Jumatano, 22 Rajab 1446 | 2025/01/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Hakuna Jipya Katika Sera Mpya ya Marekani Kuhusiana na Afrika!

Utawala wa Donald Trump ulizindua ile inayoitwa “Sera Mpya ya Afrika” siku ya Alhamisi tarehe 14 Disemba 2018 katika Taasisi ya Heritage huko Washington DC kupitia Mshauri wa Usalama wa Kitaifa, John Bolton. Sera hiyo imekitwa katika misingi ifuatao: 1.Kupanua biashara ya Marekani na mahusiano ya kibiashara kati yake na mataifa ndani ya eneo lote, 2.Kupambana na hofu juu ya Uislamu wenye misimamo mikali na ugaidi na mizozo ya kivita na 3.Kutathmini upya dori ya uenezaji amani Afrika kwa kutosaidia na kutowekeza katika misheni za Umoja wa Mataifa (UN) ambazo hazizalishi, hazifaulu na hazihesabiki.
Kwa mara nyingine sera hii imedhihirisha kuwa Afrika inacheza dori muhimu katika njama za Wamagharibi. Kwani, tokea mwanzo Wamagharibi wanaitizama Afrika kama shamba la kikoloni ambalo lastahili kuporwa na watu wake kufanywa watumwa katika kila nyanja ya maisha ikijumuisha kijamii, kiuchumi, kisiasa na kielimu kwa kuwatekelezea mfumo batili wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake zinazochipuza kutokana nayo.
Uzinduzi wa sera hiyo unafanyika wakati ambapo Marekani imeanzisha Vita vya Kiuchumi vya Karne ya 21 dhidi ya maadui wake wa kweli na inaowadhania ambao wanaojumuisha Umoja wa Ulaya, China, Urusi na marafiki zao mtawalia. Maslahi ya Marekani yaliyomakinishwa juu ya mwito wa “Make America Great Again” ndiyo inayoendesha vita hivi. Misingi mitatu ya sera hiyo inamulika wazi aina ya mahusiano kati ya Afrika na Amerika, kuwa ni kati ya mtumwa na bwana. Kwa kuwa Afrika ni soko la ununuzi wa bidhaa za magharibi, ambazo mali ghafi yake imetoka katika shamba la kikoloni na hivyo basi biashara yake inaegemea Magharibi kuliko mataifa mengine. Ama kuhusu vita juu ya Uislamu wenye misimamo mikali, ni njama tu ya Wamagharibi ili kuwadanganya watu kuwa kujifunga kikamilifu na Uislamu ni tishio kwa dini nyingine. Lakini, ukweli wa nia yake ya kuushambulia Uislamu na Waislamu chini ya pazia ya kupigana na Uislamu wenye misimamo mikali na ugaidi na mizozo ya kivita; ni kuupaka matope Uislamu kama mfumo badala ya ule batili na uliofeli wa kisekula wa kirasilimali ambao umesababisha majanga kwa binadamu ulimwenguni kote. Ama kuhusu “UN kueneza amani,” ni urongo mwingine unaopigiwa debe na utawala wa Marekani ilhali wao ndio waanzilishi wa vita duniani kwa kuzivamia nchi nyingine ima moja kwa moja au kupitia mawakala ili kufikia malengo yake maovu.
Sera hii haina tofauti na zile za Umoja wa Ulaya, China, Urusi na washirika wao mtawalia katika mtizamo wao juu ya Afrika na hususan Waislamu na Uislamu. Ama kuhusu Afrika hili ni jaa lao la kumwaga bidhaa walizotengeneza ambazo chanzo cha mali ghafi yake rahisi imeibiwa moja kwa moja au kudhaminiwa na watawala vibaraka! Ama kuhusu Waislamu na Uislamu, ni tishio kwa utawala ulioko mamlakani ulimwenguni chini ya kivuli cha mfumo wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake zinazonuka na zilizotokana nao. Na ndiyo maana tunao mfano wa Waislamu wanaoteseka ndani ya jela za Urusi, China, Guantanamo Bay chini ya Marekani na katika nchi zilizoko chini ya Umoja wa Ulaya na koloni zake za awali zinapitishia sheria zisizokuwa na huruma kumpana dhidi ya eti “Ugaidi na Misimamo Mikali.” Hatua zote hizi ni kuhakikisha kuwa Uislamu haurudi tena kama mfumo kamili wa maisha chini ya kivuli cha Khilafah kwa njia ya Utume.
Tunaipinga hii sera mpya ya Afrika ambayo imeboreshwa na Marekani kwani inazindua upya wimbi la kung’ang’ania Afrika dhidi ya mataifa mengine makubwa ambayo yanajitahidi kuipiku Marekani katika kulimiki bara la Afrika. Wakati huo huo tunaulingania uongozi wa Afrika uukumbatie ulinganizi wa Khilafah ili kuweza kufikia mwamko wake na kuweza kukata mahusiano ya waporaji.
Hizb ut Tahrir Kenya inawakumbusha viongozi na wanasiasa wa bara la Afrika wawe wakweli kwa watu wao na wayaunge mkono maslahi ya raia wao. Kwa kupitia kukataa siasa za Marekani mkoloni ambazo zimefichua ukoloni mambo leo waziwazi. Hadi lini bara hili ambalo limejaa utajiri wa rasilimali lakini ndilo masikini ulimwenguni litafikia upeo wake? Ni mpaka viongozi ambao wamesalimisha nafsi zao kwa agenda za kikoloni zikiongozwa na Amerika, waachane na kujinasuwa na utumwa wa mfumo muovu kwa kutafuta njia ya maisha badala ambayo itawapa watu hadhi na kuwalinda damu na rasilimali zao. Historia itawahukumu vibaya mno!
Hizb ut Tahrir Kenya inawapa changamoto wanafikra na wasomi ambao ni wakweli kwa watu wao waupinge ukoloni wa mambo leo kwa kutumia akili, midomo na maandishi yao. Uzinduzi wa sera hii haumuhitaji msomi kutambua ni muendelezo wa uporaji, unyanyasaji na ubabe dhidi ya bara la Afrika. Mpango wenyewe uko wazi kuwa ni kwa maslahi ya Marekani kiuchumi kisiasa, usalama… chini ya mwito wa “Marekani kwanza” licha ya athari itakayopatikana kwa bara zima la Afrika. Huu ndio uhalisia wa nidhamu ya kikoloni ya kirasilimali, kwani mahusiano kati ya nchi kubwa na ndogo ni mahusiano ya Bwana na mtumwa wake. Hakuna Bara lililoathirika zaidi na nidhamu hii kama Afrika! Haijawalazimu kwenu kutafuta mfumo badala ili kuwaokoa watu ambao wanaokutizameni, basi fahamu zenu zitawaadhibu!
Hizb ut Tahrir Kenya inawakumbusha Waislamu dori ya ulinganizi wa Uislamu kama mfumo wa maisha ulio na suluhisho juu ya matatizo ya mwanadamu na kuwahesabu viongozi ambao wanaiga kila kitu kutoka Magharibi kiasi kwamba inapelekea kuharibu nchi zao na watu wao.
“وَ اِذَا قِیۡلَ لهَمۡ لَا تُفۡسِدُوۡا فِی الۡاَرۡضِ ۙ قَالُوۡۤا اِنَّمَا نَحۡنُ مُصۡلِحُوۡنَ اَلَاۤ اِنَّهمۡ همُ الۡمُفۡسِدُوۡنَ وَ لٰکِنۡ لَّا یَشۡعُرُوۡنَ” “Na wanapo ambiwa: Msifanye uharibifu ulimwenguni. Husema: Bali sisi ni watengenezaji. Hakika wao ndio waharibifu, lakini hawatambui.” ﴾Al-Baqara:11-12﴿

H. 5 Jumada I 1440
M. : Ijumaa, 11 Januari 2019

Hizb-ut-Tahrir
Kenya

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu