Jumapili, 20 Jumada al-thani 1446 | 2024/12/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Jibu la Swali

Uchaguzi wa Pakistan
(Imetafsiriwa)

Swali:

Shirika la habari la Reuters liliripoti mnamo tarehe 19 Februari 2024, "Vyama viwili vikuu vya Pakistan vinatazamiwa kukutana mnamo Jumatatu ili kujaribu kutatua tofauti za kuunda serikali ya mseto ya wachache baada ya uchaguzi ambao haukukamilika, afisa mmoja wa ngazi ya juu wa chama alisema, akisisitiza kukosekana kwa utulivu wa kisiasa na kiuchumi ... Mazungumzo ya Jumatatu itakuwa raundi ya tano kama hii baada ya Waziri Mkuu wa zamani Shehbaz Sharif kuteuliwa na chama chake cha Pakistan Muslim League-Nawaz (PML-N) kuiongoza tena nchi hiyo." (Chanzo) Uchaguzi wa Pakistan ulifanyika mnamo tarehe 8 Februari 2024, baada ya kuakhirishwa. Je, mikutano hiyo ya Jumatatu iliyotajwa ilimaanisha kutengwa kwa watu huru watiifu kwa Pakistan Tehreek-e-Insaf (PTI) kutoka mamlakani? Je, tuhma za ulaghai na udanganyifu katika uchaguzi ni za kweli? Je, mambo yanaelekea wapi baada ya uchaguzi nchini Pakistan?

Jibu:

Uchaguzi huo ulifanyika nchini Pakistan baada ya kuakhirishwa kwa miezi kadhaa. Samaa TV iliripoti mnamo tarehe 11 Februari 2024 “Kulingana na matokeo yaliyotangazwa hadi sasa, wagombea huru wamefanikiwa kushinda viti 101. Inafaa kutaja kwamba kati ya wagombea hao huru 101, 92 wanaungwa mkono na Pakistan Tehreek-e-Insaf huku tisa wakiwa wagombea huru. PML-N iko katika nafasi ya pili ikiwa na viti 75, huku PPP ikishinda viti 54. (Chanzo). Chaguzi hizi zilikusudiwa kuongoza nchi kuelekea utulivu wa kisiasa. Hii ni baada ya kipindi kigumu cha machafuko yaliyofuatia hoja ya Bunge ya kutokuwa na imani dhidi ya serikali ya Imran Khan mnamo 9 Aprili 2022 na kupinduliwa kwake. Kisha, Shehbaz Sharif, kaka yake Nawaz Sharif, akashika wadhifa wa Waziri Mkuu nchini Pakistan kwa niaba ya Pakistan Muslim League-Nawaz. Baada ya hapo, maandamano ya vurugu yalizuka nchini humo... Kuhusu wapi mambo yanaelekea sasa, baada ya uchaguzi nchini Pakistan, mambo yafuatayo lazima yazingatiwe:

1- Pakistan ni moja ya nchi muhimu za Kiislamu. Idadi yake kubwa ya watu milioni 250 inaifanya kuwa hifadhi kubwa ya binadamu, ili kugeuza gurudumu la uchumi na kutoa rasilimali watu kwa jeshi. Pakistan ni mojawapo ya nchi za kipekee duniani katika upande wa rasilimali watu na nguvu za kijeshi, na pia kuwa katika eneo la kimkakati.

2- Leo hii, Pakistan inachukuliwa kuwa moja ya nchi masikini duniani. Hii ni licha ya wingi wa tambarare za kilimo yenye rutuba na maji. Hii ni licha ya uwezo wake wa viwanda. Hii ni licha ya rasilimali watu kuweza kuendesha uchumi mkubwa zaidi duniani. Hii yote ni kutokana na sera zilizofeli ambazo Marekani inazisukuma, ufisadi wa kifedha na kiutawala, na kuenea kwa ugonjwa wa kutegemea wengine, kama vile China au Marekani. Hii inazuia jaribio lolote la maendeleo ya kiuchumi. Nchi hii iliteseka kutoka na mafuriko makubwa mnamo 2022 ambayo yaliharibu ardhi ya kilimo. Kisha, serikali haikuweza kutoa masuluhisho yoyote ya thamani. Mbali na kufeli kwa uchumi, kuna kutofaulu kabisa katika nyanja zote nchini Pakistan, kufeli kukuu zaidi kukiwa katika utawala, kwa muda wa miongo kadhaa.

3- Ari ya Kiislamu ya jihad ililipuka nchini Pakistan kwa namna ambayo ilizua hofu duniani kote. Hii ilitokana na athari za kadhia ya Kashmir, na vile vile athari ya uvamizi wa Kisovieti wa Afghanistan, ikifuatiwa na uvamizi wa Marekani wa Afghanistan. Matukio mengi kwa miongo kadhaa yamefichua ari thabiti ya mapigano, ambayo imekita mizizi katika Aqida (itikadi) ya Kiislamu ya watu wa Pakistan. Kulikuwa na harakati nyingi za jihad za Kiislamu kukomboa Kashmir na Afghanistan. Kulikuwa na wito wa kuwaunga mkono Waislamu duniani kote. Harakati za kile ambacho Wamagharibi wanakiita Uislamu wa kisiasa zilikita mizizi nchini Pakistan, inayojulikana zaidi ikiwa ni ulinganizi wa kusimamisha Khilafah... Kutokana na hayo yote, mlipuko wa Uislamu nchini Pakistani umeifanya Pakistan, pamoja na Afghanistan jirani, kituo cha pili cha mvuto wa kisiasa wa Kiislamu, baada ya Mashariki ya Kati.

4- Jeshi la Pakistan linachukuliwa kuwa jeshi kubwa la kuzingatiwa, lililo na silaha hatari na uwezo wa nyuklia. Kwa sababu ya historia ndefu ya mzozo na India, Marekani inalisukuma Jeshi la Pakistan kuelekea vita vya wenyewe kwa wenyewe ndani ya Pakistan. Inalisukuma Jeshi la Pakistan kugombana na kuzozana na vuguvugu la Taliban, ambalo liliregea madarakani mwaka wa 2021, nchini Afghanistan. Marekani pia inalisukuma Jeshi la Pakistan kuelekea mpaka wa Iran. Haya yote ni ili kuiwezesha India kushiriki katika mkakati wa Marekani, kukomesha kukua kwa China, na kuishughulisha China na uwezekano wa vita na India. Kabla ya haya yote, Marekani ilikuwa imefaulu kuifanya Pakistan kuwa korido ya kufika Afghanistan, wakati wa kukaliwa kimabavu kwake kuanzia 2001-2021. Licha ya haya yote, macho ya Marekani hayaachi kuziona hatari za kimkakati kutokana na nguvu ya Jeshi la Pakistani hata kwa muda. Kwa hivyo mnamo 13 Oktoba 2022, Rais wa Marekani Biden aliita Pakistan, "mojawapo ya mataifa hatari zaidi ulimwenguni," kama ilivyoripotiwa kwenye wavuti wa Ikulu ya White House (Chanzo). Hii ni licha ya vibaraka wote wa utumishi wa kijeshi na uongozi wa kisiasa nchini Pakistan, na kuwezesha kwake sera za Marekani.

5- Kinachoongeza umuhimu wa Pakistan ni kwamba China, ambayo ni mpinzani mashuhuri wa kimataifa wa Marekani, inaitazama Pakistan kwa njia maalum. Inaisaidia Pakistan dhidi ya India. China inaipatia Pakistan silaha. China inawekeza makumi ya mabilioni ya dolari nchini Pakistan, kwa njia ya mikopo, na baadhi ya misaada, kusaidia miundombinu, barabara, bandari na viwanda. Ingawa Marekani ina udhibiti na ushawishi nchini Pakistan, inatilia shaka juhudi hizi za China, na uwekezaji nchini Pakistan.

6- Kwa kuzingatia ukweli huu, jambo la kwanza ambalo lazima lipatikane, wakati wa kuzingatia matukio ya kisiasa nchini Pakistan, ni kwamba kiongozi wa ukafiri, Marekani, amezingatia Jeshi la Pakistan na uongozi wake wa kijeshi. Ni muhimu katika utawala na ushawishi ndani ya Pakistan. Mojawapo ya matokeo makuu ya udhibiti wa Marekani juu ya Jeshi la Pakistan, na uongozi wake wa kijeshi, ni kuwekwa mbali nchi hii kutokana na migogoro, vita na India. Hii ni licha ya chokochoko za India zinazoendelea huko Kashmir, ambazo zinaongezeka mara kwa mara. Pia miongoni mwa matokeo hayo ni mkabala wa Jeshi la Pakistan katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, na kuwasha kwake vita kaskazini-magharibi mwa Pakistan, kuwaondoa mujahidina, ambao walikuwa wakiwaunga mkono ndugu zao nchini Afghanistan wakati wa uvamizi wa Marekani wa Afghanistan. Pia miongoni mwa matokeo haya ni mapigano yanayotokea mara kwa mara na Afghanistan. Mbali na matokeo hayo, ni kwamba uvamizi wa Marekani dhidi ya Afghanistan ulikuwa unapitia katika milango ya Pakistan. Kwa hiyo, udhibiti wa Marekani juu ya uongozi wa kijeshi nchini Pakistan ndio unaoifanya Pakistan kuwa dola ambayo ni kibaraka wa Marekani.

7- Jeshi la Pakistan linadhibiti nchi kikamilifu. linaingilia kati maisha ya kisiasa, pamoja na yale ya vyama vya kisiasa, nchini. Wakati wowote mambo yanapotoka nje ya udhibiti, Jeshi la Pakistan huingilia kati kwa mapinduzi ya kijeshi, na kuwapindua watawala. Vyama viwili vya kisiasa kwa jadi vinatawala nchi, Ligi ya Waislamu wa Pakistan- Nawaz Sharif (PML-N) na Pakistan People's Party (PPP). Chama cha kwanza kinatazamwa kama chama cha mrengo wa kulia, huku chama cha pili kinachukuliwa kuwa chama cha mrengo wa kushoto. Cha kwanza kinafurahia uungwaji mkono mkubwa katika jimbo la Punjab, ilhali cha pili kinafurahia uungwaji mkono mkubwa katika jimbo la Sindh. Kuna kufeli kwa pande zote mbili katika historia. Viongozi kutoka pande zote mbili wamezama katika ufisadi, huku uongozi ukitenda kama wababe wakuu juu ya Pakistan. Hata hivyo, mbele ya kufeli huku kwa muda mrefu, na chuki kubwa ndani ya Pakistan, ambayo inawasukuma watu kuelekea kwenye harakati za kutetea Uislamu wa kisiasa, Jeshi la Pakistan liliamua kubadilisha mlingano huo. Kwa hiyo, Jeshi la Pakistan lilimleta Imran Khan, ambaye alikuwa kiongozi wa chama ambacho si kikubwa sana wakati huo, PTI, na ambaye sauti yake ilikuwa kubwa dhidi ya ufisadi. Baada ya tuhma kuu, na kesi za kimahakama, dhidi ya Waziri Mkuu wa zamani, na kiongozi wa PML-N, Nawaz Sharif, PTI ilitawala kura za wabunge. Kwa hivyo, Imran Khan akawa Waziri Mkuu mnamo 2018.

8- Katika kipindi hicho, mahakama za Pakistan zilikuwa zikimfuatilia mtawala wa zamani Nawaz Sharif kwa mashtaka ya ufisadi. Nawaz alijiuzulu wadhifa wake mnamo Juni 2017, baada ya Mahakama ya Upeo kumtia hatiani kwa mashtaka ya ufisadi, yanayohusiana na ukwepaji kodi. Mahakama ya Upeo ilitoa hukumu kwamba Nawaz Sharif hastahili kusalia madarakani. Alihukumiwa Julai 2018 kifungo cha miaka kumi jela, kwa mashtaka ya ufisadi. Shirika la habari la Reuters liliripoti mnamo tarehe 17 Oktoba 2020 kwamba, "Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan Nawaz Sharif mnamo Jumamosi alimtuhumu mkuu wa jeshi la nchi Jenerali Qamar Javed Bajwa kwa kupindua serikali yake, kushinikiza mahakama, na kuipandikiza serikali ya sasa ya Waziri Mkuu Imran Khan katika uchaguzi wa 2018.” (Chanzo). Haya yote, kupinduliwa kwa Nawaz Sharif, kushtakiwa kwake na kufanya uchaguzi, wakati akiwa bado korokoroni nchini Pakistan, kulitokana na uamuzi wa Jeshi la Pakistan. Kumleta Imran Khan, aliye mbali na vyama viwili vya jadi nchini Pakistan, pia ilikuwa kwa uamuzi wa Jeshi la Pakistan.

9- Nawaz Sharif, ambaye alikuwa akitumikia kifungo, aliruhusiwa kusafiri kwenda Uingereza kwa madhumuni ya kiafya. Hii ilitokana na makubaliano naye kwamba angerudi, baada ya matibabu yake Pakistan, ili kukamilisha kifungo chake... Hata hivyo, baada ya Jeshi la Pakistan kumpindua Imran Khan, tulilolieleza katika swali na jibu lenye kichwa, “Marekani na Mabadiliko katika Vibaraka wake nchini Pakistan,” la 5 Shawwal 1443 H, 5 Mei 2022, Jeshi la Pakistan lilianza kuondoa vikwazo vyote vya kisheria vya kuregea kwa Nawaz Sharif. Baada ya kupinduliwa kwa Imran Khan mnamo 2022, kakake Sharif, Shehbaz Sharif, aliteuliwa kuwa waziri mkuu. Haya ni pamoja na uamuzi wa mahakama ya federali ya kumuachilia huru kwa dhamana Nawaz Sharif, kabla ya kuwasili nchini. Pia ni baada ya Bunge kutoa sheria Juni 2023 kuweka muda usiozidi miaka mitano kwa mbunge wa Bunge hilo kugombea nafasi hiyo baada ya kutostahiki milele. Hili lilimruhusu Nawaz Sharif kuregea nchini na kujipendekeza mwenyewe, hivyo akaregea. Nawaz Sharif alikuja kutoka ng’ambo na kufika mbele ya mahakama katika maandalizi ya kuachiliwa kwake kwa mashtaka dhidi yake, na kushindana katika uchaguzi. Gazeti la ‘The Independent’ liliripoti mnamo tarehe 21 Oktoba 2023 kwamba, "Mahakama Kuu ya Islamabad mnamo siku ya Alhamisi ilimpa kinga dhidi ya kukamatwa siku chache kabla ya kuregea kwake." (Chanzo). Haya ndiyo yaliyotokea kikweli! Nawaz Sharif akawa mwanasiasa "msafi" tena. Akagombea uchaguzi na chama chake cha Pakistan Muslim League-N, huku Anwaar-ul-Haq Kakar akiwa waziri mkuu wa muda akisimamia uchaguzi. (Sharif alipata uungwaji mkono wa jeshi aliporegea Pakistan Oktoba iliyopita, baada ya Miaka minne uhamishoni jijini London. (Independent Arabia, 10/2/2024)). Kwa mujibu wa chanzo hicho hicho, (Kwa upande mwingine, inaaminika kuwa Nawaz Sharif aliregea serikalini baada ya kumaliza “dili” na jeshi ya kumregesha kwenye nafasi ya uwaziri mkuu kwa mara ya nne. Chama cha Insaf kinatuhumiwa na Al-Shaab akisema kwamba mapokezi rasmi ambayo Sharif aliyapata baada ya kuregea ni ushahidi wa kuwepo kwa maelewano kati yake na taasisi ya kijeshi.

10- Ni mafanikio sana kwa Nawaz Sharif. Ama kwa Imran Khan, leo yuko gerezani, akiwa amehukumiwa kwa makosa mengi. Kutokana na hukumu yake, Imran Khan alizuiwa kushiriki katika uchaguzi, huku chama chake, Pakistan Tehreek-e-Insaf, kilizuiwa kushiriki katika uchaguzi kama chama cha kisiasa. Kwa hivyo, inakuwa wazi jinsi meza za kisiasa zimebadilika nchini Pakistan. Leo, mwaka 2024, Jeshi la Pakistan limegeuka dhidi ya Imran Khan. Imran sasa yuko katika nafasi ile ile aliyokuwa nayo Nawaz Sharif mwaka 2018. Kuhusu Nawaz Sharif, ameregea kwenye umashuhuri, baada ya vikwazo vyote kuondolewa kwake, kama tulivyoonyesha. Pamoja na haya yote, inakuwa wazi jinsi uongozi wa Jeshi la Pakistan unavyoushawishi uchaguzi wa bunge. Inadhihirika wazi jinsi Jeshi la Pakistani linavyoendesha vyama hivyo vya kisiasa, ambavyo vinatafuta idhini yake, ili kupata mamlaka. Hii sio siri. Mkuu wa jeshi alimfunga Nawaz Sharif na kumrudisha Imran Khan... Kisha mkuu wa jeshi akamfunga Imran Khan na kumrudisha Nawaz Sharif! Kwa hivyo, wanasiasa bandia, kutoka miongoni mwa viongozi wa vyama, wanatumiwa kulingana na matakwa ya Marekani, kwa ajili ya kiti kibovu cha utawala! Kisha, pindi dori ya kiongozi kama huyo inapokwisha, ima anatupwa kando, au kuwekwa gerezani!

11- Uongozi wa kijeshi peke yake ndio hudhibiti serikali, na hivyo uchaguzi, kwa njia nyingi. Inajulikana kuwa mawasiliano na mtandao ulikatwa katika baadhi ya maeneo. Serikali ilisema kuwa hii ilikuwa kwa madhumuni ya kuzuia ghasia na machafuko, siku ya uchaguzi! Serikali pia inahodhi suala la kubainisha wilaya za uchaguzi, kulingana na sensa ya watu ambayo inaifanya. Kwa mtazamo huu inaweza kuongeza, au kupunguza, wilaya kwa kupendelea vyama maalum, ambavyo vina uzito wa uchaguzi katika wilaya hizo! Uchaguzi uliakhirishwa kutoka Agosti 2023 hadi Februari 2024, kwa kisingizio cha kupanga upya wilaya za uchaguzi, kwa kuzingatia sensa ya hivi punde ya idadi ya watu. Kwa njia hizi, viongozi wa chama, wanaochukua zamu madarakani, wote wana wajibu wa kuwa watiifu kwa Marekani, na kuitumikia Washington. Njama zimepangwa kwa yeyote atakayekengeuka kutoka kuvuta mstari wa Marekani, au kujitahidi kufanya hivyo, au kugongana na Jeshi la Pakistan, kama tulivyoona. Kesi za ufisadi zinaibuliwa dhidi yake, mpaka awe gerezani. Kwa hivyo, vyama vyote hivi vinafanya kazi chini ya mwavuli wa uongozi wa kijeshi wa jeshi. Ni uongozi ambao ni kibaraka wa Marekani. Vyama hivi vinaweza tu kushindana ndani baina yao wenyewe, ili Jeshi la Pakistan kuchagua kutoka miongoni mwao anayefaa zaidi kwa uteuzi...

12- Kisha, uongozi wa kijeshi unaruhusu kwenda mbele na nyuma, kuhusiana na matokeo ya uchaguzi, ili kuonyesha kuwa uko mbali na kudhibiti matokeo! Gazeti la ‘The Independent’ liliripoti mnamo tarehe 10 Februari 2024, kwamba, "waziri mkuu wa zamani Nawaz Sharif na waziri mkuu wa zamani Imran Khan walidai ushindi katika uchaguzi mkuu." (Chanzo). Chama cha PTI kinazingatia kuwa wagombeaji huru walipata viti 101, huku wengi wao wakiwa ni wafuasi wake, ambao ni idadi kubwa zaidi ya viti vinavyopatikana kwa chama chochote. Hii inakipa sifa ya kuwa chama cha kuongoza mchakato wa kuunda serikali. Hata hivyo, PML-N, inayoongozwa na Nawaz Sharif, ambayo ilipata viti 75 katika Bunge la Kitaifa, inasema kuwa ndiyo iliyoshinda uchaguzi huo. Hili linaregelewa katika taarifa ya mkuu wa jeshi kuhusu uchaguzi. Mrengo wa vyombo vya habari wa jeshi, ISPR, uliripoti kwamba mkuu wa jeshi alisema, "Taifa linahitaji mikono thabiti na mguso wa uponyaji ili kuondokana na siasa za machafuko na ubaguzi." (Chanzo).

Hii ina maana kwamba PTI, chama cha Imran Khan, licha ya kupata idadi kubwa ya viti vya ubunge kupitia wagombea huru, viti vya wagombea huru vinaunda rasmi vile vya wagombea huru, na sio vya chama chochote cha kisiasa. Kwa hiyo, chama cha Nawaz Sharif kinasalia kuwa kile ambacho kina haki ya "kisheria" ya kuongoza mchakato wa kuunda serikali, kupitia muungano na vyama vyengine.

13- Baadhi ya viongozi walikiri kwamba wizi wa kura ulifanyika. Al-Jazeera iliripoti mnamo tarehe 17 Februari 2024 kwamba, "Afisa mmoja wa ngazi ya juu nchini Pakistan amesema alisaidia kuvuruga uchaguzi wa Pakistan, wiki moja baada ya kura za maoni zilizokumbwa na madai ya udanganyifu hazijaleta mshindi wa wazi ... "Tulibadilisha walioshindwa na kuwa washindi, na kuregesha kiwango cha kura 70,000 katika viti 13 vya bunge,” aliwaambia waandishi... Kulingana na gazeti la ‘Dawn News’ la Pakistan, kamishna huyo alikiri kuwa "alihusika sana katika uhalifu mkubwa kama vile wizi mkubwa wa kura za 2024." Wakati huo huo, tume ya uchaguzi ya Pakistan ilikataa madai ya Chattha, lakini ilisema katika taarifa kwamba "itafanya uchunguzi". Katika taarifa ya habari, shirika la kusimamia uchaguzi pia lilisema hakuna afisa wake aliyewahi kutoa maagizo yoyote kwa Chattha kwa "mabadiliko ya matokeo ya uchaguzi". (Chanzo). Licha ya hayo yote, mkuu wa majeshi, baada ya kumwachilia huru Nawaz Sharif kutoka gerezani, na kumruhusu kugombea uongozi wa chama chake, anaonekana kumwandalia uwanja katika Afisi ya Waziri Mkuu. Shirika la habari la Reuters liliripoti, mnamo tarehe 19 Februari 2024, kwamba, "Vyama viwili vikuu vya Pakistan vinatazamiwa kukutana Jumatatu ili kujaribu kutatua tofauti za kuunda serikali ya mseto ya wachache baada ya uchaguzi ambao haukukamilika, afisa wa juu wa chama alisema, akisisitiza kukosekana kwa utulivu wa kisiasa na kiuchumi... Mazungumzo ya Jumatatu yatakuwa ya raundi ya tano... Chama cha Pakistan Peoples Party (PPP) cha waziri wa zamani wa mambo ya nje Bilawal Bhutto Zardari kimetangaza kuunga mkono kwa masharti PML-N, kikisema kitampigia kura Sharif kuunda serikali, lakini hakitachukua nyadhifa katika baraza la mawaziri... Serikali mpya inaweza pia kukabiliwa na mvutano zaidi wa kisiasa, huku wabunge huru wakiungwa mkono na waziri mkuu wa zamani Imran Khan aliyefungwa jela, na kuunda kundi kubwa zaidi katika bunge.” (Chanzo). Kwa hivyo, uongozi wa kijeshi unamfanya yeyote unayemtaka kuwa mshindi leo, na kumfanya kuwa mshindwa na mfungwa kesho... na kadhalika! Amesema Mwenyezi Mungu (swt):

[أَلَا سَاءَ مَا يَحْكُمُون]

“Tazama uovu wa wanavyohukumu!” [Surah An-Nahl 16:59].

14- Ama kuhusu ujanja huu wa kina wa serikali ya Pakistan, na uongozi wa kijeshi kibaraka wa Marekani, ambapo kuna hali ya machafuko ya kisiasa, ambayo yanaweza kuendelea na kudhoofisha uthabiti wa nchi ... yote haya lazima yawe motisha kubwa, kwa watu wenye ikhlasi katika Jeshi la Pakistan, na nchini Pakistan kwa jumla, kuinuka na kukomesha utiifu wa nchi hiyo kwa Marekani... hii ni kwa kusimamisha tu utawala wa Mwenyezi Mungu, Khilafah Rashida. Khilafah ni ahadi ya Mwenyezi Mungu (swt). Amesema Mwenyezi Mungu (swt):

[وَعَدَ اللهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنْكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِنْ قَبْلِهِمْ]

“Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walio amini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyo wafanya makhalifa wa kabla yao.” [Surah An-Nur 24:55]. Khilafah iko ndani ya bishara njema ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), kuhusu kurudi kwake baada ya utawala wa kutenza nguvu ambao tuko chini yake. Hudhayfah (ra) amesema kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema,

«ثُمَّ تَكُونُ مُلْكاً جَبْرِيَّةً فَتَكُونُ مَا شَاءَ اللهُ أَنْ تَكُونَ ثُمَّ يَرْفَعُهَا إِذَا شَاءَ أَنْ يَرْفَعَهَا ثُمَّ تَكُونُ خِلَافَةً عَلَى مِنْهَاجِ النُّبُوَّةِ ثُمَّ سَكَتَ»

“‘Kisha utakuwepo utawala wa kutenza nguvu, utakuwepo kwa muda apendao Mwenyezi Mungu uwepo kisha atauondoa apendapo kuuondoa. Kisha itakuwepo Khilafah kwa Njia ya Utume.’ Kisha akanyamaza.” Imesimuliwa na Ahmad. Utekelezaji faradhi hii kubwa unatarajiwa kutoka kwa watu wa Umma wa Kiislamu, kwa mapana na marefu… hususan kwa kuwa Pakistan iliasisiwa kwa msingi wa Uislamu kuanzia siku ya kuunda kwake, na watu wake pamoja na jeshi lake wanapenda Uislamu na Waislamu.

Muunganisho wa watawala wa Pakistan, na uongozi wake wa kijeshi, na Marekani ni rahisi kwa Mwenyezi Mungu (swt) kuubadilisha, kuliko ilivyo kwao kubadilisha mapenzi ya Ummah kwa Uislamu wake. Hivyo basi, matokeo ni kwa wachamungu ikiwa wana ikhlasi, wakafanya kazi kwa bidii, na wakajitahidi kumnusuru Mwenyezi Mungu (swt), kwani Mwenyezi Mungu (swt) ndiye msaidizi wao. Amesema Mwenyezi Mungu (swt):

[وَسَيَعْلَمُ الَّذِينَ ظَلَمُوا أَيَّ مُنْقَلَبٍ يَنْقَلِبُونَ]

“Na wanao dhulumu watakuja jua mgeuko gani watakao geuka.” [Ash-Shu’ara 26:227].

10 Sha’aban 1445 H

20 Februari 2024 M

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu