- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Silsila ya Maswali Yaliyowasilishwa kwa
Amiri wa Hizb ut Tahrir
Sheikh Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah Katika Ukurasa Wake wa Facebook
Jibu la Swali
Je, Yajuzu Mtu Kumpa Zaka Dadake au Binti Yake?
Kwa: Abdullah Al-Haddad
(Imetafsiriwa)
Swali:
Assalamualaikum Warahmatullahi Wabarakatuh.
Mwenyezi Mungu azibariki nyakati zenu kwa kheri na furaha zote, na akupeni umri mrefu katika kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Ninamuomba Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa Arshi Tukufu, aharakishe kusimamisha Khilafah Rashida ya pili hali mkiwa katika afya njema na siha njema.
Swali langu ni: Je, inajuzu mtu kumpa zaka kwa dadake au binti yake?
Jibu:
Wa alaykum alsalam warahmat Allah wabarakatuh
Uislamu umefaradhisha kuwaruzuku masikini na umebainisha haya kuhusu masikini na ambao ni faradhi juu yao nk.:
Imeelezwa katika kitabu cha Nidhamu ya Kiuchumi, ukurasa wa 204-211 cha nakala ya Word: (... Mahitaji ya kimsingi, ambayo kutotimizwa kwake kunachukuliwa kuwa umaskini, ni: chakula, mavazi, na malazi. Chochote zaidi ya haya kinachukuliwa kuwa anasa. Kwa hiyo, mtu ambaye hatimizi mahitaji ya anasa lakini anakidhi mahitaji ya msingi hachukuliwi kuwa maskini.
Uislamu umewajibisha kushibisha mahitaji haya ya kimsingi na kuwapa wale wasioweza kuyapata. Ikiwa mtu binafsi anajipatia wenyewe, ni vizuri; ikiwa hawawezi kujiruzuku kwa sababu ya ukosefu wa pesa za kutosha au kutokuwa na uwezo wa kupata pesa za kutosha, Shariah inawajibisha wengine kuwasaidia hadi mahitaji haya ya kimsingi yatimizwe. Shariah imeeleza kwa kina jinsi mtu binafsi anavyopaswa kusaidiwa katika mambo haya. Ikafanya ni faradhi kwa warithi wake. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
[وَعَلَى الْمَوْلُودِ لَهُ رِزْقُهُنَّ وَكِسْوَتُهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ لَا تُكَلَّفُ نَفْسٌ إِلَّا وُسْعَهَا لَا تُضَارَّ وَالِدَةٌ بِوَلَدِهَا وَلَا مَوْلُودٌ لَهُ بِوَلَدِهِ وَعَلَى الْوَارِثِ مِثْلُ ذَلِكَ]
“Na juu ya baba yake chakula cha kina mama, na nguo zao kwa mujibu wa ada. Wala halazimishwi mtu ila kwa kadiri ya uwezo wake. Mama asitiwe taabuni kwa ajili ya mwanawe, wala baba kwa ajili ya mwanawe. Na juu ya mrithi mfano wa hivyo.” [Surat Al-Baqara:233]
Hii ina maana kwamba mrithi anawajibika kwa wajibu ule ule wa matumizi na mavazi kama baba. Haimaanishi kwamba mrithi tayari ni mrithi halisi, bali wao ni miongoni mwa wale wanaostahiki urithi wake. Ikiwa hakuna jamaa ambaye Mwenyezi Mungu amewajibisha utoaji riziki kwa jamaa yao, basi riziki yao huhamishiwa kwenye hazina ya umma, chini ya kigawanyo cha zaka. Imepokewa kutoka kwa Abu Huraira: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw): «مَنْ تَرَكَ مَالاً فَلِوَرَثَتِهِ وَمَنْ تَرَكَ كَلّاً فَإِلَيْنَا» “Mtu akiacha mali itakwenda kwa warithi wake na akiwacha wanaomtegemea wasio na rasilimali basi ni juu yetu kuwaangalia.” (Imepokewa na Muslim) na mzigo huo unakusudia mtu dhaifu ambaye hana baba wala mwana ...] Mwisho.
2. Ama ni nani anayewajibika kuwaruzuku masikini miongoni mwa jamaa, maelezo ni kama ifuatavyo: Katika Ensaiklopidia ya Fiqh ya Kuwaiti (kurasa 8267-68):
[Aina za wale ambao hawaruhusiwi kupewa zakat:
Yeyote ambaye ni jamaa wa moja kwa moja wa mtoaji zakat au ana uhusiano wa kuzaliwa. Hii inajumuisha kizazi kilicho juu yake, kama vile wazazi wake na babu na bibi, iwe ni warithi au la, na vivyo hivyo vizazi vya chini yake, kama vile watoto wake na wajukuu, bila kujali ni wako mbali kiasi gani chini ya mstari. Mahanafi wanaeleza haya kwa sababu manufaa ya umilikaji yanaunganishwa miongoni mwao, na hii ndiyo rai ya Mahanafi na Mahanbali.
Ama jamaa wengine, kama ndugu, wajomba, mashangazi na watoto wao, hakuna uharamu katika kuwapa zaka, hata kama baadhi yao wanamtegemea. Mtume (saw) amesema: «الصّدقة على المسكين صدقة، وهي على ذي الرّحم اثنتان: صدقة وصلة» “Sadaka anayopewa masikini ni sadaka tu, lakini inapotolewa kwa jamaa ina malengo maradufu, ni sadaqa na kuunga uzazi.”
Hii ni rai ya Mahanafi na ndiyo rai inayopendekezwa miongoni mwa Mahanbali.
Kwa mujibu wa kina Maliki na Mashafii, haijuzu kutoa zaka kwa jamaa ambao matumizi yao ni wajibu kwa mtoaji zaka:
Kwa kina Maliki, wale ambao ni faradhi kuwasimamia kimatumizi ni baba na mama lakini si babu na bibi, na mtoto wa kiume na wa kike lakini si watoto wao. Mtoto wa kiume lazima asimamiwe maadamu bado ni mdogo, na binti mpaka aolewe na mumewe akamilishe ndoa naye.
Kwa Mashafii, wanaopaswa kusimamiwa kimatumizi ni vizazi vilivyo juu yake na chini yake...]
3. Kama unavyoona, kumpa binti zaka kuna rai tofauti kati ya wanavyuoni kwa sababu yeye ni dhuria. Ijapokuwa hukmu iliyothibiti miongoni mwao ni kwamba haijuzu kutoa zaka kwa wale ambao mtoaji zakat inawajibika kuwapa matumizi, bali wanapaswa kusimamiwa kutokana na mali yake mwenyewe; tofauti katika rai iko katika ni nani hasa anawajibika kusimamiwa kimatumizi na mtoaji zakat kati ya kizazi kilicho juu yake na kizazi kilicho chini yake.
Baadhi wanasema: (Vigawanyo vya wale ambao hawaruhusiwi kupewa zaka ni kizazi kilicho juu yake, kama wazazi wake na babu na bibi, iwe ni warithi au la, na vivyo hivyo vizazi vilivyo chini yake, kama watoto wake na wajukuu, bila kujali wako mbali kiasi gani na mstari. Hii ndio rai ya Mahanafi na Hanbali.)
Wengine wanasema: (Wale ambao ni wajibu kuwaangalia kimatumizi kwa mujibu wa Maliki ni baba na mama lakini si babu na bibi, na mtoto wa kiume na wa kike lakini si watoto wao. mtoto wa kiume lazima asimamiwe kimatumizi maadamu bado ni mdogo, na binti mpaka aolewe na mumewe afunge naye ndoa.)
Wengine wanasema: (Wale ambao ni wajibu kuwapa matumizi kwa mujibu wa Mashafi' ni kizazi kilicho juu yake na chini yake ...)
Sasa najibu swali lako: Je, inajuzu mtu kumpa zaka dadake au binti yake?
1. Kuhusu binti, jibu ni kama ifuatavyo:
a. Ikiwa binti huyo hajaolewa na anaishi kwa baba yake, matunzo yake ni wajibu kwake, basi anapaswa kumpa matumizi yake kutokana na mali yake na sio zaka.
b. Ikiwa binti ameolewa na mumewe ana hali nzuri na anampa matunzo, haijuzu kutoa zaka hata akiwa masikini, kwa sababu anahesabiwa kuwa ni tajiri kutokana na matunzo ya mumewe. Amesema Al-Nawawi katika Al-Minhaj: “Mtu anayepewa riziki na jamaa au mume hahesabiwi kuwa ni fukara au masikini kwa mujibu wa rai iliyo sahihi zaidi. Mwisho.
c. Ikiwa binti ameolewa na ni masikini, na mumewe hawezi kumpa matumizi kamili, Ibn Qudamah amesema katika Al-Mughni: “Ikiwa mwanamke masikini ana mume mwenye hali nzuri anayempa matunzo, haijuzu kumpa zaka kwa sababu mahitaji yanakidhiwa na matunzo ya faradhi anayoyapata, sawa na yule ambaye aliye na mapato kutokana na mali. Hata hivyo, ikiwa hampi matumizi kamili na haiwezekani kuyapata kutoka kwake, inajuzu kumpa zaka, kana kwamba manufaa ya mali hiyo imepotea.” Mwisho.
Napendelea kukwepa tofauti ya rai kwa kumpa zaka mume wa binti masikini ikiwa amekidhi kigezo cha ufukara, kisha atumie kwa mke wake zaka aliyopokea. Ama baba kumpa matumizi binti yake, inatakiwa itokane na mali yake na sio zaka.
2. Kuhusu dada, jibu ni kama ifuatavyo:
Ikiwa dada yako anaishi nyumbani kwako na unampa matunzo, haijuzu kumpa zaka. Hata hivyo, ikiwa ameolewa na mumewe ni masikini, inajuzu kumpa zaka. Kwa kweli, kumpa yeye kunafaa zaidi kuliko wengine; kama Mtume (saw) alivyosema: «الصَّدَقَةُ عَلَى الْمِسْكِينِ صَدَقَةٌ، وَهِيَ عَلَى ذِي الرَّحِمِ ثِنْتَانِ ٍ صَدَقَةٌ وَصِلَةٍ “Sadaka akipewa maskini huwa ni sadaka tu, na akipewa jamaa ina malengo maradufu, ni sadaka na kiunga uzazi.” Imepokewa na Tirmidhi.
Hili ndilo jibu langu nililofadhilisha kwa swali lako, nikitaraji kuwa linatosheleza, na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi.
Ndugu Yenu,
Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
28 Dhul Hijjah 1445 H
04/07/2024 M
Link ya majibu kwenye ukurasa wa Amiri wa Facebook: