Ijumaa, 20 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Je, Kiwango cha Dhahabu kitakuwa Badali kwa Dolari?

(Imetafsiriwa)

Pamoja na mjadala wa Kuachana na Dolari, inakuja moja ya chaguzi badali za sarafu. Tunajua kuwa dolari haitabadilishwa katika mfumo huu, hata kama nchi zitaanza kuondoka kutoka kwa dolari kwenda kwa sarafu zengine kwa kujaribu kupunguza utegemezi wao kwa sarafu ya Amerika. Kwa hivyo, chaguo jengine ni Kiwango cha Dhahabu. Tunajua kwamba itatabanniwa wakati Khilafah itakaposimamishwa tena, lakini je, Marekani inaweza kurekebisha sera zake na kuanzisha upya Kiwango cha Dhahabu katika kujaribu kuleta ustawi wa uchumi wake? Na la muhimu zaidi ni je, watafanya ikizingatiwa uhalisia na athari za Kiwango cha Dhahabu?

Huu sio mjadala mpya; wanasiasa wa Marekani wamejadili matumizi ya Kiwango cha Dhahabu katika kampeni zao hapo awali. Ingawa, cha kufurahisha mnamo Oktoba mwaka jana, Mwakilishi wa Marekani Alex Mooney (R-WV) alianzisha "Sheria ya Kuregesha Kiwango cha Dhahabu".

"Sheria hiyo inataka kuambatanishwa upya kwa noti ya Hazina ya Marekani kwa dhahabu ili kushughulikia shida zinazoendelea za mfumko wa bei, deni la serikali hiyo ya majimbo lililopitiliza, na kuyumba kwa mfumo wa fedha.

Endapo Mswada huo utapitishwa, Hazina ya Marekani na Hafadhi ya Majimbo zitakuwa na muda wa miezi 30 kufichua hadharani mali zote za dhahabu na miamala ya dhahabu, na baada ya hapo noti ya Hazina ya Majimbo "dolari" itawekwa kwenye uzani usiobadilika wa dhahabu katika soko lake la wakati huo. bei. Noti za Hifadhi ya Majimbo zitaweza kufidiwa kikamilifu na kubadilishwa na dhahabu kwa bei mpya isiyobadilika, Hazina ya Marekani na akiba yake ya dhahabu zikiegemea usaidizi wa Benki za Hifadhi ya Shirikisho kama mdhamini." (Chanzo)

Mswada huu haujawa sheria, na lazima upitie mchakato mrefu ili hata kufikia mahali ambapo utazingatiwa na Seneti na kisha Rais. Lakini ni mfano mwingine tu unaoonyesha kuwa watu wana wasiwasi kuhusu hali ya uchumi, na wanaona Kiwango cha Dhahabu kama njia ya kuuimarisha.

Lakini je, Marekani itaregea kwenye Kiwango cha Dhahabu, na je itamaanisha nini endapo wangefanya hivyo?

Badala ya kulitazama hili kwa mtazamo wa kiuchumi na kujadili thamani ya dhahabu n.k., hebu tuliangalie kwa mtazamo wa kisiasa.

Mjadala kuhusu ima kuregesha au kutoregesha Kiwango cha Dhahabu ni wa kisiasa, kwani dolari ilikuwa mojawapo ya zana kuu za Marekani katika kupachika mamlaka yake duniani ilipounda upya Mfumo wa Kimataifa.

Unatumiwa pia na wanasiasa nchini Marekani kupata uungwaji mkono nyumbani. Watu wao wana wasiwasi kuhusu mfumko wa bei na wanasiasa wanahitaji kujaribu kuwapatia suluhu, ndiyo maana wapenda Republican hapo awali wametumia Kiwango cha Dhahabu kama hoja katika kampeni zao. Hii ni kwa sababu, ingawa mfumko wa bei ni tokeo lisiloepukika la mfumo wa sasa wa sarafu isiyo na thamani ya dhati (fiat), sio wachangamfu katika mfumo wa Kiwango cha Dhahabu.

Mfano wa hili unaweza kupatikana nchini Uingereza, tangu walipotumia Kiwango cha Dhahabu katika Karne ya 19 na mwanzoni mwa Karne ya 20, viwango vya bei vilikuwa vilevile mwaka wa 1914, kama ilivyokuwa mwaka wa 1816. Lakini tangu kukomesha Kiwango cha Dhahabu na kuhamia sarafu ya isiyo na thamani ya dhati (fiat), Uingereza imepitia mfumko wa bei unaoendelea, na ongezeko la kila mwaka la kiwango cha bei. (Chanzo)

Lakini kama vile uwezekano wa Kiwango cha Dhahabu unaweza kutoa matumaini kwa idadi ya watu, unaweza pia kuwatia hofu, kwani wanasiasa pia wanaweza kuangazia matatizo yote yaliyo kuja na toleo lao la Kiwango cha Dhahabu, na kuwakumbusha watu kwamba ni "mabaki ya kale ambayo hayana chochote cha kupendekeza leo." (Chanzo).

Na hoja hiyo inaweza kutumika kuhalalisha uamuzi mwingine wa kisera. Bila shaka, Marekani lazima ifanye kila jitihada ili kuepuka kuregea kwenye Kiwango cha Dhahabu sasa, hata ikiwa hii itamaanisha kuwa Hifadhi ya Shirikisho inahitaji kuongeza mfumko wa bei au serikali inahitaji kutumia pesa za walipa kodi ili kuziokoa benki. Ni nini badali? Sarafu ya kiuchumi iliyoanguka? Na labda ilisababisha Mporomoko Mkubwa kabla ya Marekani kuondokana nayo?

Lakini upotoshaji wa wapiga kura kando, je, Marekani, ingeamua kupitisha Mswada wa Uregeshaji wa Kiwango cha Dhahabu?

Ikiwa wangefanya hivyo, haitakuwa na maana sana. Kwa hakika haingetatua matatizo yote tunayokabiliana nayo, kwani matatizo hayo yanatokana na masuala ndani ya Dola ya Kibepari ya sasa ambayo yanaenda zaidi ya suala la sarafu. Urasilimali una uchumi uliojengwa juu ya maslahi, ambao unatumiwa na serikali na mashirika ya kimataifa, na rasilimali za dunia ambazo zinamilikiwa na kunyonywa na makampuni ya kibinafsi. Hatua hii ya mwisho kimsingi ina maana kwamba wakati wowote wananchi wanapohitaji kupata rasilimali, iwe mafuta au chakula, sekta ya umma inahitaji kulipa pesa kwa makampuni ya kibinafsi. Na ikiwa hawana pesa, wanapaswa kuchukua mkopo au kuchapisha pesa zaidi.

Lakini tukiweka haya yote kando, hakuna uwezekano kwamba Marekani itachukua hatua kuelekea Kiwango cha Dhahabu kwani itapunguza nguvu zao za kifalme.

Walijenga nguvu hizi katika kipindi cha Karne ya 20, wakiasisi mfumo wa kiuchumi ambao walikuwa na udhibiti juu yake. Wanadhibiti sarafu ya kimataifa, kwa hivyo wanadhibiti sarafu za nchi. Hii iliwaruhusu kuanzisha mfumo wa Ukoloni Mamboleo ambapo wangeweza kupanua ushawishi wao (kwa viwango tofauti juu ya wengine) kwa njia isiyo rasmi zaidi.

Ni muhimu pia kukumbuka kuwa hata wakati Marekani iliposimamia 'Kiwango cha Dhahabu', kilikuwa toleo lao lililozimuliwa. Wakati wa Vita vya Dunia, walisimamisha mahuruji ya dhahabu na baada ya hapo walitekeleza 'Mfumo wa Ubadilishanaji Dhahabu' ambao kwao nchi zingine zilikuwa tegemezi kwa Marekani, na sera yao ya fedha.

Walikuwa na sababu ya kisiasa ya kubadilisha kutoka kwa mfumo wa Sarafu ya Dhahabu hadi Mfumo wa Sarafu zisizo na thamani ya dhati (Fiat).

Leo, sarafu zote ni 'fiat' yaani pesa zilizotolewa na serikali, ambazo haziegemezwi kwa bidhaa au mali halisi. Zinaegemezwa kwa serikali, na thamani ya sarafu inategemea mambo kadhaa ikiwemo uhalali wa serikali na imani ambayo ulimwengu unao kwake. Kwa kuwa haijaegemezwa kwa mali halisi, nchi, muhimu zaidi Marekani, zinaweza kuchapisha pesa ili kukidhi mahitaji yao, na hii ndiyo inafanya kuwa faida zaidi kwao leo.

Ni kweli kwamba hii ina maana kwamba kuna mfumko wa juu wa bei, na kwamba hatari ya mfumko wa bei imeongezeka kwa kiasi kikubwa chini ya mfumo ulio na utoaji fedha usiodhibitiwa. Lakini dolari ya Marekani inadhibitiwa kwani dunia ina imani na uwezo wa serikali ya Marekani kulipa madeni yake. Lakini kama imani hii itatoweka, wanaweza kuwa katika hatari ya kupanda kwa mfumko wa bei sawa na ule wa Zimbabwe mwaka 2008, wakati kiwango cha mfumko wa bei kilipanda hadi zaidi ya asilimia 200 milioni.

Uwezo wa kuhakikisha kuwa kuna mtiririko endelevu wa pesa pia ni muhimu kwa sababu ya kutegemea kwao biashara. Hii ni kwa sababu nchi zilizo na akiba ya sarafu hazikabiliani na vikwazo katika uagizaji wao. Kwa hivyo, Marekani imekuwa ikiendesha upungufu wa nje bila usumbufu kwa miongo mingi. Wote hulipwa kwa dolari zilizochapishwa, ambayo ndiyo sababu ya mfumko wa bei.

Lakini pamoja na mfumko wa bei uliokithiri (na uharibifu unaowaathiri watu), uwezo wa kuchapisha pesa zilizodhibitiwa ni jambo ambalo linavutia sana katika mfumo unaopitia mporomoka wa kuendelea kwa uchumi na kukuza uchu wa mali. Na unaiwezesha Marekani kudumisha utawala wake duniani (kupitia vita na mikopo).

Kuna njia ya kudhibiti sarafu, hata kwa sarafu za fiat. Inaweza kufanywa kwa kiwango kisichobadilika cha ubadilishaji, yaani, pindi nchi itapoweka bei ya sarafu yake dhidi ya sarafu moja au zaidi za kigeni. Lakini kwa mara nyingine hii inapunguza kubadilika kwa sarafu yao ya fedha kwa kuweka mipaka kwa uhuru wa benki kuu kufanya marekebisho ya viwango vya riba ili kukuza uchumi. Kwa hivyo mfumo wa kimataifa unapendelea ‘sarafu inayoelea’ kuliko ‘sarafu iliyofungwa’ ingawa sarafu nyingi ziko kwenye sehemu, katikati ya zote mbili.

Katika mfumo wa kubadilisha sarafu unaoelea, serikali na benki kuu zina uhuru wa kiwango cha juu. Lakini kwa viwango vya kubadilisha sarafu visivyo badilika, benki Kuu za mataifa tofauti zinapaswa kuchukua hatua sanjari. Hii ni kwa sababu sera ya fedha wanayoiweka inaweza kuathiri au kuathiriwa na hali za kiuchumi za mataifa wanachama.

Katika kiwango kisichobadilika cha ubadilishaji, viwango vya riba vinahitaji kufanana na (neno linalokosekana) ili kudumisha kiwango cha ubadilishaji. Ikiwa hili halitatokea, nchi yenye kiwango cha chini cha riba itasukuma usambazaji wa pesa zake kwa nchi yenye kiwango cha juu cha riba hadi viwango vya riba vitakapokuwa sawa tena. Hatua hii inaifanya sarafu yenye kiwango cha chini cha riba kuvutia zaidi, jambo ambalo huongeza usambazaji wa fedha kwa nchi. Lakini hii inaweza kusababisha mfumko wa juu wa bei.

Kwa hivyo, wanauchumi wanasema kuwa wakati mzunguko wa pesa baina ya nchi ni shuari, ni bora kupitisha kiwango cha kuelea au kutabanni kiwango cha ndani ya nchi, lakini sio zote mbili. Na hiyo (miongoni mwa sababu nyenginezo) ndio sababu wanaepuka mfumo ambao haubadiliki kikamilifu.

Uchumi unategemea pakubwa matumizi mabaya ya fedha. Katika mfumo huu, nchi inaweza kuruhusu ubadilishanaji wake kushuka kwa kiwango chochote kinachohitajika ili kumaliza soko la ubadilishaji wa fedha za kigeni, jambo ambalo Kiwango cha Dhahabu hakitaruhusu.

Na ingawa inajadiliwa kuwa kiwango cha ubadilishanaji kinachoelea kinazipa sarafu uhuru zaidi, mjadala umeonyesha si rahisi sana kuwa suala la uhuru - hasa wakati nchi duniani kote zinapokea na kulipa madeni yao kwa dolari (ambapo zinahitaji kuwa dolari katika akiba zao za kigeni).

“Takriban asilimia 70 ya nchi zina dolari ya Marekani kama sarafu yao tegemezi au ya maregeo. Katika muktadha huu, akiba ya dolari za Marekani ni muhimu katika kudhibiti kiwango cha ubadilishanaji. Nchi zinazofungamanisha kiwango cha ubadilishanaji wao na dolari ya Marekani ni pamoja na Amerika ya Kusini, China, sehemu kubwa ya Asia, Afrika na uliokuwa Muungano wa Kisovieti. Ufungamanishaji huu mara nyingi huchochewa na sera za kigeni na mafungamano ya kiusalama na Marekani.” (Chanzo)

Kwa hivyo, Marekani hutumia mfumo huu kudumisha nguvu zake.

Katika mfumo huu, uhalali wa Marekani (ambao unatokana na njia nyingi, ikiwemo umuhimu wao kwa mfumo wa kimataifa), unawaruhusu kudumisha nguvu ya dolari.

Thamani bandia ya dolari ni kubwa zaidi kuliko ambavyo ingekuwa katika Mfumo wa Dhahabu, na kwa sababu ya mahitaji yake, haswa wakati wa mgogoro, Marekani inadumisha msimamo wake kama mtawala wa ulimwengu.

“Ongezeko la kimuundo la mahitaji ya kushikilia mali salama za Dolari ya Marekani linaongezewa na mahitaji ya mzunguko wakati wa matatizo ya kiuchumi, si haba nchini Marekani. Ingawa mgogoro wa kifedha wa 2008 ulijikita katika uchumi wa Marekani, kiwango cha ubadilishanaji cha dolari ya Marekani kilipanda wakati wa mgogoro wa mtiririko wa eneo salama kwa sababu mali za dolari ya Marekani ilibakia kuwa dau salama zaidi.” (Chanzo)

Dolari ya Marekani bado ndiyo sarafu kuu katika miamala mingi ya kiuchumi- ikijumuisha utoaji wa deni la kimataifa, deni na malipo, akiba za fedha za kigeni, kanuni za udhibiti wa viwango vya ubadilishanaji, na mauzo na malipo ya fedha za kigeni.

Na “inachangia asilimia 63 ya dhamana za madeni ambazo hazijalipwa duniani kote. Masoko ya mitaji ya Marekani hutoa makao kwa kiasi kikubwa cha akiba duniani, kuanzia akiba ya fedha za kigeni ya China hadi akiba za kustaafu ya Watu wa Australia. Utoaji wa deni la dolari ya Marekani huruhusu makampuni ya ndani na nje kuyachota masoko ya kina ya mitaji na ya pesa taslimu ya Amerika. Mtaji wa dolari ya Marekani unaokusanywa unaweza kutumika kwa urahisi zaidi kuliko fedha zinazokusanywa katika sarafu nyinginezo.” (Chanzo)

Haya yote yanawapa nguvu ndani ya mfumo wa sasa, ambayo hawangeweza kuyafurahia katika mfumo wa dhahabu kwani unategemea uwezo wao wa kuhakikisha kuwa kuna mtiririko endelevu wa dolari kote ulimwenguni.

Kurudi nyuma itakuwa ni hasara yao.

Kuregea kwenye Mfumo wa Dhahabu - hata kwa sura iliyozimuliwa - itahitaji mageuzi makubwa. Ikiwa wataiona faida katika hili, ni jambo ambalo hawatasita kulifanya. Lakini kuhamia kwenye Kiwango cha Dhahabu kutahitaji nchi zengine kufanya vivyo hivyo, ambapo hili litakuja na mkusanyiko wa matatizo yake wenyewe.

Na kuhamia kwenye mfumo ambapo dolari inaegemezwa kwa dhahabu itamaanisha kupunguza uwezo wao wa kuuchakachua uchumi. Ingewaweka pia katika hali mbaya kwa sababu Marekani ingehitaji kuwa na dhahabu ya kutosha ambayo wanahisi kujiamini katika kuhifadhi nafasi yao ya ulimwengu udhibiti katika mfumo wa ulimwengu- ambayo hawana. Hii ndiyo mojawapo ya sababu kuu kwa nini walihama kutoka kwa ‘Kiwango cha Dhahabu cha Ubadilishanaji’ hapo awali.

“Wakati wa Makubaliano ya Bretton Woods, Marekani ilishikilia takriban robo tatu ya hifadhi rasmi ya dhahabu duniani. Lakini baada ya hapo hisa ya Marekani ya pato la dunia ilipungua na hivyo ndivyo hitaji la dolari lilivyopungua, na kufanya ubadilishaji wa dolari hizo kwa dhahabu kuhitajika zaidi. Kudorora kwa mizani ya kibiashara ya Marekani, pamoja na matumizi ya kijeshi na misaada ya kigeni, kulisababisha usambazaji mkubwa wa dolari duniani kote. Wakati huo huo, ugavi wa dhahabu ulikuwa umeongezeka kidogo tu. Hatimaye, kulikuwa na dolari nyingi zaidi nje kuliko dhahabu iliyokuwa Marekani. Nchi ikawa katika hatari ya kuendesha sarafu kwa dhahabu na imani ikapotea katika uwezo wa serikali ya Marekani kutimiza wajibu wake, na hivyo kutishia nafasi ya dolari kama sarafu ya hifadhi.” (Chanzo)

Na sasa, wakati “migodi ya Marekani ina dhahabu nyingi, sisi sio mzalishaji mkuu zaidi...Wasambazaji wakubwa zaidi wa dhahabu wangekuwa na udhibiti zaidi juu ya sera yetu ya fedha.” (Chanzo)

Hili linafanywa kuwa baya zaidi na ukweli kwamba Marekani ina deni kubwa la pesa kwa nchi zingine kama China na Japan (ambazo zilinunua deni la kitaifa la Marekani). Iwapo Marekani itarudi kwenye Kiwango cha Dhahabu, yaani itaegemeza sarafu yao kwa dhahabu, basi nchi hizi zinaweza kuuliza deni linalodaiwa nazo kulipwa kwa dhahabu.

Ni kweli kwamba nchi nyingine zenye nguvu zina nia ya kudumisha mfumo wa sasa, kwani zinapata nguvu zao kutoka kwake. (Na hilo linamaanisha kudumisha utawala wa Dolari) lakini nguvu hiyo, na riba hiyo imefungamanishwa na dolari kama sarafu ya fiat - kwani kuwa na sarafu za fiat kuna faida kwao pia. Kwa mfano, China pia imepata njia za kuutumia uchumi kwa manufaa yao katika biashara.

Nguvu zao zinategemea ukosefu wa thamani ya kindani, kwa hivyo wakakomesha Kiwango cha Dhahabu

Kufa kwa Kiwango cha Dhahabu kulianza mapema miaka ya 1900. Marekani, kwa makubaliano ya nchi nyingine, ilichukua hatua za kuondoka kutoka kwa Kiwango cha Dhahabu hadi sarafu ya fiat, na kuongeza nguvu zao na ushawishi katika Mfumo wa Kibepari.

Nchi zilianza kuondokana na Kiwango cha Dhahabu walipoanza kukosa akiba ya dhahabu na kutaka kuchapisha kiasi kikubwa cha fedha za karatasi ili kuunga mkono juhudi zao za vita. Lakini mabadiliko kutoka kwa Sarafu iliyoegemezwa kwa Dhahabu kwenda kwa Sarafu ya Fiat hayakutokea moja kwa moja.

Mojawapo ya sababu kuu za kuyumba kwa uchumi ni kwamba, haswa baada ya Vita vya Dunia kuanza, hakuna nchi iliyofuata muongozo wa Kiwango cha Dhahabu, kama inavyoonyeshwa kupitia maamuzi ya kisera ambayo zilifanya wakati huo, ambayo yalipunguza matumizi ya dhahabu katika miamala yao ya kiuchumi. Kwa hivyo, walihama kutoka Kiwango cha Dhahabu hadi Kiwango cha Ubadilishanaji wa Dhahabu, ambacho pia kililazimisha nchi (muhimu zaidi Marekani) kufanya machaguo kati ya malengo yake ya kimataifa na ya ndani. Na mnamo mwaka wa 1933, na kwa kushusha thamani ya dolari, Marekani ilianzisha kanuni kwamba malengo ya sera ya ndani yalikuwa na ubora juu ya maagizo ya kiwango cha dhahabu.

Pendekezo la awali la Kiwango cha 'Ubadilishanaji' wa Dhahabu lilitolewa kwenye Kongamano la Genoa la 1922. Liliundwa ili kudhibiti dori ya dhahabu na kudhibiti mahitaji yake, na kutoa wito wa kuundwa kwa benki kuu katika nchi ambazo hazikuwa nazo, na kuanzisha hifadhi za sarafu kama ubadilishanaji wa fedha za kigeni badala ya dhahabu. Mfumo huu ulifeli, mnamo 1931, katikati ya Mporomoko Mkuu wa Kiuchumi, huku Uingereza ikijitoa kwenye mfumo huo na nchi zengine kufuata.

Kisha baada ya Vita vya Pili vya Dunia, mataifa ya kibiashara yalifanya jaribio jengine la kurekebisha mfumo wa malipo wa kimataifa, kwa kuzingatia kanuni za Mkutano wa Genoa. Mfumo wa ubadilishanaji wa 1944 ulijulikana kama mfumo wa Bretton Woods wa viwango vya ubadilishaji vya kudumu. Lengo lilikuwa kukuza ushirikiano wa kimataifa; kukuza uthabiti wa viwango vya ubadilishanaji, kuondoa vidhibiti vya ubadilishanaji na vizuizi vya biashara na mtaji, na kuzuia sera za omba-jirani yako.

Makubaliano hayo yalihusisha sarafu na Dolari ya Marekani, ambayo yalifungamanishwa na dhahabu. Dolari za Marekani zilibadilishwa kwa dhahabu kwa kiwango kisichobadilika cha dolari 35 kwa pauni moja ya dhahabu, na Marekani ilikuwa na jukumu la kuiweka bei ya dhahabu ya dolari kuwa ya kudumu na ilibidi kurekebisha usambaaji wa dolari ili kudumisha imani katika ubadilishanaji wa dhahabu wa siku zijazo.

Makubaliano hayo pia yalianzisha Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) ili kudhibiti mfumo huo; ukifanya kazi kama mkopeshaji wa mwisho na kuzuia marekebisho ya kupanda kwa thamani ya sarafu. Nchi ilibidi kudumisha kiwango cha ubadilishanaji ambacho kiliwekwa kuhusiana na dolari ya Marekani, na kutegemea kwa muda kukopa kutoka IMF kufanya mabadiliko hadi wastani. Kila nchi ilipaswa kufafanua sarafu yake kuhusiana na dolari ya Marekani na kuiweka kiwango stahiki na msambao wa asilimia ±1 sawa na pointi za dhahabu za mfumo wa kale wa dhahabu; kila nchi iliruhusiwa kushusha thamani hadi asilimia 10 ikiwa ni italazimika kwa ukosefu wa usawa wa kimsingi. Na marekebisho zaidi ya asilimia 10 yalipaswa yaidhinishwe na IMF.

Wakati Marekani ilipoamua kuiegemeza dolari kwenye Kiwango cha Dhahabu, ilikuwa ni kwa manufaa yao. Walishikilia idadi kubwa ya akiba ya dhahabu ya benki kuu ya dunia. Lakini wakati utawala wa Nixon ulipoingia madarakani mnamo 1969, waligundua kuwa uchumi wa dunia ulikuwa mkubwa sana. Kila mtu alitaka dolari, hivyo Hifadhi ya Shirikisho ilikuwa ikichapisha dolari nyingi. Kwa hiyo, kulikuwa na dolari mara nne katika mzunguko kuliko dhahabu katika hifadhi. Kiwango cha dolari 35 kwa pauni moja ya dhahabu kilikuwa kizuri mwaka wa 1944, lakini hakikuwa kimebadilika, kwa hiyo kufikia 1971, dolari ilitathminiwa thamani ya juu. Hiyo ilimaanisha uagizaji kutoka nje ulikuwa wa bei nafuu sana, na mauzo ya nje yalikuwa ghali sana. Na kwa sababu hiyo, walihisi nakisi yao ya kwanza ya biashara tangu karne ya 19 na pia walikuwa wakikabiliwa na matatizo ya ajira. (Chanzo)

Walipotupilia mbali Kiwango cha Dhahabu mwaka wa 1971, “viwango vya dhamana za Marekani zilizoshikiliwa na benki kuu za kigeni vilikuwa haviwezi kudumishwa na Marekani kwa kutumia sarafu iliyoegemezwa kwa thamani ya dhahabu.” Na nchi kama Uingereza zilikuwa zikitaka dolari zao zilipwe kwa dhahabu.

Lakini licha ya ukweli kwamba fedha za Marekani zilikuwa katika hali ya hatari, sehemu nyenginezo duniani hazikuwa na sababu ya kuondoka kwenye dolari (hasa kwa vile muundo wa mfumo wa kimataifa ulikuwa tayari unatekelezwa kipindi hiki). Zilikuwa ndio chaguo pekee la ubadilishanaji wa kimataifa na Marekani ilikuwa na udhibiti muhimu wa kisiasa juu ya taasisi za fedha ambao ungewezesha mtiririko wa mtaji unaohitajika na sarafu ya hifadhi ya kimataifa.

Kama Mfumo wa Dhahabu uliachwa hapo awali, je, utafanya kazi katika Khilafah?

Hakuna sababu kwamba Kiwango cha Dhahabu kisifanye kazi chini ya Khilafah. Kama tulivyojadili, matatizo ya sarafu iliyoegemezwa kwa dhahabu/fedha yamo kwenye mfumo, na jinsi nchi zilivyochagua kutumia vibaya Kiwango cha Dhahabu kwa manufaa yao.

Tunapaswa kufahamu kwamba katika Uislamu haturuhusiwi kuwa na sarafu ya fiat. Pesa yetu inapaswa kuegemezwa 100% na dhahabu na fedha, kwani tutakuwa na kiwango cha madini mbili. Kwa hivyo, tofauti na sarafu inayotumika ulimwenguni leo, Bait ul-Mal (Hazina ya Dola) haitaruhusiwa kuchapisha pesa zozote isipokuwa iwe na viwango vinavyolingana vya dhahabu na fedha katika hifadhi zake.

Pia tutakuwa na sarafu moja ndani ya nchi na kimataifa. Kwa hiyo, watu walio ndani na nje ya Khilafah wataamiliana katika vitengo sawa tofauti na hali ilivyo leo. Kwa kuhakikisha kwamba fedha za ndani na za kigeni ni sawa kwa miamala yote katika Khilafah, tutaoa ustawi kwa sarafu yetu ya madini mbili.

Na kwa kutumia mfumo wa dhahabu na fedha, tutaongeza wingi wa fedha katika mzunguko kwa ajili ya miamala. Hii ni kwa sababu kuna madini mbili ya thamani katika mzunguko kinyume na moja. Hii itaondoa hofu ya kuhodhi sarafu ya madini inayopatikana sokoni, ambayo, nayo itachangia utulivu wa bei. Inawezekana kuwa na utulivu wa bei unapotumia sarafu ya madini moja, lakini kutakuwa na utulivu mkubwa zaidi tunapotumia kiwango cha madini mbili.

Upatikanaji wa dhahabu na fedha hautakuwa tatizo kwani ardhi za Waislamu zina dhahabu; tatizo ni kuibiwa tu na makampuni binafsi na serikali za Kibepari. Lakini kama Waislamu, tunaelewa kwamba dhahabu na fedha, zinazopatikana katika ardhi za Waislamu, ni mali ya Ummah unaosimamiwa na dola. Dola itashughulikia uchimbaji wa dhahabu na fedha, sio tu kwa sababu sarafu halali inaegemezwa juu yake. Hii ni kwa sababu madini ya chini ya ardhi yameainishwa kama mali ya umma. Kwa hivyo, pia tutakuza uwezo wetu wa utengenezaji na kadhalika ili kuhakikisha kuwa tunadhibiti kikamilifu sarafu yetu. Ukweli kwamba dhahabu na fedha ni mali ya umma hufanya kuwa vigumu kwa makampuni binafsi kuchukua umiliki wa dhahabu, au kuihifadhi ili kuongeza bei na kuitumia kwa faida yao wenyewe.

Bait ul Maal basi itasimamia uchumi, kutabikisha na kufanya kazi kwa mujibu wa sheria za Uislamu. Kwa mfano, ikiwa bei ya bidhaa fulani itaongezeka katika jimbo la dola, basi dola lazima iiregeshe katika hali yake ya usawa kwa kusafirisha bidhaa kutoka mikoa mingine na kuregesha usambazaji wake katika masoko. Hili linachukuliwa kuwa ni uchungaji wa mambo ya Ummah, na wameharamishwa kufunga bei maalum.

Hivyo basi, sarafu itatumika kwa ajili ya kuboresha maisha ya raia ndani ya ardhi za Khilafah, na si kuziweka mifuko mwa taasisi fisadi na kuhakikisha ukoloni unaendelea kote duniani.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Fatima Musab
Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu