Ijumaa, 20 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Wako wapi Wanaume?

Mwanachuoni, Sayyid Qutb, katika kitabu chake kwa jina, “Katika Kivuli cha Qur’an” kuhusiana na aya: ﴾وَإِذۡ قَالَ رَبُّكَ لِلۡمَلَـٰٓٮِٕكَةِ إِنِّى جَاعِلٌ۬ فِى ٱلۡأَرۡضِ خَلِيفَةً۬﴿ “Na pale Mola wako Mlezi alipo waambia malaika, ‘Mimi nitamweka katika ardhi Khalifa (mfwatizi).’” [Al-Baqarah: 2:30] Alisema kwamba zipo fahamu na mazingatio msingi mawili kuhusiana na mwanadamu kama bwana wa ardhi ambayo ni kama ifuatavyo:

Kwanza – mwanadamu ni bwana juu ya ardhi; kila kitu kimeumbwa kwa ajili ya manufaa na furaha yake. Hili humnyanyua mwanadamu juu ya viumbe vingine na huharamisha kumkandamiza na kumfedhesha kwa ajili tu ya maendeleo ya kimada. Ubinadamu wa mwanadamu lazima uheshimiwe na kulindwa; hakuna katika haki zake msingi au maadili hutakiwa kukiukwa au kuharibiwa kwa sababu yoyote ile. Vitu vya kimada vipo kwa ajili ya kumtumikia mwanadamu na vimetengenezwa kwa ajili ya kupiga jeki ubinadamu wake na kuboresha uwepo wake. Hivyo basi, haingii akilini kwamba maendeleo yake yapatikane kwa kulipa gharama ambayo itatishia maadili yake, heshima na hadhi yake.  

Pili – dori ya mwanadamu ardhini ni ya umuhimu mkubwa. Mwanadamu, na wala sio njia za uzalishaji au usambazaji, ndio nguvu ya kuleta mabadiliko ardhini; yeye hushawishi na kubadilisha mambo yote katika uhai wa ardhini. Kinyume na mtazamo wa kimadaniya, mwanadamu ndio bwana, na sio mtumwa wa mashini.

Kwa kuongezea, mwanachuoni na muasisi wa Hizb ut Tahrir, Sheikh Taqiuddin an-Nabahani, asema katika kitabu chake, Kufikiri (At-tafskir): Mwanadamu ndiye kiumbe pekee kilicho fadhilishwa zaidi; hata kiasi kwamba imesemekana – ambako ni kweli – kwamba amefadhilishwa zaidi kuliko malaika. Akili (‘aql) ya mwanadamu ndiyo iliyo nyanyua cheo chake, na kumfanya kuwa juu ya viumbe vyote.

Dunia hivi sasa inasumbuka na imezama katika fujo. Kila mmoja anaotesha vidole na kuwalaumu wanawake kuwa ndio chanzo cha machafuko ya kijamii kama kuzidi kwa viwango vya talaka, kuvunjika kwa familia, na kuwepo kwa watoto wakorofi miongoni mwa maovu mengine. Kiupande wa kiuchumi, wanawake wanalaumiwa kuwa wameweka kipaumbele ajira zao na kuleta mashaka katika sekta ya uajiri kwa kutoa huduma kwa bei duni na wanapatikana kwa wepesi kutoa nguvu zao kwa waajiri walafi. Kwa upande mwingine, wanawake sasa wanashindana na wanaume katika kupanda ngazi za kisiasa. Kwa kifupi, wanawake wapo katikati wakibeba lawama zinazochipuza kutoka kwa wanaume duniani kote.

Hakika, ukweli ni kwamba wanawake ni wahanga wa wanaume waliofeli kuitikia na kubeba majukumu kama ilivyotarajiwa sio tu na Shari’ah ya Kiislamu, bali hata asili ya maumbile ya kiume. Mwanamume kiasili anacheza dori ya kiongozi na mwenye mamlaka juu ya viumbe vingine. Hivyo basi, mwanamume lazima awe na lengo / misheni ya kwa nini yupo katika dunia hii ya muda mfupi. Kwa kuongezea, lazima awe na maarifa ya kidharura kuhusiana na lengo lake na namna ya kulitimiza. Misheni ya mwanadamu hapa katika dunia ya muda mfupi imefupishwa katika aya hii,﴾وَمَا خَلَقۡتُ ٱلۡجِنَّ وَٱلۡإِنسَ إِلَّا لِيَعۡبُدُونِ﴿  “Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi.” [Adh-Dhariyat: 51:56]. Kumwabudu Mwenyezi Mungu (swt) kunamaanisha kujisalimisha kwa maagizo Yake kwa maana kujifunga na maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake pasina kuzingatia natija (madhara au manufaa) inayotoka kwayo.

Kwa hivyo, mwanadamu anaposonga mbele katika maisha kama mtumwa wa matamanio yake basi bila shaka tunatarajia maisha ya majanga na watu kuzama katika vina vya chini katika ufuska na kutobeba majukumu. Katika jamii ya leo, hatuko salama kutokamana na mporomoko wa kisiasa, kijamii, kiuchumi na kielimu. Mwanamume, kama kiongozi amefeli kuitumia akili yake kutafuta njia sahihi kumuelekea Muumba wake; hivyo basi amedumu katika kazi za kubahatisha kwa kisingizio cha uhuru usiokuwa na mipaka! Na kupelekea meli (familia) kuendelea kuzama ndani zaidi kwa sababu mwanamume, kama nahodha, hana lengo na ruwaza!

Wanaume wa karne ya ishirini na moja wamepoteza uume wao! Ni watumwa wa matamanio yao kiasi kwamba wamekuwa vipofu na hawaioni dori ya uume waliotwikwa na Mwenyezi Mungu (swt). Kidhati, wameikana dori yao ya uongozi na badala yake wamemakinisha akili na muda wao katika kuzifukuzia starehe zisizoeleweka, hadaifu na za kilafi za ulimwengu huu wa muda mfupi huku hawazingatii mahangaiko na mdororo wa kisiasa, kijamii, kiuchumi na kielimu duniani kote.  

Ala! Sio jambo la kushangaza kuwashuhudia wanaume leo ambao hawawezi kuwakidhia familia zao mahitaji msingi. Hata hivyo, watu hao hao wanaweza kumudu kununua simu za mkononi au vifaa vya kidijitali vya kisasa ambavyo vina thamani ya mahitaji msingi ya miezi miwili kwa ajili tu ya kuonekana kuwa wanakwenda na wakati ndani ya jamii. Badala ya kujenga maktaba ya nyumbani na kuijaza vitabu adhimu ambavyo vitaziimarisha familia zao, baadhi ya wanaume wanashindana na kujifahiri katika kununua runinga kubwa au vituo vya michezo vya kisasa kwa familia zao! Wanaume wa zama zetu wamezama katika upuzi na mambo duni kwa sababu hawana misheni au ruwaza; daima wanapiga miayo na wana njaa ya anasa zinazofuata. Wanaume wametingwa na shughuli zao ilhali wanawake, watoto na wazee wamesakamwa na machozi ya kukata tamaa baada ya kutaka msaada ambao hawaupati! Wanaume wamesalimu amri ndani ya nyumba zao (meli) na hivyo basi wanachama wa familia (abiria) kila mmoja amejimakia!

Ala! Haingii akilini kuwaona wanawake wakiitikia na kuchukua silaha ili kujikomboa kutoka kwa makucha ya madhalimu kama Bashar al-Assad nchini Syria. Kwa upande mwingine, wanaume wanashughulika kupiga njama ili kuubakisha mamlakani utawala huo huo! Wanaume wa zama zetu hawakuisaliti jamii tu bali hata afya zao wenyewe! Inakuwaje mwanamume kuwa na tumbo kubwa huku akiwa na majititi yote kwa kisingizio kuwa ni ishara ya kufaulu kwake ndani ya jamii! Siku hizi imekuwa vigumu kutofautisha baina ya mume na mke, nani kati yao anakaribia kujifungua? Kwa sababu wote daima wamenenepa na kuchoka! Kinyume chake, wanaume ni wembamba nje na wanene ndani (TOFI). Kuna jambo haliko sawa, na wanaume wanatakiwa kuzinduka kutoka usingizini na kuchukua uongozi. Wasipofanya hivyo, mambo yalivyo sasa lau yatabakia hivyo pasina kushughulikiwa, basi janga la kiafya lililoko mbele yetu litakuwa ni tone baharini tukilinganisha na linalo kuja!

Hayo hapo juu ni taswira tu ya hali ya kutamausha inayoikumba dunia leo. Ni kutokamana na kufeli kuwalea wanaume wa kweli ili kubeba dori ya uongozi na kuiongoza dunia. Jamii leo inawalea vijana wa kina mama ambao wanakuwa na kuchukua nyadhifa za uongozi na kuendeleza tabu za kisiasa, kijamii, kiuchumi na kielimu zinazoshuhudiwa leo!

Wakati ni sasa kuwalea na kuwakuza wanaume wenye ikhlas ambao watakuwa Waislamu wanachuoni, watawala na wanajeshi katika njia ya Mwenyezi Mungu (swt) ma Mtume Wake (saw). Wanaume ambao hawataogopa lawama kutoka kwa yeyote: Wanaume ambao watakuwa tayari kuhimili shinikizo zozote zinazochipuza kutoka kwa wale walio na akili dhaifu miongoni mwa watu: Wanaume ambao hawana muda kushiriki usengenyaji: Wanaume ambao viwango vyao vya akili tambuzi viko juu katika kutekeleza haki kwa yeyote pasina kujali kabila, rangi, hali ya kisiasa, kijamii, kiuchumi na kielumu: Wanaume ambao wako tayari kufanya biashara na uhai wao ili kununua Jannah kwa ajili ya kuilinda hadhi ya Mtume Muhammad (saw) na ujumbe wake: Wanaume walio tayari kutupilia mbali hali zao za utulivu na kujitosa katika vina vya chini katika kuitikia mwito wa Mwenyezi Mungu (swt) na Mtume Wake (saw) katika lile linalopeana uhai: Wanaume walioweka kipaumbele utafutaji wa Akhera na kuyakimbilia yale yote ambayo yatatilia shime juhudi zao kutimiza lengo lao hilo.

Suali msingi ni wako wapi wanaume? Hakika, wanaume wapo, bali tunapolitizama na kulichanganua suali kwa mtizamo wa kijuujuu, itamaanisha wanaume waliovalia suruali au kanzu za Waislamu n.k. Hata hivyo, tunapozama ndani na kulitathmini suali kwa kina, linatuchochea ili kutafakari hali iliyoko sasa ya wanaume wetu. Lau kila mmoja wetu atajitafakari kwa kina atafikia uamuzi kuwa tupo hapa tulipo kwa sababu ya mawazo ya kisekula tunayo yabeba. Mawazo yetu huzalisha fahamu zetu, nazo huepelekea kupatikana kwa vitendo vyetu. Hivyo basi, ili kubadilisha hali ya kutamausha iliyoko sasa ya wanaume duniani kote, ni lazima tujifunge na yafuatayo:

Kwanza, kujifunza Shari’ah ya Kiislamu; inayojumuisha kuisoma, kuielewa na kujifunga na Qur’an kama muongozo wa milele kwa wanadamu. Kwa kuongezea, lazima tuifahamu Sunnah (Hadith) kwa kuwa ni kiunga mkono na kipambanuzi cha Qur’an, kwa sababu vitendo vyetu vinatakiwa kuwa kwa mujibu wa Shari’ah ya Kiislamu. Na natija yake ni kuwa vitendo vyetu vikiifuata, basi itakuwa vinathibitisha utumwa wetu kwa Mwenyezi Mungu (swt) na huwa tunatarajia kupata huruma na radhi Zake. Mwenyezi Mungu (swt) asema, ﴾إِنَّمَا يَخۡشَى ٱللَّهَ مِنۡ عِبَادِهِ ٱلۡعُلَمَـٰٓؤُاْۗ﴿ “Kwa hakika wanao mcha Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wanazuoni. [Fatir: 35:28]. Kwa kuongezea, Abu Hurairah amesimulia kwamba Mtume (saw) alisema, «مَنْ يُرِدِ اللَّهُ بِهِ خَيْرًا يُفَقِّهْهُ فِي الدِّينِ» “Mwenyezi Mungu anapomtakia mtu khair, Humuwezesha kuifahamu dini.[Sunan Ibn Majah].

Pili, kujifunza elimu ya ziada inayohusiana na mambo msingi ya kimaisha; ambayo itatusaidia katika kutekeleza shughuli zetu za kila siku katika maisha mfano kama kujifunza kuendesha gari n.k.

Tatu, lazima tutenge muda wa kuwa faragha peke yetu; kwa maana tutenge sehemu faragha kwa ajili ya kutafakari, kuitathmini thamani yetu na mchango wetu katika hali ya maisha ya familia na jamii zetu na taifa na dunia yetu kwa ujumla. Lazima tujiulize maswali kama: Mimi, familia na jamii yangu, na wanadamu kwa ujumla tupo katika njia ya sawa iliyo azimiwa na Mwenyezi Mungu (swt) au sisi ni mazumbukuku tunaofuata mkumbo?

Nne, kujikurubisha na uchache; daima kujisukuma kuwa mchache. Mtu mchache ni mtu ambaye ametosheka na kichache anachohitaji ili kukamilisa safari hii maisha ya muda mfupi. Mtume Muhammad (saw) aliongoza kwa mfano, licha ya kuwa ni Mtume na mtawala, aliishi maisha mepesi kabisa, mchache asiyekuwa na mfano. Lazima iwe wazi kwamba kuwa mchache sio sawa na kujibunia matatizo, bali kunamaanisha kila kilicho cha ziada unakiwekeza (unakitoa) kama sadaqah katika njia ya Mwenyezi Mungu (swt) na Mtume Wake (saw). Hili linawezekana tu kupitia kujiuliza kiukweli, ni kiasi gani cha mali kinachotutosha katika mali tunazomiliki?

Tano, kufunga mara kwa mara; inamaanisha kwamba tule mlo mmoja au miwili kwa siku. Pia, twaweza kuigiza kufunga kwa Mtume Daud (as) kwa kufunga leo na kutofunga siku ifuatayo. Kwa upande mwingine, tunapofungua kiamshakinywa lazima tule vyakula na sio bidhaa za chakula ikimaanisha lazima tule vyakula ambavyo vinatunufaisha kwa virutubisho na SIO bidhaa za chakula zisizokuwa na virutubisho, bali huwa ndio chanzo cha kusababisha maradhi katika miili yetu. Kufunga mara kwa mara tena kwa muda mrefu hupelekea hali ya autofaji. Autofaji huruhusu miili yetu kuweza kuzisafisha seli za zamani katika miili na kuziwezesha kufanyakazi kwa ubora zaidi. Hii ni hatua ya kimaumbile ambayo huanza punde tu seli zetu zinapokosa au kunyimwa virutubisho.

Sita, mazoezi ya mara kwa mara; hususan ya kunyanyua uzani yanayojumuisha na kujulikana kwa lugha ya Kiingereza kama, ‘bench press, deadlifts, overhead (ovh) shoulder press, squats na rows.’  Kwa kuongezea, kushiriki mazoezi ya kasi mno kwa muda mfupi (HIITS) kama kukimbia mbio fupi. Kwa kifupi mazoezi ambayo yatahusisha tishu za misuli, ini, kongosho na mafuta ili kunufaika kiafya ya kiwiliwili, kiakili na kiujumla.

Saba, kusoma vitabu daima; itakusaidia kufikiri kwa umakinifu na ubunifu kwa kila suala utakalo kumbana nalo. Fauka ya hayo, kiwango chako cha kujiuliza maswali kitazidi na kukupelekea kuzidi kiu cha kutaka taarifa itakayo kupelekea kusoma zaidi. Imarisha uhai wa akili yako kwa kujenga maktaba ambayo utaitumia kama chemichemi ya kifikra ambayo utakuwa unairudia unapokwama juu ya baadhi ya masuala au unapotaka kupata msukumo au uchanganuzi juu ya suala lolote. KUMBUKA kitabu nambari moja kuwepo ndani ya maktaba yako ni Qur’an Kareem kisha vingine.

Nane, sikiza audio au tizama video; ambazo zinaongeza thamani yako na mchango wako kama mwanamume katika dori yako kama kiongozi wa familia, jamii na wanadamu kwa ujumla.

Tisa, ­ilinde akili na muda wako; hizi ndizo rasilimali zako za KWELI ambazo za kuhitajia kuwa na nidhamu, mpangilio na ujuzi ili kuweza kuzitumia ili kuweza kufikia kilele cha ufanisi. Kumbuka kwamba kila (mawazo) kinachoingia akilini mwako kitaamua utakavyokuwa. Ama kuhusu muda wetu, daima unakimbia dhidi yetu ikimaanisha kuwa hauwezi kupatikana tena, unapotoweka ndio umekwenda, lakini kila sekunde itahesabiwa na Mwenyezi Mungu (swt) Yaumul Nadama (Qiyama). Daima lazima tuufananishe ulimwengu na ubao, na katika mikono yetu, tunazo chaki zilizo fungamanishwa na wakati ambazo daima zinaandikwa kwa ajili ya kizazi chetu kijacho kutusoma. Andika uchafu na kizazi chako kitasoma hicho haswa!

 Kumi, jiunge na chama au kundi la watu ambalo limejikita katika kuleta MAPINDUZI ya KWELI na ya KIMSINGI. Pamoja nao fanyakazi kuelekea lengo moja la kubadilisha hali mbaya iliyoko sasa ya wanadamu duniani kote. Hali ya maisha ya wanadamu itaboresheka kwa sharti kuwa chama kitajituma kurudisha maisha ya Kiislamu kwa msingi wa Shari’ah ya Kiislamu. Hivyo basi, lengo kuu la chama hicho lazima liwe ni kurudisha tena Nidhamu ya Uongozi wa Kiislamu, Khilafah kwa njia ya Utume. Chama hichi si CHENGINE ISIPOKUWA ni Hizb ut Tahrir, (Chama cha Ukombozi). Chama kinacho fanyakazi usiku na mchana ili kumtoa mwanadamu kutoka katika minyororo ya utumwa kwa matamanio yake na kumrudisha katika utumwa wa Muumba wake – Mwenyezi Mungu (swt). Hizb ut Tahrir ina hamu ya kuwapata wanaume walio na afya imara, akili makinifu na wachapajikazi miongoni mwa wawajibikaji ili kuitikia mwito wake wa kusimamisha tena Khilafah.

Khilafah itatoa maana ya lengo na misheni kwa wanaume, ambao watachukia kupoteza muda wao katika kucheza kamare, kushiriki katika miamala ya riba, kutelekeza dori yao ya Jihad, nudu ya Uislamu. Wanaume watakaojiepusha na kujishughulisha na usengenyaji pamoja na wake zao au wanawake, ambao hawatolia kwa kuwa timu zao za mpira za kitaifa au vilabu zitakapofungwa! Watachukia wao kama waume pamoja na vijana wao, binti zao au wake zao kuzozana juu ya aina gani ya chakula wale, washangilie timu gani ya mpira ya kitaifa au kilabu au wazuru eneo gani kujiliwaza au kuvaa nguo gani katika harusi au tamasha la muziki lijalo?! Ewe Mwenyezi Mungu (swt) tusamehe kwa makosa yetu na upangaji wa kimakosa wa vipaumbele vyetu katika kizazi cha karne hii ya 21 kilichojikita katika mtazamo wa kimada!  

Khilafah italeta vito kutokamana na wanaume kama vile Khalid bin Walid (ra) shujaa wa kiwango cha juu na kamanda mkuu asiyekuwa na mpinzani katika Jeshi la Waislamu huko Syria chini ya Khalifah (ra) Abu Bakr (ra). Sa’d bin Abu Waqqas (ra) shujaa makini wa kiwango cha juu na kamanda mkuu wa kijeshi huko Iraq chini ya Khalifah Umar bin Khattab (ra). Wanajeshi mahiri na wasiogopa kama Rib’i bin Amir (ra) waliofanya kazi chini ya usimamizi wa Sa’d bin Abu Waqqas. Rib’i bin Amir alikuwa mwanadiplomasia kwa Rustam, waziri wa vita wa dola ya Fursi. Yafuatayo ndiyo yaliyojiri:

‘Pindi yeye (Rib’i bin Amir) alipowasili katika makao ya Rustam, yaliyokuwa yamewekwa zulia la kitambaa cha dhahabu, mito ya hariri ya thamani, ilhali kiti cha kifahari chenye kito kiliwekwa katikakati. Rib’i bin Amir (ra) alikuja mpaka juu ya sakafu ya zulia hilo na kushuka juu ya farasi wake, akamfunga katika mto mmoja. Kisha akasonga mbele huku akiwa anasaidiwa na mkuki uliokuwa unadunga na kupasua zulia hilo na kulitia matundu kwa ncha yake, kisha kukaa mkabala na Rustam. Waliokuwepo walijaribu kumtoa katika kiti hicho cha kifahari na kumpokonya silaha zake. Hapo ndipo Rib’i bin Amir (ra) akatoa mngurumo, “Nimekuja kwa mualiko na sikujijia mwenyewe. Dini yetu inamkataza katakata mtu yeyote kukaa kama Mungu na wengine wasimame mbele yake ilhali wamefunga mikono yao.” Rustam aliingiliakati na kuwaomba wasifanye kitu kinyume na matakwa ya balozi.

Hata hivyo, baada ya kutafakari Rib’i bin Amir (ra) alishuka juu ya kiti hicho cha kifahari, akapasua sehemu ya zulia kwa jambia lake na kukaa ardhini na kumwambia Rustam, “Hatuhitaji kattu zulia lako. Ardhi iliyokunjuliwa na Mwenyezi Mungu (swt) inatutosha sisi.” Rustam kisha akamuuliza Rib’i bin Amir (ra) kupitia mkalimani, “Nini lengo lenu kuandaa vita dhidi yetu?” Rib’i bin Amir (ra) akajibu, “Tuna nia ya kuwaleta watumwa wa Mwenyezi Mungu (swt) katika upana wa maisha yajayo kutokamana na uchache wa maisha haya na kulingania haki na Uislamu kila palipo na mauaji na dini za uongo. Yeyote anayejifunga na haki na Uislamu atatupata sisi hatuingilii katika utajiri wake, mali yake na nchi yake. Lakini tutapigana na yeyote anayetuwekea vikwazo mpaka ima tuingie Peponi au tupate ushindi. Mukitaka kulipa Jizyah, tutaikubali na tutasita kwenda kinyume dhidi yenu na mutatupata tukisimama pamoja nanyi lau na pale ambapo mutakapotuhitaji kwa ajili ya usalama wa maisha na mali zenu.” Baada ya kusikia haya Rustam aliuliza, “Wewe ndio mkuu wa Waislamu?” Rib’i bin Amir (ra) alijibu, “La, mimi ni mwanajeshi wa kawaida. Lakini kila mmoja wetu, hata yule aliye kawaida zaidi anaweza kuzungumza kwa niaba ya mtu mwenye nguvu zaidi, na kila mtu ana nguvu kamili katika kila suala.”

Matamshi ya Rib’i bin Amir (ra) yalimuacha Rustam na waliokuwepo na mshangao mkubwa. Rustam kisha akasema, “uo wa upanga wako umeoza kiasi.” Rib’i bin Amir (ra) akautoa upanga wake nje ya uo na kusema, “Lakini umeharibika hivi karibuni tu.” Rustam kisha akasema, “sehemu ya makali ya mkuki ni ndogo. Yaweza kuwa na matumizi yoyote katika vita?” Rib’i bin Amir (ra) akajibu, “Hii sehemu ya makali inapenya ndani katika kifua cha adui na kutokeza hadi upande mwingine. Kwani haujaona cheche moja kuwa inatosha kuchoma mji mzima.” Baada ya vita hivi vya maneno,

Rustam alisema, “Sawa, nitatafakari juu ya matamshi yako na kufanya mkao kutaka ushauri na wanaume wangu walio makini katika kufanya maamuzi.” Rib’i bin Amir (ra) alisimama na kurudi kwa Sa’d bin Abu Waqqas (ra).

Siku iliyofuata, Rustam alituma ujumbe kwa Sa’d (ra) na kumuomba kutumana balozi kwake. Sa’d (ra) alimtuma Hudhaifah bin Mihsan (ra). Naye pia aliingia katika makao ya Rustam akiwa anamuendesha farasi wake na kuonyesha ushupavu, kama alivyofanya Rib’i bin Amir (ra) hapo awali. Akasogea mbele karibu na kiti cha kifahari akiwa juu ya farasi. Rustam, alisema, “Ni sababu gani umetumwa wewe leo badala ya yule aliyekuja kwangu awali?” Hudhaifah bin Mihsan (ra) akajibu, “Kamanda wetu hufanya uadilifu kwa kila mmoja na humpa fursa kila mmoja kufanya kila kitu. Jana ilikuwa ni zamu yake na leo ni zamu yangu.” Rustam kisha akamuuliza, “Munanipa muda gani wa kupumua?” Hudhaifah bin Mihsan (ra) alisema, “Siku tatu pekee kuanzia siku ya leo.” Rustam alinyamaza kimya, na Hudhaifah bin Mihsan (ra) akarudi moja kwa moja kwa kambi ya Waislamu. Ushupavu na umakinifu wa akili ya Hudhaifah bin Mihsan (ra) kulimwacha Rustam na waliokuwepo kustaajabu.

Siku iliyofuatia Rustam aliomba balozi kutoka kwa kambi ya Waislamu na Mughirah bin Shu’bah (ra) alitumwa kucheza dori yake. Rustam alijaribu vishawishi na vitisho lakini Mughirah bin Shu’bah (ra) hakutishika na kumjibu kwa kama alivyofanya. Kwa kukata tamaa na kuaibika Rustam alisema huku akiwa amejaa hasira, “Sitoingia katika makubaliano aina yoyote nanyi, na nitawaua nyote.” Mughirah bin Shu’bah (ra) alisimama na kuondoka kwa amani akielekea katika kambi yake.  

Hayo hapo juu ni taswira ya hali ya Waislamu wanaume wakweli ambao kwamba hii dunia inawahitajia. Wanaume ambao watajituma ili kuishi na kufa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (swt) kwa kuitikia mwito wake pale Aliposema, ﴾يَـٰٓأَيُّہَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ ٱسۡتَجِيبُواْ لِلَّهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمۡ لِمَا يُحۡيِيڪُمۡ‌ۖ وَٱعۡلَمُوٓاْ أَنَّ ٱللَّهَ يَحُولُ بَيۡنَ ٱلۡمَرۡءِ وَقَلۡبِهِۦ وَأَنَّهُ ۥۤ إِلَيۡهِ تُحۡشَرُونَ﴿ “Enyi mlio amini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapo kuitieni jambo la kukupeni uzima wa milele. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu huingia kati ya mtu na moyo wake, na kwamba hakika kwake Yeye tu mtakusanywa.[Al-Anfal: 8:24]. Wanaume walio na misheni barabara juu ya hii dunia ya muda mfupi, ambao Mwenyezi Mungu (swt) amewazungumzia kuwahusu, Aliposema, ﴾مِّنَ ٱلۡمُؤۡمِنِينَ رِجَالٌ۬ صَدَقُواْ مَا عَـٰهَدُواْ ٱللَّهَ عَلَيۡهِ‌ۖ فَمِنۡهُم مَّن قَضَىٰ نَحۡبَهُ ۥ وَمِنۡہُم مَّن يَنتَظِرُ‌ۖ وَمَا بَدَّلُواْ تَبۡدِيلاً۬﴿ “Miongoni mwa Waumini wapo watu walio timiza waliyo ahidiana na Mwenyezi Mungu. Baadhi yao wamekwisha kufa, na baadhi wanangojea, wala hawakubadilisha (ahadi) hata kidogo.[Al-Ahzab: 33:23].

Wanaume adhimu walio na malengo watazaliwa, kukuzwa na kulelewa chini ya ngao na mlinzi wa kweli wa wanadamu, Khilafah. Mpaka itakaposimamishwa, tutaendelea kushuhudia majanga duniani kote. Wakati ni sasa kujiunga na mwito ulioshamiri na kutokota wa kuleta MAGEUZI YA KWELI yanayowasilishwa na Hizb ut Tahrir katika machapisho yake yanayofahamika. Usibakie nyuma; muda wetu ni sekunde tu.

Kufanyakazi na Hizb ut Tahrir ni fursa ya kuwa juu ya mzunguko wa kila siku maarufu ‘mbio za panya’ na kujikwamua kutokamana na kufikiria duni ambako idadi kubwa ya watu ambao wamezama ndani ya uhadaifu na ujinga kwa jina la kuleta mageuzi. Hata hivyo, kiuhalisia sio chochote bali ni kundi la mabawabu wa kisiasa za kisekula za kidemokrasia ambao wapo kwa ajili ya kubakisha hali iliyoko sasa kwa gharama na njia yoyote ile. Hakika, kufanyakazi na Hizb ut Tahrir sio kutembea mbugani kwa wale wanaofahamu ukubwa wa majukumu yake na aina ya kazi zake juu ya mabega yao. Hata hivyo, baada ya wokovu usio na kipimo pale ambapo lengo litatimia katika hii dunia ya muda mfupi na Akhera haidirikiki kattu.  

Enyi Wanaume! Tuamkeni, tukazeni mikanda na tupatilize fursa ya kujiunga na kutoa juhudi ya ubora wetu katika mchakato wa kufikia mageuzi msingi. Rizq na ajal zetu HAZIPO katika mikono yetu kwa hiyo hesabu zetu na juhudi zetu kuu zielekezwe katika ulinganizi wa Da’wah. Tuchukue uongozi wa kuziongoza familia, jamii zetu na wanadamu katika nyanja zote za maisha kwa kufanyakazi kwa kujizatiti pasina kuchoka kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (swt) na ilivyoelekezwa na Mtume Wake (saw). Tuweni wanaume walioko hai, makini na mashujaa kimaneno na vitendo. 

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu