Jumapili, 22 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/24
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Je, Waislamu Wanapaswa Kukubali Hali ya Kawaida ya Migogoro?

 (Imetafsiriwa)

Habari:

Zaidi ya wakimbizi 100 wa Rohingya walikwama huko Aceh, Indonesia, mapema Jumapili, Machi 6, 2022. Warohingya 114, wakiwemo wanaume 68, wanawake 21 na watoto 35, walikwama huko Kuala Muara Raja, Wilaya ya Kuala, Bireuen Regency, Aceh. Republika iliripoti mnamo Machi 18 kwamba hali ya wakimbizi wa Rohingya huko Aceh ilikuwa inazidi kuwa mbaya kutokana na kupuuzwa.

Maoni:

Matukio kama haya katika karne ya 21 ni jambo la kawaida kuyaona. Kwa Waislamu wa Indonesia na Malaysia, tukio la Waislamu wa Rohingya waliokwama si geni. Kama mduara mbaya, kipindi baada ya kipindi cha hadithi ya kusikitisha ya ndugu na dada zetu Waislamu, walioteswa na kufukuzwa kutoka katika nchi yao wenyewe, haujaacha kuzunguka.

Enyi ndugu zangu na dada zangu Waislamu wa Rohingya, kuweni na subira! Imani pekee moyoni na imani ya Akhera ndio silaha ya kustahamili mateso haya. Mwenyezi Mungu (swt) asema:

(فَٱلَّذِينَ هَاجَرُوا۟ وَأُخْرِجُوا۟ مِن دِيَٰرِهِمْ وَأُوذُوا۟ فِى سَبِيلِى وَقَٰتَلُوا۟ وَقُتِلُوا۟ لَأُكَفِّرَنَّ عَنْهُمْ سَيِّـَٔاتِهِمْ وَلَأُدْخِلَنَّهُمْ جَنَّٰتٍ تَجْرِى مِن تَحْتِهَا ٱلْأَنْهَٰرُ ثَوَابًا مِّنْ عِندِ ٱللَّهِ ۗ وَٱللَّهُ عِندَهُۥ حُسْنُ ٱلثَّوَابِ)

“...Basi walio hama, na walio tolewa makwao, na wakateswa katika Njia yangu, na wakapigana, na wakauliwa, kwa yakini Mimi nitawafutia makosa yao, na kwa yakini nitawaingiza katika Mabustani yanayo pita mito kati yake. Hayo ndiyo malipo yanayo toka kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu kwake yapo malipo mema kabisa.” [Aali ‘Imran: 195].

Hii ndio sifa ya kipekee ya Waislamu, imani ya msamaha na ahadi ya Mwenyezi Mungu hutufanya tuwe na uwezo wa kustahimili migogoro na majanga yoyote. Lakini kwa kiwango kikubwa zaidi, Mwenyezi Mtukufu pia anatuamrisha kupambana kwa ajili ya mabadiliko, kuanzia kuelewa kiini cha tatizo. Mgogoro huu unatokana na ukosefu mkubwa wa haki wa kimfumo na unatokana na uharibifu wa kimsingi wa hadhara ya mwanadamu leo. Dhulma hiyo ilianza kutokana na kupuuzwa kwa sheria za Mwenyezi Mungu na kutekelezwa kwa sheria za kisekula zilizotungwa na mwanadamu katika ardhi za Waislamu.

Kuishi katika ulimwengu wa Urasilimali kunatufanya tushuhudie misukosuko na mikasa isokwisha, moja baada ya mwengine, katika sehemu mbalimbali za dunia na katika nyanja mbalimbali za maisha. Kadiri muda unavyosonga, misiba imekuwa kawaida, na maafa yamekuwa ya kawaida. Kitu hicho kwa hicho kinawatokea Waislamu wa Rohingya. Mgogoro wa Rohingya umekuwa ukiendelea kwa takriban muongo mmoja. Waislamu wa Rohingya wamevutia hisia za kimataifa baada ya ghasia za Jimbo la Rakhine za mwaka 2012, miaka kumi iliyopita. Kilele cha mkasa wao kilitokea mwaka 2017 ambapo takriban Waislamu 7000 wa Rohingya walikufa kutokana na mauaji ya halaiki yaliyotekelezwa na utawala wa junta wa Myanmar kwa ushirikiano na vuguvugu la itikadi kali la Mabudha nchini humo. Mgogoro wa Rohingya bado haujakwisha, mithili ya karma, Myanmar kwa sasa inakabiliwa na mgogoro wa ndani wa muda mrefu kutokana na mapinduzi ya kisiasa ya Junta ya Kijeshi dhidi ya matokeo ya uchaguzi wa hivi karibuni ambao ulishinda upande wa Aung San Suu Kyi. Chama cha Msaada kwa Wafungwa wa Kisiasa kiliripoti kwamba tangu mapinduzi hayo yafanyike Februari 2021, takriban waandamanaji 1,600 na waangalizi wamekufa. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, linakadiria kuwa watu 837,000 wamefurushwa kutoka Myanmar.

Mfumo huu fisadi wa kiulimwengu umetulazimisha kukubali hali ya kawaida ya  dhulma na migogoro. Migogoro hii imewafanya Waislamu kila wakati kuishi katika hali ya kustahamili, jinsi ya kuendelea kuishi katikati ya migogoro, kama janga la Korona ambalo linatulazimisha kuishi katika hali mpya ya kawaida. Hata hivyo, matokeo yake Ummah huu umepoteza hisia ya dhulma, na taratibu umekubali misiba kama kitu cha kawaida. Na'udzubillah min dzalik!

Mipaka ya dola za kitaifa pia imewatenga Waislamu wa Rohingya kutoka kwa ndugu zao Waislamu wa Bangladesh, Malaysia na Indonesia, pamoja na Waislamu wa Uyghur waliotelekezwa katika ukatili wa China na watawala Waislamu kwa sababu walitanguliza maslahi yao ya kiuchumi ya kitaifa, hii ikiwa ni mbali na mamia ya maelfu ya wakimbizi Waislamu wasio na uraia waliofukuzwa kutoka Syria, Iraq na Palestina. Hakika hii ni gharama kubwa ya mgawanyiko wa Ummah. Urasilimali na utaifa umegawanya, kudhoofisha na kuwafanya Waislamu mithili ya mayatima waliopoteza walezi na maisha yao yanategemea majambazi washambuliaji wanaotulenga mmoja baada ya mwengine kila uchao.

Maisha ya Waislamu yamekuwa duni sana. Takriban Waislamu milioni 12.5 wameuawa katika vita katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, kulingana na mtaalam wa Historia - Refik Turan ambaye alizungumza kwenye mkutano mnamo 2018 jijini Istanbul. Takwimu hii haijumuishi takwimu za Waislamu wa Rohingya na Uyghur. Zaidi ya hayo, mamilioni ya Waislamu walikufa kutokana na njaa, maradhi, uhamiaji na majanga yanayosababishwa na wanadamu pia hayamo katika orodha hii.

Enyi Waislamu, inukeni! Tuchukueni hatua na tusongee ipasavyo. Msiendelee kuitikia juu juu, kwa muda mfupi au katika hali ya kujitetea! Msikubali kamwe hali ya kawaida kwa misiba! Badala yake ni lazima tupigane dhidi ya dhulma zote na kuregesha mfumo wa maisha wa Kiislamu ambao utalinda uhai, mali na heshima ya Umma wa Muhammad. Mwenyezi Mungu Mtukufu asema:

 (اِنَّ اللّٰهَ لَا يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتّٰى يُغَيِّرُوْا مَا بِاَنْفُسِهِمْۗ) “Hakika Mwenyezi Mungu habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo naf- sini mwao.” [Ar-Ra’d: 11].

Sentensi "maa bi anfusihim" au yaliyomo ndani yao, ina upeo mpana wa maana. Maana yake inajumuisha fikra, maadili, na roho ya mwanadamu katika muktadha wa mwamko wa Umma. Hii ina maana kwamba mabadiliko hayatatokea kamwe ikiwa watu hawatabadilisha mtazamo wao, madhumuni ya maisha na ufahamu wao wa janga na mgogoro. Kwa hivyo, mara nyingi tunakutana na watu ambao hawawezi kujibu udhalimu kwa sababu hawaelewi kile hasa kilichotokea. Hawana uwezo wa kujibu kuwa ni dhuluma kwa sababu ya kutojua kusoma na kuandika na michakato dhaifu ya kufikiria.

Rasulullah saw ametoa mfano bora wa mapambano ambayo yamerithishwa kwetu. Alianza na kujenga nafsi na akili za Waislamu, kwa ujenzi wa kisiasa, hivyo kwamba Ummah uliinuka na kuwa na hisia kali kwa dhulma. Pia daima aliuwekea Ummah ulinzi kwa sheria za Mwenyezi Mungu na kuzuia migawanyiko baina yao. Pia anauwajibisha Ummah wake kuishi chini ya uongozi mmoja wa kisiasa (Khilafah). Ni haramu kwa Ummah kuishi katika vipande vipande chini ya uongozi wa kisiasa zaidi ya mmoja, achilia mbali kuishi kwa kudhulumiwa chini ya dhulma ya wengi wa Makafiri.

Kwa hivyo kwa Waislamu, migogoro na misiba daima itakuwa ni hali isiyo ya kawaida, hata matokeo ya udikteta unaowakumba. Mapambano na harakati za Ummah ni lazima zijikite kwenye dhamira ya kuregesha ngao iliyopotea kwa Ummah. Ngao ambayo itaondoa dhulma ya makafiri juu ya Waislamu na kulinda damu na heshima ya Waislamu wanawake na watoto katika ulimwengu wa Kiislamu! Wokovu pekee kwa Ummah ni kurudi kwa kwa msingi wa manhaj ya utume.

«إنما الإمام جنة يقاتل من ورائه ويتقى به» “Hakika Imam ni ngao, watu hupigana nyuma yake na hujihami kwayo." [Sahih Muslim]

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari Hizb ut Tahrir na
Dkt. Fika Komara
Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu