- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Washindi na Watakaoshindwa kwenye Uchaguzi wa Agosti Wote ni Mawakala wa Mfumo Uliofeli wa Demokrasia
Habari:
Huku zikiwa zimesalia siku chache kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa Agosti 9, baadhi ya viongozi wa Kiislamu pamoja na Wanazuoni wa Serikali nchini, wamewataka Waislamu kuwafanyia tathmini na kuwahakiki wagombea wa viti tofauti ili kufanya maamuzi sahihi. Imekuwa ni hulka kwa wanavyuoni hawa kupindisha maana ya aya na kutumia vibaya kanuni za kifiqhi kama vile ‘uovu mdogo’ kuwataka Waislamu kushiriki kikamilifu katika uchaguzi.
Maoni:
Kutoa hukmu ya Kiislamu juu ya kushiriki kwenye chaguzi za Kidemokrasia kunatupasa kwanza kuangalia kwa kina maana ya uchaguzi wa Kidemokrasia na hali hii itatubidi tuangalie kile kiitwacho uhalisia wa jambo (Tahqiq il Manat’) yaani ni uchaguzi na nini hasa maana ya Demokrasia kama mfumo wa kiutawala. Uchaguzi ni uwakilishaji ambapo mtu huchagua mtu amwakilishe kwenye kufanya jambo kwa niaba yake. Kinachofanya uchaguzi kuwa halali au haramu sio ule uchaguzi wenyewe kwa dhati yake bali ni kile kinachofungamana nao.
Neno la Demokrasia asili ni mkusanyiko wa matamshi mawili yenye asili ya Kigriki Demos ambao humaanisha watu na cratos ikimaanisha utawala kwa maana ni utawala wa watu. Utawala huu humaanisha wanadamu wanamiliki ubwana (sovereignty) unaowawajibisha watunge kanuni ambazo ndio hutukuzwa kuliko sheria za Mwenyezi Mungu (swt). Hivyo Bunge au baraza la seneti, la wawakilishi au Congress zote katika demokrasia ni taasisi za kutunga kanuni. Sasa Demokrasia huchukua mbinu ya uchaguzi kila baada ya miaka 5 au 4 ya watu kuwachagua watu wawe ni wawakilishi wao katika kazi ya kutunga kanuni. Kwa kifupi chaguzi za Kidemokrasia zinafungika katika kitendo cha kutunga sheria ambacho kinagongana na Uislamu.
Kwa mujibu wa Uislamu, sheria sio miliki ya yeyote yule ila ni ya Mwenyezi Mungu (swt). Yeye Mwenyezi Mungu (swt) ndiye mteremshaji sheria hivyo sheria yoyote ile inayotungwa na mwanadamu haifai na ya kimakosa hata kama inaafikiana na ile ya Mwenyezi Mungu hii ni kwa kuwa kazi ya kuweka sheria si ya yeyote yule ila ni ya Mwenyezi Mungu (swt). Bali Uislamu umewajibisha kufuata sheria za Mwenyezi Mungu (swt). Asema Mwenyezi Mungu (swt):
فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُواْ فِىٓ أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُواْ تَسْلِيمًا
“La! Naapa kwa Mola wako Mlezi! Hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye muamuzi katika yale wanayo khitalifiana, kisha wasione uzito katika nyoyo zao juu ya hukumu utayo toa, na wanyenykee kabisa.” [An-Nisai: 65]
Huu ndio uhalisia wa uchaguzi, hivyo kinachofanya uchaguzi uwe halali au haramu sio uchaguzi wenyewe bali ni kazi inayofungamana nao. Kwa ujumla chaguzi za Kidemokrasia ni kinyume na sheria ya Kiislamu hivyo ni haramu kwa Waislamu kupigia debe na kuunga mkono vyama vya kisiasa vya Kidemokrasia na kushiriki kwa uchaguzi wake. Ni dhahiri shahiri kwamba kufanywa kwa chaguzi za kila mara za kidemokrasia ni jaribio la kuteka nyara hisia za mabadiliko kwa watu kwa mfumo uliofeli tayari. Washindi na wanaoshindwa kwenye chaguzi hizi za Kidemokrasia ni vibaraka wa mabeberu ambao kazi yao msingi ni kuziba aibu za Demokrasia zilizoitumbukiza Kenya na Afrika kwa ujumla kwenye maafa na mizozo.
Baya zaidi ni kuwaona wanavyuoni wa Serikali ambao baadhi yao wamekuwa ni wapambe wa wanasiasa wakipinda matumizi ya maana ya qaida ya “madhara mepesi” wakiwataka Waislamu wasijifunge na sheria za Kiislamu na kufanya kazi ya kuleta mabadiliko ya kweli, yaani kuulingania Uislamu uweze kutawala dunia chini ya Khilafah Raashida kwa njia ya Utume. Kiini cha majanga yanayokabili Kenya sio nani anatawala bali ni anatawalisha kwetu mfumo gani. Maadamu nchi inaendelea kutawaliwa na kanuni na tungo za Kidemokrasia tofauti na sheria za alizoteremsha Mwenyezi Mungu basi hatutoona mabadiliko ya kikweli.
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut-Tahrir na
Shabani Mwalimu
Mwakilishi kwa Vyombo Vya Habari wa Hizb ut Tahrir Kenya