- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Silsila ya Maswali Yaliyowasilishwa kwa
Amiri wa Hizb ut Tahrir
Sheikh Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah Katika Ukurasa Wake wa Facebook
Jibu la Swali
Biashara ya Mtandaoni (E-Commerce)
Kwa: Hamam Ibrahim
(Imetafsiriwa)
Swali:
Assalam Alaikum Wa Rahmatullah Wa Barakatuh,
Mwenyezi Mungu aubariki wakati wenu, ndugu zangu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu,
Nataka kukuulizeni swali na nataraji kupata jibu lenye ufafanuzi wa kina
Swali: Je, biashara ya mtandaoni (e-commerce) na kampuni ya DXN ya Malaysia inaruhusiwa? Kampuni hii inategemea uuzaji wa virutubisho vya lishe, shampoo, krimu za ngozi...nk. Unapo nununua kutoka kwake kiasi fulani, inatoa punguzo (discount). Pindi pointi zako zikifika 100 inakupa punguzo la asilimia sita. Kadiri unavyopata pointi zaidi, ndivyo inavyokupa punguzo kubwa zaidi, na pointi hizi hubadilishwa kuwa kiasi cha pesa ambacho huhamishiwa kwako ama kwa njia ya bahasha au barua ambayo hutolewa kwako kila mwezi, au kuhamishiwa kwenye salio (balance) lako la benki. Nataka kutaja kwamba unaweza kuongeza wanachama kwenye kampuni hii, kila mwanachama anayenunua kutoka kwa kampuni hii anapata pointi, na kwa kurudi unapata pointi kwa sababu mwanachama huyu alisajiliwa kupitia wewe. Bila shaka, unaweza kusajili idadi ya watu unaotaka, na kadiri watu hawa wanavyopata pointi zaidi, ndivyo pointi zako zinavyoongezeka. Kwa hivyo, salio la pesa zilizohamishwa kwako zinaongezeka, na mchakato huu unaendelea kukua hadi uweze kuwa mshirika katika kampuni hii na kupata faida kubwa. (Tafadhali someni kwa makini kuhusu kampuni hii na munipe jibu la kina kuhusu hilo) Shukran
Jibu:
Wa Alaikum Assalam Wa Rahamtullah Wa Barakatuh,
Hapo awali dada mmoja alituuliza swali kama hili kuhusu kuamiliana na kampuni ya DXN ya Malaysia, na tulilijibu mnamo 7/11/2024 M. Lina maelezo ya kina zaidi kuliko swali lako. Ninakufikishia swali lililotangulia na jibu letu kwake, na pengine litatimiza lengo, Mwenyezi Mungu akipenda:
[Swali: Sheikh wetu mkubwa, Assalam Alaikum Wa Rahmatullah Wa Barakatuh,
Ninafanya kazi katika kampuni ya Malaysia inayoitwa DXN, ambayo hutengeneza bidhaa za afya na uchunzaji wa kibinafsi. Nilikutana na rafiki mmoja kutoka Jordan na alinisajili katika kampuni hii na kunipa nambari ya uanachama. Niliuliza watu kadhaa kuhusu kazi ya kampuni hii, je ni halali au haram? Wakanijibu kuwa ni halali. Lakini baada ya kuhudhuria mafunzo na mihadhara kuhusu mpango wa fedha, nilianza kuwa na shaka juu ya kazi yake na iwapo kuna chochote cha haram ndani yake?
Kazi ya kampuni hii imeegemezwa juu ya njia mbili za uuzaji:
Njia ya kwanza: Njia ya uuzaji wa moja kwa moja: Ambapo ninanunua bidhaa kwa bei ya jumla na nambari yangu ya uanachama kutoka kwa sehemu za mauzo za kampuni na kuziuza kwa faida yangu mwenyewe, ambapo kampuni hunipa idadi fulani ya pointi kwa kila bidhaa ninayonunua, na nikikusanya pointi 100 au zaidi kila mwezi, inanipa bonasi ya pesa taslim, ambapo asilimia yangu mwanzoni ni 6%, lakini nikikusanya pointi chini ya pointi 100, hainipi pesa, lakini pointi zinabaki katika akaunti yangu binafsi ili kukusanywa kufikia cheo cha wakala nyota.
Njia ya pili ya uuzaji (lakini sikuifikia), ambayo ni: Njia ya masoko ya mtandao wa ngazi mbalimbali: Ambapo timu huundwa na udalali kupigiwa hesabu, ambapo, kwa mfano, Kiongozi S hukusanya timu inayojumuisha S, A, na J, na kila mmoja wa timu ya Kiongozi S anakusanya pointi 100. Kiongozi S hapati faida zake isipokuwa apate pointi 100, na vivyo hivyo, hakuna mtu kutoka kwa timu anayepoteza haki yake.
Udalali kwenye timu ni kama ifuatavyo: Tofauti kati ya asilimia ya kiongozi na asilimia ya mwanachama wa timu huzidishwa kwa 35% huzidishwa kwa idadi ya pointi zilizokusanywa na mwanachama. Pointi zinazokusanywa na mwanachama na timu zinasalia katika akaunti ya jumla ya mwanachama hadi apate cheo cha wakala nyota.
Naomba radhi kwa urefu wa swali na maelezo. Mwenyezi Mungu akulinde ili usimamishe Khilafah Rashida. Natumai nimeliweka swali wazi. Mwenyezi Mungu akubariki na atuongoze sisi na wewe kwa yale anayoyapenda (swt) na kuyaridhia.) Mwisho.
Jibu: [Wa Alaikum Assalam Wa Rahamtullah Wa Barakatuh,
Awali ya yote, Mwenyezi Mungu akubariki kwa dua zako nzuri kwa ajili yetu, na tunakuombea kheri.
1- Kuhusu njia ya kwanza ya kuamiliana na kampuni hiyo, umesema katika swali kwamba unanunua bidhaa kwa bei ya jumla na kuziuza na kupata faida, na juu ya hiyo, ikiwa unauza asilimia fulani ya bidhaa kulingana na masharti yaliyowekwa na kampuni, unapata faida nyingine kutoka kwa kampuni (cash bonus)... ikimaanisha kuwa kampuni inajifunga kukupa bonasi ya pesa taslim (cash bonus) ikiwa unauza asilimia inayotakiwa ya bidhaa kila mwezi, na hii aghlabu ni kwa ajili ya kuwashajiisha wateja kuongeza maradufu mauzo yao... Ikiwa jambo ni kama tulivyoeleza hapo juu, basi njia hii ya muamala inaruhusiwa kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu kwa sababu kununua bidhaa kwa bei ya jumla na kuziuza kwa faida inajuzu na ni biashara inayojulikana vyema iliyojumuishwa katika maneno ya Mwenyezi Mungu (swt): وَأَحَلَّ اللَّهُ الْبَيْعَ وَحَرَّمَ الرِّبَا “Lakini Mwenyezi Mungu ameihalalisha biashara na ameiharimisha riba.” [Al-Baqara: 275]
Pia kampuni inaweza kukuahidi kiasi cha pesa ikiwa utauza asilimia fulani ya bidhaa, na hii inachukuliwa kuwa zawadi, na tulitaja katika jibu la swali la tarehe 14/5/2007 M, kuhusu jambo kama hilo, yafuatayo: [Kumpa mtu anayenunua kiasi fulani kiasi cha ziada, zawadi au kitu mithili ya hicho, inajuzu. Uuzaji huo ni halali, na kiasi cha ziada kinaanguka chini ya zawadi, ambayo ni halali.].
Walakini, ruhusa hii ya muamala huu na kampuni ni sahihi kwa masharti mawili:
Kwanza: Kwamba ununuzi wako uwe kwa bei ya jumla kama ilivyo bei ya jumla sokoni, yaani ndani ya mipaka ya bei ya jumla sokoni, na usiivuke kwa njia ambayo inaifanya kufikia kiwango cha ulaghai mkubwa kwa kumnyonya mnunuzi kwa kumdanganya kuwa atapata bonasi ya pesa taslim...nk. Ulaghai umeharamishwa, kama alivyosimulia Al-Bukhari kutoka kwa Abdullah bin Omar (ra) kwamba mtu mmoja alimtajia Mtume (saw) kwamba anadanganywa katika mauzo, hivyo akasema: «إِذَا بَايَعْتَ فَقُلْ لَا خِلَابَةَ» “Unapouza, sema: ‘Hakuna udanganyifu.’” Khilaba (neno katika Hadith) – lenye kasra kwenye herufi kha – ni udanganyifu. Udanganyifu ni haramu.
Pili: Kwamba njia hii ya muamala iwe huru na njia ya pili iliyotajwa katika swali, yaani ikiwa kuifanyia kazi njia hii ya kwanza iko kando na kuifanyia kazi njia ya pili, lakini ikiwa imeshikamana nayo na ni sharti kwa njia ya pili, basi yale tutakayoyataja kuhusu njia ya pili yatatekelezeka kwake pia.
2- Kuhusu njia ya pili ya kuamiliana na kampuni hiyo, kile kilichotajwa katika swali hakiko wazi, lakini inaonekana kuwa hakina tofauti sana na uuzaji wa mtandaoni ulio maarufu, na tumejibu mada ya uuzaji wa mtandaoni katika zaidi ya jibu moja lililotangulia, na tumeonyesha kuwa haijuzu kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu.
Kutokana na majibu haya, nitakutajia majibu mawili ya maswali yanayofanana na swali lako:
Jibu kwa Swali la tarehe 19/8/2015 M, ambalo linahusu kampuni ya Quest Net, ambayo ni aina ya uuzaji wa mtandaoni, na haya ndiyo maandishi yake:
[Baada ya kuhakiki uhalisia wa kampuni ya “Quest Net”, na tofauti ya mbinu zake za muamala, ingawa fikra ni lile lile, ambayo ni kwamba kampuni inaamiliana na wauzaji wanaoleta wanunuzi “wateja” kwake, na kuwapa kamisheni (commission) kulingana na masharti fulani, ikimaanisha kwamba wao ni madalali wa kampuni, wanaleta wanunuzi na kuchukua kamisheni kwa ajili yao... Kutokana na kutafakari uhalisia wa muamala huu, yafuatayo yanadhihirika:
Kwanza: Aina hii ya makampuni yanaamiliana na mtandao huu wa masoko katika bidhaa kadhaa, na makampuni haya yanaweka masharti kwamba yeyote anayeuza bidhaa zake anunue baadhi ya bidhaa hizo, na baada ya hapo wanampa haki ya kuleta wateja kwao, na kumpa kamisheni kwa malipo yao (yaani yeye ni dalali wa kampuni ambaye huleta wanunuzi kwake na kuchukua kamisheni kutoka kwa kampuni). Kampuni haitampa kamisheni hadi alete wanunuzi sita kulingana na swali la Asia ya Kati, na hadi alete wawili kulingana na swali la eneo jengine ... yaani kulingana na programu ya kampuni ambayo inaitayarisha kwa kusudi hili. Kwa maana nyengine, mnunuzi wa kwanza anachukua kamisheni kwa wale wawili “au sita” aliowaleta, pamoja na kamisheni nyengine kwa wanne ambao wawili hao wa kwanza waliwaleta, au kwa sita ambao wawili hao wa kwanza waliwaleta.
Na kazi ya uuzaji “udalali” inaendelea kwa njia hii, yaani katika mfumo wa mlolongo wa udalali au mtandao wa uuzaji.
Pili: Aina hii ya biashara ni kinyume na Shariah, na hii ndiyo sababu:
1- Kampuni inaeleza kuwa “muuzaji” lazima anunue kutoka kwa bidhaa zake ili awe na haki ya kuifanyia kazi kama dalali kwa ajili ya kamisheni, yaani analeta wateja kwake na kuchukua kamisheni kutoka kwao, iwe kamisheni hiyo ni baada ya kuleta wanunuzi sita au baada ya kuleta wanunuzi wawili.
Hii ina maana kwamba mkataba wa ununuzi na mkataba wa udalali ni mikataba miwili ndani ya mkataba mmoja, au miamala miwili ndani ya muamala mmoja, kwa sababu ni sharti la mmoja kwa mwingine. Haya yameharamishwa, kwani Hadith inasema: «نَهَى رَسُولُ اللهِ ﷺ عَنْ صَفْقَتَيْنِ فِي صَفْقَةٍ وَاحِدَةٍ» “Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amekataza mikataba miwili ndani ya mkataba mmoja.” Imepokewa na Ahmad kutoka kwa Abd al-Rahman ibn Abd Allah bin Mas`ud kutoka kwa baba yake. Yaani ni kama nikwambie: Ukiniuzia, nitakuajiri au nitakuwa dalali wako, au nitanunua kwako... nk. Ni wazi kuwa huu ndio uhalisia uliopo kwa mujibu wa swali, kwani uuzaji na udalali viko ndani ya mkataba mmoja, ikimaanisha kwamba ulazima wa kununua kutoka kwa kampuni ni sharti la kazi ya udalali, yaani wa masoko na kamisheni kwa wanunuzi wanaoletwa kwenye kampuni.
2- Udalali ni mkataba kati ya muuzaji na yule anayemletea wateja. Kamisheni ya udalali katika mkataba huu inapewa wale ambao mtu huwaleta kwa kampuni, si kwa wale ambao wengine huwaleta. Kwa kuwa kamisheni ya udalali katika muamala uliotajwa hapo juu inachukuliwa na dalali “muuzaji” kwa niaba ya wateja ambao huwaleta kununua kutoka kwa kampuni, na pia kwa niaba ya wale ambao wengine huwaleta, hii ni ukiukaji wa mkataba wa udalali.
3- Bei ya manunuzi kutoka kwa kampuni inaambatana na ulaghai mkubwa, na ingawa mnunuzi anafahamu hilo, jambo hilo halikosi hadaa kutokana na mbinu “potofu” zinazotumiwa na kampuni kukuza biashara yake kwa njia ambayo hupelekea mnunuzi kulipa bei kubwa ya bidhaa ya kampuni ambayo haina thamani hata ya sehemu ndogo ya bei halisi... Yote hii ni kwa sababu kampuni inakuza mustakabali (mzuri) wa mnunuzi huyu kwa sababu atapata fursa ya kuitafutia soko bidhaa ya kampuni kwa badali ya kamisheni ya (wanunuzi) anaowaleta kwenye kampuni, pamoja na wanunuzi wanaoletwa na wale aliowaleta kwanza!
Mnunuzi anaposhindwa kuleta wanunuzi, hasa wale walio mwisho wa mlolongo wa wanunuzi, anazungukwa na udanganyifu, na anapoteza bei kubwa aliyolipa kwa bidhaa isiyo na thamani hata ya ushuri moja ya kile alicholipa! Udanganyifu umeharamishwa katika Uislamu. Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema: «الخَدِيعَةُ فِي النَّارِ...» “Udanganyifu unapelekea Motoni...” Imepokewa na Al-Bukhari kutoka kwa Ibn Abi Awfa. Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alimwambia mtu mmoja aliyekuwa akidanganywa katika mauzo: «إِذَا بَايَعْتَ فَقُلْ لَا خِلَابَةَ» “Unapouza, sema, 'Hakuna udanganyifu.'” Imepokewa na Al-Bukhari kutoka kwa Abdullah ibn Umar (Mwenyezi Mungu awe radhi nao wote wawili). Khilaba ni udanganyifu. Hii ndiyo maana halisi ya Hadith, maana yake inaashiria kuwa udanganyifu umeharamishwa. Hivyo, muamala huu hauruhusiwi kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu.
Kwa kumalizia, kuamiliana na kampuni ya “Quest Net” kwa namna iliyoelezwa katika maswali ni muamala ambao ni kinyume na sheria ya Kiislamu...] Mwisho wa kunukuu.
Hii ndiyo ninayoiona kuwa rai yenye nguvu zaidi katika jambo hili, na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi na ni Mwenye Hekima.
Yote haya yanamaanisha kuwa njia ya pili iliyotajwa hapo juu haiendani na sheria ya Kiislamu. 7/11/2024]
Natumai kuwa jibu letu la hapo awali lililotajwa hapo juu litatosheleza.
Mwenyezi Mungu ndiye Msaidizi.]] Mwisho.
Ndugu Yenu
Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
17 Jumada Al-Akhira 1446 H
19/12/2024 M