Alhamisi, 23 Rajab 1446 | 2025/01/23
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Furaha na Faharasa Hadaifu ya Furaha

(Imetafsiriwa)

Watu wanaondoka Pakistan kwa wingi. Mnamo 2022 pekee, zaidi ya Wapakistani 800,000 waliondoka nchini mwao kutafuta maisha bora ng’ambo. Sio tu ukosefu wa utulivu wa kisiasa na ukosefu wa usalama wa kiuchumi ndio unaochangia msafara huu wa watu wengi, lakini pia dhana kwamba kuhamia nchi ya Magharibi kutatufanya kuwa na furaha zaidi. Matokeo ya kila mwaka ya Faharasa ya Furaha yanasukuma zaidi simulizi hii, kwani ni wazi nchi za Magharibi ndizo zinazoongoza katika viwango. Vipi basi, endapo hii ni ndoto pekee? Makala haya yanalenga kueleza maana ya furaha hasa na pia kuumbua Faharasa ya Furaha.

Furaha ni hisia ya kibinafsi. Kwa sababu hii, kumekuwa na mijadala mingi na ukosoaji juu ya ufafanuzi wake mbalimbali na mbinu za kuipima. Mijadala na ukosoaji kama huo pia huenea hadi Faharasa ya Furaha, ambayo ni kipimo cha kura ya maoni cha furaha ya kitaifa kote ulimwenguni na huchapishwa kila mwaka kama viwango vya nchi. Faharasa inategemea idadi ya watu waliohojiwa kwenye kile kinachoitwa ngazi ya Cantril, ikiweka viwango vyao vya furaha alama 1 hadi 10. Mpya zaidi kutolewa ilikuwa mwaka wa 2023 wakati Finland ilipoongoza chati kwa kuvunja rekodi mara ya sita. Uangaziaji mzima wa vyombo vya habari unataka kwamba fahamu ya furaha ieleweke ndani ya mtazamo wa ulimwengu wa mtu mwenyewe, ambao, bila shaka, kwa Waislamu unapaswa kuwa wa Kiislamu.

Furaha inaweza kufafanuliwa tu kama hali ya kutosheka. Kwa mujtamaa za kisekula za Kimagharibi, kuridhika huko kwa kibinafsi kunafungamanishwa na kufurahia kiwango cha juu zaidi cha starehe za kimwili. Kama ilivyo kwa hisia yoyote ya kibinafsi, furaha pia inategemea ushawishi wa kitamaduni wa mtu, maadili ya kibinafsi, na matarajio. Tunaishi katika ulimwengu uliounganishwa sana ambao unasonga kuelekea utamaduni mmoja na mjumuiko mmoja maalum wa maadili ambayo hutawala matarajio ya mtu. Wanaopenda na wasiopenda watu huathiriwa zaidi na thaqafa na maadili yanayotawala, ambayo ni ya Kimagharibi. Ulimwenguni, hii imesababisha ufadhilishaji mkubwa wa:

  • Ubinafsi juu ya Mkusanyiko
  • Kupenda mali kuliko Usahali
  • Mafanikio ya kibinafsi juu ya Majukumu ya Kifamilia
  • Usekula juu ya Kujitolea Kidini
  • Usawa wa Kijinsia juu ya Dori za Kijadi za Jinsia
  • Utumiaji juu ya Kujizuia

Maana yake ni kwamba watu wangefikiri wangekuwa na furaha zaidi ikiwa wangekuwa na sehemu nyingi za upande wa kushoto wa nukta hizo zilizo hapo juu, hata kama hilo lilikuja kwa gharama ya upande wa kulia. Je, hilo linamaanisha kwamba mtu anaweza kudanganywa afikiri kwamba ana furaha wakati hana? Ndiyo, ni kweli! Fikiria mfano wa moja kwa moja wa mraibu wa dawa za kulevya ili kuelewa hili. Akiwa chini ya ushawishi wa dawa za kulevya, angeweza kukadiria furaha yake kuwa kamili. Kwa viwango vyake vya kujitegemea, angeishi maisha ya furaha ikiwa asalia kwenye stimu kwa maisha yake yote. Sisi, kama watazamaji, tunajua kwamba maisha kama hayo ni ya kuchosha na hayana maana. Maisha na matarajio ya watu wa nchi za Magharibi ni sawa na mfano huu. Wana mipaka katika uwezo wao wa kuona kupita malengo fulani ya kibanafsi na ya uchoyo.

Kielelezo kifuatacho kitakusaidia kuelewa suala jengine la kujiripoti kama hivyo: Mtu ambaye hivi majuzi alishinda dolari milioni moja katika bahati nasibu bila shaka angekadiria kiwango chake cha furaha kuwa cha juu sana. Hata hivyo, kushinda dolari milioni moja katika bahati nasibu kwaweza kukufanya usahau kwa muda kifo cha mpendwa wako, kuteseka kwa mzazi mgonjwa, au mshtuko wa kuvunjika mahusiano, lakini hiyo haimaanishi kwamba matokeo ya hasara hiyo yametoweka. Kinyume chake, watu hatimaye watakuja kuelewa kwamba mali haiwezi kuchukua nafasi ya ‘hasara’. Fikra za unyogovu na wasiwasi zinaweza kuandamana na utambuzi huu. Bila kujali upuuzi wa yule wa kwanza au busara ya yule wa pili, mara kwa mara wanadamu huonyesha mwelekeo wa kutafuta kuridhika mara moja huku wakipuuza malengo muhimu zaidi, ya muda mrefu, hasa yanapoathiriwa na mfumo huria, wa kisekula wa Kimagharibi. Hili linafafanuliwa kwa wingi na alama za furaha, ambazo zinapendelea nchi za WEIRD (za Kimagharibi, Zilizoelimika, Zenye Viwanda, Tajiri, za Kidemokrasia). Kulingana na tafiti, faharasa ya furaha ya nchi hupanda jinsi inavyozidi kuwa WEIRD. Kipimo cha kiwakilishi cha furaha kinapaswa kulenga kuwa huru dhidi ya sifa ya WEIRD ya taifa.

Sasa kuuleta Uislamu katika mjadala kunabadilisha mtazamo wa furaha hata zaidi—hilo pia, kwa kiasi kikubwa. Waislamu wanafanya vitendo vyao vyote kwa mujibu wa maamrisho na makatazo ya Mwenyezi Mungu kwa sababu wao peke yao ndio wanaopaswa kutawala mambo yote ya jamii. Njia pekee ya kuleta furaha na utulivu kwa Muislamu ni kujiendesha kwa mujibu wa maamrisho na makatazo ya Mwenyezi Mungu. Hivyo basi, furaha ya kweli huitafutwi kwa starehe za kimwili, bali kwa kupata radhi za Mwenyezi Mungu bila kupuuza mahitaji yoyote ya kimwili au ya ghariza.

Qur’an na Sunnah zimetumia aina tofauti za neno ‘sa’adah’ ambalo limetafsiriwa kilugha kuwa furaha, lakini neno rasmi zaidi ‘linalostahiki’ linatumika katika tafsiri. Imetajwa mara mbili ndani ya Qur’an, zote mbili katika Surah Hud, kama ifuatavyo:

[يَومَ يَأتِ لا تَكَلَّمُ نَفسٌ إِلّا بِإِذنِهِ فَمِنهُم شَقِيٌّ وَسَعيدٌ]

“Siku hiyo itakapo fika, hatosema hata mtu mmoja ila kwa idhini yake Mwenyezi Mungu. Kati yao watakuwamo waliomo mashakani na wenye furaha.” [Surah Hud:105]

[وَأَمَّا الَّذينَ سُعِدوا فَفِي الجَنَّةِ خالِدينَ فيها ما دامَتِ السَّماواتُ وَالأَرضُ إِلّا ما شاءَ رَبُّكَ عَطاءً غَيرَ مَجذوذٍ]

“Na ama wale walio bahatika, wao watakuwamo Peponi wakidumu humo muda wa kudumu mbingu na ardhi, isipo kuwa apendavyo Mola wako Mlezi. Hicho ni kipawa kisio na ukomo.” [Surah Hud:108]

Jambo la kuvutia ni kwamba, kutajwa kwa furaha zote mbili ni katika muktadha wa Akhera, ambapo inatuleta kwenye tofauti kuu kati ya fahamu ya furaha katika tamaduni za Kimagharibi na Kiislamu. Kwa Waislamu, furaha ya kweli na ya milele inapatikana Akhera. Zaidi ya hayo, fursa yoyote, hata kama ni ngumu, ya kufikia furaha hiyo ya milele, itawafanya Waislamu kuwa na furaha katika maisha haya. Hii ina maana kwamba, ugumu, mitihani, na majaribio yatakuwa na safu hii nzuri ya kumkumbusha mtu juu ya raha ya milele na hivyo kuchangia furaha jumla, au angalau kupunguza mateso.

Kwa kuregelea Sunnah, inafafanua zaidi fahamu hii. Hadith ifuatayo inafafanua kwa uwazi sana furaha: Sa’d ameripoti: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:

«مِنْ سَعَادَة ابْنِ آدَمَ رِضَاهُ بِمَا قَضَى اللهُ لَهُ وَمِنْ شَقَاوَةِ ابْنِ آدَمَ تَرْكُهُ اسْتِخَارَةَ اللهِ وَمِنْ شَقَاوَةِ ابْنِ آدَمَ سَخَطُهُ بِمَا قَضَى اللهُ لَهُ»

“Miongoni mwa furaha ya mwanadamu ni kutosheka na yale aliyomwandikia Mwenyezi Mungu. Miongoni mwa masaibu ya mwanadamu ni kuacha kumuomba Mwenyezi Mungu uongofu, na miongoni mwa masaibu ya mwanadamu ni kuchukizwa na yale aliyomwandikia Mwenyezi Mungu.” [Sunan at-Tirmidhī]

Hadith hii inatwambia kwamba kupata kuridhika na kile mtu alicho nacho kunaweza kuchangia furaha. Leo, kukubali uhalisia kunaweza kuwa vigumu sana kwa watu wengi. Mara nyingi watu wanataka kubadili hali zao badala ya kuzitabanni, jambo ambalo linaweza kuwafanya wasiwe na furaha. Kutoridhika huku kunaweza kuwa ni matokeo ya ujumbe wa kijamii, ambayo mara nyingi huimarisha dhana potofu kwamba mtu anaweza kupata kile anachokitaka jinsi vile anavyotaka.

Hebu turudi kwenye Faharasa ya Furaha, ambapo Finland iliongoza katika viwango kwa mwaka wa sita mfululizo. Hebu na tuangalie kwa karibu zaidi Finland na baadhi ya masuala yake yaliyoenea zaidi.

Huku 5.6% ya wakaazi wake wakiwa na tatizo la kiafya la msongo wa mawazo, Finland ni taifa la nane lenye msongo mkubwa wa mawazo duniani. Kwa mujibu wa viwango vya watu kujiua, ambavyo vinasimama katika 14.2 kwa kila watu 100,000, imeorodheshwa hivyo hivyo (ya 8) kote duniani. Ushirikiano wa Finland wa Afya ya Akili, ambao una mashirika 34 ya afya ya akili, hivi majuzi uliweka pamoja ripoti kwa ajili ya wajumbe wa bunge la Finland. Ilifichua kwamba matatizo ya afya ya akili ndiyo sababu kubwa ya kustaafu mapema katika hali za kupungua uwezo wa kufanya kazi. Iliongeza kuwa masuala ya afya ya akili yanagharimu serikali karibu dolari bilioni 13 kwa mwaka. Mnamo Julai 2021, Nambari ya Msaada wa Janga la Kitaifa iliweka rekodi wakati zaidi ya watu 28,000 waliomba msaada katika mwezi huo mmoja tu, katika nchi yenye jumla ya watu zaidi ya milioni 5.5. Helsinkimissio ni shirika la kazi za kijamii linalofanya kazi ya kujitolea. Lilianzishwa mwaka wa 1883. Tangu wakati huo, lengo la shirika hili limekuwa kupunguza upweke. Hata hivyo, maombi ya kuomba msaada yaliongezeka kwa asilimia 30 mwaka wa 2020. Sababu kubwa ya kuwasiliana na Helsinkimissio ilikuwa moja kwa vijana na wazee: upweke. Je, unaweza kupata maana gani kutokana na takwimu hizi? Ni nini kinachoweza kuelezea nchi yenye furaha zaidi inayopambana na upweke na kuorodheshwa kati ya 10 bora katika viwango vya watu kujiua na msongo wa mawazo zaidi ya uelewa kimakosa wa nini furaha?

Je, hii inamaanisha kuwa jamii za Kiislamu hazina matatizo? La hasha; tunakabiliwa na changamoto mbalimbali, nyingi zikiwa ni za kiuchumi. Hata hivyo, uchunguzi wa karibu wa jamii zetu utafichua haraka kwamba matatizo yetu ni matokeo ya uporaji wa kihistoria na unaoendelea wa nchi za Magharibi wa rasilimali zetu. Kihistoria, ilitokana na ukoloni wa Waingereza, na inaendelea hadi leo kwa namna ya hila zaidi: ukoloni wa kitaasisi. Haitakuwa sahihi kudai kwamba furaha yoyote, sawa au mbaya, nchi nyingi za Magharibi zinazoihisi leo inakuja kwa gharama ya nchi zinazoendelea kutokana na mfumo wa kidunia uliyoibiwa dhidi yao. Hii, hata hivyo, ni mada ya makala mengine.

Kwa kumalizia, fahamu ya furaha ni ya kibinafsi na inaathiriwa na maadili ya kitamaduni na matarajio ya kibinafsi. Mtazamo wa Kimagharibi juu ya ubinafsi na fikra ya mada unaweza kusababisha uelewa potofu wa furaha. Uislamu unatoa mtazamo tofauti, unaosisitiza furaha ya milele kesho Akhera na kupata radhi za Mwenyezi Mungu kwa kutimiza mahitaji ya kimwili au ya ghariza kwa mujibu wa maamrisho ya Mwenyezi Mungu. Faharasa ya Furaha, ingawa ina dosari, hupima alama za kujiripoti kibinafsi ambazo huenda zisinase furaha ya kweli. Mfano wa Finland, nchi inayoshikilia nafasi ya juu kwenye faharasa lakini inakabiliwa na viwango vya juu vya msongo wa mawazo na watu kujiua, inaangazia vikomo vya kutegemea viashiria vya nje pekee. Furaha ya kweli inapatikana katika kuukubali uhalisia, kuheshimu mipaka ya Mwenyezi Mungu, na kutafuta kuridhika na yale aliyoyakidhia Yeye (swt).

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Dkt. Abdul Baseer Qazi – Wilayah Pakistan

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu