Jumatano, 22 Rajab 1446 | 2025/01/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi

Zana ya Kuendeleza Mamlaka ya Kikoloni

Habari:

Mnamo Jumanne, 9 Machi 2021 Bunge la Kenya liliidhinisha Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi (EPA) na Uingereza. Makubaliano hayo yatazipa bidhaa za Uingereza miaka 25 ya kutotozwa ushuru zinapoingia Kenya. (Daily Nation).

Maoni:

Kuidhinisha kwa Kenya kunafuatia yale ya Bunge la Uingereza ambalo lilikuwa na mjadala mnamo Jumanne, 2 Machi 2021. (Business Daily, 09/03/2021). Hata hivyo Bunge la Kenya lilipitisha makubaliano hayo ya kibiashara huku likiwa na mashaka nayo. Mwanzoni kutokana na wasiwasi wao ilipelekea kuhairishwa kwa mjadala kuhusiana na makubaliano hayo baada ya kutopokea orodha ya bidhaa ambazo hazitotozwa ushuru! Wabunge walikasirishwa na kipengee ndani cha sheria ya EPA ambacho kinaelezea kwamba hakutakiwi kufanywa marekebisho wakati makubaliano hayo yanaidhinishwa.  (The Star, 26/02/2021). Kwa kuongezea, kamati ya Bunge ya Fedha ilidai kuwa haikuhusishwa katika mchakato wa mazungumzo licha ya kwamba wao ndio wanaosimamia masuala ya ushuru. (Daily Nation, 26/02/2021).

Hatimaye, Bunge la Kenya lilidhinisha mpango huo likiwa na matumaini kwamba baadhi ya vipengee ndani ya EPA vinampa Waziri wa Kenya kujitoa katika mpango huo na anaweza kufanya marekebisho wakati wa utekelezaji wake. Kwa kuongezea, baadhi ya Wabunge waliahidi kubadilisha Sheria ya Mikataba ili bunge liwe linahusishwa katika mazungumzo kuanzia mwanzo siku zijazo. Hivyo basi, hayo ndiyo yanayohitimisha mchakato ulioanza kwa kutiwa saini mpango wa kibiashara mnamo Jumanne, 8 Disemba 2020 mjini London baina ya Waziri wa Biashara ya Kimataifa Ranil Jayawardena na Waziri wa Biashara Betty Maina kwa niaba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), licha ya kwamba Jukwaa la Wakulima Wadogo na Econews Afrika kwenda mahakamani ili kusitisha kuidhinishwa kwa makubaliano hayo wakisema kwamba hakukuwepo na mashauriano mapana baina ya washikadau kuhusiana na suala hilo!

Ni jambo la kuvunja moyo kushuhudia kutiwa saini na kuidhinishwa kwa mpango huu. Kijuujuu unaonekana kuwa unanusuru taifa letu kiuchumi. Inadaiwa kwamba tunaweza kusafirisha bidhaa zetu kwenda Uingereza pasina kutozwa ushuru punde makubaliano yatakapoidhinishwa.  Ukweli uliowazi ni kwamba taifa letu hadi sasa limebakia kuwa ni sehemu ya shamba la bwana mkoloni wa zamani ambalo sera na kanuni zake zinategemea maslahi ya bwana. Inajulikana wazi kwamba wale wanaosafirisha bidhaa kwenda Uingereza ni kipote cha mabwenyenye wachache walioko uongozini kwa niaba ya wakoloni Wamagharibi. Baadhi yao wanamiliki na kudhibiti sekta muhimu nchini kama ukulima wa chai, kahawa, maua n.k. Hivyo basi, ni wao ndio watakaoendelea kufurahia matunda ya mpango huo. Kwa upande mwingine, itawakandamiza wengi katika wanaotaabika kujitafutia riziki na kuwatia katika shida zaidi kutokana na kufurika kwa bidhaa za Uingereza nchini. Kwa hiyo, uchumi wetu utaendelea kuwa katika minyororo ya Uingereza.

Kwa hakika hizi ni njama mpya kutoka kwa Uingereza iliyokata tamaa kwa kuwa haiba yake inaendelea kudorora duniani kote kabla na baada ya kujitoa katika Muungano wa Ulaya. Kuyaelekea makoloni yake ya zamani ni sehemu ya mchoro wake mpana ili kuinusuru sura yake kiulimwengu. Ili kufikia malengo yake, inawapatiliza watawala wake vibaraka wakoloni kupitisha sheria hatari. Na kupelekea kuzifichua zile zinazoitwa taasisi huru kama vile bunge letu kwa umma na kuzifedhehesha kwa kuwa ni mamlaka za kutia sahihi kwa kushurutishwa na serikali!

Wakoloni Wamagharibi wanaendelea kutia sumu na kutawala kwa kutumia mfumo wao wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake za sumu. Wanaendelea kusababisha majanga katika maisha yetu kiasi kwamba watu wanaomba kufa kuliko kuishi, kutokana na kuporwa kwa rasilimali zetu na kukazanishwa kwa vitanzi vya kiuchumi kupitia sera za utozaji ushuru zinazopigia debe umasikini na kulimbikiza utajiri kwa wachache. Hivyo basi kuzidisha pengo kati ya matajiri na masikini. Kwa kuhitimisha EPA inaoneka kuwa nzuri katika karatasi lakini ni yenye maangamivu katika utekelezaji. Kama ilivyofichuliwa na maelezo  yaliyotolewa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Miradi ya Maendeleo kupitia nakala aliyoiambatanisha na EPA iliyo wasilishwa Bungeni mnamo 22 Disemba 2020 ili kutaka uidhinisho. “Kenya inataka kufungua asilimia 82.6 ya thamani ya biashara jumla kwa Uingereza kwa zaidi ya kipindi cha mpito (miaka 25 huku kukiwepo na miaka 7 kuhairisha) ikijumuisha mali ghafi, bidhaa za kuzalisha bidhaa na huduma, bidhaa zinazotumika katika mchakato wa kuzalisha bidhaa na huduma na bidhaa zote muhimu.” (Daily Nation, 22/02/2021).

Imeandikwa kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Ali Nassoro Ali

                                 Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu