Jumatatu, 06 Rajab 1446 | 2025/01/06
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Mauaji ya Halaiki mjini Gaza Hayatamalizika hadi sisi kama Waislamu Tumalize Utegemezi wetu kwa Demokrasia

(Imetafsiriwa)

Habari:

Uchaguzi wa Marekani wa 2024 ulifanyika mnamo tarehe 5 Novemba huku Donald Trump, akipata ushindi mkubwa dhidi ya Kamala Harris. Waislamu wengi nchini Marekani, kwa mara nyengine tena walishiriki katika chaguzi hizi za kidemokrasia kwa matumaini kwamba kura yao ingesaidia kumaliza mauaji ya halaiki huko Gaza. Wengine walimuunga mkono Trump, ima wakiamini katika ahadi yake kwamba angeleta amani katika eneo hilo, au “kumuadhibu” Harris na utawala wa Biden kwa kuendelea kuunga mkono na kufadhili umbile la mauaji ya halaiki la Kizayuni. Wengine walimuidhinisha Harris, wakiamini kwamba yeye ndiye ‘la hafifu ya madhara mawili’ na njia bora kwa wapinzani wa vita vya Gaza kuendeleza ajenda zao. Wengine walipiga kura zao kwa mwakilishi wa Green Party, Jill Stein na mgombea wa People's Party Cornel West, kutokana na msimamo wao thabiti wa kupinga vita na kuahidi kukomesha mauaji ya halaiki.

Maoni:

Katika chaguzi hizi, pamoja na chaguzi za kidemokrasia ndani ya dola zengine za magharibi, Waislamu wengi walipanga mikakati juu ya njia bora ya kucheza mchezo wa kidemokrasia ili kushawishi matukio nchini Palestina. Hata hivyo, mauaji ya halaiki huko Gaza, kukaliwa kwa mabavu Palestina, na ukandamizaji wa Waislamu kwengineko duniani havitakwisha hadi tutupilie mbali udanganyifu huu kwamba kujihusisha na mfumo wa kidemokrasia na mchakato wa uchaguzi kutatatua matatizo yetu sisi kama Umma wa Kiislamu. Kuna msemo wa Kiingereza: “Kichaa ni kufanya jambo lile lile tena na tena na kutarajia matokeo tofauti.” Je, hatujashuhudia tena na tena kufeli kabisa kwa dola za magharibi na zengine za kidemokrasia kusitisha mauaji ya halaiki au mauaji ya kikabila dhidi ya Waislamu nchini Syria, Yemen, Myanmar, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Kashmir, Turkestan Mashariki na kwengineko, bila ya kujali ukubwa wa ukatili huo unaotekelezwa na bila kujali maoni ya Waislamu? Je, hatujaona vita vya kikoloni vya kimagharibi vikitokea Afghanistan na Iraq, licha ya upinzani mkubwa wa ndani? Nchini Uingereza, mamilioni waliandamana kupinga uvamizi wa Iraq wa 2003, na bado serikali ya Blair bado iliingia vitani licha ya maoni haya mengi ya umma. Hii ni kwa sababu serikali za kidemokrasia za kibepari za Magharibi hazifafanui ajenda na vitendo vyao vya sera za kigeni kwa msingi wa kura za watu wachache wa ndani au maoni ya umma, bali maslahi ya muda mrefu ya kisiasa na kiuchumi ya dola - taasisi, vyombo na miundo yake - na kudumisha ubabe wao juu ya maeneo ya ulimwengu, bila kujali msimamo wa kifikra wa chama au rais aliye madarakani. Katika mfano huu, Marekani na serikali nyengine nyingi za kikoloni za kibepari za Magharibi zinaona ni kwa manufaa yao ya kitaifa kuhifadhi na kuimarisha umbile la Kizayuni, bila kujali nguvu ya upinzani ndani ya umma wao wenyewe. Kwa hiyo, kama Waislamu, kuamini kwamba tunaweza kuathiri ajenda za Marekani au sera za kigeni za nchi za Magharibi huko Palestina au ulimwengu wote wa Kiislamu kwa kushiriki katika mchakato wa uchaguzi wa kidemokrasia ni ‘mangati’!!

Zaidi ya hayo, upigaji kura katika chaguzi hizi za kidemokrasia si tu kuonyesha kumuunga mkono mgombea na sera zake; ni uidhinishaji wa uhalali wa mfumo wanaouwakilisha, kuunga mkono na kuusimamia. Ni kuhalalisha na kuidhinisha mfumo mchafu wa kikoloni wa kibepari uliosaidia kuanzisha, kufadhili, kulinda, kuhifadhi na kuimarisha umbile la Kizayuni. Ni kukubali mfumo uliowezesha uvamizi huu wa mauaji kufanya mauaji yake ya halaiki bila kuadhibiwa na ambao ulizalisha viongozi kama Trump, Biden na Harris ambao hawana wasiwasi wa kueleza waziwazi uungaji mkono wao usioyumba kwa umbile la Kiyahudi la mauaji bila kujali ukubwa wa uhalifu. Moira Donegan, mwandishi wa gazeti la ‘the Guardian’ la Marekani anaandika: “Je, Marekani inastahili Trump? Katika miaka ya tangu aingie madarakani, nadharia moja inadai kwamba yeye ni dhihirisho tu la mapepo ya taifa ambayo hayajafukuzwa - ishara ya ubaguzi wa rangi ambayo iliruhusu nchi hii kujenga uchumi wake kutoka kwa migongo ya watumwa, ya uhusiano wa kawaida na vurugu ambayo iliiruhusu kujenga eneo lake na utawala wake wa kimataifa kupitia ushindi mkali na ulazimishaji, wa kupenda pesa kupita kiasi na kutojali kusiko aibu kanuni ambayo siku zote imekuwa ikichochea uchumi wetu mbovu. Katika toleo hili la hadithi, Trump sio tu ni dalili mbaya, lakini kitu kama adhabu kwa Amerika…” Uhalisia kama huo unaonyeshwa ndani ya mfumo wa kidemokrasia wa kibepari wa dola katika ulimwengu wa magharibi. Je, hii kweli ni aina ya mfumo unaoweza kufikia haki kwa Wapalestina? Je, hii kweli ni aina ya mfumo ambao sisi kama Waislamu tuko tayari kuuunga mkono kwa kushiriki katika chaguzi za kidemokrasia za nchi hizi? Je, kweli tunatarajia usaidizi wowote kutoka kwa muundaji, mfadhili na muungaji mkono wa muuaji?

Kama Waislamu, ili kukomesha mauaji ya halaiki huko Gaza, na ukandamizaji wa Waislamu mahali pengine, tunahitaji kuinua mtazamo wetu zaidi ya mikakati iliyofeli ya mabadiliko. Tunatakiwa tuondokane na imani potofu kwamba tunaweza kutatua matatizo yetu kupitia mfumo wa kidemokrasia ambao umefumbatwa na ukoloni na wenyewe uliendesha mauaji mengi ya halaiki katika ardhi zetu za Kiislamu. Tunahitaji kuvunja udanganyifu na kuondoa dhana kwamba sanduku la kura lina uwezo wa kubadilisha maamuzi ya sera za kigeni za dola za kibepari tunazoishi ndani yake. LA HASHA! Hakika, mojawapo ya njia bora zaidi za kuonyesha hasira na upinzani dhidi ya mauaji ya halaiki yanayofadhiliwa na serikali mjini Gaza ni kutojihusisha na mfumo unaounga mkono na kuyawezesha!

Ikiwa kweli tunataka kukomesha mauaji mjini Gaza, tunahitaji kutafuta suluhisho sahihi ambalo litaikomboa ardhi yote ya Palestina milele. Ni jeshi linalowauwa na kuwaangamiza watu wa Gaza na maeneo mengine ya Palestina. Kwa hiyo, kukomesha mauaji haya ya halaiki kunahitaji kuhamasishwa kwa jeshi ili kuwatetea na kuwakomboa watu. Kwa hiyo, wito lazima uende kwa maafisa wa majeshi ya Waislamu kuitikia wajibu wao wa Kiislamu wa kuulinda na kuukomboa Uislamu wao. Hata hivyo, hakuna mtawala au dola hivi leo katika ulimwengu wa Kiislamu ambayo ina utashi wa kisiasa wa kuhamisha jeshi lao ili kutimiza faradhi hii. Kwa hiyo, kama Waislamu, tunatakiwa kuelekeza mtazamo wetu katika kubadili uongozi na mifumo katika ardhi za Waislamu kwa kuondoa tawala potovu za khiyana zinazozisibu nchi zetu, na kusimamisha kwa haraka dola iliyojengwa juu yake, inayowakilisha na kupigania Uislamu na Umma. Dola hii ni Khilafah kwa njia ya Utume. Hakika, hapawezi kuwa na ushindi kwa Ummah huu bila ya utiifu kwa Mwenyezi Mungu (swt) na kutegemea masuluhisho na mfumo Wake pekee. Mwenyezi Mungu (swt) asema:

[إِنَّمَا كَانَ قَوْلَ الْمُؤْمِنِينَ إِذَا دُعُوا إِلَى اللَّهِ وَرَسُولِهِ لِيَحْكُمَ بَيْنَهُمْ أَن يَقُولُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا وَأُوْلَئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ]

“Haiwi kauli ya Waumini wanapo itwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili ahukumu baina yao, ila ni kusema: Tumesikia, na tumet'ii! Na hao ndio wenye kufanikiwa.” [An-Nur:51]

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Asma Siddiq
Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu