Ijumaa, 20 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

UFISADI NI USO WA PILI WA SARAFU YA MFUMO WA KIBEPARI WA URASILIMALI 

Ulimwenguni kote kumejaa vilio, majonzi na ukosefu wa utulivu, si kwa matajiri wala masikini, kwa kukosekana amani na hali mbaya ya kiuchumi. Hii ni kutokana na mfumo batil wa urasilimali uliopo mamlakani ambao umeasisiwa juu ya “Aqeedah” ya kutenganisha dini na maisha. Hivyo basi kuwapelekea wanadamu kujipa mamlaka ya kujitungia sheria zitakazowaongoza katika maisha yao ya kila siku kinyume na mpangilio wa Mwenyezi Mungu aliyewaumba. Kujipa kwao binadamu mamlaka ya utungaji sheria ndio ufisadi wa juu kabisa. Mwenyezi Mungu (swt) asema:

إِنِ الْحُكْمُ إِلاَّ لِلّهِ﴿ “Hapana hukumu ila ya Mwenyezi Mungu” [Surah Al-An’am: 57]

Mfumo huu batili wa kibepari umejifunga juu ya kipimo cha maslahi, manufaa au madhara, na kumtwika mwanadamu kuwa lengo lake la kuwepo hapa duniani ni kujistarehesha kwa kiwango cha hali ya juu kinyume na alivyosema Mwenyezi Mungu (swt):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ﴿ “Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi” [Surah Adh-Dhariyat: 56].

Kwa sababu hiyo ufisadi chini ya mfumo huu unatazamiwa kushamiri katika kila sekta ya maisha kuanzia uchumi, elimu, michezo, utawala n.k.

Hivi majuzi tumeshuhudia kashfa kadha za ufisadi nchini Kenya kama ilivyo kawaida, ambapo Kenya ilishiriki katika Michezo ya Olimpik 2016 iliyofanyika huko mji mkuu wa Rio de Janeiro, Brazil na kuisha siku ya Jumapili, 21 Agosti, 2016. Taifa la Kenya kupitia wasimamizi katika Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi wa Olimpiki (NOCK) lilihusika katika kuiba vifaa vya wachezaji ikiwemo pamoja na mavazi ya wachezaji hao yaliodhamiminiwa na NIKE hili likithibitishwa kwa kushikwa kwa mavazi hayo baada ya ofisa wa Tume ya Maadili na Ufisadi (EACC) kuvamia ofisi za kamati hiyo na kupata masanduku yaliyojaa mavazi ya michezo yaliyo stahiki kugawiwa wanariadha! Hii ikapelekea baadhi ya wasimamizi kutiwa korokoroni. Kabla ya hapo kulikuwa na kashfa ya wanariadhaa kujihusisha na dawa za kusisimua misuli n.k. ambazo zilipelekea Shirika la Kimataiafa la Kusimamia Riadha kuitaka nchi ya Kenya kupitisha sheria zitakazodhamini kupambana na wanariadha wake watakaojihusisha na madawa hayo. Napia kikosi cha Kenya kilicho shiriki katika michezo ya Rio 2016 kilikuwa hakina motisha wa hali ya juu vile ikizingatiwa baadhi yao walikuwa wamecheleweshwa kusafiri, wengine hawakuambatana na wakufunzi wao, na wengine wao licha ya kuwasili mapema lakini hawakupata stakabadhi zilizotakiwa ziwawezeshe kuingia katika sehemu maalumu iliyokuwa imetengewa wanariadha hao watakaoshiriki mashindano hayo! Yote hayo yakidhirishwa na utepetevu na ufisadi wa hali ya juu uliosababishwa na NOCK!

La kushangaza na kutamausha ni kuwa Mwenyekiti wa EACC ambayo walitekeleza uvamizi wa ofisi za NOCK na ndio taasisi kikatiba inayodaiwa kupambana na ufisadi, yeye mwenyewe amejiuzulu kutokana na mashtaka ya ufisadi wa kujihusisha na Kashfa ya Shirika la Kitaifa la Huduma kwa Vijana (NYS) baada kubanika kushiriki kwake katika kampuni yake ya Esaki Ltd kupokea kiharamu kitita kinachokadiriwa kuwa Milioni Ksh.281 mnamo Februari, 2014 baada ya kushinda zabuni ya Kuchimba Visima katika eneo la Kapenguria!

Awali aliyekuwa waziri wa Wizara ya Ugatuzi na Mipango, licha ya kujibandua mamlakani baada ya kupata shinikizo kutoka kwa raia kuwa hawana imani naye tena kutokana na wizara yake kukumbwa na kashfa ya takribani Ksh.791 Milioni ambazo zilipeanwa kupitia zabuni filfinyange! Leo hii ameibuka tena na kugonga vyombo vya habari na kutamka kuwa anagombania kiti cha Ugavana wa Kirinyaga licha ya kuwa hajapata idhinisho rasmi kutoka kwa EACC kuwa hana mashtaka ya kujibu kuhusiana na kashfa iliyoikumba wizara aliyoisimamia na hatimaye kujiuzulu kwa tuhuma za kuhusika na ufisadi huo!

Huku kashfa ya Eurobond ambayo mpaka sasa imekwenda na maji na wahusika wakibakia katika mamlaka yao na ilhali wengine wakitolewa kafara kwa kufichua kashfa hiyo! Huku shule zikichomwa na wanafunzi kwa kushirikiano kwao na wazazi na wezi wa mitihani ili kuweza kutafuta vijisababu ili wanapofeli basi ionekane kuwa hawakuwa na wakati muafaka wa kusoma na hivyo kuanguka kwao kuonekane kumesababishwa na hasara hiyo!

Aidha ripoti ya utafiti wa hivi majuzi kutoka kwa Shirika la Utamaduni wa Afrika wa Utawala Bora (Africog) uliofanyika kati ya 31 Mei, 2016 – 8 Juni, 2016 ulithibitisha kuwa Ofisi ya Naibu Rais wa Kenya inaoongoza kwa Ufisadi kwa asilimia 51 ikifuatiwa na Ofisi ya Rais wa Kenya kwa asilimia 46.4! Na pia utafiti huo ulisema kuwa Ufisadi uko kwa kiwango cha juu katika taasisi ya Police kwa asilimia 89 ikifuatiwa na Serikali za Kaunti kwa asilimia 78!

Matukio yote hayo na mengine ambayo hatukuyaorodhesha yanadhihirisha wazi kuwa Mfumo wa Urasilimali umefeli na ndio chanzo cha ufisadi na hakuna badala yake isipokuwa Mfumo wa Uislamu kama mfumo adilifu unaotoka kwa Muumba. Hili likidhihirishwa na Utawala wa Mtume Muhammad (saw) kama kiongozi wa Dola ya Kiislamu huko Madina na baada yake Ma-Khalifa waongofu waliotawala. Ufisadi ulipigwa vita moja kwa moja mfano Umar Bin Khattab (ra) alipotawazwa kama Khalifa wa Pili baada ya kufa kwa Abubakar (ra) alitamka maneno haya “Nimepata habari kuwa watu waogopa ukali na ukakamavu wangu.  Wakisema: Umar alikua mkali wakati Mtume (saw) tunaye, akawa mkali pia wakati wa Abu Bakr.... Sasa itakuwaje na utawala ni wake? Basi Jueni! Huo Ukali hakika sasa umeongezeka! Lakini ni kwa wale Madhalimu, na wanaowaendea kinyume Waislamu. Ama kwa wenye dini na msimamo, basi kwa hakika nitakua laini zaidi kwao. Na wala sitomuacha yeyote kumdhulumu yeyote… (Na akithubutu kumdhulumu mtu) basi nitamkanyaga shavu lake nimueke chini. Hadi ainyenyekee haki! Nami nitaliweka chini shavu langu kwa wale wenye haki na wanaojichunga!” [Omar Ibnul Khatwab. Mtunzi: Dr. Ali Muhammad Sallabi]

Matamshi hayo ni Kinyume na zama hizi ambapo watawala wa Nchi hushirikiana na mabwenyenye waliomuweka madarakani kufanya ufisadi wa kila aina ikiwemo kuwadhulumu umma kwa kufuja na kuiba mali zao pasina kumuogopa yeyote! Ufisadi huu umeenea watawala wa mashariki na magharibi kama ilivyofichuliwa na kashfa ya ‘Panama Leaks’. Katu Ufisadi hautarajiwi kuwa sehemu ya mfumo wa Uislamu kwa kuwa viongozi na raia watakao kuwa chini ya Utawala wa Serikali ya Kiislamu watahukumiwa juu ya Uislamu unaotokamana na Qur’an; aidha watakuwa wakihesabiwa kivilivyo na mahkama ya kuwahesabu watawala (Mahkamat ul-Madhalim), Baraza la Umma, vyama vya kisiasa na Umma jumla.

Hizb utTahrir / Kenya inawalingania walimwengu, haswa bara Afrika ambalo limezama kwenye dimbwi la ufisadi na umasikini, kujikomboo na uovu huu uloletwa na mfumo mchafu wa Urasiliamali. Na badala ya kulaumu tu watu wachache wafisadi; lawama ielekezwe pale panapo stahiki nao ni mfumo wenyewe unaozalisha ufisadi huu na badala yake kuukumbatia mfumo wa Uislamu kupitia kwa serikali yake ya Khilafa kwa njia ya Utume itakayo ihifadhi jamii na kuukomesha ufisadi. Na hili limethibitishwa na tarekhe ya kung’ara ya Utawala wake wa zaidi ya karne kumi na tatu na namna jamii Ilivyotengenea pamoja na kuungana na ustawi wake bora kuonekanwa. Kinyume na utawala wa Kirasilimali usofika hata karne tatu lakini tayari ufisadi umetanda bara na baharini, ilhali jamii imebaki na taharuki za kimaisha na umasikini uso na kifani. Mwenyezi Mungu (swt) asema:

وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ لاَ تُفْسِدُواْ فِي الأَرْضِ قَالُواْ إِنَّمَا نَحْنُ مُصْلِحُونَ * أَلا إِنَّهُمْ هُمُ الْمُفْسِدُونَ وَلَـكِن لاَّ يَشْعُرُونَ﴿ “Na wanapo ambiwa: Msifanye uharibifu ulimwenguni. Husema: Bali sisi ni watengenezaji. La wao ni waharibifu lakini hawatambui!” [Surah Al-Baqarah: 11]

H. 28 Dhu al-Hijjah 1437
M. : Ijumaa, 30 Septemba 2016

Hizb-ut-Tahrir

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu