Jumatano, 23 Jumada al-thani 1446 | 2024/12/25
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Jibu la Swali
Maandamano Makubwa Yaliyo Zagaa Amerika na Athari yake kwa Sera ya Kigeni

(Imetafsiriwa)

Swali:

Karibu wiki mbili zilizo pita, Amerika ilizongwa na maandamano makubwa katika baadhi ya maeneo yaliyojaa ghasia, uporaji wa maduka, na uteketezaji vituo vya polisi. Je, mauaji ya mtu mmoja mweusi nchini Amerika yaweza kuchochea maandamano kama hayo? hili limetokea mara nyingi katika miaka michache iliyo pita na hakukuwepo na maandamano kama haya! Je, kuna athari zozote za maandamano haya ya Amerika kwa sera ya kigeni?

Jibu:

Ili kupata majibu ya wazi kwa maswali hayo ya juu, tunatathmini yafuatayo:

1- Polisi wa Amerika alimuua mtu mwenye asili ya Kiafrika, George Floyd, jijini Minneapolis, katika jimbo la Amerika la Minnesota, mnamo 25/5/2020, na ulikuwa ni uhalifu wa kinyama, ambapo polisi huyo alitumia mafunzo aliyopokea katika jeshi la polisi; kwa kusimama juu ya shingo na kuufinyilia mshipa wa damu wa carotid. Uhalifu huo ulichukua dakika tisa, ambapo Floyd alikuwa akipiga mayowe "Siwezi kupumua" hadi kufa. Uhalifu huu wa kuogofya ulishuhudiwa na Waamerika wote, na waliona kwa macho yao wenyewe ukatili wa polisi wa Amerika dhidi ya weusi. Siku iliyofuatia, maandamano yalilipuka jijini humo kushutumu kiwango hiki cha ukatili katika kuamiliana na wanadamu. Kisha maandamano hayo kuenea katika miji mengine ya Amerika, na kusambaa kwa video hiyo ya uchungu wa kuzibwa pumzi, kupitia mitandao ya kijamii, hadi maandamano hayo kuenea zaidi ya miji 80 ya Amerika katika majimbo mengi …

Kisha mamlaka zikatangaza marufuku ya kutotoka nje usiku ili kuzuia maandamano hayo, mengi yao, yaliandamana na vitendo vya ghasia, mauaji, uporaji, na uteketezaji maduka na vituo vya polisi. Polisi wa Amerika waliamua kutumia njia za kikatili dhidi ya waandamanaji na kuwakamata zaidi ya watu 4000 katika miji tofauti tofauti ikitangazwa mauaji ya watu wachache, Askari wa kitengo cha National Guard waliitwa kuweka usalama na udhibiti wa barabara, na hata jeshi la Amerika liliitwa, hali ambayo haijawahi kutokea kabla nchini Amerika, ili kuweka usalama katika jiji kuu la Washington. Rais Trump alifichwa katika sehemu salama chini ya ardhi kwa hofu ya waandamanaji kuvamia ikulu ya White House.

2- Matukio ya maandamano ya Amerika yalichafua sura ya utulivu wa kindani ambao serikali za Amerika mtawalia zimekuwa zikijigamba nao, huku moto ukizuka, maduka yaliporwa, na vituo vya polisi kuharibiwa kwa idadi kubwa, hili likitoa onyo kwa Waamerika la mateso ambayo serikali za Amerika zimeyatekeleza kwa muda mrefu katika nchi nyenginezo. Na kuwatishia kwa unyanyasaji na uharibifu ambao Amerika inayatumia kuamiliana na ulimwengu kumbe ndio njia itakayo amiliana na Waamerika wenyewe. Matukio haya yalikuwa ya kushtua kwa viwango vyote: raisi anaye waonya na kuwatishia waandamanaji wa amani kwa mbwa wenye ugonjwa wa kichaa cha mbwa pambizoni mwa ikulu ya White House, na kwa silaha hatari zaidi ulimwenguni endapo watajaribu kuvamia kuta za White House, ambayo umezungukwa kwa vizuizi vya waya na kuta za simiti. Raisi huyo alitoa wito kwa magavana wa majimbo kuwajibu kwa ukali waandamanaji hao katika majimbo yao, na kushinikiza usalama kwa lazima, na akawaruhusu kutumia askari wa National Guard, na kuliweka jeshi la Amerika katika hali ya tahadhari ili kuingilia kati ndani ya masaa inapo hitajika ikiwa polisi na askari hao watashindwa kuweka usalama, na kwa hakika jeshi lilipelekwa jiji kuu la Washington DC kabla ya hatua hii kugeuza, baada ya kusambaa kwa tuhma za Raisi dhidi ya mandhari ya kulitoa Jeshi la Amerika dhidi ya watu. Upande mwengine, umati wenye hasira, sehemu nyengine ukiwa na amani, ambao hawakuweza kusitishwa na polisi, askari, au hatari ya virusi vya korona, wanaolalamikia kudai haki za watu, kuwahisabu wauaji, na kufanya mabadiliko polisi, na sehemu ya pili ya waandamanaji inalenga kushambulia vitua vya serikali, hususan polisi, na kuviteketeza na kuviharibu. Baadaye Rais Trump alitangaza kuwa vuguvugu la Antifa la mrengo wa kushoto linalo pinga urasilimali! Na sehemu ya tatu ya waandamani wanapora, kuiba, na kutekeleza vitendo vya uharibifu.  

3 – Uhalisia wa polisi wa Amerika, ambao kiungo kikuu chao ni kiungo cheupe, wanatumika kuwatusi watu weusi, na wengi wao waliuwawa na polisi. Baadhi ya matukio haya yalinakiliwa na kuonyeshwa, kama mauaji ya hivi majuzi ya Floyd, na matukio haya hayakuadimika, bali yanajirudia. Ubaguzi wa rangi nchini Amerika ni tukio la kuu, linalo onekana ndani ya mujtamaa zao. 

Lakini kuna sababu kwa nini mauaji ya Floyd mnamo 25/5/2020 katika jiji la Minneapolis yalipanua upeo wa ghadhabu dhidi ya sera ya ubaguzi wa rangi inayo fuatwa na vyombo vya dola nchini Amerika dhidi ya weusi hususan kutokana na sababu hizi, baadhi yazo ni za zamani na baadhi ni mpya, sababu hizi ni:

a- Kufeli katika mchakato wa uwiano katika mujtamaa wa Amerika: mujtamaa wa sasa wa Amerika umeasisiwa waziwazi juu ya ubaguzi wa rangi. Wahamiaji haswa wa Kiingereza, na Wazungu kwa jumla, waliikoloni Amerika kwa kuwauwa mamilioni ya Waamerika Wanati, wenyejii asili. Na kwa sababu ya haja ya koloni mpya kwa ajili ya kazi, watumwa waliletwa kutoka Afrika, hivyo Waamerika wenye asili ya Kiafrika wanatazwa kama watumwa. Hili lilikuwa rasmi kwa karne nyingi, ambapo Waafrika hawa wanakumbwa na ubaguzi wa rangi, kulazimishwa kufanya kazi katika mashamba ya weupe na viwanda vyao. Sheria ya Utoaji Uraia ya 1790 iliwapa uraia wa Amerika weupe pekee, huku ikikataa kuwatambua weusi kama raia, licha ya Waafrika kupata baadhi ya haki, kama vile kupiga kura katika miaka ya 1860s. Lakini, ubaguzi wa rangi ulibakia kama sera rasmi iliyo tekelezwa nchini Amerika hata baada ya kumalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe, na baada ya katikati mwa karne ya ishirini vuguvugu kubwa lililoitwa vuguvugu la haki za umma lilizuka na Martin Luther King Mwana akawa ndio kiongozi wake maarufu wa weusi nchini Amerika, na kupelekea kutambuliwa rasmi kwa haki zao kamili kama raia wa Amerika…

Hivyo, Waafrika hawa walidhani kuwa wamepata haki zao za umma ambazo wazazi wao na babu zao walinyimwa lakini hilo halikubadilisha sana fikra ya Waamerika weupe, ambapo mtazamo wao finyo kwa Waafrika hawa ulibakia, na vitendo vya kibaguzi dhidi yao viliendelea. Licha ya kupayuka kwa viongozi wa Amerika kuwa ubaguzi wa rangi umekwisha, ripoti kadhaa zilijadili mtazamo wa ubaguzi wa rangi uliokita mizizi nchini Amerika dhidi ya watu wenye asili ya Kiafrika … na katika viashiria vya ubaguzi wa rangi dhidi ya watu weusi nchini Amerika ni ongezeko wazi la idadi ya wafungwa weusi ikilinganishwa na Waamerika weupe, na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira miongoni mwao, na tofauti kubwa na wazi katika pato la wastani kati ya familia za Kiamerika zenye asili ya Kiafrika na za Waamerika weupe, pamoja na kupungua kukubwa katika huduma za afya, na huduma nyenginezo, baina ya maeneo ambayo aghlabu ya wakaazi wake ni raia weusi na kuitwa mitaa ya weusi. Maeneo ambayo yanakadiriwa kuwa ni ya kifahari, yana huduma bora za afya, bei za nyumba wanamoishi Waamerika weupe ziko juu.  

b- Kuwasili kwa Utawala wa ubaguzi wa rangi wa Trump na kuwakumbatia wapigiaji debe ubwana wa Asili Nyeupe: Makundi yanayo muunga mkono Raisi Trump yanaamini ubwana wa Asili Nyeupe juu ya nyenginezo, ni makundi ambayo yametukuzwa baada ya kuwasili kwa Trump ikuluni White House, na watu hawa wamepata kutoka kwa Trump kiongozi wao wa kitaifa: wamechanganyika na Wakristo wa kiinjili wanao ongeza mambo ya kidini katika ubwana huu. Uwazi wa Raisi Trump dhidi ya Waislamu, na kuwazuia baadhi yao kupata stakabadhi za usafiri (visa) ili kuingia Amerika, taarifa zake dhidi ya Mexico, na mipango yake, ambayo baadhi yake ilikuwa ni kujenga ukuta katika mipaka ya Mexico, na vita vyake vya kibiashara dhidi ya China, na kuviita virusi vya Korona virusi vya China, na kuibuka kwa wimbi la uadui dhidi ya Wachina nchini ya Amerika, kuridhia kwake maandamano mapya ya Nazi jimboni Virginia mnamo 2017, lugha yake ya matusi dhidi ya walio wachache, pamoja na maoni yake juu ya mauaji ya mtu mweusi Floyd na haja ya kuzima vuguvugu la maandamano katika kuunga mkono haki za weusi nchini Amerika … na matokeo ya yote haya, Raisi Trump amekuwa mmoja wa wachochezi wakubwa kabisa wa ubaguzi wa rangi nchini Amerika, hivyo idadi ya uadui dhidi ya weusi, Waislamu, Wamexico, na Wachina nchini Amerika imeongezeka katika kipindi cha uraisi wake. Wanaonekana kuwa wageni zaidi kuliko nyuma waliokuja kuwanyang'anya Waamerika nafasi zao za kazi na kufuja utajiri wa Amerika, na ubaguzi wa rangi umekuwa maarufu katika sekta nyingi za mujtamaa wa Amerika…

c- Athari za virusi vya Korona ndani ya mujtamaa wa Amerika: Mojawapo ya sababu zilizo ongeza moto maandamano dhidi ya mauaji ya Floyd nchini Amerika ni kuwa yalisadifiana na kusambaa kwa virusi vya Korona, na hatua za karantini zilizo fuata, ambazo zilisababisha ugumu kwa Waamerika upande mmoja, na upande mwengine, zilisababisha kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira. Ziliongeza wasiwasi wa Waamerika kuhusu mustakbali wao na tatu, Waamerika waliona kufeli kukubwa kwa serikali yao katika kukabiliana na kuenea kwa janga hili la maambukizi nchini Amerika, ambako kuna uhaba mkubwa wa bidhaa na vifaa vya matibabu na kushindwa kujiandaa kwa ajili ya virusi hivi, licha ya ukweli kwamba Amerika ilichapwa na wimbi la virusi hivi baada ya Ulaya na China, ambapo iliipa fursa nzuri ya kujiandaa kwa ajili yake, lakini haikupatiliza hili. Vilevile idara ya Amerika ilishindwa katika kukabiliana na janga hili la maambukizi na matokeo yaliyojitokeza ni mgawanyiko katika jamii ya kisiasa ya Amerika kuhusiana na namna idara ya Trump ilivyo kabiliana na janga hili la maambukizi …

Mojawapo ya kadhia nzito na muhimu za kindani ni kuwa hisia za mujtamaa wa Amerika zimekuwa kuhusu namna ya ubovu wa mfumo wa kirasilimali ulivyo. Mchakato wa ugavi wa utajiri nchini Amerika umezorota na kutishia kuzidi kuzorota, kwa kukipendela kikundi kigogo cha Warasilimali, walio na nguvu za upigiaji upatu zenye kushawishi siasa, sera inayo elekea upande wa kuwaondolea zaidi wao kodi, wakati ambapo watu walio na pato la wastani na la chini wanalipa kodi kubwa zaidi. Maandamano haya ya Amerika yameangazia nguvu inayoibuka ya vuguvugu hili dhidi ya urasilimali nchini Amerika, Antifa, ambalo Raisi Trump ametaka liorodheshwe kama la kigaidi, vuguvugu ambalo limeuita uvamizi wa masoko ya hisa katika Wall Street kama alama kuu ya Urasilimali baada ya mgogoro wa kifedha wa 2008, vuguvugu hili limeongeza wafuasi wake na linakita mizizi zaidi katika mujtamaa wa Amerika, na linatoa wito wa ghasia dhidi ya Urasilimali, na linatuhumiwa leo kuwaelekeza waandamanaji kuteketeza na kuharibu asasi za serikali kama vile vituo vya polisi.

4- Yote haya yamekuwa na athari juu ya sera ya kigeni ya Amerika, ambapo athari yake ni kutokana na sababu zifuatazo:

a- Hali ya mgawanyiko nchini Amerika: idara ya Trump imeonyesha kuwa tangu 2017 Amerika haina umoja, na sera zilizo wafanya Waamerika kugawanyika kwazo ni nyingi, kama vile vita, na usaidizi wa kimataifa unaotolewa na Amerika kwa vibaraka wake kote ulimwenguni, kama vile sera ya kodi, uamilianaji na walio wachache, uhamiaji, na sera nyingi nyenginezo. Lakini kuwasili kwa Raisi Trump, yeye mwenyewe amekuwa moja ya sababu kuu za mgawanyiko nchini Amerika, na shakhsiya yake imesaidia kwa kiburi chake kilicho pitiliza, kukwamia mamlaka, kupenda kuwa kimbelembele, ukosefu wa hekima, kupenda kupigana mizozo ya kindani, na kupenda uzuzuaji kupitia kuwavunja mahasimu. Yote haya yameifanya Amerika kugawanyika mno kuhusu Raisi Trump, ima wako pamoja naye au dhidi yake. Kufutwa kazi na kujiuzulu katika idara yake kumeongezeka, katika kiwango hiki ambacho hakijawahi kutokea kwa raisi yeyote wa zamani wa Amerika, na janga la virusi vya Korona, na malumbano kati ya raisi na magavana wa baadhi ya majimbo, yameonyesha ongezeko la ukali wa mgawanyiko wa Amerika. Mgawanyiko huu umevishambulia vituo vya kisiasa na vya kifedha vya Kiamerika, na unaakisiwa katika mujtamaa wote kwa jumla. Na namna raisi na idara yake walivyo kabiliana na mgogoro wa maandamano hayo maarufu, pia, imekuwa ni sababu imara inayo chochea mgawanyiko.

Trump anapinga vuguvugu hilo la maandamano baada ya Floyd kuuwawa, na anataka kuweka usalama kwa lazima, anapingwa katika hilo kupitia Chama cha Democrat na magavana wa majimbo, hata waziri wake wa ulinzi, aliomba radhi kwa kushiriki katika ziara ya Raisi kwenye kanisa moja karibu na ikulu ya White House baada ya vikosi vya usalama kuwafurusha waandamanaji kutoka katika eneo lake, ilikadiriwa kuwa propaganda ya kisiasa ya Trump. Miongoni mwa mifano mipya na ukali wa mizozo hii ("mawaziri wa zamani wa ulinzi wa Amerika na maafisa kadhaa wa kijeshi walimtuhumu – katika taarifa ya pamoja – Raisi Trump kukhini kiapo na katiba, kwa kuzingatia kwake kupeleka majeshi kukabiliana na waandamanaji; miongoni mwa walioitia saini ni Waziri wa zamani wa Ulinzi James Mattis." (Chanzo: Al-Jazeera.net 7/6/2020). Kadhia hii haikufungika kwa mawaziri wa zamani wa ulinzi, bali ilijumuisha wa sasa na kwa majibu makali, kwa mujibu wa chanzo kilicho tangulia chenyewe:

(CNN ilimnukuu afisa mmoja wa Pentagon akisema kwamba Raisi Donald Trump aliomba kupelekwa kwa wanajeshi elfu kumi katika jiji kuu, Washington DC, na miji mengine ya Amerika, ili kupambana na maandamano ya wiki iliyopita, na kwamba Waziri wa Ulinzi Mark Esper na Mwenyekiti wa Wakuu Wote wa Majeshi Mark Milley alikataa ombi hili kuhusiana na maandamano makubwa jijini Washington na miji mingine ya Amerika na Ulaya dhidi ya ubaguzi wa rangi na ukatili wa polisi. Jarida la 'The New Yorker' lilikuwa limeripoti kwamba limepata taarifa, kutoka kwa duru za ikulu ya White House, kwamba majibizano yalitokea kati ya Raisi Trump na Jenerali Mark Milley. Katika ripoti ya jarida hilo ilitaja kuwa Jenerali Milley alipandisha sauti yake usoni mwa Raisi kupinga dhidi ya ombi lake la kupeleka majeshi katika barabara za miji ya Amerika ili kumaliza maandamano, kwani Milley anaamini kuwa upelekaji majeshi barabarani ni kinyume na sheria.) 

b- Kipindi cha uchaguzi wa uraisi: kimekoleza jambo hili. Maandamano haya yalizuka kwa kusadifiana na kampeni za uchaguzi wa mgombezi wa Democtrat Joe Biden pamoja na wa Republican Trump. Raisi Trump ana wasiwasi mno kuhusu mustakbali wake kama Raisi, na anataka kuchaguliwa tena mnamo Novemba mwaka huu, bali kadhia hii ndio kipaumbele chake nambari moja lakini wasiwasi wake mkubwa ni natija za virusi vya Korona, athari zake juu ya uchumi wa Amerika, kupotea kwa mamilioni ya kazi za Waamerika, na yale yanayo semwa kuhusu kutokabiliana kwake vyema na janga la virusi hivi. Anahofia kwamba hili litakuwa ndio jambo ambalo mpinzani wake wa Democtrat atalitumia dhidi yake katika kampeni za uchaguzi. Kisha linakuja wimbi la maandamano ya hivi karibuni ambayo Raisi Trump alitaka kuangazia shakhsiya yake kama mtu imara anaye weza kudhibiti usalama, kudumisha rasilimali, ambapo inaongeza fursa zake za uchaguzi… Lakini mpinzani wake, Joe Biden (Chama cha Democtrat) na nguvu nyenginezo zinafanya kazi kuonyesha haya kuwa kinyume, hivyo wanamuonyesha kama mtu anaye fanya kazi kudumisha mgawanyiko nchini Amerika, na hawezi kupoza vidonda ambavyo mujtamaa wa Amerika umeteseka navyo baada ya mauaji ya Floyd na maandamano, na wanamhisabu kwa maumbile ya ghasia na fujo katika maandamano hayo, kwa sababu ya taarifa zake kali dhidi ya waandamanaji.

c- Uzimaji wa dola wa maandamano: Nchi za ulimwengu zimeshuhudia njia chungu na ya kinyama ambayo kwayo serikali ya Amerika inakabiliana na maandamano hayo maarufu, mazungumzo ya raisi kuhusu kuweka usalama kwa lazima, mbwa wenye ugonjwa wa kichaa cha mbwa na kwa silaha hatari zaidi. Na kutazama maelfu ya watu wakikamatwa, marungu na gesi za kutoa machozi nchini Amerika, baada ya kuwa na kinga kwa matukio kama hayo kwa miongo mingi. Yote haya yanaifanya Amerika kupoteza hoja yake iliyoitumia kwa muda mrefu dhidi ya wapinzani wake kote ulimwenguni chini ya anwani ya haki za kibinadamu, haki ya kutoa rai, uungaji mkono upinzani, nk. hili lina athari ya moja kwa moja, inayoifanya sera ya kigeni ya Amerika kupoteza mojawapo ya uhalalishaji wake maarufu zaidi … Haya yanathibitishwa na yale aliyo sema msemaji wa Wizara ya Kigeni ya Urusi Maria Zakharova, ("Kuanzia mwishoni mwa Mei na mwanzoni mwa Juni 2020 Amerika imepoteza haki yoyote ya kuelekeza maoni yoyote kwa yeyote duniani juu ya kadhia za haki za kibinadamu." Zarakhova aliongeza, akitoa maoni juu ya namna mamlaka za Amerika zilivyo kabiliana na waandamanaji, walioshiriki katika maandamano dhidi ya ubaguzi wa rangi na ukatili wa polisi nchini Amerika: "Imekwisha! Kuanza sasa, hawana haki hii." (Chanzo: Al-Yowm As-Sabi’, 2/6/2020)).

5- Hivyo, ubaguzi wa rangi umekita mizizi nchini Amerika, huenda ukawa umenyamaza kwa muda lakini mara nyingi uko hai. Ni maradhi ya kifikra katika vyanzo vya kuibuka kwa mfumo wa Kiamerika wa kirasilimali, bali hayakosekani katika sheria yoyote iliyo tungwa na mwanadamu, kwa sababu huegemea matamanio na hawaa za wanadamu ambao ndio wanao amua ubwana wa weupe juu ya wenye rangi ya kahawa, na wekundu juu wenye rangi ya manjano .. hata kama baadaye tofauti hii itasababisha madhara yote kwa wengine, bali hata kwao binafsi!    

Ni Uislamu pekee ndio ulio ondoa, na unao ondoa, ubaguzi huu wa rangi, hivyo hakuna utofautishaji baina ya watu kwa msingi wa rangi, hadhi ya juu au utajiri. Bali, wote wako sawa, na hutofautishwa pekee kwa uchaMungu (Taqwa). Mwenyezi Mungu (swt) asema:

 [يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُمْ مِنْ ذَكَرٍ وَأُنْثَى وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوباً وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِنْدَ اللَّهِ أَتْقَاكُمْ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ خَبِير]

“Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari.” [Al-Hujurat: 13]

Mtume (saw) amesema katika hadith iliyo ripotiwa na Al-Bayhaqi (384-458 H) kutoka kwa Abu Nadhrah kutoka kwa Jabir Ibn Abdullah, aliye sema, Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alisema katikati ya siku za Tashreeq (za Hajj) katika hotuba ya Hijja ya mwisho:

«يَا أَيُّهَا النَّاسُ، إِنَّ رَبَّكُمْ وَاحِدٌ، وَإِنَّ أَبَاكُمْ وَاحِدٌ، أَلا لا فَضْلَ لِعَرَبِيٍّ عَلَى عَجَمِيٍّ، وَلا لِعَجَمِيٍّ عَلَى عَرَبِيٍّ، وَلا لأَحْمَرَ عَلَى أَسْوَدَ، وَلا أَسْوَدَ عَلَى أَحْمَرَ، إِلا بِالتَّقْوَى، إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِنْدَ اللهِ أَتْقَاكُمْ، أَلا هَلْ بَلَّغْتُ؟»، قَالُوا: بَلَى يَا رَسُولَ اللهِ، قَالَ: «فَلْيُبَلِّغِ الشَّاهِدُ الْغَائِبَ»

"Enyi watu, hakika Mola wenu ni mmoja, na hakika baba yenu ni mmoja. Hakuna ubora kwa Muarabu juu ya asiye kuwa Muarabu, wala kwa asiye kuwa Muarabu juu ya Muarabu, wala kwa mwekundu juu ya mweusi, wala kwa mweusi juu ya mwekundu, isipokuwa kwa uchaMungu (Taqwa). Hakika, mbora wenu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu ni mcha Mungu zaidi wenu. Je, nimewafikishia?" Wakasema: "Bila shaka umetufikishia ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu." Akasema: "Basi yule aliyeko na amfikishie yule asiye kuwepo"

Hadith hii pia imeripotiwa na Al-Busairi (762-840 H), na hadith hii pia imesimuliwa na At-Tabarani (260-360 H), amesema katika riwaya yake:

«وَلَا لِأَسْوَدَ عَلَى أَبْيَضَ وَلَا لِأَبْيَضَ عَلَى أَسْوَدَ»

“wala kwa mweusi juu ya mweupe wala kwa mweupe juu ya mweusi.”

Ni Uislamu pekee ndio unao maliza ubaguzi wa rangi, umeteremshwa na Mola wa Walimwengu, unaongoza katika haki na kueneza kheri kote ulimwenguni.

 [أَفَمَنْ يَهْدِي إِلَى الْحَقِّ أَحَقُّ أَنْ يُتَّبَعَ أَمَّنْ لا يَهِدِّي إِلا أَنْ يُهْدَى فَمَا لَكُمْ كَيْفَ تَحْكُمُونَ]

“Basi, je, anaye stahiki kufuatwa ni yule Mwenye kuongoa kwendea Haki au asiye ongoa ila aongozwe yeye? Basi nyinyi mna nini? Mnahukumu namna gani?” [Yunus: 35]

20 Shawwal 1441 H

11/6/2020 M

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoAlhamisi, 18 Juni 2020 15:35

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu