- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Jibu la Swali
Ni Kipi Kilicho Nyuma ya Kukola Moto na Uchokozi wa Ukraine kwa Urusi
(Imetafsiriwa)
Swali:
Raisi wa Ukraine, Petro Poroshenko, aliliambia lishirika la habari la American Fox News: “Urusi imeanzisha vita vikali dhidi ya nchi yake pindi walinzi wake wa mipakani walipozisimamisha manuari za Ukraine katika mkondo wa Kerch, unaounganisha Bahari Nyeusi na Bahari ya Azov.” Baada ya kuangazia tukio hiyo aliongeza kusema, “Bwana Putin, hiki ni kitendo cha uvamizi. Bwana Putin, hivi ni vita. Na huu sio mzaha, na sio tukio tu, na sio mgogoro,” (Arabic.Sputniknews, 12/12/2018). Urusi imetangaza kuwa Walinzi wa Pwani ya Urusi walizizuilia manuari tatu za Ukraine mnamo 25/11/2018 wakidai kuwa zilikiuka bahari za Urusi karibu na mkondo wa Kerch baina ya bahari mbili; Nyeusi na Azov masharaki mwa Crimea, kufuatia hilo, ilitoa wito kwa Amerika kuiwekea Urusi vikwazo vikali, lakini Ulaya ikakataa. Bado kungali na taharuki baina ya pande hizo. Ni nani aliye nyuma ya matukio haya? Ni kwa nini taharuki zilianza tena upya huko?
Jibu:
Tutayarudia matukio yaliyotokea na bado yangali yanatokea huko juu ya kadhia hii ili kupata jibu, Mwenyezi Mungu akitujaalia:
1- Mnamo Februari 2014, Urusi, Amerika na Ulaya walikubaliana kuwa aliyekuwa Raisi wa Ukraine Viktor Yanukovych angesalia mamlakani, yeye ni mtiifu kwa Urusi. Lakini, pindi makubaliano yalipoafikiwa, ghasia zilizuka na kugeuka kuwa vitendo vya kisilaha kutokana na hayo Yanukovych alilazimika kukimbilia nchini Urusi. Hatimaye iligunduliwa kuwa Magharibi ilikuwa nyuma ya matukio haya … Urusi ilitambua kuwa Magharibi iliihadaa na ikaipoteza Ukraine. Hivyo basi ikatangaza kuiunganisha Crimea na Urusi, na kuchochea wafuasi wake mjini Donbass, mashariki ya Ukraine, kutangaza uhuru wa maeneo yao kama Jamhuri za Donetsk na Luhansk. Kufuatia hayo, Amerika na Ulaya ziliiwekea Urusi vikwazo na kuiondoa kutoka katika kongamano la nchi za G-7.
2- Amerika ilitoa wito wa kupewa silaha Ukraine, lakini Ulaya ilikataa, kwa sababu inajua kuwa upewaji silaha huu utaleta taharuki na Urusi na utakapopamba moto utamulika juu ya Ulaya… Kwa hivyo Ufaransa na Ujerumani ziliwasiliana na Urusi ili kuzima taharuki na kutafuta suluhisho la kisiasa. Zilitia saini makubaliano ya Minsk mnamo 6/2/2015 baina ya nchi tatu hizo na kutoijumuisha Amerika. Tumetaja hili katika jibu la swali la tarehe 21/2/2015 ambapo tulisema: “Ulaya (Ufaransa na Ujerumani) zinahofia kuwa matukio haya moto katika msimamo wa Amerika yatapelekea kupamba moto kwa kitendo cha kijeshi cha Urusi dhidi ya Ukraine, itakuwa ni fedheha kwa Ulaya endapo haitasimama upande wa Ukraine, ambapo itasababisha vita au vita bandia barani Ulaya lakini havitaathiri Amerika. Hii ndio sababu iliyoisukuma Ulaya kubadilisha sera yake ambayo inaafikiana na Amerika nchini Ukraine, iliyoamua kuwasiliana na Raisi wa Urusi ili kufikia suluhisho la kisiasa, na kusitisha kuzidi moto kwa aina yoyote kati ya Ulaya na Urusi, na hili ndilo lililotokea. Viongozi wa Ulaya (Ufaransa na Ujereumani) walijadiliana kuhusu hili na kukubaliana juu yake mnamo 06/02/2015. Kisha Merkel akenda Washington mnamo 08/02/2015 ili kumuarifu Obama kuhusu hili na wala sio kuomba ruhusa yake … na ilikuwa dhahiri kuwa Ulaya kwa mara ya kwanza ilichukua udhibiti juu ya kadhia kabla ya kupata idhini kutoka Amerika. Utekelezwaji wa waraka huo uliidhinishwa na kuamuliwa na viongozi hao watatu Vladimir Putin, Angela Merkel, na Raisi wa Ufaransa Francois Hollande mnamo Ijumaa, 06/02/2015, kilichobakia pekee ni kuziita pande za Ukraine “raisi na waasi” kuutia saini, kisha Merkel alikwenda Washington ili kumuarifu Obama!”
3- Kitendo hiki hakikuifurahisha Amerika, ingawa baadaye ilidai kutangaza uungaji mkono wake wa makubaliano hayo, lakini sio katika utekelezwaji wake, bali katika kufutilia mbali yaliyomo ndani yake na kufanya kazi ili kuuangamiza. Tumetaja katika jibu la swali hilo hilo: “Msimamo wa Ufaransa na Ujerumani uliathiri pakubwa utawala wa Obama, ulipelekea vita vya kimaneno katika kongamano la Munich kati ya Kerry na Merkel, hususan kuhusu taarifa za Amerika za kuipa Ukraine silaha ambapo Ulaya inakataa.” Tuliongeza kusema: “Ama kuhusu matarajio, inatarajiwa kuwa Amerika itatafuta matatizo mengi ili kuchelewesha utekelezwaji wake (makubaliano hayo), ina wafuasi nchini Ukraine, ingawa Raisi wa Jamhuri hiyo Poroshenko yu karibu na Ulaya lakini pia yu karibu na Amerika … na huenda ikachochea zaidi hali hiyo kwa moja ya mambo matatu au kwa yote matatu:
- Kuipa Ukraine silaha na mapema.
- Au kufanya mazungumzo nayo ya kuijumuisha katika NATO.
- Au kupitia kupelekea baadhi ya wanajeshi wake nchini Ukraine.
Na kupitia haya huenda ikapambana na makubaliano hayo, kwa sababu kila moja ya haya matatu linaishinikiza Urusi na kuathiri matukio, na kupelekea kufeli kwake.” Huu ndio mwisho wa nukuu …
Na haya ndiyo yanayotendeka; Amerika inafanya kazi ili kufelisha makubaliano hayo na kuifanya hali kuwa ya taharuki …
4- Na kwa haya yametokea matukio ya hivi karibuni, pindi Urusi ilipozizuia manuari za Ukraine pamoja na mabaharia wake … Inaonekana kana kwamba Ukraine iliishinikiza Urusi … na haingejaribu kuchukua hatua hii lau si kwa idhini kutoka Amerika, shirika la Urusi la TASS liliripoti mnamo 25/11/2018 kuwa “Manuari tatu za Ukraine ziliingia eneo la bahari ya Urusi kinyume na sheria na zilijihusisha na mienendo hatari.” Natija yake, Ukraine ilitoa wito kwa Magharibi kuingilia kati. “Ujerumani ni moja ya washirika wetu wanne wa karibu, na tunataraji kuwa nchi za NATO ziko tayari kutuma meli katika Bahari ya Azov ili kuisaidia Ukraine na kuhakikisha usalama huko”, Raisi wa Ukraine Petro Poroshenko aliliambia gazeti la Bild la Ujerumani mnamo 29/11/2018. “Putin hataki chochote isipokuwa kuikalia Bahari ya Azov. Lugha pekee anayoielewa ni umoja wa ulimwengu wa Kimagharibi … Ujerumani pia ni lazima ijiulize je, Putin atafanya lipi jengine endapo hatutamzuia … Hatuwezi kukubali sera hii ya kivamizi ya Urusi: kwanza ni bara la Crimea na kisha mashariki mwa Ukraine na sasa Putin anataka Bahari ya Azov anataka kurudi kwa ufalme wa kale wa Urusi: Crimea, Donbass, anataka nchi yote.”
Aliongeza kusema: “Merkel aliiokoa nchi yetu mnamo 2015 kupitia majadiliano yake huko Minsk, kwa hivyo tunataraji kupata hifadhi tena kupitia muungano wa wengine pamoja na sisi.” Lakini Ujerumani ilikataa kitendo cha kijeshi. Chansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema: “Hakuna suluhisho la kijeshi kwa haya makabiliano …” (DPA 29/11/2018) na kumuomba Poroshenko kuwa “kati na kati” na kuomba kuwa “hali hiyo itasalia kuwa tulivu … na kuweka mambo mezani na kuona yale yatakayotokea …” na aliapa kujadili jambo hili na Putin nchini Argentina. Alikataa kuongezwa vikwazo juu ya Urusi. “Berlin haitarajii vikwazo vya EU dhidi ya Urusi kwa sababu ya mzozo wake na Ukraine maadamu juhudi za kuzuia kupamba moto zinaendelea”, Waziri wa Kigeni wa Ujerumani Heiku Maas alisema baada ya mkutano wake na mwenzake wa Ukraine Pavlo Klimkin nchini Italy katika kongamano la mawaziri wa kigeni wa EU mnamo 6/12/2018. Aliongeza kusema: “Kwa sasa nadhani itakuwa ni makosa kuzungumzia kuhusu vikwazo vipya kwa sababu juhudi zinafanywa kupunguza taharuki …
Hakutakuweko na mapendekezo kutoka upande wa Ujerumani ya vikwazo vipya … Sitarajii itifaki ndani ya EU ya kulazimisha vikwazo vipya,” (Reuters, 7/12/2018). Ujerumani na nyingi ya nchi za Ulaya zinajua uzito wa hali hii na madhara yake kwa Ulaya, hivyo basi haitaki vitendo vya kijeshi na haitaki kukazanisha vikwazo, kwa sababu huo ni upanga wenye makali pande mbili kwa Urusi na Ulaya.
5- Msimamo wa Amerika uko wazi yaani kwa taharuki na ukazanishaji vikwazo. Trump alifutilia mbali mkutano wake na mwenzake wa Urusi Putin juu ya kadhia za kongamano la G20 nchini Argentina mnamo 30/11/2018 kwa sababu ya kutoridhika kwa utawala wake na kuzuiliwa kwa meli za Ukraine. Trump aliwaambia maripota kabla ya mkutano wake na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe katika mji mkuu wa Argentina Buenos Aires, kuhusiana na kuzuiliwa kwa meli za Ukraine na Urusi: “Hatupendezwi na kile kilichotokea na hatufurahishwi nacho na hakuna anaye furahishwa nacho” (RT Online, Novemba 30, 2018 – Novosti). Balozi wa Amerika kwa Ukraine, Kurt Volker, alisema manmo 27/11/2018: “Uongozi wa Urusi unatafuta kulazimisha udhibiti wa upande mmoja juu ya bandari hizo, ikiwemo Mariupol pasi na yeyote mwengine kuzifikia … Jaribio la Urusi la kudhibiti, lenyewe linaibua wasiwasi mkubwa, na akasisitiza kuwa Urusi ni sharti ijifunge na makubaliano ya 2003 juu ya usafiri katika Bahari ya Azov … Haamini kuwa Urusi itaanzisha mashambulizi mapya ya nchi kavu kwa eneo la Ukraine, endapo tukio kama hilo litatokea itakuwa ni mshangao mkubwa kwake …” (Ukurasa wa Ukraine, Al-Arabiya 28/11/2018).
Makubaliano haya yanathibitisha kuwa Bahari ya Azov na mkondo wa Kerch ni bahari ndani ya Urusi na Ukraine. Idhaa ya redio ya VOA iliripoti mnamo 6/12/2018 kuwa: “Balozi maalumu Kurt Volker atafanya ziara nchini Ukraine katika wiki mbili zijazo na kuitaka Urusi kuwaachilia huru mabaharia wa Ukraine walio katika kizuizi chao na kuthibitisha kuwa Urusi inapaswa kurudi na kushirikiana na Ukraine katika mkondo wa Kerch na Bahari ya Azov kwa msingi wa makubaliano maalumu ya pande zote mbili yaliyotiwa saini mnamo 2003.” Kama ilivyo dhahiri katika taarifa hizo, Amerika hayaendi kwa kasi, haina haraka, Balozi wake Maalumu kwa Ukraine alitangaza kuwa atazuru Ukraine baada ya wiki mbili! Ikimaanisha kuwa hana hamu na kutatua hali hiyo, bali kuidumisha hali hiyo kuwa ya taharuki, na kuendeleza taharuki hiyo na wala sio kutatua tatizo hilo!
6- Ni muhimu kutaja kuwa Amerika inaipa Ukraine silaha na vifaa na kulipa mafunzo jeshi lake. Balozi wa Amerika nchini Ukraine, Kurt Volker, aliiambia tovuti ya Deutsche Welle ya Ujerumani mnamo Novemba 29, 2018 kuwa “Kiev na Washington zimefungamanishwa na ushirikiano wa kawaida katika sekta ya ulinzi … na kwamba nchi yake inaisaidia Ukraine katika njia iliyo na mpangilio na katika mageuzi ya majeshi yake kwa mtazamo wa kuiwezesha dola ya Ukraine kuwa na uwezo imara wa ulinzi wa kisasa.” Afisa huyo wa Amerika anakiri kuwa nchi yake inaipa silaha Ukraine.
Tovuti ya Russia Today ilitaja, tarehe kabla ya 9/6/2018: “Amerika ilituma ndege nne katika uwanja wa ndege wa jiji la Lvov magharibi mwa Ukraine ili kuzipa ndege hizo za ulipuaji za kimikakati mafuta katika mpangilio wa ushirikiano na washirika wa Kiatlantiki ili kuhakikisha usalama wa Ulaya Mashariki, kwa mujibu wa Washington, na kuwasili pamoja na ndege hizo wahudumu na mafundi wake 150 wa Kiamerika. Ilinukuu afisi ya habari ya Jeshi la Anga la Amerika barani Ulaya na Afrika ikisema kuwa: “Lengo la hatua hii ni kupata usalama zaidi wa Amerika eneo la Ulaya Mashariki na ushirikiano zaidi wa kijeshi baina ya wanachama wa NATO na washirika wake.” Gazeti hilo la Urusi liliongeza kusema: “Ushirikiano wa Amerika na Ukraine unaongezeka imara tangu mapinduzi dhidi ya serikali ya Ukraine mnamo 2014, Ukraine ilianza kupokea zana za Kiamerika, ndege zisizo rubani, mitambo ya rada, vifaa, bunduki na mifumo ya kujihami dhidi ya vifaru, Waamerika wameweka sharti kuwa visitumiwe Donbass”. Kwa sasa Amerika inafanya kazi ili kuleta hali ya taharuki kupitia kuipa silaha Ukraine na inaishajiisha kuichokoza Urusi; hivyo basi Urusi inalazimika kujibu uchokozi huo. Hili ndilo inalotaka Amerika ili kuidumisha hali kuwa ya taharuki, na kisha kuzipeleka kadhia za Crimea na Ukraine kwa mujibu wa maslahi yake … Tunajikumbusha yale tuliyosema katika jibu la swali 22/3/2014 baada ya Urusi kutangaza mnamo 18/3/2014 kuiunganisha Crimea, ambayo ilikuwa sehemu ya Ukraine, tulisema, “Ukraine itasalia kuwa bomu linalo subiri kulipuka pindi masharti ya kimataifa na ya kieneo yatakapo badilika ima kwa manufaa ya Urusi au Magharibi, kisha kila upande utajaribu kuichukua Ukraine yote kwa mujibu wa dhurufu za kimataifa za wakati huo … Ukraine ni kiuno cha Urusi, wakati huo huo ni mlango wa Ulaya.
7- Amerika inaisukuma Ukraine kisiri siri ili kuichokoza Urusi, kupitia kuishajiisha kuichukua tena haki yake ya Crimea na kupanua mamlaka yake juu ya sehemu ya mashariki chini ya ushawishi wa Urusi na kutetea haki zake katika Bahari ya Azov katika Mkondo wa Kerch, ambao ni mkondo muhimu mno na wa kistratejia kwa nchi zote mbili. Ndio mkondo wa pekee kutoka Bahari ya Azov upande wa kaskazini hadi Bahari Nyeusi upande wa kusini … Inaipa silaha, na hili linakiuka Makubaliano ya Minsk. Na hivyo basi Amerika inafanya kazi kuyahujumu makubaliano haya kati ya Ulaya na Urusi, pamoja na kuongeza taharuki … huku Ulaya ikifanya kazi ya kuzima taharuki hiyo, kwa sababu imeelekezwa dhidi yake, na hivyo basi tunaona kuwa Ulaya inafanya kazi kwa maelewano na Urusi huku ikifanya kazi kuikomboa kutokana na utawala wa Amerika juu yake. Miito ya Muungano wa Ulaya ya kuunda jeshi huru ili kuihifadhi kutokana na Urusi na Amerika inakua … hasira za Amerika juu ya hili iko dhahiri kama kile kilicho tokea katika mkutano wa Raisi wa Ufaransa Macron pamoja na mwenzake wa Amerika Trump jijini Paris mnamo 9/11/2018, pamoja na tangazo la vita na biashara ililenga Ulaya, na wito wa hadharani wa Amerika wa kuvunjwa kwa Muungano wa Ulaya, na kutoridhika na sintofahamu baina ya wazungu na Waamerika katika mikutano ya NATO katika kongamano la G-7 mwaka huu na mwaka jana, na majaribio ya wazungu kupambana na Amerika katika baadhi ya kadhia, ikiwemo Ukraine … Yote haya yaliifanya Amerika kuongeza hali ya taharuki baina ya Ukraine na Urusi katika mpaka wa Ulaya.
8- Urusi iko katika hali ngumu. Iko matatizoni kuhusiana na Ukraine, ambayo inaikadiria kuwa kadhia muhimu kwake. Endapo itaipoteza, itafichuka kwa Magharibi, na mji wake mkuu, Moscow, utakuwa uko hatarini, hususan baada ya kuipoteza Ulaya Mashariki, ambayo ilikuwa ndio kina chake cha kistratejia cha kujihami kwake. Imehadaiwa na Magharibi na hususan Amerika, mara nyingi, kupitia kukubali kuanguka kwa ukuta wa Berlin, na kuikabidhi Ujerumani Mashariki kwa Ujerumani Magharibi, kuisalimisha Poland, kukubali uhuru wake na uhuru wa nchi za Mashariki mwa Ulaya. Na sasa inahadaiwa tena nchini Ukraine! Baada ya kukubaliana nao mnamo 2014 juu ya kusalia mamlakani kibaraka wake Yanukovych, Magharibi iliwashajiisha watu wa Ukraine kumng’oa. Kisha njama nchini Syria! Amerika imeihadaa Urusi kupitia kuisukuma kupigana kwa niaba yake na bila yake nchini Syria, hivyo basi Urusi ilidhani kuwa Amerika itanyamazia kimya juu ya kuiunganisha kwake Crimea na udhibiti wake juu ya mashariki mwa Ukraine, hii ilikuwa ni bila ya kuchukua utambuzi wowote wa Amerika wa udhibiti wake juu ya maeneo haya! Lau kama Urusi haingekuwa mjinga, haingeingilia kati nchini Syria na ingeiwacha Amerika ijiingize katika vita hivyo na kubakia imekwama ndani yake kama ilivyo nchini Afghanistan.
9- Kwa kutamatisha:
a- Viashiria vya matukio vyaonyesha kuwa Amerika haiko mbali na kuwa kishajiisho nyuma ya harakati ya meli za Ukraine katika Bahari ya Azov pasi na mawasiliano na Urusi … Na kwamba malengo ya Amerika ni kutia hali ya taharuki ili kuipatiliza kuhudumia maslahi yake katika maumbile haya matatu: Urusi, Ulaya na Ukraine … Amerika inataka “kutia hali ya taharuki” na sio kutatua tatizo, ili ibakie mahali pake na taharuki iendelee!
b- Ulimwengu huu, maadamu unadhibitiwa na dola hizi za kisekula za kirasilimali, utasalia kuwa mandhari ya njama ovu, uhalifu wa kinyama na kuenea kwa dhulma katika aina zake zote … Fahamu za ukoloni zimekita mizizi katika nchi hizo, na hujitokeza kila waendako.
c- Mfumo mtukufu wa Uislamu ndio pekee unao okoa ulimwengu kutokana na uovu wa nchi hizo na mifumo yao iliyo undwa na binadamu. Hii ni kwa sababu Uislamu umeteremshwa na Muumba wa binadamu, na Muumba huyu ndiye pekee anayejua kheri ya viumbe Vyake.
(أَلَا يَعْلَمُ مَنْ خَلَقَ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ)
“Asijue aliye umba, naye ndiye Mjua siri, Mwenye khabari?” [Al-Mulk: 14]
Huu ndio ukweli unaosimamisha uadilifu na kueneza kheri
(فَمَاذَا بَعْدَ الْحَقِّ إِلَّا الضَّلَالُ)
“Na kipo kitu gani baada ya haki, isipokuwa upotovu?” [Yunus: 32]
(إِنَّ فِي ذَلِكَ لَذِكْرَى لِمَنْ كَانَ لَهُ قَلْبٌ أَوْ أَلْقَى السَّمْعَ وَهُوَ شَهِيدٌ)
“Hakika katika hayo upo ukumbusho kwa mwenye moyo au akatega sikio naye yupo anashuhudia." [Qaf: 37]
7 Rabii’ Al-Akhar 1440 H
Ijumaa, 14/12/2018 M