Jumapili, 02 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/03
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Serikali ya Kiislamu Inakuwa Vipi?

(Imetafsiriwa)

Hadi katikati mwa karne ya kumi na nane, Uislamu ulikuwa kama mti mzuri wenye matawi imara ya kijani yaliyostawi ambayo huzaa matunda muda wote wa mwaka. Imani ya Uislamu ilikuwa mbegu kutokana nayo mti huu ulizaliwa, wakati fikra ya Uislamu na kanuni kuhusiana na maisha zimekuwa ndio mizizi yake. Sheria na mamlaka ya Uislamu yamekuwa ni shina lililorefuka lililotokana na mizizi hii. Neema, maendeleo na nguvu zilizofuatia katika jamii ilikuwa ni matawi mwanana yenye kuvutia ambayo yalidhibiti njia ya maisha ya Kiislamu na kueneza wito wa Uislamu ulimwenguni kote.

Hata hivyo, Mapinduzi ya Viwanda katika Ulaya mnamo katikati ya karne ya kumi na nane yalipelekea mabadiliko katika mandhari ya ulimwengu. Dola ya Kiislamu ilipoteza hadhi yake ya kuwa ni dola kiongozi na kuporomoka kwake kukawa dhahiri. Zaidi ya hivyo, Waislamu wakawa ni wenye kutishika na maendeleo ya Ulaya ambapo walianza kufikiria upya na kutengeneza upya mtazamo wa Kiislamu. Mashaka yote haya yalipelekea katika kudhoofisha utekelezaji wa Uislamu, ambapo, kwa upande mwengine, imeharakisha kuanguka kwa Dola ya Kiislamu. Udhaifu huu wa kifikra kwa Waislamu, ulijumuisha katika kushindwa kwao kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia, kwa msaada wa Mustafa Kamal, na kuiwezesha Uingereza kuivunja Dola ya Kiislamu. Baada ya kuvunjika Dola ya Kiislamu, kilichobaki pekee kwa Waislamu ni fikra zao za Kiislamu na mitazamo. Hata hivyo, mara baada ya nchi zenye nguvu za kikoloni zilipokalia ardhi za Waislamu, walitumia kila mbinu iliyowezekana kudhoofisha msingi muhimu wa Uislamu. Yakiwa ni matokeo ya juhudi hizi za wakoloni, fikra nyingi za msingi za Uislamu zilifutwa kabisa kutoka miongoni mwa Waislamu, fikra nyingi ziliwekwa kando kutoka kwenye mahubiri ya wazi, na nyengine zilibadilishwa kwa nyengine au kutiwa doa na fikra mpya ambazo zilikuwa ngeni kabisa na Uislamu. Ikawa kila kizazi kinachoikumbuka Khilafah kikipotea kwa kupitiwa na muda, kilichukuliwa nafasi yake na kizazi kipya cha Waislamu, ambacho japo kuwa kilisikia juu ya Serikali ya Kiislamu, lakini hakikujua chochote juu ya muundo wake, sheria na nidhamu zake. Kwa hakika, waliizingatia Serikali ya Kiislamu kuwa ni njozi tu. Kwa hiyo, ule uliokuwa mti mzuri wenye kuvutia wa hadhara ya Kiislamu ukawa umefungiwa tu kwenye mizizi yake.

Kwa kuzingatia kuvunjika kwa Khilafah, iliyowahifadhi Waislamu na Uislamu kwa karne nyingi, ukiwa ni ushindi mkubwa kabisa usio na kifani, mataifa makuu ya Magharibi yaliamua kuzigawa ardhi za Waislamu. Hatimaye, hadhara ya kimagharibi ilianza kutawala katika ardhi za Waislamu ambapo sasa ukawa ni uwanja wa mapambano wa mataifa ya kilimwengu kama Ulaya, Urusi na Amerika. Ili kuingiza fikra za Kimagharibi, walianzisha mifumo yao, ya elimu, habari, utamaduni, kupitia watawala wao vibaraka. Pindi Waislamu katika eneo lolote wakikataa na kuasi dhidi ya ajenda hii ya Wamagharibi, hushindikizwa kupitia njia za kijeshi na uchumi. Hivi leo, katika karne ya 21, hata hivyo, ulimwengu wa Kiislamu umechoshwa na matokeo haribifu na ya kuhuzunisha ya mfumo wa Kimagharibi. Hata hivyo, wamekosa fikra na mawazo yanayohitajika kurejesha tena hadhara ya Kiislamu. Hivyo, hitajio la sasa ni kuwapa thaqafa Waislamu kuhusiana na fikra za Uislamu ambazo zitarejesha hadhara ya Kiislamu. Ni kupitia fikra hizi ndipo Waislamu hatimaye wataweza kubuni Dola ya Kiislamu, ambayo kusimama kwake huwa ni muhimu kwa ajili ya kurejesha njia ya maisha ya Kiislamu. Kwa kuwa harakati nyingi za Kiislamu duniani zinafanya kazi ya kurejesha mfumo wa Kiislamu kwenye nchi za Waislamu, ni muhimu zaidi hivi sasa kuweka wazi na kuelezea kwa watu fikra sahihi za Kiislamu, licha ya juhudi njema kwa ajili ya mabadiliko, Wamagharibi huchukua fursa ya ufinyu wa kifikra kwa baadhi ya Waislamu kuwaweka mbali na dola ya kweli ya Kiislamu. Hapo chini ni baadhi ya sifa miongoni mwa sifa nyingi msingi za dola ya Kiislamu ambazo ni muhimu kwa kila dola iwe nazo ili iwe ni dola ya Kiislamu.

1. Dola yoyote ili iwe ni dola ya Kiislamu, lazima ijiegemeze moja kwa moja juu ya Aqida ya Kiislamu, ambayo iwe ndio msingi wa matendo yake yote, yaani ubwana kamili katika Dola lazima uwe kwa Sharia ya Kiislamu.

Sababu ya kuanzishwa serikali yoyote ni kuhifadhi fikra na imani kwa watu wake na kuwahudumia kwa mujibu wa fikra hizi. Hivyo, ni muhimu kwa Dola kujiegemeza juu ya fikra na imani hizo ambazo watu wake wamejifungamanisha nazo. Aqida ya Ummah wa Kiislamu ni aqida ya Uislamu, na fikra, vigezo na usadikishaji ambao Ummah umejifunga nao ni ule unaotokana na aqida ya Uislamu. Pia, uoni wa Waislamu kuelekea maisha pia unategemea Uislamu, na pia mtazamo wa Waislamu kuhusu maslahi. Hivyo, uoni wa Kiislamu, wa kimaumbile na kiakili, ni kuwa Ummah wa Kiislamu lazima utawaliwe kwa mujibu wa Uislamu.

Misingi ya Dola ya mwanzo ya Kiislamu ambayo Mtume (saw) ameiasisi inaegemeo maalum, ambalo lilikuwa ni aqida ya Kiislamu. Hivyo, ni wajibu juu ya Waislamu kuhakikisha kuwa Dola wanayoishi nayo lazima pia iegemee juu ya Uislamu, muda wote na mahala popote. Mtume (saw) amehakikisha kuwa Dola aliyoiasisi Madina imeundwa juu ya msingi wa aqida ya Kiislamu tokea mwanzoni kabisa. Pia, alianza kutekeleza Jihad ili kuueneza Uislamu kwa wanaadamu wote na akaifanya ni lazima juu ya Waislamu waliobaki kutenda hivyo hivyo. Mtume (saw) amesema, «أُمِرْتُ أَنْ أُقَاتِلَ النَّاسَ حَتَّى يَشْهَدُوا أَنْ لاَ إِلَهَ إِلا اللَّهُ وَأَنَّ مُحَمَّدًا رَسُولُ اللَّهِ وَيُقِيمُوا الصَّلاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ، فَإِذَا فَعَلُوا ذَلِكَ عَصَمُوا مِنِّي دِمَاءَهُمْ وَأَمْوَالَهُمْ إِلا بِحَقِّ الإِسْلامِ، وَحِسَابُهُمْ عَلَى اللَّهِ» “ “Nimeamrishwa nipigane na watu hadi washuhudie kuwa hakuna anayepaswa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na wasimamishe swala na watoe zaka, pindi wakifanya hivyo basi wamejikinga kutokana nami damu zao na mali zao isipokuwa kwa haki ya Uislamu na hisabu yao iko kwa Mwenyezi Mungu.” [Muttafaqun alayhi]. Pia, Mtume (saw) amewaamrisha Waislamu kupambana na mtawala anayetenda ukafiri wa wazi. Imepokewa kutoka kwa Ubada bin Samit kuwa Mtume (saw) amesema, «وَأَنْ لا نُنَازِعَ الأمْرَ أَهْلَهُ إِلا أَنْ تَرَوْا كُفْرًا بَوَاحًا» “Na tumechukua bay’ah kwamba tusizozane (tusipambane) na Amir (mtawala) isipokuwa tutakapoona ukafiri wa wazi” [Muttafaqun alayhi]. At-Tabari ametumia tamko «كفراً صُراحاً» “ukafiri wa wazi” katika upokezi wake, ambapo Ibn Hibban ametumia tamko «إِلاَّ أَنْ تَكُونَ مَعْصِيَةُ اللَّهِ بَوَاحَاً»  “Isipokuwa kutapokuwa na maasi ya wazi kwa Mwenyezi Mungu.” Pia, Mwenyezi Mungu (swt) amesema katika Quran,

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُـوْنَ حَتّـٰى يُحَكِّمُوْكَ فِيْمَا شَجَرَ بَيْنَـهُـمْ﴿

“La! Naapa kwa Mola wako Mlezi! Hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye muamuzi katika yale wanayokhitilafiana.” [An-Nisa: 65]. Dalili zote hizi zinaashiria juu ya suala la kuwa aqida ya Kiislamu lazima iwe pekee ndio msingi wa dola, na kuwa mambo yote lazima yatatuliwe kwa mujibu wa Sharia ya Kiislamu. Chanzo chengine mbadala – ima kiwe kinatokana na hadhara isiyo ya Kiislamu au kilichovuliwa na akili – kitazingatiwa ni ukafiri.

Hivyo, fikra yoyote isiyotokana na aqida ya Kiislamu haina nafasi katika jamii ya Kiislamu, ima iwe ni demokrasia, utaifa, uzalendo, ufalme, udikteta, uliberali au dola ya kitaifa. Sio tu fikra zote hizi hazitokani na chimbuko la  Uislamu, bali zinagongana na hukmu za wazi za Uislamu. Pia, tamko la kuwa aqida ya Kiislamu itakuwa ni msingi wa jamii ya Kiislamu ina maana ya kuwa sheria zote zitajifunga kwa maamrisho ya Mwenyezi Mungu (swt) na kwamba hakuna mfumo mwengine au fikra itakayorudiwa kwenye jambo hili. Kwa hivyo, chini ya serikali ya Kiislamu, mambo yote yakiwemo yanayohusiana na sheria, uchumi, jamii, sera za nje na za ndani, elimu, viwanda, afya, jeshi, hazina yatashughulikiwa kwa msingi wa aqida ya Kiislamu.

2. Ili Dola iwe ya Kiislamu, ni wajibu kwa sheria zote zinazotumiwa ziwe ni za Uislamu tu na ulinzi (wa Dola) wake uwe chini ya nguvu za Waislamu pekee.

Dola itakuwa ni ya Kiislamu wakati tu usalama wake wa ndani na nje umedhibitiwa moja kwa moja na Waislamu, na sheria za Uislamu tu ziwe ndio zenye kutekelezwa. Ikiwa moja ya masharti haya yatakiukwa basi Dola haitohisabiwa kuwa ni Dola ya Kiislamu, kama ikiwa ulinzi wa ndani na wa nje kudhibitiwa na wasiokuwa Waislamu au ikiwa hukumu ni kutoka kwenye sheria zisizotokana na Uislamu. Hili halihitaji ukiukwaji wa masharti yote mawili, bali likikiukwa japo moja tu itatosheleza kwa dola kuwa sio ya Kiislamu.

Dola ya mwanzo aliyoiasisi Mtume (saw) ilikamilisha masharti haya mawili. Al-Bayhaqi ameripoti kwa njia ya Ubada bin al-Samit ambaye alisema: «إِنَّا بَايَعْنَا رَسُولَ اللَّهِ ﷺ عَلَى السَّمْعِ وَالطَّاعَةِ فِي النَّشَاطِ وَالْكَسَلِ، وَالنَّفَقَةِ فِي الْعُسْرِ وَالْيُسْرِ، وَعَلَى الأَمْرِ بِالْمَعْرُوفِ وَالنَّهْيِ عَنِ الْمُنْكَرِ، وَعَلَى أَنْ نَقُولَ فِي اللَّهِ لاَ تَأْخُذُنَا فِيهِ لَوْمَةُ لاَئِمٍ. وَعَلَى أَنْ نَنْصُرَ رَسُولَ اللَّهِ ﷺ إِذَا قَدِمَ عَلَيْنَا يَثْرِبَ مِمَّا نَمْنَعُ أَنْفُسَنَا وَأَزوَاجنَا وَأَبْنَاءَنَا وَلَنَا الجَّنَّةَ. فَهَذِهِ بَيْعَةُ رَسُولِ اللَّهِ ﷺ الَّتِي بَايَعْنَاهُ عَلَيْهَا»  “Hakika tulichukua bay’ah kwa Mtume (saw) juu ya kusikiza na kutii wakati wa nguvu na udhaifu, wepesi na uzito, na juu ya kuamrisha mema na kukataza maovu, na kwamba tutasema juu ya Mwenyezi Mungu bila kuhofu lawama ya mwenye kulaumu, na kwamba tutamnusuru Mtume (saw) atakapokuja Yathrib (Madinah), tutamuhifadhi kama tunavyohifadhi nafsi zetu na wake zetu na watoto wetu na kwamba tutapata Pepo. Hii ndio bay’ah tuliyompatia Mtume (saw).” Hii pamoja na dalili nyengine zinatuelekeza juu ya suala la kuwa Mtume (saw) alichukuwa Bay’ah ya Pili ya al-Aqabah, juu ya masharti yote mawili utiifu na usalama.

Vile vile, makabila ambayo yalikataa kusimamisha Dola ya Kiislamu, yalikataa sharti moja au yote mawili ya msingi. Al-Bayhaqi ameripoti kwa njia ya Ali (ra) kuwa Mtume (saw) aliwaambia Banu Shayban: «مَا أَسَأْتُمْ فِي الرَّدِّ إَذْ أَفْصَحْتُمْ بِالصِّدْقِ، وَإِنَّ دِينَ اللَّهِ لَنْ يَنْصُرَهُ إِلاَّ مَنْ حَاطَهُ مِنْ جَمِيعِ جَوَانِبِهِ» “Hamjatoa jibu baya, bali mmesema ukweli, lakini dini ya Mwenyezi Mungu hainusuriwi ila kwa yule anayeinusuru katika pembe zake zote.” Watu hawa walikusudia kutoa nusra na msaada kwa Mtume (saw) katika eneo la Arabia tu, na sio dhidi ya Himaya ya Fursi.

Kwa hivyo, ili Dola iwe ya Kiislamu, ni lazima ikamilishe masharti haya mawili, ambayo Mtume (saw) aliyahitaji alipotaka kuunda serikali ya mwanzo ya Kiislamu. Kukiuka sharti lolote katika haya mawili kutapelekea dola kuwa siyo ya Kiislamu.

3. Ili dola iwe ya Kiislamu, ni lazima mfumo wake wa serikali ujengwe juu ya muundo wa serikali kuu (centrality) na umoja, na kwamba dola ibebe jukumu la Ummah wote na kuwaongoza.

Katika dola ya Kiislamu, mamlaka sio ya pamoja bali ni ya kibinafsi. Hivyo, katika serikali ya Kiislamu, utawala haujengwi juu ya hekima za wanaadamu, bali juu ya msingi wa Wahyi unaoegemea hekima isiyo na mipaka ya Mwenyezi Mungu (swt), ambao utekelezaji wake unalazimishwa na kiongozi wa dola, Khalifah. Katika serikali ya Kiislamu, maoni ya kisheria ni yenye kuchukuliwa yanayoegemea juu ya nguvu za fikra zake, wakati katika serikali ya pamoja, maoni ya kisheria yenye kuchukuliwa yanaegemea juu ya kukubalika na umma na maslahi. Uislamu unapinga serikali shirikishi na hairuhusu zaidi ya mtawala mmoja wa dola. Khalifah ni mtu ambaye kupitia kwake raia Waislamu wa dola wanakabidhi mamlaka ya kutekeleza na kueneza Uislamu kupitia bay’ah, hivyo mkataba wa jukumu la kutawala linakamilishwa na mtu anayeitwa Khalifah ambaye ni kiongozi wa dola. Kwa hivyo, dola ya Kiislamu ni ile ambayo utawala unaegemea juu ya serikali kuu. Hivyo baada tu ya kushika mamlaka ya Ukhalifah, inakuwa ni wajibu kwa Waislamu wote kumtii. Mtume (saw) amesema: «وَمَنْ مَاتَ وَلَيْسَ فِي عُنُقِهِ بَيْعَةٌ مَاتَ مِيتَةً جَاهِلِيَّةً» “Anayekufa hali ya kuwa hana baya’h shingoni mwake, anakufa kifo cha kijahilia.” Kutokana na umuhimu wa utiifu kwa Khalifah, maeneo yote ya ulimwengu wa Kiislamu yanazingatiwa kuwa ni sehemu ya Dola ya Kiislamu, na lazima yajisalimishe kwa mamlaka ya Khalifah. Kama watakataa kufanya hivyo, watazingatiwa kuwa ni waasi. Hivyo, dola ya Kiislamu ni moja ambapo utawala unaegemea juu ya umoja wa ulimwengu wa Kiislamu.

Imepokewa kutoka kwa Abu Said Khudri (ra) kuwa Mtume (saw) amesema: «إِذَا بُويِعَ لِخَلِيفَتَـيْنِ فَاقْتُلُوا الآخَرَ مِنْهُمَا» "Watakapopewa bay’ah Makhalifah wawili basi muuweni wapili wao." Ahmad ameripoti kuwa Abdullah bin Amr amenukuu kuwa Mtume (saw) amesema, «لا یحل لثلاثۃ نفریکونون بأَرض فلاۃ إِلا أَمّروا علیھم أَحدھم» “Haistahili kwa watu watatu kuwa katika ardhi ya wazi isipokuwa wamchague mmoja wao kuwa kiongozi wao.” Abu Daud ameripoti kutoka kwa Abu Said kuwa Mtume (saw) amesema, «إِذا خرج ثلاثۃ فی سفر فلیؤ مروا أَحدھم» “Watu watatu wanapotoka kwa ajili ya safari, basi wamchague kiongozi kutoka mmoja wao.”

Katika hadithi zote hizi mbili, neno أحد humaanisha mtu mmoja, ambapo inaonyesha ni mtu mmoja tu anayechaguliwa kuwa kiongozi. Matendo ya Mtume (saw) pia yanathibitisha kuwa hakutakiwi zaidi ya kiongozi mmoja, kwa kuwa hakuchagua zaidi ya mtu mmoja kuwa kiongozi katika shughuli yoyote.

Kwa hiyo, katika serikali ya Kiislamu, mamlaka hasa ya kutawala yanabaki kwa mtu ambaye Ummah umemchagua kuwa Khalifah. Viongozi wote wengine waliobaki ambao ni wasaidizi au manaibu wa Khalifah katika muundo wa utawala, huchaguliwa na Khalifah na wanachukua mamlaka yao kutoka kwake akiwa ni Khalifah. Kwa hivyo, katika dola ya Kiislamu, watawala wote chini ya Khalifah, wakiwemo wasaidizi wake, waangalizi na mawakala, hawana mamlaka kamili ya kutawala. Badala yake mamlaka yao yanatokana na mamlaka ya Khalifah, ambaye anaweza kuyachukua muda wowote anapotaka. Japokuwa Uislamu unamuhimiza Khalifah kuwashauri watu katika mambo yao, uamuzi wa mwisho na hukumu ni haki ya kipekee kwa Khalifah na hakuna yeyote wa kugawanya naye (mamlaka hayo). Hivyo dola yenye zaidi ya mtawala mmoja haiwezi kuwa ni dola ya Kiislamu.

4. Ili dola iwe ya Kiislamu, ni lazima kwa Ummah kuwa na haki ya kumchagua na kumteuwa mtawala, yaani Ummah uwe na haki ya kumteuwa Khalifah kuwa kiongozi wa dola kupitia mkataba.

Katika serikali ya Kiislamu, haki ya kumteuwa mtawala ipo kwa Ummah. Ummah unatoa bay’ah kwa mtawala aliyechaguliwa na kumfanya kuwa Khalifah wao, juu ya sharti la kutekeleza mfumo wa Kiislamu na kueneza ujumbe wa Uislamu kote duniani. Uislamu umeupa Ummah haki ya hiyari ya kumchagua mmoja wao kuwa Khalifah na kutoa bay’ah yao kwake. Kwa hivyo, dola inaweza kuwa ni ya Kiislamu iwapo Ummah utakuwa na haki ya kumteuwa mtawala hapo.

Mtume (saw) amekuwa mtawala wa Madina wakati Bay’ah Aqaba ya Pili ilipofanyika katika bonde la Aqaba katika mwezi wa Muharram. Waislamu kutoka makabila ya Aus na Khazraj walitoa bay’ah kwa Mtume (saw) na kuahidi kumtii na kumhifadhi. Vile vile, mara tu baada ya kifo cha Mtume (saw), viongozi na wawakilishi wa Muhajirin na Ansar walikusanyika pamoja katika Saqifa ya Bani Sa’ida na baada ya majadiliano baina yao, kwa hiyari walimpa bay’ah Abu Bakar Siddiq (ra) na kumfanya Khalifah wao. Katika masiku yake ya mwisho kabla ya kifo chake, Waislamu wa Madina walimuomba Abu Bakar (ra) kumtaja atakayeshika nafasi yake na akamchagua Umar (ra). Baada tu ya kifo cha Abu Bakar (ra), watu wa Madina walimpatia bay’ah Umar (ra) na akachaguliwa kushika nafasi ya Khalifah. Baada ya kifo cha Umar (ra), watu wa Madina walipitia mchakato mpana wa kumchagua Khalifah aliyefuatia kutoka wagombea sita. Hatimaye walimchagua Uthman (ra) na kumpatia bay’ah. Vivyo hivyo, siku chache tu baada ya kifo cha Uthman (ra), watu walikuja kwa Ali (ra) na kumshawishi kuchukua nafasi ya Utawala. Ali (ra) alikubali na kuwa Khalifah na kupatiwa bay’ah. Katika vipindi vilivyofuatia, njia ya kumchagua Khalifah kwa kumpatia bay’ah iliendelea. Hata hivyo, Ummah ulipoteza hamu katika kufuata mchakato wa uchaguzi wa Khalifah. Japokuwa huu ulikuwa ni udhaifu kwa Ummah, hata hivyo haki ya kumchagua Khalifah bado imebakia kwa Ummah. Wakati wa kipindi cha Mtume (saw) na Makhalifah waongofu, Ummah uliendeleza, na bila kuvunja kanuni, walimchagua mtawala kwa ridhaa yao wenyewe, na kufanya bay’ah yao kuwa ni msingi wa kuteuliwa mtawala. Katika serikali ya Kiislamu, mamlaka ya kuchagua Khalifah yanabaki kwa Ummah, ambao humchagua kwa hiyari kwa kumpa bay’ah. Bay’ah ni utaratibu wa kisheria wa Kiislamu wa kukabidhi mamlaka kutoka kwa Ummah kwenda kwa Khalifah. Kwa hivyo, dola haitokuwa ni dola ya Kiislamu, pindi haki ya kumchagua mtawala itachukuliwa kutoka kwa Ummah na kupewa tabaka fulani au kikundi, au ikiwa uteuzi wa mtawala hautofanywa kupitia bay’ah.

Abu Hurayra (ra) amepokea kwa Mtume (saw) akisema, «كَانَتْ بَنُو إِسْرَائِيلَ تَسُوسُهُمُ الأَنْبِيَاءُ، كُلَّمَا هَلَكَ نَبِيٌّ خَلَفَهُ نَبِيٌّ، وَإِنَّهُ لا نَبِيَّ بَعْدِي، وَسَيَكُونُ خُلَفَاءُ فَيَكْثُرُونَ، قَالُوا: فَمَا تَأْمُرُنَا؟ قَالَ: فُوا بِبَيْعَةِ الأَوَّلِ فَالأَوَّلِ، أَعْطُوهُمْ حَقَّهُمْ فَإِنَّ اللَّهَ سَائِلُهُمْ عَمَّا اسْتَرْعَاهُمْ» “Walikuwa Banu Israil Viongozi wao wa kisiasa ni Mitume. Kila anapofariki Mtume hufuata Mtume mwengine. Lakini hakutakuwa na Mtume baada yangu na kutakuwa na Makhalifa na watakuwa wengi. Wakasema: nini unatuamrisha? Akasema: Wapeni bay’ah mmoja baada ya mwengine, wapeni haki zao, kwani Mwenyezi Mungu (swt) atawauliza juu ya raia wao.” [Muslim]. Nafy ameripoti kuwa alimsikia Abdullah bin Amr kuwa Mtume (saw) amesema, «مَنْ خَلَعَ يَدًا مِنْ طَاعَةٍ لَقِيَ اللَّهَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ لا حُجَّةَ لَهُ، وَمَنْ مَاتَ وَلَيْسَ فِي عُنُقِهِ بَيْعَةٌ مَاتَ مِيتَةً جَاهِلِيَّةً» “Yeyote anayejivua kutoka kwenye twaa, atakutana na Mwenyezi Mungu (swt) siku ya kiyama hali ya kuwa hana hoja, na anayekufa bila kuwa na bay’ah shingoni mwake basi hufa kifo cha kijahilia.” [Muslim]. Hadithi hizi zinajulisha kuwa mamlaka na nguvu za Khalifah zinatokana na bay’ah kwake, kwa sababu Mwenyezi Mungu (swt) amefanya ni wajibu kwake kutiiwa muda wa kwamba amepewa bay’ah. Hivyo, yeyote anayetoa bay’ah kwa Khalifah lazima amtii. Kwa hivyo, mtu huwa Khalifah kwa sababu ya bay’ah anayochukua na utiifu kwake unakuwa ni wajibu kwa sababu yeye ni Khalifah aliyepewa bay’ah na Ummah. Kwa maneno mengine, Khalifah huchukua mamlaka kutoka kwa Ummah kupitia bay’ah.

5. Ili dola iwe ya Kiislamu, ni Khalifah pekee ndio awe mwenye mamlaka ya kutabanni (kuweka) rai yoyote ya Kiislamu ya kisheria na kuwa sheria, katika masuala yenye rai tofauti.

Uislamu una njia ya kutatua tofauti na kuchukua rai moja ili kuifanyia kazi. Njia ya Uislamu, hata hivyo, kimsingi ni tofauti kabisa na ya Demokrasia. Wakati kunapokuwepo uoni tofauti juu ya suala, katika dola ya Kiislamu, kiongozi wa dola, Khalifah, ana mamlaka ya kutabani rai yoyote anayoiona ina nguvu zaidi. Katika Uislamu, rai hupimwa kwa msingi wa nguvu ya dalili za kisharia. Kwa kuchukua rai, Khalifah huifanya iwe ni sheria na huwa ni wajibu kwa Ummah kuifuata. Ushahidi wa hili ni maafikiano ya Maswahaba (Ijmaa as-Sahaba) ambapo wote walikubaliana kuwa pindi Khalifah akitabanni hukmu maalum ya kisharia, basi huwa ni wajibu kwa kila mtu kuifuata. Kwa mfano, Abubakar (ra) alitamka kuwa mume akimuacha mke wake mara tatu katika kikao kimoja, basi talaka hizo tatu huhisabiwa kuwa ni moja. Hivyo hivyo, aliagiza ngawira za vita zigawiwe kwa usawa miongoni mwa Waislamu na kusitafautishwe baina ya waliosilimu mwanzo na wapya katika ugawanyaji huu. Waislamu wote walimfuata katika maagizo haya. Hata maqadhi na magavana walitekeleza maamuzi yao kulingana na rai zake hizi. Hivyo hivyo, wakati Umar (ra) alipokuwa Khalifah, alitoa rai zilizo kinyume na za Abu Bakar (ra) katika masuala haya. Kwa mfano aliamua kwamba talaka tatu zinazotolewa katika kikao kimoja zihisabiwe ni tatu. Pia alitofautisha baina ya Waislamu waliosilimu mwanzo na wapya katika kugawanya mali, na aliwapa nafasi ya kwanza wale wa mwanzo dhidi ya wapya. Waislamu walimfuata na maqadhi na magavana waliweka maamuzi yao kwa mujibu wa rai hizi. Pia, Umar ibn al-Khattab (ra) alishikilia rai ya kuwa ardhi za ngawira kutokana na vita hazitogawiwa baina ya wapiganaji, bali haki ya umiliki wake upo kwa hazina ya serikali. Pia, aliamuru kuwa ardhi hizi zibakie kwa wamiliki wake wa mwanzo kabla ya kutekwa (kwa ajili ya matumizi). Waislamu na wapiganaji hawakuzozana au kumpinga Omar katika hili na maqadhi na magavana walitoa maamuzi yao kwa mujibu wa tabanni yake hii. Kwa hivyo, Makhalifah Waongofu wote walifanya kuwa ni wajibu juu ya watu kuacha rai zao juu ya tabanni alizoziweka Khalifah. Kwa hivyo katika maelezo haya tunapata vitu viwili. Moja ni kuwa Khalifah anayo haki ya kutabanni, na pili ni kuwa ni wajibu kufuata tabanni ya Khalifah. Zikafuata hukumu za kisharia zilizozalikana kutoka kwenye Ijma ya Masahaba: للسلطان أن يحدث من الأقضية بقدر ما يحدث من مشكلات “Khalifah (Sultan) ana mamlaka ya kuamrisha utekelezaji wa tatuo maalum kwa suala lolote jipya,” أمر الإمام يرفع الخلاف “Amri ya Imamu huondosha khilafu” na أمر الإمام نافذ “Amri ya Imamu (Khalifah) ni yenye kutekelezwa.”

Hivyo, licha ya kuwepo tofauti za rai miongoni mwa Maswahaba kuhusiana na masuala ya Kisharia kwa sababu ya namna tofauti ya ufahamu wa dalili kwa kila mmoja wao, wote walikubaliana kuwa Khalifah anaweza kutatua tofauti zozote kwa kutabanni rai moja anayoiona ina nguvu zaidi na kuifanya kuwa ni sheria. Hivyo japokuwa Uislamu unapendekeza kwa Khalifah kuwashauri watu juu ya masuala ya mizozo, jambo hili la kutabanni rai katika kipindi chote cha utawala wa Kiislamu, wakati wa Makhalifah Waongofu na baada yake, inathibitisha kuwa njia ya Uislamu ya kuweka sheria zinazoegemea juu ya Sharia ni haki ya kipekee ya Khalifah. Njia yoyote nyengine ya kutengeneza sheria ni alama ya dola isiyo ya Kiislamu.

 6. Ili dola iwe ya Kiislamu, ni lazima katiba yake, sheria na sera ziwe zimeegemezwa juu ya Wahyi pekee.

Njia pekee ya kupata wokovu siku ya Kiyama ni kwa kufuata Wahyi wa Mwenyezi Mungu (swt). Uislamu umewataka waumini kuufanya Wahyi wa Mwenyezi Mungu (swt) kuwa ndio msingi pekee wa kutatua masuala yote ya kimaisha na kwa kutaka uongofu. Wahyi ni chanzo pekee cha Dini na ni kupitia kwake tu mtu anaweza kufahamu maagizo na makatazo ya Mwenyezi Mungu (swt). Hivyo ni lazima kwa dola inayotaka kuwa dola ya Kiislamu iwe katiba yake, sheria na sera ziwe juu ya wahyi na zisiegemee juu ya vyanzo vyengine vyovyote. Wahyi hapa unarejea kwenye Quran na Sunnah za Mtume (saw). Kwa hivyo, msingi wa sheria za kiutawala na mfumo uwe ni Quran na Sunnah, na vyanzo vinavyoegemea Quran na Sunnah pekee.

Mwenyezi Mungu (swt) anasema:

وَمَن لَّمۡ يَحۡكُم بِمَآ أَنزَلَ ٱللَّهُ فَأُوْلَـٰٓٮِٕكَ هُمُ ٱلۡكَـٰفِرُونَ﴿

“Na wasiohukumu kwa aliyoteremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio makafiri.” [Surah Al-Maidah 5:44].

وَمَن لَّمۡ يَحۡڪُم بِمَآ أَنزَلَ ٱللَّهُ فَأُوْلَـٰٓٮِٕكَ هُمُ ٱلظَّـٰلِمُونَ﴿

“Na wasiohukumu kwa aliyoteremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio madhalimu.” [Surah Al-Maidah 5:45]. Na amesema Mwenyezi Mungu (swt),

وَمَن لَّمۡ يَحۡڪُم بِمَآ أَنزَلَ ٱللَّهُ فَأُوْلَـٰٓٮِٕكَ هُمُ ٱلۡفَـٰسِقُونَ﴿

“Na wasiohukumu kwa aliyoteremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio mafasik.” [Surah Al-Maidah 5:47]. Na amesema Mwenyezi Mungu (swt),

وَأَنِ ٱحۡكُم بَيۡنَہُم بِمَآ أَنزَلَ ٱللَّهُ وَلَا تَتَّبِعۡ أَهۡوَآءَهُمۡ﴿

“Na wahukumu baina yao kwa aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate matamanio yao.” [Surah Al-Maidah 5:49]. Aya hizi na nyengine nyingi mfano wake ni ushahidi unaothibitisha kuwa ni wajibu juu ya Waislamu kuhukumu kwa kile alichokiteremsha Mwenyezi Mungu (swt) kwa Mtume Wake (saw), ambacho ni Wahyi katika muundo wa Quran na Sunnah.

Kwa hivyo dola huweza kuwa ni ya Kiislamu pindi hukmu zake zitaegemea juu ya Shariah. Mwenyezi Mungu (swt) ameukamilisha Uislamu kwa kuweka uongofu kwenye mambo yote ambayo watu kote duniani wanaweza kukumbana nayo hadi Siku ya Kiyama. Mwenyezi Mungu (swt) amesema katika Quran,

ٱلۡيَوۡمَ أَكۡمَلۡتُ لَكُمۡ دِينَكُمۡ وَأَتۡمَمۡتُ عَلَيۡكُمۡ نِعۡمَتِى وَرَضِيتُ لَكُمُ ٱلۡإِسۡلَـٰمَ دِينً۬ا﴿

“Leo nimekukamilishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini.” [Surah Al-Maidah 5:3]. Kwa hivyo Uislamu tayari unayo maelezo yote na amri za kisheria ambazo mtawala huenda akahitajia muda wowote au mahala popote. Hivyo, kutabanni fikra, sheria au sera zinazovuliwa kutoka kwenye vyanzo vyengine visivyokuwa vile vinavyotokana na kile ambacho Mwenyezi Mungu (swt) amekiteremsha haikubaliki katika Uislamu. Kuna tofauti kubwa baina ya kutohoa sheria kutoka kwenye Uislamu na zile zitokanazo na vyanzo vyengine na kujaribu kuhalalisha utumiaji wake kupitia Uislamu. Katika hali ya mwanzo sheria zitakuwa ni za Kiislamu wakati katika hali ya pili itakuwa kinyume. Katika hadithi zilizoafikiwa, Mtume (saw) amesema, «مَنْ أَحْدَثَ فِي أَمْرِنَا هَذَا مَا لَيْسَ فِيهِ فَهُوَ رَدٌّ» “Mwenye kuzuwa katika jambo letu hili (Dini) ambalo halimo (katika Dini hii) basi ni lenye kurejeshwa.” Haya ni maneno katika Bukhari ambapo katika Muslim kumeripotiwa maneno «ما ليس منه» “ambalo halimo kutoka humo”. Pia, Ibn Hazm na Ibn Abdul Bar ameripoti maneno, «كُلُّ عَمَلٍ لَيْسَ عَلَيْهِ أَمْرُنَا فَهُوَ رَدٌّ» “Kila amali ambayo haiendani na jambo letu ni yenye kurejeshwa.” Hadithi hizi zinathibitisha kuwa kila jambo ambalo linachukuliwa kutoka kwengine kusikotokana na wahyi halikubaliwi na Uislamu. Haijalishi kama hukumu hiyo iliochukuliwa kutoka kwenye chanzo chengine inaunga mkono Uislamu au ni dhidi yake. Kwa hivyo, dola inaweza kuwa ya Kiislamu ikiwa katiba yake kamili, sheria na nidhamu zimeegemea juu ya Uislamu tu.

7. Ili dola iwe ya Kiislamu, ni lazima mahusiano yake na dola nyengine yawe kwa msingi wa Uislamu tu na ibebe ujumbe wa Uislamu katika maeneo mengine yaliobaki duniani.

Bay’ah ambayo Waislamu wanaitoa kwa Khalifah ina maudhui mbili. Kwanza ni kuwa Khalifah atalazimisha utekelezaji wa Sharia kwa mamlaka aliyokabidhiwa na Ummah, ambayo ni kuwa atatawala kwa Uislamu, na pili ni kuwa Khalifah ataeneza ujumbe wa Uislamu katika maeneo yaliobaki duniani. Ili kukamilisha takwa la pili pia inahitaji kufanya mapigano ya kisilaha (Jihad) kwa lengo la kuondoa vikwazo katika njia ya Da’wah hii. Kwa hivyo, katika Uislamu, mtawala anawajibika kwa mambo yote haya mawili, ambayo ni utekelezaji wa Uislamu ndani, na Da’wah na Jihad nje. Mtume (saw) amesema: «أُمِرْتُ أَنْ أُقَاتِلَ النَّاسَ حَتَّى يَشْهَدُوا أَنْ لاَ إِلَهَ إِلا اللَّهُ وَأَنَّ مُحَمَّدًا رَسُولُ اللَّهِ وَيُقِيمُوا الصَّلاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ، فَإِذَا فَعَلُوا ذَلِكَ عَصَمُوا مِنِّي دِمَاءَهُمْ وَأَمْوَالَهُمْ إِلا بِحَقِّ الإِسْلامِ، وَحِسَابُهُمْ عَلَى اللَّهِ» Nimeamrishwa kupigana na watu hadi washuhudie kuwa Hakuna Mola anayepaswa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni mjumbe wake, na kusimamisha swala, na kutoa zaka; pindi wakifanya hayo watakingwa nami damu yao na mali yao isipokuwa kwa haki ya Uislamu, na hisabu yao iko kwa Mwenyezi Mungu.” [Muttafaqun alayhi].

Ushahidi mwengine kwa hili ni kuwa licha ya kujua kuwa Waislamu walikuwa dhaifu zaidi kijeshi  kuliko Maquresh wa Makkah, Mtume (saw) bado alishikilia kujenga mahusiano yake na Maquresh juu ya msingi wa Uislamu. Aliendelea kufuata sera ya kukomboa Makkah, na hatimaye alifanikiwa. Pia, Mtume (saw) alipeleka barua mbalimbali kwa wafalme na watawala wa mataifa makubwa ya wakati wake, sio kwa kuweka mahusianao juu ya maslahi ya pamoja, bali kuwataka waukubali Uislamu na kutambua mamlaka yake. Vile vile, Mtume (saw) alitayarisha jeshi chini ya Usama kabla ya kifo chake, na kusisitiza juu ya kulipeleka japokuwa alikuwa mgonjwa taabani wakati huo, ili likapigane na Himaya ya Roma na kuiweka chini ya mamlaka ya Uislamu. Baada ya kifo chake, dola ya Kiislamu iliendelea kutanuka na Waislamu waliendelea kupigana jihad, kutoa changamoto kwa mifumo iliyopo katika maeneo yaliobakia ya dunia.

Dhumuni la Mwenyezi Mungu (swt) la kuuleta Uislamu duniani ni kusimamisha mamlaka ya Uislamu duniani kote. Mwenyezi Mungu (swt) anasema:

هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ﴿

“Yeye ndie aliyemtuma Mtume wake kwa uongofu na Dini ya Haki, ili aitukuze juu ya dini zote.” [Surah Al-Fath:28]. Uwepo wa mifumo isiokuwa ya Kiislamu kwa hakika ni ukumbusho kuwa kazi hii ambayo Mwenyezi Mungu (swt) amewapa Waislamu bado haijakamilika, baada ya kifo cha Mtume (saw), Ummah ulitoa bay’ah kwa Makhalifah.

Hivyo hakuna katika Uislamu dhana ya kuwa dola isieneze Uislamu katika maeneo mengine ya dunia na kuzishinda dini nyengine na mifumo. Vivyo hivyo, Uislamu hautambui dola ambayo kwa ndani inadai kushindikiza mafundisho ya Uislamu lakini inaendelea kutambua mfumo wa dunia uliopo, ikifanya maamuzi kutafuta kuidhinishwa na mataifa makubwa. Pia, hakuna dhana ya dola iliojifungamanisha na sheria za kimataifa za Kimagharibi, kutambua au kujiunga na mashirika ya Kimagharibi kama Umoja wa Mataifa, Baraza lake la Usalama, IMF au Mahakama ya Jinai ya Kimataifa. Wala hakuna dhana ya dola ya kitaifa katika Uislamu, ambapo dola inatambua na kujifunga yenyewe na utaifa, mipaka ya kubuni badala ya kufanya jitihada ya kukomboa maeneo yaliokaliwa kimabavu ya Waislamu kutoka kwa wavamizi makafiri. Dola kama hii haina dalili juu ya uwepo wake kutoka kwenye Uislamu.

Hitimisho:

Kwa kuchunguza misingi ya hapo juu, inadhihirika wazi kuwa dola haiwezi kuwa ya Kiislamu ikiwa itafuata baadhi ya misingi muhimu ya Uislamu kwenye utawala, lakini ikawa nidhamu yote ya serikali, muundo wa uchumi wake, jamii, mahakama, elimu na viwanda, na masuala ya ndani na nje na usalama yamejengwa juu ya misingi ya Kimagharibi. Wala dola haiwi ya Kiislamu kama itaamua kuacha kazi ya kueneza Uislamu katika maeneo yaliobakia duniani, na badala yake ikawa na jitihada ya kulinda mipaka yake ya kitaifa tu. Vivyo hivyo, dola haiwezi kuwa ya Kiislamu kama itaanza kujiunga na mashirika ya kimataifa kama Umoja wa Mataifa, au mfano ikaanzisha mahusiano na Amerika yanayoegemea mapatano na fikra ya nipe nikupe, au kuweka maslahi ya kitaifa dhidi ya Uislamu, au kuchukua fikra za Kimagharibi na dhana zinazohusiana na masuala kama haki za binadamu za Kimagharibi, haki za wanawake, haki za msingi na sheria za kimataifa. Ni jambo la kuangaliwa sana katika wakati wetu huu, wakati Wamagharibi wanataka kuzivua kabisa fikra na hisia za Kiislamu kutoka kwenye mabongo ya Waislamu kupitia mashambulizi ya nguvu ya  kithaqafa na kifikra, Waislamu lazima wafahamu fikra msingi zinazojenga thaqafa ya Kiislamu, ili waweze kuzuia mashambulizi haya ya mataifa ya nje, na pia wasiweze kudanganywa na vibaraka  wanaotawala ardhi za Waislamu. Bila shaka, kwa ufahamu huu sahihi wa fikra ya Uislamu ambao utawasaidia Waislamu kutambua serikali inayotarajiwa kusimama karibuni inshaa Allah. Katika siku hiyo, waumini watafurahi na dunia yote itashuhudia utekelezaji wa kweli wa Uislamu na matunda yatayofuatia.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Mun’im Ahmed – Wilayah Pakistan

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu