- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Vipi Khilafah Itatatua Umasikini – SEHEMU 2
Mifano ya Kivitendo kutoka katika Sunnah na Historia ya Kiislamu
- Kwanza kabisa ni kuanza kwa ukumbusho mfupi wa nguzo kuu za Uislamu katika kuzuia umasikini:
- Uislamu umeidhibiti kadhia ya umilikaji katika njia wazi na thabiti. Kila mtu binafsi anaruhusiwa kupata na kumiliki mali ya kibinafsi juu ya kila kitu ambacho si mali ya Ummah au Dola, kupitia njia ambazo Uislamu umeziruhusu (kazi, biashara, urathi, zawadi, nk.), yaani isipokuwa wizi, ulaghai, rushwa, kamari na riba, ufichaji mali …
- Uislamu umeharamisha ufichaji mali, unaoitwa kanz (ufichaji dhahabu na fedha, hata kama Zakah inalipwa juu yake), na ufichaji wa chakula, Ukiritimba, unaoitwa ihtikar. Huku ni kuzuia, kuficha bidhaa, kwa matarajio ya kuongezeka kwa bei. Nususi za kiShari'ah na fiqh zafafanua waziwazi kitendo hiki kuwa ni haramu. Kuna riwaya kadha wa kadha kutoka kwa Rasulullah (saw) zinazo elezea waziwazi kuwa ihtikar ni haramu … Said ibn Al-Musayyib amesimulia kutoka kwa Mu’ammar ibn Abdullah Al-‘Adawi katika Bukhari kuwa Mtume (saw) amesema: «لاَ يَحْتَكِرُ إِلاَّ خَاطِئٌ»“Hafanyi ukiritimba isipokuwa mkosefu.” Al-Athram amesimulia kutoka kwa Abu Umamah, amesema: «نَهَى رَسُولُ اللهِ ﷺ أَنْ يُحْتَكَرَ الطَّعَامُ» “Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amekataza ukiritimba wa chakula”. Na Muslim amesimulia kupitia silsila yake ya wasimulizi kutoka kwa Said ibn Al-Musayyib kuwa Mu’ammar alisema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema: «مَنِ احْتَكَرَ فَهُوَ خَاطَئٌ» “Mwenye kufanya ukiritimba basi yeye ni mkosaji.” Ukiritimba umeharamishwa katika vitu vyote pasi na tofauti kati ya vyakula au vyakula vya wanyama, vyakula au visivyo vyakula, na katika mahitaji msingi ya watu au ya ziada. Hivyo mwenye kufanya ukiritimba kiuhalisia huwa anataka kuongeza bei kiuadui kwa ajili ya kuwafanyia uadui Waislamu, jambo ambalo ni haramu, kutokana na yale yaliyo simuliwa kutoka kwa Ma’akal ibn Yasar, kuwa alisema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema: «مَنْ دَخَلَ فِي شَيْءٍ مِنْ أَسْعَارِ الْمُسْلِمِينَ، لِيُغْلِيَهُ عَلَيْهِمْ، كَانَ حَقَّاً عَلَى اللهِ أَنْ يُقْعِدَهُ بِعُظْمٍ مِنَ النَّارِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ» “Yeyote anayetia chochote katika bei za Waislamu, ili kuwaongezea, itakuwa ni haki juu ya Mwenyezi Mungu kumtia Motoni kwa uadui Siku ya Kiyama.”
- Uislamu umeharamisha kampuni na biashara za hisa. Ushirika na biashara ni lazima zijengwe juu ya ushirikiano halisi baina ya watu binafsi kwa msingi wa pesa + juhudi na/au ujuzi, huku bidhaa ya ushirikiano au biashara ni lazima iwe bidhaa halisi yenye thamani halisi.
- Na Uislamu umefanya dhahabu na fedha kuwa sarafu pekee ya dola na umeifanya kuwa huru na sarafu nyengine yoyote au dola au makubaliano ya kimataifa.
- Hakuna riba katika sehemu yoyote ya uchumi iwe kwa watu binafsi au Dola. Benki iliyopo pekee ni benki ya dola, inayotoa mikopo bila ya riba yoyote. Na Dola hairuhusiwi kuchukua mikopo kutoka kwa dola nyenginezo kwa msingi wa riba.
- Hakuna ushuru katika Uislamu. Khilafah haito na haipaswi kuchukua ushuru kutoka kwa watu …
Umasikini uliopo katika ardhi zetu na kote ulimwenguni unasababishwa na ukosefu wa hukmu hizi! Hivyo ikiwa hukmu zote hizi zitatabikishwa hakuna sababu itakayo bakia ambayo huenda ikapelekea kutokea au kuongezeka kwa umasikini ndani ya Dola. Hivyo basi, Khilafah ina mbinu fulani za kugawanya utajiri miongoni mwa watu, bila ya kujali dini zao, rangi au jinsia. Ni lazima tutambue kuwa haitawezekana, au kwa ufupi haiwezekani, kutabikisha siasa hizi za Kiislamu chini ya nidhamu zisizo kuwa za Kiislamu zilizoko leo.
* Kwanza kabisa, Uislamu unazalisha kazi, unasahilisha ajira na hautilii maanani upungufu wa nafasi za kazi/ufutaji kazi kama chombo cha kiuchumi kama ilivyo katika urasilimali. Urasilimali huzingatia upunguzaji wa nafasi za kazi na hivyo basi kiwango fulani cha ukosefu wa ajira kama njia ya kuhifadhi mtaji wa wenye mtaji. Kwa haya, dola itamshajiisha kila mwanamume, aliye na uwezo wa kufanya kazi, kutafuta kazi au kutafuta njia za kupata mapato ili kukidhi mahitaji yake, na mahitaji ya walio chini ya jukumu lake, kama mkewe, watoto, dada zake na wazazi. Usimamizi wa kifedha hulazimishwa juu ya mume kwa mkewe, watoto kwa baba yao, wazazi wawili kwa watoto wao wa kiume, na mrathi juu ya jamaa zake. Yote haya yamedhibitiwa kupitia nususi wazi za kiShari'ah. Uislamu umedhamini mahitaji msingi yaliyo tajwa kwa raia wote wa dola kupitia usimamizi wa kifedha, isipokuwa katika hali mbili: ya kwanza endapo mtu hana mrathi, pili endapo mtu aliye kalifishiwa usimamizi hana uwezo wa kutoa. Katika hali hii usimamizi utakalifishiwa Hazina ya Dola (Bait ul-Mal), kama alivyosema Mtume (saw): «مَنْ تَرَكَ كَلّاً فَإِلَيْنَا وَمَنْ تَرَكَ مَالاً فَلِوَرَثَتِهِ» “Yeyote aliye wacha kallan basi ni jukumu juu yetu na yeyote aliye wacha mali basi ni ya warathi wake” (Kall ni mtu dhaifu asiyekuwa na mtoto wala baba).
- * Dola katika Uislamu pia hudhamini mahitaji msingi ya raia wake wote, ambayo ni: usalama, matibabu na elimu, kwa mujibu wa nususi husika za kisheria, na kwa namna iliyo tangulia. Inapaswa kuzingatiwa kuwa mapato ya Bait ul-mal aghlabu huwa yanatosheleza kukidhi mahitaji haya pasi na kutoza ushuru juu ya Waislamu matajiri kwa ajili yake. Endapo lakini mapato ya kudumu ya Bait ul-Mal yatakuwa hayatoshelezi mahitaji hayo, ushuru hutozwa Waislamu matajiri ili kukidhi yanayo hitajika. Sheikh Ata’ bin Khalil Abu Al-Rashtah, Migogoro ya Kiuchumi: Uhakika Wake na Suluhisho kutoka katika Mtazamo wa Uislamu)
Kutokana na hayo, ikiwa tunakumbuka mfano wetu kutoka Sehemu ya 1 ya Makala haya, unaoeleza kuwa wakati wa Umar (ra) dola haikumpata yeyote wa kumgawanyia Zakah barani “Afrika”, huu hapa ndiyo ufafanuzi wake wa ni kwa nini Zakah hii haikuweza kugawanywa! … Alhamdulillah …
- * Uchumi wa Kiislamu unaweza kufanya kazi pekee ndani ya utabikishaji kamilifu wa kila utawala na nidhamu ya Kiislamu. Hivyo basi hitajio msingi zaidi lilikuwa na litakuwa ni uwepo wa Khilafah, na kiongozi wake mcha Mungu, Khalifah. Historia imejaa shakhsiya za watu zisizokuwa na idadi, walio watawala watu wao juu ya Taqwa, lakini Khalifah Omar bin al-Khattab (ra) amewacha mifano mingi zaidi na inayong’aa ya ni zipi sifa ambazo mtawala huyu anapaswa kuzimiliki. Uislamu umetoa malengo na sheria kwa ajili ya kutabikishwa nidhamu ya kisiasa na kiuchumi zenye kujali.
- * Khalifah Omar ibn Khattab (ra) alikuwa ndiye Khalifah wa mwanzo kubuni muundo msingi wa sera ya kijamii iliyo na taasisi na muundo kwa mujibu wa majukumu na mahitaji kutoka katika Qur’an na Sunnah, iliyowarahisishia Makhalifah waliofuata kutimiza majukumu yao kama wachungaji na wasimamizi wa watu ndani ya Dola ya Kiislamu ya Khilafah. Aliweka utaratibu wa huduma za Ummah na nidhamu ya kuangalia maslahi ya masikini na mafukara. Alikuwa wa kwanza kuweka taasisi za Manufaa kwa watoto, mayatima, wajane na walemavu, vile vile mafao kwa wazee, marupurupu kwa wasio na ajira na hata huduma za matibabu ya Ummah… Na hata masikini miongoni mwa Mayahudi na Manaswara katika ardhi zilizo funguliwa, ambao Uislamu uliwakadiria kama raia kamili wa Dola, walipokea malipo kutoka kwa Bait ul-Mal. Wale waliofanya ukiritimba, au kuzuia bidhaa msingi kwa lengo la kuongeza bei waliadhibiwa kwa njia tofauti tofauti, ikiwemo kufukuzwa nchi hadi ardhi nyenginezo.
- * Katika zama za utawala wote wa Makhalifah Waongofu (Khulafah u-Rashideen), KILA mtoto, hususan wale wanaohitajia msaada, walipokea manufaa kutoka kwa Bait ul-Mal. Umakinifu maalum ulipewa hususan usimamizi wa haki za kisheria, kielimu, na kifedha za watoto mayatima. Khalifah Umar (ra) kwa mfano, aliagiza walezi na wasimamizi wa watoto wasio na baba kuiongeza mali yao kupitia kuifanyia biashara ili kuiepusha kupunguzwa kupitia ulipaji Zakah. Alisema: “Ifanyieni biashara mali ya mayatima na hapo haitaliwa na Zakah.” Na pindi mtu mmoja alipokuja kwake na mtoto aliyempata ametelekezwa, alimwambia mtu huyo: “Yuko huru, ulezi wake ni juu yako, na nafaqa yake ni jukumu letu na itatolewa na Bait ul-Mal.” Khalifah Ali (ra) alitenga Dirham 10 kwa mtoto mchanga aliye telekezwa.
- * Pindi Umar (ra) alipo pokea zawadi ya tamu tamu kutoka kwa wali wake nchini Azerbaijan, alitaka kujua ikiwa watu wote huko wamekula tamu tamu hizo. Jibu lilikuwa zilitengewa mabwenyenye katika jamii. Umar (ra) kisha akatoa agizo lifuatalo kwa wali huyo: “Usijishibishe kutokana na chakula cha aina yoyote hadi Waislamu wote wale shibe yao kutokana nacho kabla yako.”
- * Rasulullah (saw) aliyapa umakinifu maalum mahitaji ya wanawake wajane. Jukumu hili lilibebwa na Makhalifah kwa umakinifu na uchungaji huo huo. Abu Bakr (ra) alinunua nguo na kuzigawanya kwa wajane masikini wakati wa miezi ya baridi. Umar (ra) aliwalipa malipo ya kudumu wanawake, waliohama kutoka Makka hadi Madina. Ali (ra) aliendelea kutimiza jukumu hili kwa watu wote masikini, wajane, na watu wengineo waliohitaji – Malipo ya usaidizi!
- * Khalifah Umar (ra) mara kwa mara alimzuru na kumkidhia mahitaji mwanamke kipofu mjini Madina, aliyekuwa hana mtu wa kumkidhia mahitaji yake. – Manufaa ya Walemavu! Pia alitoa maagizo kuwa malipo yangeruhusiwa kwa ajili ya watoto wanao nyonyeshwa na baadaye kupanua hilo hadi kwa kila mtoto kuanzia siku anapozaliwa. Kiwango kilikuwa Dirham 100 kuanzia siku ya kuzaliwa, Dirham 200 anapo kua na hata zaidi anapo baleghe. Pia alitenga Dirham 6 zaidi kwa kila mtoto, wa kiume au wa kike, juu ya zile alizompa baba kwa usaidizi. Malipo haya yaliendelea chini ya makhalifah waliofuata – Manufaa ya Watoto! (http://dergipark.gov.tr/download/article-file/399406)
Taasisi maalumu ilibuniwa ili kusimamia mambo ya kisaikolojia, kijamii na kifedha ya familia za wanajeshi, hususan wanapokuwa hawako, au ulemavu kutokana na utekelezaji majukumu yao, au katika hali wanapouwawa mashahidi vitani, kwa mujibu wa mfano wa Rasulullah (saw).
- * Khalifah Umar (ra) alimwita mke wake mwenyewe kumsaidia kama mkunga mwanamke wa kibedui aliyekuwa na uchungu wa uzazi, huku yeye mwenyewe akiitayarishia chakula familia hiyo wakati huo mgumu. Wakati wote huo aliketi nje ya hema akisubiri kuzaliwa kwa mtoto. Siku iliyofuatia alitenga malipo ya kudumu kutoka kwa Bait ul-Mal kwa familia hiyo – Manufaa ya Uzazi na Nafaqa na Usaidizi!
Na hakutofautisha baina ya Muislamu na asiyekuwa Muislamu. Alimtumikia kila raia wake: Alitenga malipo ya kila siku kutoka katika Bait ul-Mal kwa Yahudi mmoja mzee masikini kwa kusema: “Wallahi, ni kinyume na ada ya uadilifu kuwa tuchukue Jizyah (kodi kwa Wasiokuwa Waislamu) kwao wanapokuwa vijana na wenye afya, na tuwaache pasi na uchungaji wanapokuwa wazee?” – Usaidizi wa Wazee / Mafao! Alikiona kikundi cha Manaswara wakiugua Ukoma, na hivyo kutumia kutoka katika Bait ul-Mal kuwatibu. – Huduma za Matibabu! Na wale, ambao hawatibiki, walipewa marupurupu ya kudumu hadi siku yao ya mwisho. – Manufaa ya Maradhi!
- * Khilafah Uthmaniyya ilichunguza na kufuatilia kila chakula kabla ya kutoa ruhusa ya kuuzwa sokoni. Ili kudhibiti bei wakati wa upungufu wa usambazaji katika maeneo fulani, Khalifah angeshajiisha ushindani kupitia uagizaji kutoka sehemu nyenginezo za Khilafah. Mfano mmoja ni wakati wa utawala wa Khalifah Abdul Hamid I (1774 – 1789). Wakati wa uhaba wa usambazaji wa nyama jijini Istanbul, ambapo wauza nyama walianza kuongeza bei za nyama, na hata kuacha kuiuza, aliwaamuru wauza nyama kutoka Thrace kuja na kufungua mabucha jijini Istanbul. Hivyo basi kupitia ongezeko la ushindani, bei zilishuka tena kwa kiwango cha kuweza kumudiwa. Khilafah pia ilitabikisha faini kwa mauzo maovu. Wale walio punja katika mizani walilazimika kulipa faini: sarafu 1 ya fedha (Akce) kwa gramu 5 za nyama iliyouzwa kimakosa. Vifungu vya sheria vya wauza nyama pia vimeashiria kukamatwa kwa wauza nyama, ambao hawakutaka kuuza nyama. (http://dergipark.gov.tr/download/article-file/185222 na makala mengineyo tofauti tofauti ya historia)
Hii ni mifano michache tu ya namna Khilafah inavyo chunga mambo ya watu wake na kuchangamka katika kuchukua hatua thabiti katika vita dhidi ya umasikini. Mwenyezi Mungu (swt) aturuzuku siku hizi za baraka kwa kurudi Khilafah Rashidah kwa Njia ya Utume hivi karibuni mno bi’idhnillah!
﴾لَا تَقْنَطُوا۟ مِن رَّحْمَةِ ٱللَّهِ﴿ “…Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu”
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Zehra Malik
Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir
Usomaji kwa ufafanuzi zaidi kuhusu Misingi ya Uchumi wa Kiislamu:
- Nidhamu ya Kiuchumi ya Uislamu; Taqiuddin an-Nabhani, Hizb ut Tahrir
- Migogoro ya Kiuchumi: Uhakika Wake na Suluhisho kutoka katika Mtazamo wa Uislamu; Sheikh Ata’ Bin Khalil Abu Al-Rashtah