Ijumaa, 20 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 ‘Mama’ Wasiyewahi Kuwa Naye…

Ni mara ngapi macho hayo makali yametilia shaka hadhi yake? Na ni mara ngapi, wanawake hawa walio kiguu na njia masaa ishirini na nne kwa wiki, juhudi zao zimedunishwa kwa kuwa tu ‘mke nyumbani’?

Je, hali ni nzuri zaidi kwa kina mama wanaofanya kazi?

Si kweli! Wanavumilia mzigo wa matarajio yasiokuwa ya kihakika – wote walio ndani ya nyumba na nje. Pamoja na msururu wa tuhuma, wanaonekana kama ‘washukiwa’ katika jukumu lao la mama na mke!

Kina mama wanaofanya kazi dhidi ya mke nyumbani – hakuna la kusitisha mdahalo huu katika upande wa kuvunjika kwa kasi muundo wa kijamii na kifamilia. Hakuna chochote kizuri au kibaya kinachohusishwa na hadhi ya kina mama – iwe wanafanya kazi au la. Hawapaswi kuhukumiwa kupitia fikra iliyojifunga iliyopo katika jamii yetu, ambapo kila Tom, Dick na Harry (yaani watu jumla) wanawabandika majina kulingana na hawaa na matakwa yao.

Lakini, kabla ya kufikia hatma ya kisawa, twahitaji kufahamu maudhui haya katika hali yake ya kihakika.

Si muafaka kujadili juu ya je anastahili kwenda kufanya kazi au la. Tatizo haliko katika kufanya au kutofanya – lipo katika kukiuka kwake mipaka ya kimajukumu kwa mwengine. Tatizo huja wanawake wanapo bwagwa jukumu lao msingi walilotengewa – la mke na mama – kwa ajili ya kutafuta maisha ya kimada yasiyokuwa ya kawaida pamoja na uhuru wa kifedha; maneno haya yanaweza kusikika kama ya kuvutia masikio, lakini nyuma ya kioo upo ukweli mzito unao chukiza…

Natija zake ziko wazi kwetu sisi kuziona na kujifunza kutokana nazo. Kuvunjika kwa familia, watoto wakaidi, ukosefu wa furaha na kutoridhika zimetanda.

Zamani, wanawake hawaku changanyikiwa kuhusu jukumu lao, wawe wanafanya kazi au la. Alitambua kuwa jukumu lake msingi ni kuchunga familia yake, mumewe na kulea watoto wake. Kwa masikitiko kwa kutokea kwa mapinduzi ya kiviwanda, ufahamu huu ukabadilika baada ya vita vya kwanza vya dunia, ambapo mfumo huu wa kimaslahi wa kirasilimali uliwatoa wanawake majumbani mwao, ukawafanya watumwa kifikra kupitia kuwapa 'uhuru', na kuwasukuma katika ajira ili nao wachangie uzalishaji.

Kwa sasa, wanawake wako nje kuinufaisha serikali. Serikali iko juu katika kiwango cha uzalishaji (GDP), wanawake wanatengeza pesa ambazo hawakuwa nazo mwanzoni, pato la mume na mke limeinua kiwango cha maisha kuwa juu wakati wote, huku jukumu la mama likipotea machoni.

Kuna msemo wa kale usemao: "ukimuelimisha mwanamke, umeelimisha kizazi kizima… kwa hivyo, sasa wanawake wameelimika sana, wamefuzu na wamekombolewa pia, ilistahili basi wakilee kwa muangaza kizazi chote… lakini ukweli unasaliti hili. Vijana wa leo wana habari tofauti ya kuhadithia iliozingirwa na mtandao wa majanga ya kutojitambua, upweke, kuchanganyikiwa, madawa ya kulevya, mahusiano yasio halali, msongo wa mawazo, kujiuwa, matatizo ya kiakhlaqi, uhalifu, wizi nk.

Je, ni kitu gani kilichokoseka?

Kuna nukuu moja nzuri iliyowahi kusemwa na swahaba mmoja, walipokuwa katika msafara wa kivita kwenda kueneza ujumbe wa kiislamu, "Nimekuja kuwakomboa kutoka katika kumuabudu mja kwenda katika kumuabudu muumba wa mja"

Hapa ndipo tatizo lililopo: maneno haya ni ukumbusho kamili wa hali ya wanawake leo ambapo wamewaruhusu waja kama wao kuwatia thamani yao – mafanikio yao na kufeli kwao. Wanaume wamewakalia juu yao, huku wakiwatawala kama bwana wao. Wamewaruhusu wanaume hawa kuwaendesha – hisia zao, miili yao, fikra zao, nafsiya zao, matakwa yao, na hawaa zao.

Tangu lini wanaume hawa wachafu, wanaoendesha serikali wamekuwa kigezo chetu? Tangu lini wamekuwa ndio wanaotufafanulia sera zetu? Tangu lini wamekuwa ndio watunzi wetu wa kanuni? Tangu lini jinsia ya kike imekuwa dhaifu kwetu? Tangu lini kuwa kwetu kina mama kikamilifu imetudunisha?

Badala ya kumuacha Mola wetu, Allah (swt) kutufafanulia mambo yetu, wanawake wakaanza kujipima thamani yao kwa kujilinganisha na wanaume, kwa kuitikia mwito wa kile serikali inacholingania, na kile vyombo vya habari vinavyosema. Wakadhani kuwa ili kufikia kilele, ni lazima awe kama mwanamume, apate pato kama la mwanamume, avae kama mwanamume, na adhibiti hisia kama mwanamume. Hapo ndipo akaanza kufuata vitu kwa upofu: ikiwa mwanamume aweza kufanya, yeye pia aweza kufanya; huu ndio wimbo. Akaanza kujifakhiri kwa kuitwa dume-jike! Kimakusudi au kwa kutokusudia, hisia hii ikaanza kumzunguka, ya kwamba kile walicho nacho wanaume ndicho kizuri zaidi – kizuri zaidi kuliko kuta nne za nyumba yake na watoto wake.

Allah (swt) amempa mwanamke fadhila ya kipekee ya kuwa mama… kwa nini jambo hili sio tena chimbuko la fahari yetu?

Mtume (saw) atwambia:

«الجنة تحت أقدام الأمهات» “Pepo iko chini ya miguu ya kina mama.”


جاء رجل إلى رسول الله e فقال‏: يا رسول الله من أحق الناس بحسن صحابتي؟ قال: »أمك« قال: ثم من؟ قال: ‏»أمك« قال: ثم من؟ قال: »‏أمك« قال: ثم من؟ قال: »‏أبوك« ((متفق عليه)).

Alikuja mtu kwa Mtume wa Allah (saw) akamuuliza, 'ni nani miongoni mwa watu anayestahiki usuhuba mzuri kwangu?' Mtume (saw) akasema: "mamako", akauliza tena, 'kisha nani?' Mtume (saw) akajibu: "mamako", akauliza tena, 'kisha nani?' Mtume (saw) akajibu: "mamako", akauliza tena, 'kisha nani?' Mtume (saw) akajibu: "babako" (Bukhari na Muslim)

Ukweli wa mambo ni kuwa tumesahau kile Allah (swt) alichotupa ndio bora kwetu. Jamii imetutaka tutoke majumbani mwetu, kuwaacha watoto wetu, tukae ndani ya ofisi tuwe mashini za kutengeza pesa. Na sisi wanawake, pasi na majuto yoyote, tukapiga makamama. Tumekubali ghururi ya jamii – uhuru wa kifedha juu zaidi kuliko kulea watoto wetu, ambapo kwalo kizazi cha binadamu hubakia hai.

Ni kitu gani wanawake hawa walichopata hatimaye?

Watoto wakustaajabisha, kuvunjika kwa nyumba, na kufilisika kinafsi na kihisia. Ufukara wa nafsi zao uko katika aina tofauti tofauti – la muhimu zaidi ni katika malezi ya watoto, ambalo kwalo kizazi cha binadamu hubakia hai.

Hii ndio sababu, twaona msururu wa matatizo miongoni mwa watoto – ni vipi mtoto ataweza kumpenda mamake, wakati hajawahi kuwa naye? Wanalolijua ni jina pekee!

Wazazi leo wanalalamika kutelekezwa umri wa uzeeni, je hawakumbuki namna walivyo athiri pia hamu ya mtoto kwao katika miaka ya utotoni mwake yaani kukosa makini. Jinsi gani alivyo pigana na upweke wakati wao wakitengeza pesa…

Je chekechea au mayaya, wanaweza kuchukua nafasi adhimu ya mama kwa mtoto wake? Natija yake, hili huathiri ukuaji wa mtoto kihisia na kijamii. Tabia isiyokuwa salama na ya kihuni ya mfanyikazi humuathiri mtoto kisaikolojia.

Twahitaji kutafakari tena upya – ni nani anayetufafanulia majukumu na masuuliya yetu msingi, ni yule aliye tuumba, au miondoko iliyobuniwa na watu wasiofikiri ili kutimiza ulafi wao?

Twahitaji kufahamu, watungaji sera hawa wa kirasilimali, wanawatumia wanawake, kwa maslahi yao wenyewe. Hawako kuwajali wanawake bali kujali faida. Kama kweli wanazingatia kuhusu kupewa uwezo mwanamke, mbona basi hutuoni msururu wa maraisi wanawake?

Kumbuka, ni Allah, ndiye aliye tukirimu kwa ule uhalisia wetu kuwa kina mama, waliotukuzwa zaidi.

Mwanamke mmoja alimwambia Mtume (saw), 'Ewe Mtume wa Allah, umewapa bishara wanaume na sio wanawake'. Mtume (saw) akasema,

«أفما ترضى إحداكن أنها إذا كانت حاملا من زوجها وهو عنها راض أن لها مثل أجر الصائم القائم في سبيل الله، فإذا أصابها الطلق لم يعلم أهل السماء وأهل الأرض ما أخفي لها من قرة أعين، فإذا وضعت لم يخرج منها جرعة من لبنها، ولم يمص مصة، إلا كان لها بكل جرعة وبكل مصة حسنة، فإن أسهرها ليلة كان لها مثل أجر سبعين رقبة تعتقهن في سبيل الله» “Je haridhiki mmoja wenu kwamba anapokuwa na uja uzito wa mumewe na huku yuko radhi na yeye ana ujira mfano wa aliye funga na aliye simama katika njia ya Allah, anapopatwa na uchungu wa uzazi watu wa mbinguni na ardhini hawajui kilichofichika tumboni mwake kinachomfurahisha yeye machoni. Na anapojifungua hakuna tone la maziwa linatoka na hakuna tone la maziwa mtoto analo nyonya isipokuwa atapa ujira wa jema moja. Na mtoto anapomkesheza usiku atapata ujira mfano wa aliye waacha watumwa sabiini huru kwa ajili ya Allah" [Tabarani]

Kulingana na uislamu, jukumu msingi la mwanamke ni mama na mjengaji nyumba kwa sababu ni kupitia kitendo hichi ndipo kizazi husimamishwa…

"Kina mama hucheza dori kubwa katika kuunda kizazi. Kila mama anavyo kuwa mzuri katika kulea watoto wake, ndivyo umma unavyo faulu kuundwa na unavyofaulu kuzalisha mashujaa. Ni nadra kuona mwanamume imara isipokuwa nyuma yake kuna mwanamke imara aliye acha suluki zake ndani ya shakhsiya yake kwa njia ya maziwa ambayo kwayo alinyonyeshwa na harara ya kikumbatiwa kila alipohitaji hifadhi." Sheikh Abdullah Azzam (Rahimahullah).

Ni muhimu sana kwa wanawake leo kuunganisha vitendo vyao na hukmu za kisheria kujilinda na fitna za nje. Tusiwalee watoto wetu kwa kuwa tu ni ada iliyowekwa katika jamii, hivi ndivyo wanawake walivyokuwa wakifanya kwa makarne, bali ni kutambua kuwa ni jukumu ambalo Allah (swt) ametupa sisi, ambalo tutahesabiwa, na kwa amali zetu ndogo, tutalipwa na Allah (swt). Na hii ni ibadah kwetu.

Sio waislamu pekee, hata wasiokuwa waislamu wanajua umuhimu wa wanawake kukaa majumbani na kulea watoto wao. Mmoja katika mjumbe wa bunge la congress la Amerika alisema kuwa, 'Kwa kuwa Allah amempa uwezo wa kuzaa, hawapaswi kuwaacha na kwenda kufanya kazi.  Ni nani atakaye kaa nyumbani kuwachunga?'

Samuel Smilles, muanzilishi wa tafakari ya uzazi upya (renaissance thinking), alisema pindi serikali zilipoanza kuwaajiri wanawake, licha ya mchango wao kwa utajiri wa taifa, ilisababisha matokeo ya kuumiza kila ongezeko na tegemeo la wanawake katika nguvu kazi lilivyozidi. Ilishambulia muundo wa maisha ya nyumba, ikawapokonya watoto mama zao, waume wake zao, na watoto jamaa zao, iliwapokonya wanawake haki yao na majukumu yao kwa familia zao.

Mwanafalsafa wa kiuchumi, Jules Simon alisema katika majarida ya journal v. 17, wanawake wameingizwa katika kila sekta kuanzia mitambo ya ushonaji mpaka katika taasisi za benki ilhali wengi wa wanawake hawa walikuwa na uwezo mkubwa juu ya waajiri wao lakini wakalipwa pauni chache. Mume sasa akawa amepata faida ya kimada kwa kuwa na mke anayepata mshahara; huku wakati huo huo mke ikitishia kuchukua nafasi yake katika nguvu kazi. Pili alitaja kuwa waajiri wamewavua wanawake majumba yao na familia zao.

Daktari Ida Ellen adai katika matokeo ya utafiti wake kuwa kuna uhusiano mkubwa baina ya idadi ya wanawake wanaofanya kazi na kiwango kikubwa cha uhalifu katika jamii hiyo. Alihitimisha kwa kusema kuwa mzizi wa mgogoro wa kifamilia Amerika na kiwango kikubwa cha uhalifu katika jamii ni kutokana na mwanamke kuacha nyumba yake kwenda kuongeza mara dufu kiwango cha pato la familia. Huku kiwango cha pato kikiongezeka ndivyo kiwango cha maadili kilivyo pungua. Daktari Ellen alitoa wito wa kurudi kwa mwanamke nyumbani kwake kurekebisha jamii na maadili yake, kuwa ndio njia pekee ya kukiokoa kizazi kipya kutokana na muozo.

Bwana Byron, malenga wa kiingereza, adai kuwa wanawake wanapaswa kuhudumia nyumba zao na kuwafundisha dini watoto huku akitahadharisha juu ya matangamano huru baina ya wanawake na wanaume.

Chimbuko la muongozo wetu daima liwe ni Quran na Sunnah, na wala si kile kinachosemwa na jamii. Hebu tusimameni, tujitose, na tusimamishe kizazi chenye shakhsiya za kiislamu, tuwaelimishe watoto wetu kumpenda Allah (swt), kufuata kitabu chake kabla hatujachelewa. Chaguo ni letu pekee, ikiwa twataka starehe za muda za dunia, au pepo ya milele chini ya miguu yetu.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Nilofar Shamsi

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumapili, 12 Aprili 2020 07:36

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu