Alhamisi, 06 Ramadan 1446 | 2025/03/06
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Ramadhan, Fursa ya Kutafakari na Kubadilika
(Imetafsiriwa)

Mwezi wenye baraka umetujia, mwezi ambao kuwasili kwake tunafurahia licha ya maumivu, huzuni, na majanga tunayopata. Mwezi ambao baraka na utukufu wake umetajwa katika Aya na Hadith nyingi: ikiwemo kauli ya Mtume, rehma na amani zimshukie, kuhusu usiku wa mwanzo wa Ramadhan:

«وَيُنَادِي مُنَادٍ يَا بَاغِيَ الْخَيْرِ أقْبِلْ وَيَا بَاغِيَ الشَّرِّ أقْصِرْ»

“Na hunadi mwenye kunadi, ‘Ewe mtafutaji wa kheri, songea. Na ewe mtafutaji wa maovu acha.’” Yeyote mwenye kutaka kheri huitafuta na kuifanyia juhudi, na anayetaka shari huitafuta na kuifanyia juhudi, maana yake kila mtu anafanya kazi kulingana na lengo analolitarajia na analotaka.

Ramadhani ni mwezi wa kheri na baraka, na fursa adhimu ya kujitahidi kupata mafanikio ya duniani na akhera. Ni msimu wa utiifu, na uwanja wa kushindana katika mambo ya kheri na kufikia uchamungu ili kupata radhi za Mwenyezi Mungu, ambayo ndio mafanikio ya kweli. Ni mwezi maalum wa fadhila, si kwa sababu tu ni mwezi wa saumu na ibada, bali pia kwa sababu ni fursa adhimu ya kutafakari uhusiano wetu na Mwenyezi Mungu na kutathmini upya mwenendo wa maisha yetu ili kubadilika na kuwa bora zaidi, na kuzingatia malengo yetu ya kweli na kufafanua fahamu ya mafanikio katika maisha yetu, si kwa mtazamo wa Kidunia, bali kwa mtazamo wa kidini, kiroho na kiakhlaqi.

Watu wamegawanyika katika aina mbili: wale ambao wameweka lengo au malengo yao na wanajua nini wanataka na nini watafanya, na wale ambao hawajui jinsi siku zao zitapita! Hii pia hutokea katika Ramadhan: wale ambao wameweka lengo lao na wanajua nini wanataka kutoka kwa Ramadhan na matunda gani wanayotarajia kuvuna. Aina nyingine ni ya wenye kughafilika, kutojali, na wazembe, ambao huvutiwa na vipurukushi mbalimbali vinavyoenezwa wakati wa Ramadhan kutoka kwa chaneli za satelaiti zenye vipindi vyake vya kejeli na visivyo na maana, na wanaopoteza muda wao kwenye mitandao ya kijamii na kukesha na marafiki zao hadi alfajiri bila mafanikio, kisha kulala siku nzima. Miongoni mwao wamo wenye fikra finyo wanaowatendea wengine ubaya kwa kisingizio cha kuwa wamefunga, waliopotea katika upotofu wao na uvunjaji wa sheria ya Kiislamu kana kwamba kufunga ni kujinyima kula na kunywa pekee!!

Tujihadhari na haya yote, kwani yanatupora nyakati bora na malengo bora. Hebu na tuweke malengo yetu ya kufuata njia ya mafanikio kwa kujitahidi kupata ujira na malipo na kupata radhi za Mwenyezi Mungu Mtukufu. Hebu na tutafute Msaada Wake, na tusiwe wanyonge au wenye kubabaishwa. Aliyenyimwa ni yule anayenyimwa ujira katika msimu wa thawabu, na aliyelaghaiwa ni yule anayepoteza bidhaa ya bei ghali kwa bei nafuu.

Hebu na tujiangalie wenyewe, kila mmoja aiangalie hali yake kwa ukweli na uwazi na kuona malengo yake:

Je, tabia zetu zinaendana na hali ya kiroho ya mwezi huu?!

Je, tunafunga mchana kama tunavyopaswa kufunga kwa kujiepusha na kila kinachomkasirisha Mwenyezi Mungu, iwe kwa kauli au vitendo, au kwa vyakula na vinywaji pekee?

Je, tunafanya mambo ya kheri nyakati za usiku, mfano swala, kutukuza, kusifa, kumkumbuka Mwenyezi Mungu nk, au tunafanya mambo ya kupurukushwa tuliyotaja hapo juu ambayo yanawavutia watu wengi ndani ya Ramadhan?!

Je, tunazitafakari aya za Qur’an, au ni kurasa tu tunazosoma na kukimbia kumaliza kusoma bila ya kutafakari, kuakisi, au utekelezaji wa hukmu zake?!

Je, tunaonyesha mshikamano na familia, marafiki na majirani na kutenda ili kutimiza mahitaji ya maskini na wahitaji, hasa wale wanaojizuia kuomba, na wamekuwa wengi sana siku hizi chini ya hali ya sasa, au sote tunasema, “Ewe Mwenyezi Mungu, nakuomba kwa ajili ya nafsi yangu na familia yangu, na mzigo wangu na wasiwasi wangu vinanitosha”?

Kama sote tunavyojua kuwa Ramadhan ni mwezi wa ibada, tusisahau kuwa pia ni mwezi wa uzalishaji na kazi, sio mwezi wa kulala, kutofanya kazi na uvivu. Wapo wengi wanaotumia msimu wa Ramadhan kama kisingizio cha kuacha kazi au kuipuuza, hasa baadhi ya wafanyikazi wa utumishi wa umma. Tunawakuta hawafanyi kazi zao inavyopaswa na ni wavivu. Labda mmoja wao ameshakwambia, “Je, huoni kwamba ninafunga?” Bila kusahau wasiwasi na tabia mbaya kwa kisingizio cha kufunga!!

Ramadhan ni mwezi wa baraka na kheri, ikiwemo kutoa futari kwa waliofunga. Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:

«مَنْ فَطَّرَ صَائِماً كَانَ لَهُ مِثْلُ أَجْرِ الصَّائِمِ، وَإِنَّهُ لَا يَنْقُصُ مِنْ أَجْرِ الصَّائِمِ شَيْءٌ»

“Mwenye kumfuturisha mfungaji, atapata ujira sawa na aliyefunga, bila ya kupunguza ujira wa mfungaji”. Ndio, kuna karamu na meza za iftar, lakini ni watu gani wanaofunga na ni watu gani? Je, ni kwa ajili ya masikini, mafukara, na jamaa, au kwa ajili ya matajiri tu na wale wenye maslahi? Je, karamu zinafanyika kwa ajili ya kumridhisha Mwenyezi Mungu Mtukufu na kupata thawabu za kufuturisha saumu ya mfungaji, au kwa ajili ya kujionyesha, kujikweza, na unafiki?!

Kadhalika Misikiti imejaa wenye kuabudu, na baada ya Ramadhan unaiona mitupu isipokuwa wachache, kana kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ameagiza swala ya jamaa Misikitini ndani ya Ramadhan pekee!!

Hali ya kiroho iko wapi katika mwezi huu mtukufu?!! Uko wapi ukaribu wa kihakika na Mwenyezi Mungu ndani yake?

Vile vile tunavyopamba nyumba zetu kwa furaha kwa kuwasili kwa mwezi uliobarikiwa, ni lazima tupambe nafsi zetu, nyoyo na ndimi zetu ili kuukaribisha; kwa kuzifanya nyoyo zetu kuangazwa kwa imani, upendo, mshikamano na uvumilivu wa kweli, kuwafikiria wengine mema na kuwataja kwa namna inayowapendeza, na kuepuka kuwasengenya, pamoja na akhlaqi na maadili mengi mazuri ya Kiislamu ambayo tunakosa katika miamala yetu.

Ramadhan ni siku chache tu, kama alivyosema Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw):

«رَغِمَ أَنْفُ امْرِئٍ أَدْرَكَ رَمَضَانَ فَلَمْ يُغْفَرْ لَهُ» “Amefedheheka yule ambaye amefikiwa na Ramadhan na kisha hakusamehewa.”

Kwa kumalizia, tunasema kwamba Ramadhan inaweza kufupishwa katika sentensi mbili: “Ramadhan ni fupi na haivumilii uzembe, na kuwasili kwake ni mapito yasiyokubali ulegevu.” Kwa hivyo, wakati wowote tunapohisi uvivu, tukumbuke maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika aya kuhusu kufunga:

[أيَّاماً مَعْدُودَاتٍ] “siku maalumu za kuhisabika.” Ndiyo, ni siku chache na malipo yake ni makubwa na makubwa zaidi tukizikamata vyema. Mwenyezi Mungu atujaalie sisi na nyinyi kuwa miongoni mwa anaowaongoza ili tuzikamate.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu tuwe miongoni mwa wanaotakabaliwa katika mwezi wa Ramadhan na miezi isiyokuwa Ramadhan. Ewe Mwenyezi Mungu tujaalie tufikie Usiku wa Cheo (al-Qadr) na utujaalie tuwe miongoni mwa washindi. Ewe Mwenyezi Mungu tutimizie Ramadhan na uiregeshe kwetu kwa kheri, baraka na ufanisi, na kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na bishara njema ya Mtume Wake, rehma na amani zimshukie kuhusu dola ya Kiislamu itimie. Mwenyezi Mungu atutakabalie utiifu na amali zetu na zenu njema.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Muslimah Al-Shami (Um Sohayb)

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu