Jumatatu, 23 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/25
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Sababu za Kuvunjika kwa Familia Miongoni mwa Jamii za Waislamu walioko Magharibi

Ndoa ni moja katika mahusiano muhimu tutakayojifunga nayo maishani mwetu. Ni fungamano linaloathiri na lililokitwa chini ya mafungamano mengine muhimu, kwa mfano mafungamano tutakayokuwa nayo na watoto na wajukuu wetu. Uislamu unatufunza kuwa ndoa ni taasisi ya kisheria ambayo mwanamume na mwanamke wanaweza kuingia katika mahusiano ya ukaribu. Tunapojifunga na mahusiano aina hiyo tunamatumaini ya kujenga mahusiano ya utulivu kwa msingi wa uswahiba ambao si tu kwa ujenzi wa mazingira ya uchajimungu ya malezi ya watoto bali pia ni njia ya kuimarisha mahusiano na Muumba wetu (swt).

«إِذَا تَزَوَّجَ الْعَبْدُ فَقَدِ اسْتَكْمَلَ نِصْفُ الدِّيْنِ فَلْيَتَّقِ اللهَ فِي النِّصْفِ الْبَاقِي» “Mtume Muhammad (saw) ametuambia kuwa mtu anapooa, amekamilisha nusu ya dini na hivyo anatakiwa kumcha Mwenyezi Mungu kuhusiana na nusu iliyobakia." [Al-Tirmidhi Hadith 3096 imesimuliwa na Anas ibn Malik]

Lakusikitisha, uhalisia uliopo leo Magharibi ni kuwa ndoa nyingi ndani ya jamii ya Waislamu zinavunjika na kuishilia katika talaka, na ndoa ambazo bado zimehimili ziko mbali na matumaini tuliyoyataja hapo juu. Utafiti wa mwaka 2000, uliofanyika ndani ya jamii ya Waislamu ndani ya Marekani, uliiweka talaka kuwa asilimia 30. Utafiti mpya unaonyesha kuwa asilimia hii inazidi kukuwa na kwamba matatizo yanayohusiana na kuvunjika kwa maisha ya ndoa yanazidi ndani ya jamii ya Waislamu wanaoishi Magharibi.

Kwa sababu hii, ni muhimu kwamba tunafahamu hatari iliyopo ndani ya mujtama za uhuru (kiliberali) za kimagharibi hususan zinazopelekea talaka. Hivyo basi, tutaweza kujilinda kwa kadri ya uwezo wetu dhidi ya vigezo hivi na kutumaini kupunguza idadi ya ndoa zinazovunjika ndani ya jamii ya Waislamu.

Ufahamu juu ya ndoa unatofautiana pakubwa tunapolinganisha mtizamo wa kiliberali wa kimagharibi na ule wa Kiislamu. Ndani ya Magharibi ndoa ni kitu cha khiyari kuhusiana na mwanamume na mwanamke kuingia katika mahusiano baina yao kwa kuwa uhuru (uliberali) hauzingatii maadili katika ukaribu. Unamuachia mtu binafsi kujiamulia ima kuingia katika ndoa kabla kuingia katika mahusiano au kuwa na mahusiano kabla ya ndoa, mfano ngono ya usiku mmoja au hata mahusiano ya ndani ya ndoa. Hili limefungua milango ya kila aina ya mahusiano yanayoifanya taasisi ya ndoa kuwa dhaifu na kuchukiwa kiukweli. Hii fikra ya kufuata matamanio na kufanya unavyotaka ili kujifurahisha pia inaathiri jamii ya Waislamu. Kwa hivyo tunaona matatizo kila aina kwa nini na lini Waislamu kiukweli wanaingia katika ndoa (mfano msukumo kutoka kwa familia na jamii baada ya kuwa na mahusiano ya nje ya ndoa ya muda mrefu au baada ya mtu kuona kuwa maisha yake yamekuwa "sawa"). Sababu hizi kiasili hazitokani na Uislamu na zinaweza pia kuathiri kufaulu kwa ndoa hususan pale ambapo wanandoa wana sababu tofauti za kuoana.

Wakati ufahamu wa ndoa unapoingia maradhi ya fahamu zisizokuwa za Uislamu, kikawaida hili hupelekea matatizo mengi. Kwa mfano, ndoa ndani ya Magharbi zimekuwa biashara ambazo kupitia kwake kiwanda kikubwa kimechipuza. Kupeana kipaombele juu ya "siku kubwa" hilo pekee limekuwa na athari juu ya jamii ya Waislamu. Pale ambapo eneo la ufanyaji harusi limejaa israfu ya chakula, mavazi ya maharusi, mapambo ya dhahabu na magari ya ghali yanakuwa "jambo la lazima" katika siku hiyo kubwa, wachumba wachanga wengi wanalazimika kuisimamisha harusi yao au kuchukua mikopo ya haramu. Hatima yake ni kuifanya siku ya ndoa kuwa kikwazo katika kushikamana na hukumu za Uislamu. Ziada ni kuwa watu wana lazimisha mahari kubwa na kuwa uzito zaidi kwa wachumba wachanga kuanza maisha ya ndoa. Wakishinikiza zaidi siku ya harusi yenyewe na kuyapa kipaombele mambo ya kimada na kuyasahau maneno ya Mtume (saw) aliposema kuwa:

«أعظم النساء بركة أيسرهن صداقا» “Mmoja (kati yenu wanawake) anayepokea kiwango cha chini cha mahari ndiye mwenye baraka zaidi. [Imepokewa na al-Haakim kutoka kwa Aisha]

Lakusikitisha ni kuwa wachumba wachanga ndani ya Magharibi wanaanza maisha yao ya ndoa wakiwa na madeni makubwa yakiidhuru ndoa yao kwa matatizo ya kifedha kabla hata hayajaanza. Mbegu za kupenda mali (ulafi) huendelezwa katika ndoa pale ambapo wanandoa Waislamu wanapotaka kuwa kama kina "Joneses" au kina "Ahmed." Kulelewa katika mujtama za kimagharibi pia tunajikuta katika ushindani wa matumizi (upapiaji) kiasi kwamba mambo yasiyo lazima yanaharibu maisha ya familia kutokana na kuyaendea mbio mahitaji yasiyomuhimu na kuishi kwa mujibu wa kiwango cha maisha kilichowekwa na wengine!

Zaidi ya hayo, wanandoa hawashauriwi kwa mtizamo wa Kiislamu juu ya ndoa, mitizamo inayohusiana na maadili ya kiliberali ya kimagharibi hupenyezwa katika akili za wanandoa hawa. Mfano, tunaona namna wanawake wanavyowasilishwa kama zana za ngono katika mujtama za kimagharibi zinavyoathiri ndoa kwa ubaya. Wanawake wanawasilishwa kama vyombo vya matamanio na mapicha ya ngono yakisambazwa kupitia biashara ya kujifurahisha na kiwanda cha video za ngono, si tu kwamba tunajenga mujtama ya ngono bali pia tunabuni matarajio ya kirongo kuhusu mahusiano kati ya mwanamume na mwanamke yanavyotakiwa kuwa na ni yupi mwanamke mrembo na mwanamume anayestahili. Wote wanaume na wanawake wanaathiriwa na picha na mawazo haya, kiasi kwamba kuwapelekea kutafuta matarajio haya ya kirongo ndani ya nyumba zao na kuwaondosha humo ikiwa hawafikii viwango hivyo vya kipuzi. Ziada ni kuwa utafiti uliowasilishwa na Muungano wa Amerika wa Masuala ya Kijamii wa mwaka 2016 uliashiria kuwa idadi ya talaka huzidi pale wanandoa wanapoanza kuangalia video za ngono. Kudumu katika ngono na kutizama video za ngono ni tatizo la kweli ndani ya mujtama za Magharibi kama madawa na pombe, tatizo hili kwa masikitiko limeingia kisirisiri ndani ya jamii ya Waislamu pia na kuwafanya wanandoa Waislamu kuwa dhaifu na kupelekea talaka. Kwa kusikitisha, kuna ongezeko la mahusiano kabla ya ndoa katika jamii ya Waislamu na kuzidi kwa talaka kutokana na mahusiano zaidi ya ndoa

Kuna mkanganyiko juu ya majukumu na haki za mume na mke kutokana na fikra zinazohusiana na thaqafa tofauti wanazoishi ndani yake – Thaqafa ya kimagharibi ambayo vijana wengi wanavutiwa na thaqafa ya Mashariki (inayoonekana kuwa ya Kiislamu) ambayo wazee wetu wengi wanaathiriwa nayo. Waislamu mara nyingi wana mchanganyiko wa mawazo yanayoathiriwa na thaqafa zisizokuwa za Kiislamu. Mchanganyiko huu wa fikra ndiyo pia chanzo cha mgogoro kati ya wanandoa. Kwa mfano ikiwa mmoja kati ya wanandoa amebeba mtizamo wa kimagharibi ambao uhuru na usawa wa kijinsia wa wanawake unapigiwa debe, inakuwa tatizo kwa mwanandoa mwengine ambaye amebeba mtizamo wa kimashariki unaomuangalia mwanamke kama mtumwa kwa mumewe ambaye jukumu lake ni kutumikia mahitaji ya mumewe. Kiuhalisia, tunaona mchanganyiko wa fikra ambapo dori ya mchumaji mkate na msimamizi wa nyumba inakabidhiwa wanawake. Kwa hiyo anajipata akibeba mzigo wa kifehda kuisimamia familia na kuendelea kubeba majukumu ya kinyumbani. Hili limepelekea kuvunja thamani ya umama, jukumu adhimu la mwanamke katika Uislamu. Ni muhimu tujifunze kuwa kuna chaguo la tatu: Uislamu –ambao umeweka wazi majukumu na haki za wanandoa wote ndani ya ndoa. Mwanamume ndiye kiongozi wa nyumba na hivyo ana majukumu ya kuisimamia kifedha ili kukimu mahitaiji ya familia yake. Ilhali majukumu ya mke ni kuwa msimamizi wa nyumba na mlezi wa watoto wake. Anaweza kufanya kazi nje ya nyumba lakini haitakiwi kamwe kuliona suala hilo kuwa la lazima. Uwazi katika haki na majukumu ya wote wanaume na wanawake kwa mujibu wa Uislamu ndiyo msingi wa utulivu ndani ya ndoa.

Pamoja na hayo ni kuwa wanandoa Waislamu wanapokumbana na matatizo yao ndani ya ndoa, tunaona kuwa talaka imekuwa jambo la rahisi kama chaguo katika kusuluhisha matatizo yao kama inavyoshuhudiwa katika mujtama jumla ndani ya Magharibi. Katika mujtama za kiliberali, mtizamo ni kuwa ndoa hazitakiwi kudumu kimsingi bali zilitakiwa kuboresha furaha yetu na punde hili linapokosekana, kwa nini tuendelee na mahusiano hayo? Huu ndio mtizamo wa kufikiria unaotokamana na mtizamo wa kiliberali wa kimagharibi juu ya maisha ambapo furaha ya mtu binafsi ndiyo kipaombele kinyume na ahadi na uaminifu.

Mwisho, ni lazima tusisahau kwamba katika Uislamu mke sio mshirika wa mumewe; bali ni mwandani wake. Kuishi kwao pamoja hakukujengwa kwa mujibu wa ushirika bali kwa uswahiba na hukamilika na kuwa kitu kimoja katika nyanja ya maisha. Uswahiba ni pale ambapo kila mmoja anapata utulivu kutoka kwa mwenziwe. Mwenyezi Mungu ameifanya ndoa kuwa ndiyo chimbuko la utulivu kwa wanandoa wote.

هُوَ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ وَجَعَلَ مِنْهَا زَوْجَهَا لِيَسْكُنَ إِلَيْهَا﴿

“Yeye ndiye aliye kuumbeni kutoka katika nafsi moja; na katika hiyo hiyo akamfanya mwenzi wake, ili akae naye kwa utulivu."

[Al-A'raf: 189] 

Imeandikwa Kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Yasmin Malik
Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumapili, 12 Aprili 2020 07:12

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu