- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Vichwa vya Habari: 26/08/2022
Vichwa vya Habari:
• Ulaya Imefikia Ukingoni: Dola Zapambana Kuzuia Kushuka kwa Uchumi
• Amerika Yatoa Onyo la Vikwazo Dhidi ya Uturuki juu ya Mafungano na Urusi
• Pakistan Yaidhinisha Rasimu ya Makubaliano ya Kupeleka Majeshi kwa ajili ya Kombe la Dunia
Maelezo:
Ulaya Imefikia Ukingoni: Dola Zapambana Kuzuia Kushuka kwa Uchumi
Takriban miezi sita baada ya Vladimir Putin kuamuru wanajeshi wa Urusi kuingia Ukraine, kiwango cha uharibifu wa uchumi wa Ulaya kinadhihirika. Tahadhari za kushuka kwa uchumi zinawaka. Uchumi wa nchi kubwa nne za zoni ya euro - Ujerumani, Ufaransa, Italia na Uhispania - zote zimeshuka utabiri wa ukuaji wa 2023 wa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa, huku mchanganyiko wa vita hivyo na viwango vya juu vya riba ukisitisha shughuli. Nchini Uingereza, mfumko wa bei ni zaidi ya 10% kwa mara ya kwanza katika miaka 40 huku familia zikipambana na kupanda kwa bili za nishati. Benki Kuu ya Uingereza inatabiri mfumko wa bei kufikia kilele cha zaidi ya 13% katika msimu wa vuli baada ya ongezeko jipya la gharama za nishati, wakati uchumi utaanguka katika mdororo wa muda mrefu. Huku Uingereza ikikabiliana na shinikizo la ziada kutokana na kujiondoa katika Muungano wa Ulaya (Brexit), athari za kupanda kwa bei ya nishati, kukatizwa kwa usambazaji, uhaba wa wafanyikazi na ukame pia yanaathiri sehemu zengine za Ulaya. Wachambuzi katika Kitengo cha Ujasusi wa Kiuchumi wanasema maumivu yanaweza kuendelea kwa muda, kwa sababu nchi lazima ziondokane na hidrocarbon za Urusi, na uundaji bidhaa zilizo na uwezo kwa kurudishwa tena upya kama njia mbadala itachukua muda. "Katika muda mfupi ujao tunatarajia kushuka kwa uchumi barani Ulaya katika msimu wa baridi wa 2022-23 kama matokeo ya uhaba wa nishati na mfumko wa bei ulioinuka", EIU ilisema. "Msimu wa baridi wa 2023-24 pia utakuwa na changamoto, na kwa hivyo tunatarajia mfumko wa bei wa juu na ukuaji duni hadi angalau 2024." [Chanzo: The Guardian]
Amerika imetumia kwa ustadi vita vya wakala dhidi ya Urusi nchini Ukraine ili pia kudhoofisha Ulaya. Msingi wa Muungano wa Ulaya ni Ujerumani na Marekani imeilazimisha nchi hiyo kuachana na gesi ya Urusi. Kwa kufanya hivyo, Ujerumani iko kwenye kilele cha maangamivu ya kiuchumi, ambayo yatahujumu vibaya sana mradi wa Ulaya. Kupitia kuudhoofisha Muungano wa Ulaya, Marekani inalenga kubadilisha makubaliano ya kimataifa na EU kwa makubaliano ya nchi mbili na nchi wanachama.
Amerika Yatoa Onyo la Vikwazo Dhidi ya Uturuki juu ya Mafungano na Urusi
Chama kikuu cha wafanyibiashara nchini Uturuki kimethibitisha kupokea barua kutoka kwa Hazina ya Marekani ikionya uwezekano wa kuwekewa vikwazo iwapo itaendelea kufanya biashara na Urusi. Washington inazidi kuingiwa na hofu kwamba serikali ya Urusi na wafanyibiashara wanaitumia Uturuki kukwepa vikwazo vya fedha na biashara vya Magharibi vilivyowekwa ili kukabiliana na uvamizi wa Kremlin nchini Ukraine miezi sita iliyopita. Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin walikubaliana kuongeza ushirikiano wa kiuchumi katika mkutano wa kilele katika hoteli ya ufuoni mwa Bahari ya Black Sea Resort huko Sochi mapema mwezi huu. Takwimu rasmi zinaonyesha thamani ya mahuruji ya Uturuki kwenda Urusi kati ya Mei na Julai ikiongezeka kwa karibu asilimia 50 kutoka takwimu za mwaka jana. Uagizaji mafuta ya Urusi wa Uturuki unapungua na pande hizo mbili zimekubaliana kubadili malipo ya ruble kwa gesi asilia inayosafirishwa nje na kampuni kubwa ya Gazprom inayofungamana na Kremlin. Naibu Waziri wa Hazina wa Marekani Wally Adeyemo alifanya ziara ya nadra jijini Ankara na Istanbul mwezi Juni kuelezea wasiwasi wa Washington kwamba kipote cha watawala wachache wa Urusi na wafanyibiashara wakubwa walikuwa wakitumia vyombo vya Uturuki kuepusha vikwazo vya Magharibi. Mwanachama wa NATO Uturuki - kwa maelewano mazuri na Moscow na Kyiv - imejaribu kutoegemea upande wowote katika mzozo huo na kukataa kujiunga na bogi la vikwazo vya kimataifa. Adeyemo alifuata hilo kwa barua kwa chama cha wafanyibiashara cha Uturuki cha TUSIAD na Chama cha Wafanyabiashara cha Marekani nchini Uturuki akionya kwamba makampuni na benki ziko katika hatari ya kuwekewa vikwazo vyenyewe. Ushirikiano mpana na Urusi unaweza kusaidia uchumi unaodorora wa Uturuki kuelekea katika uchaguzi mkuu mwaka ujao. Erdogan aliwahi kusema kuwa Ankara haiwezi kujiunga na vikwazo vya Magharibi dhidi ya Moscow kwa sababu ya utegemezi mkubwa wa Uturuki kwa uagizaji wa mafuta na gesi asilia kutoka Urusi. "Uchumi wetu ni ule ambao tukiweka vikwazo kwa Urusi vinaweza kuidhuru zaidi Uturuki," mshauri wa sera za kigeni wa Erdogan Ibrahim Kalin alisema mnamo Juni. “Tumechukua mwelekeo ulio wazi. Hivi sasa, Wamagharibi wamekubali hili. [Chanzo: Arab News]
Baada ya kuitumikia Marekani kwa uaminifu katika kupinga maslahi ya Urusi nchini Armenia, Syria na Libya, Marekani sasa inataka kuweka shinikizo zaidi kwa Urusi kupitia Uturuki. Uturuki kwa uratibu wa karibu iliachana na S400, kupeana droni za kuua kwa vikosi vya Ukraine na sasa inaagizwa kukata mafungamano ya kibiashara na Moscow. Erdogan ni mtumishi mtiifu wa Marekani na hatimaye atakubali kuwatumikia mabwana zake Kiamerika.
Pakistan Yaidhinisha Rasimu ya Makubaliano ya Kupeleka Majeshi kwa ajili ya Kombe la Dunia
Baraza la mawaziri la Pakistan limeidhinisha rasimu ya makubaliano ambayo inaruhusu serikali kutoa askari kwa ajili ya usalama katika Kombe la Dunia la kandanda la FIFA nchini Qatar baadaye mwaka huu, waziri wa habari wa Pakistan alisema mnamo Jumatatu. Mukhtasari unaoelezea makubaliano hayo, yatakayotiwa saini kati ya Doha na Islamabad, yaliidhinishwa na baraza la mawaziri, waziri Marriyum Aurangzeb aliambia Reuters, kabla ya ziara ya Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif nchini Qatar. Mukhtasari wa baraza la mawaziri, uliopitiwa na Reuters, ulisema serikali ya Qatar iliomba usaidizi katika masuala yanayohusiana na usalama wa Kombe la Dunia kati ya Novemba 21 na Disemba 18 2022, na kwamba jeshi la Pakistan lilipendekeza kusainiwa kwa makubaliano kati ya mataifa yote mawili kwa kusudi. "Makubaliano yanalenga kufafanua majukumu ya pande hizo mbili, taaluma maalum, na idadi ya wafanyikazi wa usalama watakaotumwa na Pakistan kushiriki katika operesheni za ulinzi na usalama," muhtasari huo ulisomeka.
Afisi ya habari ya serikali ya Qatar haikuthibitisha mara moja au kujibu ombi la kueleza kwa nini Doha imeomba wanajeshi wa Pakistan au watafanya nini wakati wa mashindano hayo. Pia hakukuwa na majibu ya haraka kutoka kwa Kamati Kuu ya Uwasilishaji na Urithi, ambayo inasimamia kuandaa Kombe la Dunia, ikiwemo usalama. Mukhtasari haukutoa maelezo yoyote ya makubaliano kama vile wafanyikazi wangapi huenda wakatumwa. [Chanzo: Reuters]
Makubaliano hayo ya aibu yanaibua maswali mapya kuhusu kujitolea kwa jeshi kulinda Pakistan. Pakistan haihitaji tu jeshi lake kutoa usaidizi unaoendelea kwa wahanga wa mafuriko lakini pia inahitaji jeshi kulinda maslahi yake muhimu. Hii ni pamoja na kulinda mpaka wake na India na muhimu zaidi kuikomboa Kashmir. Hata hivyo licha ya maslahi hayo muhimu jeshi la Pakistan sasa limekuwa bunduki la kukodi ili kuwazuia wahuni wa Kimagharibi kuleta matatizo katika Kombe la Dunia nchini Qatar. Nini kinachofuata? Je, jeshi la Pakistan litapigana na Waislamu nchini Yemen ili kulinda maslahi ya Saudia au pengine baya zaidi litatoa usalama kwa umbile la Kiyahudi katika kuwakandamiza Wapalestina au kulitiisha jimbo lenye utulivu la China la Xinjiang kwa dolari duni!