- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Vifo, Uharibifu na Umaskini ni Urithi wa Kuamini Ahadi za Magharibi
(Imetafsiriwa)
Habari:
"Bado hatuna habari zote juu ya kile kilichotokea, lakini inaonekana kama hili ni janga baya zaidi kuwahi kuliona katika Bahari ya Mediterania," alisema Kamishna wa Mambo ya Ndani wa EU mnamo tarehe 16 Juni baada ya mashua iliyobeba wahamiaji kutoka Libya hadi Italy kupinduka katika pwani ya Ugiriki. Miili sabini na nane imepatikana na mamia wakiwemo wengi wa wanawake na watoto wamepotea wakidhaniwa kuwa wamekufa. Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Msalaba Mwekundu na Mwezi Mwekundu, Francesco Rocca, alisema "inashangaza na haikubaliki kwamba watu bado wanakufa mbele ya mipaka ya EU, wakitafuta mahali salama."
Maoni:
Hili linaweza kusifiwa kuwa ‘janga baya zaidi’, lakini je, janga ndilo neno sahihi la kutumia wakati mazingira yaliyosababisha hilo yamekuwa sera ya serikali kwa miaka mingi? Hata hivyo, Kamishna wa Mambo ya Ndani wa Muungano wa Ulaya alilaumu “wasafirishaji haramu” wanaowaweka watu kwenye mashua hizo: “Hawawapeleki Ulaya, wanawapeleka kwenye kifo. Hili ndilo wanalofanya na ni muhimu kabisa kulizuia,” na “linapokuja suala la kupambana na walanguzi hawa, hatuwezi kutegemea njia moja pekee ya kufanya hivyo. Tunapaswa kutumia ujasusi - tunapaswa kutumia uchunguzi wa kawaida wa polisi pamoja na nchi za asili, nchi za usafiri, na nchi za kuondokea," alisema.
Kuna maelezo yanayokinzana kutoka kwa manusura na mamlaka za Ugiriki kuhusu iwapo mashua hiyo ilizamishwa kutokana na majaribio yaliyofeli ya walinzi wa pwani ya Ugiriki au chombo kingine cha kuvuta mashua hiyo iliyokuwa ikijitahidi. Mtu mmoja aliyenusurika aliripotiwa kusema bila kujulikana: "Mashua ya walinzi wa pwani iliondoka kwa kilomita 3 baada ya kuzama kutokea na walioweza kuogelea umbali huo walifanikiwa," ambapo inamaanisha kuwa mashua ya walinzi wa pwani iliwaacha wahamiaji wengi kimakusudi kutoka kwa mashua iliyopigwa na dhoruba kuzama. Manusura walikuwa ni wanaume pekee. Kuhusiana na hili ni swali la kwa nini walinzi wa pwani hawakuchukua hatua wakati walikuwa katika mawasiliano na mashua hiyo kwa takriban masaa 12 kabla ya kuzama?
Walinzi wa pwani wa Ugiriki walisema, "Msafirishaji mashua hiyo hakuomba msaada wowote kutoka kwa walinzi wa pwani au kutoka Ugiriki." Walinzi wa pwani pia walisema kuwa "Kati ya 3:30 pm [12:00 GMT] na 9 pm [18:00 GMT], kituo cha operesheni za Kibiashara za Baharini cha Wizara kiliwasiliana mara kwa mara na nahodha huyo kupitia simu ya setilaiti. Katika mawasiliano haya yote, walirudia mara kwa mara kwamba wanataka kusafiri kwa meli hadi Italia na hawakutaka msaada wowote kutoka Ugiriki.” Hadithi tofauti inaibuka kutoka kwa Shirika lisilo la Kiserikali (NGO) liitwalo Alarm Phone, ambalo linafuatilia mashua za wakimbizi katika bahari ya Mediterania. Kulingana na wao, wakimbizi walikuwa wakiomba msaada wakisema kwamba “hawawezi kuokoka usiku, kwamba wako katika dhiki kubwa.” NGO hiyo ina maelezo ya kukinaisha juu ya tofauti kati ya kile walichosikia kutoka kwa wakimbizi na kile walinzi wa pwani wa Ugiriki waliripoti. Sababu ya wakimbizi kutoomba msaada wa walinzi wa pwani wa Ugiriki ni kwamba: "watu walio safarini wanajua kwamba maelfu wamepigwa risasi, kupigwa, na kutelekezwa baharini na vikosi hivi vya Ugiriki". Zaidi ya hayo, “wanajua kwamba kukutana na Walinzi wa Pwani, Polisi wa Ugiriki, au Walinzi wa Mpaka wa Ugiriki mara nyingi humaanisha vurugu na mateso. Ni kwa sababu ya misukumo ya kiserikali kwamba mashua zinajaribu kuepuka Ugiriki, kusafiri kwa njia ndefu zaidi, na kuhatarisha maisha baharini.”
Je, ni ‘misukumo hii ya kiserikali’ ni ipi ambayo wakimbizi wanaiogopa sana? Uchunguzi uliofanywa na gazeti la ‘The Guardian’ mnamo 2021 ulihitimisha kuwa nchi wanachama wa EU zilirudisha nyuma "angalau watu 40,000 wanaotafuta hifadhi kutoka kwa mipaka ya Ulaya wakati wa janga hilo, njia hizo zikihusisha vifo vya zaidi ya watu 2,000." Kusukuma nyuma baharini ni hatari sana, na pia ni kawaida sana. Wakimbizi wengi ambao wametua kwenye visiwa vya Ugiriki walirudishwa baharini na kuwekwa kwenye mashua ndogo ili kuelea. Mfano mmoja uliripotiwa na Gazeti la ‘The Guardian”: “Mnamo tarehe 15 Septemba 2021, Sidy Keita kutoka Ivory Coast na Didier Martial Kouamou Nana kutoka Cameroon, walipanda mashua kutoka Uturuki hadi Ugiriki. Licha ya kufika kisiwa cha Ugiriki cha Samos, miili yao ilipatikana siku chache baadaye, ikiwa imesombwa na maji katika mkoa wa Aydin, kwenye pwani ya Aegean. Wale walionusurika walisema kwamba “polisi walitupiga kwa vurugu kubwa zaidi” kabla ya kuwatupa kwenye mashua na kuwasukuma baharini.
Kesi iliyowasilishwa dhidi ya dola ya Ugiriki katika Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu inaishutumu Athens kwa kiwango cha kutisha cha vurugu katika operesheni za kisasa za mashirika ambayo ni sehemu ya mkakati wa kurudisha nyuma uhamiaji haramu ili kuzuia kuwasili kwa wakimbizi na wahamiaji. Vurugu hizi ni kwa ajili ya kuzuia watu kuja, lakini bado wanakuja. Mkimbizi mmoja kutoka Damascus alisema: “Sikutaka hata kwenda Ugiriki. Tulijua kwamba walikuwa wakiwadhuru wakimbizi wanapowasili, lakini ilishangaza kuona hali halisi, ambayo ni kwamba Ulaya haijali hata kidogo haki za binadamu na utu.” Hata hivyo, alisema, “Licha ya hayo yote, bado nitajaribu tena. Siwezi kujenga maisha nchini Syria au Uturuki." Kwa nini watu wengi wanatamani sana kufika Ulaya hivi kwamba wanahatarisha sana?
Wazungu waliwahi kuionea wivu hadhara ya Kiislamu na mamlaka katika Bahari ya Mediterania, na walijitahidi kwa karne nyingi kuangamiza mamlaka ya Khilfah Uthmani huko hadi hatimaye Khilafah yenyewe ikavunjwa. Waliita iliyopitwa na wakati, na kuwaahidi Waislamu demokrasia, uhuru na maisha mapya mazuri bila ya Khilafah.
Badala yake, Waislamu walipata unyonywaji wa kikoloni, serikali fisadi zinazotumikia maslahi ya Magharibi na kuzishikilia nyanja nyingi zaidi za maisha yao. Hata juhudi za Waislamu wanyoofu kuwaasi watawala hawa zilikengeushwa na nchi za Magharibi. Wengi wa wahanga wa 'janga' la hivi punde walitoka Syria ambapo mapinduzi yao dhidi ya utawala katili wa Assad yaliavywa huku Muungano wa Ulaya ukiweka vikwazo vya silaha katika uuzaji wa silaha zote kwa Wasyria, huku Marekani ikimwaga pesa zake chafu nchini humo kuundwa kwa wanamgambo ambao wangetumikia maslahi ya Marekani badala ya maslahi ya watu wa Syria. Vifo, uharibifu na umasikini ni urithi wa kuamini ahadi na maadili ya Magharibi.
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Dkt. Abdullah Robin