Jumatano, 22 Rajab 1446 | 2025/01/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Je, Mbio za Imran Khan Zimefikia Ukingoni?

Mandhari ya kisiasa ya Pakistan inazizima kwa minon’gono kuhusu mustakbali wa Waziri Mkuu Imran Khan. Matumaini mema yaliovutia Pakistan miaka miwili iliopita hivi sasa yamekuwa ni kumbukumbu ilio mbali wakati mcheza kriketi alipogeuka kuwa waziri mkuu, Imran Khan, akikumbana na matatizo ya tsunami. Baada ya ahadi zisizoweza kutekelezeka za Naya Pakistan (Pakistan mpya), uanzishaji wa mfano wa Madina na dola yenye ustawi, mradi wa PTI (chama cha Pakistan Tahreek-e-Insaf) hivi sasa uko mahututi wakati wafuasi wakereketwa wameshiba ahadi zisizotekelezeka, hotuba kali na muendelezo wa kuwasukumizia lawama wengine. Waziri Mkuu yuko chini ya lawama kutokana na kushindwa kwa serikali yake kuleta maendeleo katika upande wa kiuchumi na kisiasa pamoja na kushindwa kabisa kukabiliana na maambukizi ya COVID-19. Vyombo vya habari vimejaa taarifa za kufeli kwa Imran Khan kama kichwa cha habari kimoja kikisomeka: “Mradi wa Imran Khan wa Jeshi la Pakistan Umekwenda Mrama.” Mwana diplomasia na mwana habari mmoja wa zamani amekwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa kufeli kabisa kwa serikali ya Imran Khan katika sera zake za kupambana na COVID-19 kumehalalisha Majenerali kurudia kuchukua nafasi za mbele katika kuidhibiti Pakistan.

Kufeli kukubwa zaidi kwa Imran Khan kumekuwa katika upande wa uchumi, licha ya ahadi za mito ya asali na maziwa kwa wananchi. Katika kipindi cha miaka miwili tu serikali ya PTI imerudisha nyuma kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi (GDP) kutoka zaidi ya asilimia 5 hadi chini ya asilimia 2.4. Mfumko wa bei hivi sasa ni wa tarakimu mbili na unaendelea kupanda wakati serikali ya PTI ikimlaumu kila mtu isipokuwa yenyewe tu. Akiwa mgombea, Imran Khan aliahidi kuusawazisha uchumi wa Pakistan unaodidimia bila kuchukua mikopo yoyote. Hata hivyo, serikali yake imevunja rekodi zote za nyuma kwa kukopa dola bilioni 16 katika kipindi cha mwaka mmoja tu – kiwango cha juu zaidi cha mkopo wa nje kwa mwaka kuwahi kufikiwa tokea kuanzishwa taifa la Pakistan mwaka 1947. Imran Khan amekengeuka nyingi ya ahadi zake za wakati wa kampeni, mgeuko huu umempelekea kubambikwa jina la aibu la utani la “U-turn Khan.”

Kwa miongo kadhaa, Imran Khan amejenga heshima yake kama ni mwana harakati wa kupinga ufisadi akiwashutumu wapinzani wake kwa kupora utajiri wa nchi na kupeleka fedha nje ya nchi. Baada ya kupata madaraka, Imran Khan alitegemewa kuanzisha juhudi za kuendelea dhidi ya ufisadi wa kifedha kwa kuregesha kile kinachoitwa pesa zilizoporwa kwenye hazina ya serikali. Lakini jitihada zake dhidi ya ufisadi zimeishia zaidi katika kulenga kuwaweka gerezani wanasiasa wa upinzani wa chama cha Pakistan Muslim League wa aliyekuwa waziri mkuu Nawaz Sharif na hakukuonekana pesa zilizoregeshwa kwenye hazina. Lakini sura nzuri ya Imran Khan ilipata pigo kubwa wakati matokeo ya ripoti moja ya uchunguzi, iliovuja kwa vyombo vya habari kuhusu kuhusika kwa wanachama wa baraza lake la mawaziri katika kuunda sakata ya uhaba bandia wa sukari na unga mwaka 2019 na kuuza bidhaa hizo kwa bei kubwa katika soko la ndani ili kujivunia fedha nyingi. Waliweza pia kupata msamaha wa kodi kwa kuzisafirisha nje!

Likiwa limekumbwa na tsunami ya matatizo makubwa, baraza la mawaziri la chama cha PTI limeanza kuvunja safu. Katika mahojiano nyeti na Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Fawad Chaudhry na Sauti ya Amerika (VOA), aligusia tofauti za ndani ya PTI na kuwalaumu viongozi wakuu kwa kula njama kutimuana; na kuwa kiongozi mkuu Jahangir Tareen aliunda mipango wa kumuezua waziri wa majimbo Asad Umar kutoka kwenye baraza la mawaziri wakati na yeye alikuwa nyuma ya mpango wa kuondolewa kwa Tareen kutoka kwenye nafasi nyeti ya katibu mkuu wa chama. Akielezea “mategemeo makubwa ya watu kutoka kwa PTI na Imran Khan”, Fawad alisema serikali ya kitaifa imeshindwa vibaya mno kuufanya mfumo uwe wa kitaalamu zaidi na ulio huru kupitia marekebisho ya kimfumo. Alisisitiza kuwa “umma haukutuchagua sisi au waziri mkuu kufunga nati na bolti lakini kurekebisha mfumo”. Fawad alikuwa akikariri kuvunjika moyo kunakohisiwa na Wapakistan wengi, waliokipigia kura chama cha Imran Khan kuingia madarakani, walizizuia pumzi zao, katika matarajio yenye kukatisha tamaa ya kuwa muda wa mageuzi ya hatima yao unakaribia. Kulingana na uchunguzi wa karibuni uliofanywa na Gallup: “Asilimia ya Wapakistan wanaoamini kuwa utendaji wa serikali ya sasa ya PTI hadi muda huu katika madaraka yake ni mbaya zaidi kuliko wa serikali iliopita imeongezeka kutoka asilimia 35 mwezi wa Disemba 2018 hadi asilimia 59 mwezi wa Februari 2020.” Imran Khan akijitahidi kuleta umoja wa kinjozi miongoni mwa serikali yake mwenyewe!

Hatua za serikali ya PTI za kukabiliana na maambukizi ya virusi vya korona hivi sasa ni tukio jipya la kushindwa. Kuongezeka kwa kasi kwa visa vya COVID-19 na kuongezeka kwa idadi ya vifo vinahusishwa na uzembe wa Imran Khan katika kuweka amri ya kufunga nchi. Wakati maeneo mengi duniani yakikazania kutekeleza ufungaji nchi ili kupunguza ueneaji wa virusi vya korona, serikali ya Pakistan imekuwa ikifanya mageuzi ya sera zake kuanzia kutokuwepo kwa ufungaji nchi hadi ufungaji nchi wa kijanja. Ukosefu wa uongozi katika mazingira haya yasiyo tarajiwa uliongeza hali kuwa mbaya zaidi. Matokeo yake, Imran Khan hivi sasa ametengwa na jeshi baada ya kushindwa kuwa na maamuzi imara juu ya janga la virusi vya korona. Mnamo Machi 22, waziri mkuu aliliambia taifa kuwa serikali yake haitafunga nchi maeneo yote. Lakini chini ya masaa 24 baadaye, msemaji wa jeshi Meja Jenerali Babar Iftikhar alitangaza kuwa jeshi litasimamia ufungaji ili kuzuia ueneaji wa maambukizi. Tokea hapo, jeshi limepeleka askari kote Pakistan na limekuwa likiongoza utatuzi wa virusi vya korona kupitia Kamati Kuu ya Taifa. Serikali ya PTI imetengwa kikamilifu.

Mradi wa PTI umesimamiwa na kitengo kikuu cha jeshi kwani umma ulikwisha katishwa tamaa na enzi za Musharraf, PPP na PML-N na wamepoteza imani katika serikali. Vijana nchini wameikataa kabisa serikali na kujiingiza kwenye fikra za misimamo mikali. Ni katika muktadha huu ambapo kitengo kikuu cha jeshi kilisimamia maandamano dhidi ya Nawaz Sharif kujenga uaminifu kwa Imran Khan na kuwasukuma wanasiasa waliojijenga kujiunga kwenye safu za PTI na hivyo Imran Khan kuweza kushinda uchaguzi mwaka 2018. Imran Khan bado anapambana dhidi ya madai ya kuwa ‘ameteuliwa’.

Imran Khan kama walivyo watangulizi wake hivi sasa atakumbana na udhalili wa kutengwa ambapo jeshi limeshaanza. Kushindwa kwake hakukuwa tu kwamba alikuwa mchezaji kriketi aliyejifanya mtawala, lakini ni kushindwa kufahamu kuwa alikuwa ni mtumishi tu. Mtumishi kwa ajili ya tabaka teule la watu waliojizatiti na wasiochaguliwa na watu kuanzia viongozi wa juu jeshini na Idara ya Huduma za Ujasusi wa Ndani (ISI) wanaolitegemea kundi la wanasiasa, wataalamu wakuu, na familia zilizoungana vizuri za wafanya biashara ili kufanyakazi kwa ajili yao. Tabaka hili huitazama Pakistan kama ni akaunti zao za kibinafsi inayopaswa kuwahudumia wao, badala ya umma. Hakuna kiwango cha mageuzi kitakachoweza kubadilisha mfumo huu – ni lazima ung'olewe kabisa ili mageuzi ya kweli yaweze kupatikana.

Hili ndilo funzo ambalo watu wa Pakistan sasa lazima wajifunze baada ya kutarajia mcheza kriketi aliyegeuka kuwa mtawala angekuwa tofauti.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Adnan Khan

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu