- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Zawadi Kubwa Zaidi ya Rabi Ul-Awwal:
Rehma kwa Walimwengu Wote, Muhammad (Saw)
(Imetafsiriwa)
Mwezi wa Rabi ul-Awwal ni mwezi wenye umuhimu mkubwa kwa Ummah wa Sayyidna Muhammad (saw). Sio tu Rabi ul-Awwal unashuhudia zawadi kwa uzawa wa Muhammad (saw), bali umeshuhudia kuja kwake (saw) katika utawala, kupitia Hijrah ambayo imemuweka (saw) kuwa ni mtawala wa Madinah. Na Rabi ul-Awwal umeshuhudia kurejea kwake kwa Mwenyezi Mungu (swt), kumpandisha kuwa muombezi kwa Ummah katika Siku ya Malipo.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amepewa hadhi ya juu zaidi miongoni mwa Mitume wote (as). Kwa kuwa Muhammad (saw) hakuwa kwa ajili ya watu fulani kwa muda fulani, kama Mitume waliomtangulia kama wale waliotumwa kwa watu wa Aad, Thamud, Lut au Bani Israil. Hakuwa hivyo, Muhammad (saw) alikuwa kwa jamii zote kwa muda wote, kutokea muda alipoteuliwa hadi mwisho. Mwenyezi Mungu (swt) amesema,
(وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلاَّ رَحْمَةً لِلْعَالَمِينَ) “Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehma kwa walimwengu wote” [Surah Al-Anbiyya 21:107]. Hivyo Mtume (saw) amekuja kwa watu wote, Waarabu, na wasio Waarabu, Waafrika na Waasia, Wazungu na Waamerika. Ujumbe wake (saw) umekuwa ni rehma kwa wanaadamu wote na ni wenye kushinda mifumo yote ya maisha, hata kama washirikina watachukia.
Kwa namna gani Yeye (saw) amechukua jukumu hili kubwa ambalo hajabebeshwa mwengine yeyote kabla katika viumbe wa Mwenyezi Mungu (swt) na halitotokea tena! Kwa namna gani Yeye (saw) alipambana bila kuchoka, akivumilia shida kubwa kwa kuwa na subira, akizungumza kwa hekima na upole, akizisafisha nyoyo za ufisadi na kubuni msingi imara wa Ummah mkubwa katika milima ya wanaume, Maswahaba wake (ra). Kumekuwa na ushahidi ndani ya Maswahaba hawa (ra) juu ya hadhi ya Mtume (saw) akiwa ni Mjumbe wa jamii zote, kwani miongoni mwao alipatikana Suhaib (ra) Mrumi, Salman (ra) Mfursi na Bilal (ra) Muafrika, pamoja na Maswahaba kutoka makabila kadhaa ya Bara Arabu. Aliwafinyanga juu ya Iman ya udugu uliojengwa juu ya fungamano imara zaidi ya lile la uzawa na la damu, fungamano la mapenzi kwa Mwenyezi Mungu (swt) na Mtume wake (saw). Safu hizi zilizofungamana vyema za Maswahaba (ra) baadaye ziliibuka kuwa muundo wa ajabu mbele ya mifumo ya kikabila ya wakati huo. Udugu wao uligonga kwenye fungamano la kikabila, kitaifa na kitabaka, mafungamano dhaifu yanayowanyima wanaadamu rehma ya kuwa na huruma badala ya uadui, ushirikiano badala ya ushindani na amani badala ya ugomvi.
Baada ya kuibuka kwa watu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) mjini Makkah, ujumbe adhimu wa Rehema uliing'arisha Bara Arabu. Ulikuwa ni ujumbe wa matumaini kwa wanaodhulumiwa, wanaoteseka chini ya nidhamu ya kikabila, na ni onyo kwa madhalimu, makatili miongoni mwa viongozi wa kikabila. Watu kutoka kila pembe walivutiwa na ukweli wake. Hata hivyo, katika muda huo madhalimu walikuwa wamezama katika ukanushaji wa kiburi, nyoyo zao zilikuwa ngumu na kuzibwa kwa Ukafiri wao. Walitumia mamlaka yao kumuadhibu Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) na wote waliojifunga na Uislamu. Walieneza uongo kuhusu ujumbe na Mtume (saw), na hivyo (Waumini) walisakwa na kuteswa hadi kufa mashahidi. Lakini, Mtume (saw) alishikilia ulinganizi wake, bila kumhofu yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu (swt). Mtume (saw) alijitahidi katika hali ya usiri, kwa tahadhari na hekima, kuomba Nussrah, Nguvu za Kimada, kutoka kwa watu wake, watu wa vita, ili kwayo aweze kusimamisha Ujumbe kuwa ni mamlaka na utawala.
Katika kipindi hichi cha majaribio magumu, Rabi ul-Awwal, kilikuwa ni cha kushuhudia zawadi nyengine, ambayo ni Hijra ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kusimamisha Uislamu kuwa dola kwa mara ya kwanza, katika Madinah Al-Munawwara, ilionawirishwa kwa muangaza wa Uongofu. Kwa kuipata Nussrah kutoka kwa makabila mawili yenye nguvu ya Madina, Bani Khazraj na Bani al-Aws, hatua ilipigwa kwa Hijra yake (saw) kutoka kwenye dhulma katika Makkah kuelekea kwenye Uislamu Madinah. Bukhari katika Sahih yake kutoka kwa Ibn Shihab amesema kuwa Urwah ibn al-Zubayr alimwambia,
«وَسَمِعَ المُسْلِمُونَ بِالْمَدِينَةِ مَخْرَجَ رَسُولِ اللَّهِ (ص) مِنْ مَكَّةَ... فَتَلَقَّوْا رَسُولَ اللَّهِ (ص) بِظَهْرِ الحَرَّةِ، فَعَدَلَ بِهِمْ ذَاتَ اليَمِينِ، حَتَّى نَزَلَ بِهِمْ فِي بَنِي عَمْرِو بْنِ عَوْفٍ، وَذَلِكَ يَوْمَ الِاثْنَيْنِ مِنْ شَهْرِ رَبِيعٍ الأَوَّلِ...»
“Waislamu wa Madinah walisikia kuondoka kwa Mtume (saw) kutoka Makkah... na wakakutana naye Mtume (saw) katika mchana wenye joto, akawatokea upande wa kulia, mpaka akawashukia katika kabila la Bani Amr Ibn Auf, na ilikuwa ni siku ya Jumatatu katika mwezi wa Rabi ul-Awwal ...” Na amepokea Ibn Hibbaan katika Sahih yake kutoka kwa al-Baraa aliyesema:
أَنَّ قُدُومَهُ (ص) الْمَدِينَةَ كَانَ يَوْمَ الِاثْنَيْنِ لِاثْنَتَيْ عَشْرَةَ لَيْلَةً خَلَتْ مِنْ رَبِيعٍ الْأَوَّلِ
“Kwamba kuwasili kwa Mtume (saw) Madinah kulikuwa siku ya Jumatatu katika usiku wa kumi na mbili wa Rabi ul-Awwal.” At-Tabari amesema katika kitabu chake cha Historia alichokiita “Historia ya Mitume na Watawala”:
(حَدَّثَنَا ابْنُ حُمَيْدٍ، قَالَ: حَدَّثَنَا سَلَمَةُ، عَنِ ابْنِ إِسْحَاقَ، عَنِ الزُّهْرِيِّ، قال: قدم رسول الله (ص) الْمَدِينَةَ يَوْمَ الاثْنَيْنِ، لاثْنَتَيْ عَشْرَةَ لَيْلَةً خَلَتْ مِنْ شَهْرِ رَبِيعٍ الأَوَّلِ)
“Ametuhadithia Ibn Hamid, akisema: Ametuhadithia Salamah kutoka kwa Ibn Is-haaq kutoka kwa Az-Zuhri amesema: Mtume (saw) aliwasili Madinah siku ya Jumatatu ya usiku kumi na mbili wa Rabi ul-Awwal.”
Hivyo Rabi ul-Awwal, ulikuwa ni mwezi ambao Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), aliyepewa Unabii (Utume) sasa amepewa Hukmu (Utawala). Ikawa dola ya mwanzo ya Kiislamu imesimamishwa, ikaruhusu Uislamu kutekelezwa kwa heshima zote. Mtume (saw) aliwaweka watawala katika maeneo yote, aliwachagua mahakimu na kuweka misingi makini ya kimahakama, aliunda bayt ul-mal, alikuza mapato na kuyatumia kwa raia na aliunda jeshi imara lenye nguvu. aliyalingania makabila na mataifa mengine, akituma ujumbe kwa wafalme. Aliitanua dola ya Kiislamu, ukiwa ujumbe wake ni kuubeba Uislamu kuwa ni Rehma kwa walimwengu wote, na kwa watu kuingia katika Uislamu kwa makundi. Mwenyezi Mungu (swt) amesema,
(إِذَا جَاءَ نَصْرُ اللَّهِ وَالْفَتْحُ * وَرَأَيْتَ النَّاسَ يَدْخُلُونَ فِي دِينِ اللَّهِ أَفْوَاجًا)
“Itakapokuja Nusra ya Mwenyezi Mungu na ushindi. Na ukawaona watu wanaingia katika Dini ya Mwenyezi Mungu kwa makundi.” [Surah An-Nasr 110: 1,2]
Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ameuarifu Ummah huu juu ya kukamilisha ujumbe wake kuwa ni Rehma kwa Walimwengu wote huko mbeleni. Amefikisha uoni ambao Mwenyezi Mungu (swt) amempatia, kuwa neema za Uislamu zitaishukia dunia yote. Na kuwa baada ya Mtume (saw) kurejea kwa Mwenyezi Mungu (swt), kusonga mbele kwa Uislamu kunaendelea. Chini ya Khilafah Rashida, Ummah ulihakikisha kuwa Uislamu umeenea kwenye himaya za Fursi na Roma. Yeye (saw) ameuarifu Ummah huu juu ya kukombolewa Konstantinopoli, kulikotokea wakati wa Khilafah Uthmaniya, na kukombolewa Roma, ambako tutakushuhudia inshaaAllah baada ya kurejea tena Dola ya Kiislamu. na inshaaAllah wakati wa kurejea Khilafah, Ummah huu utanyanyuka tena kuhakikisha kuwa Uislamu unashinda juu ya mifumo mengine yote hadi ujumbe wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ukamilike.
Hivyo, Rabi ul-Awwal na zawadi tunayoishuhudia itusukume kuunyanyua ujumbe wa Uislamu, kuwa ni kitulizo kwa wanaodhulumiwa na kuwa ni karipio kali kwa watawala dhalimu. Shukrani kwa zawadi yake itupatie subira na ujasiri usioyumba katika kuelekea kwetu kwenye Uislamu, licha ya udhalimu wa watawala makatili. Kumpenda kwetu Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kutuchochee kuivua mipaka bandia ya kitaifa iliyotugawa katika nchi zaidi ya hamsini na kutuunganisha kuwa dola moja chini ya bendera ya La ilaaha illa Allah Muhammad ur-RasulAllah. Na iwe Hijra ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ambayo inashuhudiwa na Rabi ul-Awwal iwahamasishe watu wa vita miongoni mwetu hivi leo, ndani ya majeshi yetu, kutoa Nguvu za Kimada kwa ajili ya kusimamisha Uislamu kuwa dola. Na iwe Rabi ul-Awwal ni yenye kututia hima ya kukamilisha ujumbe wa Mtume (saw) kuwa ni Rehma kwa walimwengu wote. Na tuhangaike kwa ajili ya kuurejesha Ummah, kuwa ni mashahidi juu ya Walimwengu wote, kutekeleza Uislamu kuwa ni dola na kuubeba uongozi wake ili uishinde mifumo yote mengine ya maisha.
Imeandikwa kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Musab ibn Umair – Pakistan