Jumapili, 12 Rajab 1446 | 2025/01/12
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Mfumo wa Kisekula wa Kirasilimali Unapigia Debe Wanawake Wenye Mamlaka Ambao Hawajaolewa: Shambulizi kwa Jamii Ambayo Tayari Imesambaratika

Habari:

      Katika uzinduzi wa ripoti kuhusu wanawake wenye mamlaka, Kitengo cha Takwimu za Kitaifa nchini Kenya (KNBS) kiliwalinganisha wanawake walioko katika ndoa za mke mmoja, wake zaidi ya mmoja na wajane. Kiwango cha mamlaka kiko juu miongoni mwa wanawake ambao hawajaolewa (asilimia 37), lakini kinashuka kuwa asilimia 27 punde wanapofunga ndoa au wanapoanza kukaa na mwanamume. KNBS ilielezea kuwa mamlaka ni uwezo wa kufanya maamuzi (The Star, 12/08/2020).

Maoni:

Ripoti hii kutoka kwa KNBS ni uthibitisho uliochungu kwamba maadili huria ya kijamii yamekita mizizi nchini Kenya. Hata hivyo, utafiti huu haushtushi kwani Kenya ilikuwa na bado imebakia kuwa ni ‘koloni’ la Uingereza, ambalo limejifunga na nidhamu huria ya kijamii kutoka kwa bwana wake. Kwa kuongezea, haya ni matunda ya juhudi za muda mrefu kutoka kwa wale wanaoitwa wakombozi wa wanawake ambao wanaungwa mkono na mashirika ya Kimagharibi kama vile Wanawake wa UN, UNICEF miongoni mwa mengine ambayo yanakwenda mbio kuhakikisha kuwa kiungo cha familia na uwiano wa kijamii unaangamizwa duniani kote.

Ni muhimu kutambua kuwa ripoti hii inakuja siku nne tu baada ya vyombo vya habari kuripoti matamshi ya Fellister Abdalla, Mratibu wa Jamii ya Wafanyakazi wa Ngono nchini Kenya aliyesema kwamba wafanyakazi wa ngono ‘wasichana’ huko Nairobi watapoteza zaidi ya milioni Sh20 za mapato ndani ya kipindi cha siku 30 kwa kuwa mabaa na madanguro yatabakia kufungwa kutokana na agizo la Rais kuhusiana na kafyu iliyowekwa chini ya kisingizio cha kupambana na janga la Covid-19 (The Standard, 08/08/2020). Viwango vya talaka viko juu huku uzinifu, miradi ya kukuza mamlaka katika usawa wa kijinsia kama vile elimu ya masomo ya juu na fursa za ajira zikitajwa kuwa ni moja ya sababu kubwa za kuwepo kwa janga hilo la ndoa na kuvunjika kwa jamii nchini Kenya. Hivi sasa kuna viwango vya juu vya mimba kwa mabarobaro!

Hali hiyo hapo juu inaashirikia sifa ya maumbile ya mfumo tawala wa kisekula wa kirasilimali ambao Kenya imeasisiwa juu yake. Hivyo basi, mtazamo wa Kenya juu ya wanawake upo ndani ya ushindani wa usawa wa kijinsia kwa muktadha wa mahusiano ya uwezo wa uzalishaji unaozingatia gurudumu la kiuchumi. Katika nidhamu kama hiyo, ndoa hudunishwa na kuonekana kuwa ni mzigo au gereza ambalo kwamba wanawake hutaabika wakiwa jikoni pasina mustakbali ‘mzuri’ wakilinganishwa na wenzao wanawake ambao wako huru, hawajaolewa na wana mamlaka wanaoishi kwa raha tele! Kwa kuongezea, vyombo vya habari vinatumika kupepeprusha vipindi na michezo ya kuendelea ambayo inamakinisha dhana ya kuwa wanawake waliofaulu ni wale walioko katika taasisi wakipigia debe sera muhimu na kuchanganyika na wanaume katika kushindana kwao daima katika dori ya mchumaji mkate na kudai haki sawa! Hivyo basi, mamlaka kwao ni uhuru wa kubakia pweke lakini wakiwa na uwezo wa kujitegemea kisiasa, kijamii na kiuchumi!

Katika nidhamu ya Kiislamu, ndoa inathaminiwa kwani ndio kiunganishi kinachozalisha kiungo cha familia ambayo ndio uti wa mgongo na jiwe la ujenzi wa jamii. Shari’ah ya Kiislamu inaamrisha kwamba jamii ilindwe kutokamana na fahamu za sumu ambazo zinachipuza kutoka kwa chochote kile kigeni kinachojumuisha sio tu mfumo wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu yake ya kihuria ya kijamii. Katika Uislamu jukumu msingi la mwanamke ni kwamba yeye ni mama na muwajibikaji wa nyumba na ni tunu inayostahiki kulindwa. Mwenyezi Mungu (swt) alimpa mwanake jukumu hilo na wakati huo huo akamruhusu kuyaendea majukumu ya ziada kama kuwa muajiriwa, muajiri, mfanyibiashara n.k kwa sharti kwamba jukumu lolote la ziada lisiwe kizuizi katika kutekeleza jukumu lake msingi. Dola ya Kiislamu ya Khilafah iliyosimama kwa njia ya Utume ndio ngao na mlinzi wa ndoa, kiungo cha familia na jamii ambayo itahakikisha kuwa kuna maendeleo na ustawi wa kweli kama natija ya utulivu utakaoshuhudiwa na raia wake. Lazima #TuikoeFamilia kwa kulingania Khilafah.

Imeandikwa kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumatatu, 17 Agosti 2020 14:16

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu