Ijumaa, 20 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Uliberali Umepora Unyoofu wa Watoto

(Imetafsiriwa)

Habari:

Ripoti ya Tume ya Watoto ya Uingereza, iliyochapishwa mnamo Januari 31, 2022, iliripoti kwamba mtoto 1 kati ya 10 nchini ameonyeshwa ponografia ya mtandaoni akiwa na umri wa miaka 9, na kufikia umri wa miaka 13, asilimia 50 ya watoto wameona ponografia. Ripoti hiyo pia ilisema kuwa robo ya watoto wenye umri wa miaka 16-21 waliona ponografia kwenye mtandao kwa mara ya kwanza wakiwa bado katika shule ya msingi, huku karibu 50% ya vijana wa rika moja wanaamini kuwa wasichana "wanatarajia unyanyasaji wa kimwili" katika ngono, hasa kutokana na uhalalishaji unyanyasaji wa kingono unaoonyeshwa kwenye ponografia. Na karibu 80% ya vijana walio na umri wa miaka 18-21 walikuwa wameona ponografia inayohusisha unyanyasaji wa kingono wakiwa watoto. Kamishna wa Watoto wa Uingereza, Dame Rachel de Souza alitoa maoni kwamba utumiaji wa ponografia "umeenea" miongoni mwa watoto na akaangazia athari zenye madhara kwa vijana.

Maoni:

Suluhu duni zinazolinganiwa kwa kiwango cha kutisha cha tatizo hili kuu ni udhibiti bora wa ufikiaji wa watoto kwenye tovuti hizi haribifu, kama vile hatua za kuthibitisha umri kwenye majukwaa mbalimbali ya mtandaoni na mitandao ya kijamii, au kuboresha ufundishaji wa elimu ya ngono shuleni. Hata hivyo, kile ambacho jamii huria hushindwa kuhoji au kukubali ni athari haribifu ya uhuru wa kijinsia wenyewe ambao unaidhinisha utayarishaji na usambazaji wazi wa ponografia na picha na mawazo mengine ya kingono katika matangazo ya biashara na tasnia ya burudani. Hii ni licha ya kujua madhara yanayoletwa kuhusiana na kushushwa thamani ya wanawake, kuchochea unyanyasaji wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya wanawake, kudunisha uhusiano kati ya jinsia na kudhuru ndoa na hadhi ya kitengo cha familia. Hii ni kwa sababu chini ya mfumo wa uliberali wa kirasilimali, furaha na faida daima vitatawala juu ya usalama wa wanawake na ustawi wa watoto na jamii kwa jumla.

Uhuru huria wa kijinsia pia umehalalisha na kusherehekea uasherati ndani ya jamii, na mahusiano ya kimapenzi ya nje ya ndoa yanayosifiwa - ambayo yameathiri vijana bila shaka. Takriban nusu (54%) ya vijana nchini Marekani wenye umri wa miaka 15-19 wamepitia aina fulani ya ngono. Miongoni mwa wanafunzi wa shule ya upili, 10% ya wanaume na 7% ya wasichana wanaripoti kuwa na wapenzi 4 au zaidi katika maisha yao. Na kati ya maambukizi mapya milioni 26 ya magonjwa ya zinaa (STI) yanayoripotiwa nchini kila mwaka, karibu nusu hupatikana miongoni mwa vijana wenye umri wa miaka 15-24. (ACT for Youth Center for Community Action). Maoni kama haya pia kwa bahati mbaya yameathiri ardhi za Waislamu. Katika Utafiti wa Afya na Demografia wa Indonesia wa 2012 (SDKI) kuhusu afya ya uzazi miongoni mwa vijana, ni asilimia 77 pekee ya wanawake waliohojiwa na 66% ya wanaume waliohojiwa walisema ni muhimu kutunza ubikira wao kabla ya ndoa, chini kutoka utafiti wa 2007, ambapo 99% ya wanawake na 98% ya vijana wa kiume waliohojiwa walisema walithamini ubikira. (Jakarta Post)

Kuanzishwa kwa elimu ya ngono shuleni yenyewe ni zao la matatizo yanayosababishwa na maadili huria, na hutumiwa na serikali kujaribu kutatua matatizo kama vile mimba za utotoni, watoto kutazama ponografia, kuenea kwa magonjwa ya zinaa kwa vijana, na kiwango kikubwa cha kutisha cha unyanyasaji wa kijinsia na ukatili unaofanywa na wavulana dhidi ya wasichana mashuleni, vyuoni na taasisi za elimu ya juu, pamoja na viwango vya janga la ubakaji na uhalifu mwingine dhidi ya wanawake katika jamii kwa jumla. Kwa mujibu wa Ofsted, chombo kinachohusika na kukagua taasisi za elimu nchini Uingereza, 59% ya wasichana na wanawake wachanga kati ya umri wa 13 na 21 wanasema wamepitia unyanyasaji wa kijinsia shuleni au chuoni, lakini waathiriwa "hawaoni sababu ya kupambana au kuripoti tabia hii mbaya kwa sababu inaonekana kama uzoefu wa kawaida." Kwa kweli, watoto wengi wa shule walielezea unyanyasaji wa kijinsia na unyanyasaji wa kijinsia mtandaoni kama sehemu ya maisha ya kawaida. Katika shule na vyuo 32 ambavyo wakaguzi wa Ofsted walitembelea kama sehemu ya ukaguzi wao wa tatizo hili, wasichana 9 kati ya 10 walisema kwamba kutumiwa picha au video chafu kumetokea "sana" au "baadhi ya wakiti" kwao au wenzao, huku robo tatu ya wasichana waliripoti kuwa shinikizo la kutoa picha zao za uchi hutokea sana au baadhi ya wakati shuleni na vyuoni.

Masomo ya elimu ya ngono huongeza zaidi mmomonyoko wa unyoofu kwa watoto kupitia kuonyesha picha na video chafu na kushiriki katika mijadala yenye lugha chafu, na kukuza uhuru wa kuchagua - jambo ambalo pasi na budi huzidisha tatizo hili. Somo hilo limejikita katika kuhakikisha 'ridhaa' katika mahusiano na kuzuia mimba na kuambukizwa magonjwa ya zinaa, badala ya kushughulikia fahamu za msingi zinazosababisha uasherati na mahusiano nje ya ndoa pamoja na mashambulizi dhidi ya wanawake - ambayo ni uhuru huria unaoruhusu wanaume na wanawake kuwa na uhusiano wowote wanaotaka na kuwashajiisha wanaume kuwatazama na kuamiliana na wanawake kulingana na matakwa na matamanio yao ya kibinafsi.

Hii ndiyo hali ya kutisha ya mambo inayoathiri watoto na vijana ndani ya dola za kiliberali kote duniani. Na bado tunaona serikali katika ardhi za Kiislamu zikiwa na shauku kubwa ya kufuata unyo unyo dola za kiliberali za Magharibi kwa kuimarisha uenezaji wa maadili ya kiliberali ndani ya jamii zao kupitia tasnia ya burudani na tasnia nyenginezo, pamoja na kuanzisha aina zao wenyewe za elimu ya ngono katika mitaala yao. Swali ambalo kwa hakika linahitaji kuulizwa kama Waislamu ni - ni aina gani ya mustakabali tunaoutaka kwa vijana wetu? Je, tunatengeneza aina gani ya kizazi kijacho? Je, ni aina gani ya jamii tunayotaka kuzalisha katika ardhi zetu? Je, ni ile inayoakisi wingi wa matatizo yanayoathiri vijana, wanawake, familia na uhusiano baina ya jinsia? Au ni ile ambayo vijana wetu wanalelewa kwa maadili matukufu, mema, na ya uongofu ambayo yanawafanya kuwa raia bora wa dola; jamii ambapo utu na usalama wa wanamke unahifadhiwa na utukufu wa ndoa na kitengo cha familia kulindwa; na jamii ambayo uhusiano kati ya wanaume na wanawake umejengwa juu heshima na ushirikiano?

Ni mfumo wa Uislamu pekee, na sheria zake za kijamii ndio ambao unadhibiti kikamilifu uhusiano kati ya wanaume na wanawake unaoweza kuunda jamii na dola kama hiyo. Ni mfumo huu peke yake, unaotabikishwa na Khilafah kwa njia ya Utume ndio unaweza kulinda unyoofu wa watoto na kujenga shakhsiya zinazokumbatia na kusherehekea fahamu kama vile Hayah na  kujistiri kimwili na unaoepuka aina zote za mawazo, mitindo ya maisha na tabia potofu.

[وَلَوِ اتَّبَعَ الْحَقُّ أَهْوَاءهُمْ لَفَسَدَتِ السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ وَمَن فِيهِنَّ بَلْ أَتَيْنَاهُم بِذِكْرِهِمْ فَهُمْ عَن ذِكْرِهِم مُّعْرِضُونَ]

“Na lau kuwa Haki ingeli fuata matamanio yao, basi zingeli haribika mbingu na ardhi na waliomo ndani. Bali tumewaletea ukumbusho wao, nao wanajitenga mbali na ukumbusho wao.” [Al-Mu'minun: 71]

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Dkt. Nazreen Nawaz
Mkurugenzi wa Kitengo cha Wanawake katika Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu