodhihirika kivitendo katika kuanzishwa kwa Khilafah (Ukhalifa). Utekelezaji wa mfumo wa Uislamu—kama ulivyoshuhudiwa katika historia tajiri ya miaka 1400—una uwezo wa kuwaunganisha kihalali watu kutoka jamii mbalimbali, makabila, kanda, na hata imani katika jamii yenye uwiano, mshikamano na iliyolindwa. Ulimwengu wenyewe unashikilia pumzi yake chini ya mzozo, migawanyiko, unyonyaji na taabu ya leo inayoonekana kutokuwa na mwisho tangu kuvunjwa kwa Mfumo na Taasisi ya Uislamu mwaka 1924 M.

Katika Uislamu, ubwana ni kwa Mwenyezi Mungu (swt) pekee na wanadamu hawatungi sheria. Kwa hiyo, kanuni za kimsingi za jamii zimeegemezwa juu ya uadilifu na utekelezaji wa sheria ya Mwenyezi Mungu (swt), na tofauti na leo, haziathiri na ukomo, mapendeleo, na kubadilika kila mara kwa maadili au matakwa ya watu au kipote cha wenye mamlaka.

(إِنِ الْحُكْمُ إِلَّا لِلَّه)  

“Hapana hukumu ila ya Mwenyezi Mungu.” [Al-Anam: 57].

H. 5 Jumada I 1444
M. : Jumanne, 29 Novemba 2022

Hizb-ut-Tahrir
Amerika

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu