Jumanne, 07 Rajab 1446 | 2025/01/07
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Je, Kazi ya Kusimamisha Tena Khilafah Imefikia Wapi?
(Imetafsiriwa)

Pindi Allah (subhanhu wata’ala) alipo taka kuinusuru dini yake, Uislamu, Yeye (subhanhu wata’ala) alifungua njia ya kuibuka kwa dola ya Kiislamu mjini Al Madinah kupitia kuzifanya hali za ndani na nje kuwa tayari kwa mazazi yake.

Kuhusu hali ya ndani, A'ishah, (ra) ameripotia kuwa Allah (subhanhu wata’ala) alifungua njia ya ushindi kwa dini yake kupitia vita vya Bua'ath vilivyo pelekea vifo vya viongozi wakongwe wa makabila ya Al-Aws na Al-Khazraj; tofauti na Makkah na Taif. 

Kuhusu hali za nje, kulikuweko na mgogoro baina ya Ufalme wa Kifursi na Ufalme wa Kirumi. Zaidi ya hayo, kulikuweko na ufisadi, dhulma na umasikini yaliyo sababishwa na dola hizo.

Ingawa mazazi ya Khilafah leo yanatarajiwa wakati wowote chini ya hali yoyote ya kieneo au ya kimataifa, mtu anaweza kushangazwa na matukio ambayo Allah (subhanhu wata’ala) anayatumia kutoa mwanya wa kuzaliwa tena Khilafah. Matukio haya na hali hizi yanajumuisha (1) kuanguka kwa maadui zetu, (2) kuamka kwa Umma wa Kiislamu, na (3) maendeleo ya Hizb ut Tahrir ("Hizb").

Makala haya yamekusudia kuelezea nukta hizi tatu kwa ufafanuzi; na wala hayakusudii kuchambua Aya na Hadith zinazo toa bishara njema ya kurudi kwa Khilafah. 

Ama kuhusu kuanguka kwa maadui zetu:

Waandishi wengi, kama Noam Chomsky na Emmanuel Todd, walianza kuiita Amerika "mtu mgonjwa" na wengine wakaanza kuzungumza wazi wazi kuhusu kuporomoka kwa Amerika na kujadiliana kuhusu hali ya kisiasa baada ya ufalme wake. Hii ni kutokana na yafuatayo:

1. Magharibi, na hususan Amerika, imekengeuka kutoka katika shina la mfumo wa urasilimali ambapo miito ya uhuru, haki za kibinadamu na demokrasia imeonekana kuwa feki. Kwa mfano:

(a) Mauaji ya watoto nusu milioni wa Iraq mnamo 1991, bila ya kutaja mamilioni ya wanaume na wanawake mnamo 2003,

(b) Aliyekuwa Raisi wa Amerika Bush mwana alisema katika dhifa nyingi kuwa Mungu alimzungumzisha na kumwambia afanye kadha na kadha. Hii ni licha ya kuwa Amerika ni dola ya kirasilimali na kimfumo inatakikana kutenganisha baina ya maisha na dini,

(c) Unyama uliotendwa katika jela za Abu Ghraib na Guantanamo mnamo 2003,

(d) Ufuatiliziaji wa Amerika wa maongezi ya simu, sio tu kwa raia wake, bali hata kwa Merkel na viongozi wengine,

(e) Hivi majuzi Theresa May aliulizwa ikiwa angetoa idhini ya shambulizi la kinyuklia linaloweza kuwaua maelfu ya wanaume, wanawake na watoto wasiokuwa na hatia. Alijibu "Ndio".

Urongo wa miito ya Kiamerika imewafanya Waamerika kuanza kuchukiwa ulimwengu mzima kutokana na serikali yao kuingilia mambo ya serikali zengine au nchi zengine. Hili limedhihirishwa kupitia maandamano ya mataifa yasiyo kuwa ya Kiislamu dhidi ya Raisi wa Amerika au dhidi ya maafisa wake wanao hudhuria makongamano au mikutano ya kimataifa. Kwa mfano:

(a) Mnamo 2014, kura ya maoni ilipigwa katika nchi 65, nchi marafiki na zisizo kuwa marafiki wa Amerika, na kura hizi zikatamatisha kuwa Amerika ni tishio kubwa la amani ulimwenguni,

(b) Mnamo Machi 2016, Raisi wa Cuba Raul Castro aliukukuta mkono wa Obama baada ya kumaliza mkutano wa pamoja wa waandishi habari mjini Havana, Cuba.

(c) Mnamo Septemba 2016, Barack Obama alilazimika kutoka kwa mlango wa nyuma wa ndege alipo zuru China kwa sababu Wachina hawaku muandalia ngazi zenye zulia jekundu la heshima,

(d) Barack Obama alifutilia mbali mkutano wake na Raisi wa Ufilipino Rodrigo Duterte mjini Laos kwa sababu alimuita Obama mtu aliye laaniwa,

(e) Miezi michache iliyopita, watu walio kuwa na hasira jijini Brussels waliandamana kupinga ziara ya Trump huku wakiwa na michoro ya vinyago vyake vikiwa na pua ndefu kuashiria kuwa ni mtu mrongo.     

Ama kuhusu hali ya ndani nchini Amerika, haina afadhali. Kwa mfano:

(a) Mnamo 2011, na kwa mara ya kwanza katika historia ya Amerika, waandamanaji (walio zingira barabara ya Wall Street) walilalamika na kutaka kubadilisha mfumo wa kirasilimali,

(b) Mnamo 2012, zaidi ya majimbo 15 ya Amerika yaliomba kujitenga kutokana na serikali ya majimbo ya Amerika,

(c) Mnamo 2016, watu walikusanyika dhidi ya ghasia kwa watu weusi,

(d) Punde baada ya kutangazwa Trump kuwa Raisi, watu waliandamana wakibeba mabango yaliyo andikwa "Wewe si raisi wangu".

2. Amerika, nchi ya kwanza duniani, imefeli kijeshi nchini Afghanistan na Iraq na kutokana na haya, kupoteza nguvu zake nyingi za kijeshi licha ya kuwa Afghanistan ni nchi dhaifu na Iraq ni nchi waliyokabidhiwa. Hili ni wazi kutokana na matamshi ya amiri jeshi mkuu Ray Odierno aliye sema, "Jeshi letu kwa sasa liko katika kiwango cha chini sana kimatayarisho tangu nianze kulitumikia muda wa miaka 37 iliyopita." Pia, katika Makala ya tarehe 16 Julai 2017 katika jarida la National Interest Magazine, Douglas Macgregor, kanali mstaafu, alisema, "Jeshi liko katika ukingo wa kupoteza pesa zaidi endapo Raisi Trump hata teua waziri mwenye nguvu na maarifa kwa jeshi hili – mtu ambaye atakuwa tayari kuwahisabu kwa lazima majenerali wake na kuitisha mabadiliko kamili. Litashindwa katika mapigano ya kwanza katika vita vinavyo kuja. Na, katika karne hii ya ishirini na moja, Waamerika hawatapata fursa nyengine ya kupigana vita vya pili."

Hili limeleta athari mbaya kwa Waamerika wenyewe ambapo siku hizi hufikiria mara elfu moja kabla ya kuamua kutuma vikosi vyake sehemu nyengine za ulimwengu wa Kiislamu. Hili lime dhihirika nchini Libya mnamo 2011 ambapo Amerika haikutuma vikosi vyake nchini humo, bali ilishiriki tu kijuu juu katika mashambulizi ya angani kupitia muungano wa NATO.

Kwa upande mwengine, hapana budi kuzingatiwa kuwa nguvu ya kijeshi haipimwi kwa idadi ya wanajeshi au silaha (Umoja wa Kisovieti uliporomoka huku ukiwa na hazina kubwa ya silaha) bali hupimwa kwa ari na kujitolea. Kwa mfano, wanajeshi wa Amerika nchini Iraq walidhani kuwa wako likizoni na kwamba hatimaye watarudi kwa familia zao na kupokea malipo yao ya kimada na kuishi maisha yao yaliyo bakia raha mustarehe, lakini hali haikuwa hivyo. Wanajeshi wa Amerika nchini Iraq walifikia hatua ya kuvaa vibinda kutokana na hofu ya kutoka ndani ya vifaru vyao kukabiliana na mahitaji yao, bila ya kutaja wale waliorudi kwa familia zao huku wakilalamikia maradhi mabaya ya msongo wa mawazo. 

3. Mgogoro wa kifedha wa kiulimwengu ulikuwa ni risasi ndani ya moyo wa Amerika (na ulimwengu). Mgogoro huu wa kifedha umeidhoofisha athari ya Amerika (ya moja kwa moja au isiyo kuwa ya moja kwa moja) kwa Waislamu na watawala wa Waislamu, na kupelekea pia udhaifu kwa watawala hawa kibinafsi na kwa huduma zao za usalama kwa watu wao. Hususan gharama kubwa za kijeshi inazotumia Amerika kwa kambi 737 za kijeshi za Kiamerika zilizoko ndani ya nchi 130 ikiongezewa na kambi 6000 zilizoko ndani ya Amerika, zinazo hitaji pesa nyingi mno, pamoja na gharama za vita vya kiulimwengu dhidi ya ugaidi, usaidizi kwa majeshi ya kigeni, kufadhili miradi mengine itokanayo na bajeti ya umma ya Kiamerika, na gharama za vita vya muda mrefu vya Iraq na Afghanistan.  

Walter Andrusyszyn, profesa wa biashara ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Florida Kusini, alisema "Deni kubwa la Amerika haliumizi tu uchumi wetu, linadhoofisha pia usalama wetu wa kitaifa na kuufanya ulimwengu kuwa mahali pa hatari zaidi. Hakuna taifa linaweza kudumisha au kudhihirisha nguvu yake ikiwa uchumi wake ni dhaifu. Hii ni kwa Sparta (Ugiriki ya kale), Roma, na Amerika."

Hivyo basi, idara iliyopo sasa ya Amerika imeamua kupunguza usaidizi wake wa kimaendeleo kwa asilimia 30, itakayo kuwa na athari mbaya kwa Amerika kwani misaada hii hukadiriwa kuwa moja ya nguzo tatu zinazo changia katika uwepo wa Amerika duniani, mbali na ulinzi na diplomasia. Zaidi ya hayo, hivi majuzi, Trump alizuru Saudi Arabia na kuchukua utajiri wa umma kwa njia isiyoeleweka.

Kutokana na yote hayo ya hapo juu, Amerika haina uwezo wa kushinikiza suluhisho la kisiasa kwa Mashariki ya Kati, iwe ni Syria au Afghanistan au kwengineko. Ni wazi kuwa, siasa ya kigeni ya Amerika leo inaporomoka. Kwa mfano, Trump alibadili maoni yake juu ya NATO kuwa ni muungano uliopitwa na wakati, kama alivyouita, na kisha kugeuza msimamo wake huu hadharani. Pia alijiondoa kutoka kwa makubaliano ya hali ya anga ya jijini Paris, na kisha kuitisha majadiliano mapya, alisimama katika ukingo wa vita na Korea Kaskazini, na kisha kurudi nyuma. Zaidi ya hayo, alikuwa na mtazamo mbaya juu ya China, na hatimaye kusimama nayo huku akisubiri matokeo ya faili yake nchini Korea Kaskazini, alitoa taarifa kali juu ya ardhi ya Syria, na kisha kuziachia mambo yake Astana na Geneva ambazo ni majirani zake.

Kwa haya na mengine mengi, yamemfanya Fukuyama kuzingatia upya fikra zake awali kuhusu Mwisho wa Historia. Zaidi ya hayo, haishangazi kumuona Raisi Obama akisoma kitabu kwa jina "Ulimwengu Baada ya Amerika".

Kwa mukhtasari, yote yaliyo tangulia juu yanathibitisha kuwa Amerika inazidi kudhoofika. Zbigniew Brzezinski amethibitisha haya alipo sema, "Amerika bado ni dola iliyo na nguvu zaidi kisiasa, kiuchumi na kijeshi duniani lakini, kutokana na mabadiliko makubwa katika mizani ya siasa za kimaeneo, sio tena serikali iliyo na nguvu za kipekee duniani." 

Kuanguka kwa Amerika kumesababisha kuibuka kwa mafahali wengi wa kimfumo baada ya kuwa fahali alikuwa ni mmoja tu akiwakilishwa na Amerika baada ya kuporomoka kwa Umoja wa Kisovieti. Lakini habari njema kwa umma ni kuwa hakuna yoyote kati ya mafahali hawa aliye na nguvu za kutosha kama inavyo fafanuliwa hapo chini.

4. Ama kuhusu Ulaya, Ulaya kuitwa "kikongwe" imethibitika leo. Udhaifu wao ukokatika kushindwa kwao kutenda kimataifa, kugongana kwao kimaslahi na kuwepo kwa sera tofauti tofauti zinazo pelekea kuwepo na migongano katika kadhia nyingi.

Kwa mfano, huku Ujerumani ikienda dhidi ya sera za Amerika, Ufaransa inajikaribisha kwa Amerika, ilhali Uingereza bado haina uhakika kuhusu kujiondoa katika Muungano wa Ulaya.

Bila ya kutaja udhaifu wa Ulaya kutokana na mgogoro wa kifedha wa kiulimwengu, uliouweka Muungano wa Ulaya katika hali mbaya sana.

Kwa upande mwengine, kupungua kwa viwango vya watoto wanao zaliwa pamoja na vijana imepelekea kurudi nyuma kwa wakaazi wa Ulaya kisiasa na kiuchumi na kuhatarisha muelekeo wa bara hili kimikakati.

5. Umoja wa Kisovieti, uliyo kuwa dola ya pili kinguvu ulimwenguni umeporomoka.

Ama kuhusu Urusi, haina tena nguvu kama zile ilizokuwa nazo Umoja wa Kisovieti. Hili ndilo linalo elezea sababu kwa nini Urusi inajiuza kwa thamani ndogo katika kuisaidia Amerika nchini Syria huku ikishindwa kuizuia Amerika kuingilia majirani zake kama Ukraine au kuiondolea vikwazo ilivyowekewa na Amerika.

6. Ama kuhusu China, ingawa imeibuka kuwa na nguvu kiuchumi na kuwa na jeshi lenye nguvu, hili peke yake halitoshi kuiwezesha kuipiku Amerika kuwa dola inayoongoza duniani. Licha ya hayo, kuinuka kwa China na kuongezeka kwa mvutano kati ya Amerika na China kwaweza kuwa na manufaa kwa umma na kuzaliwa kwa Khilafah.

Ama kuhusu kuamka kwa Ummah:

Allah (subhanahu wata’ala) asema:

أَوْ كَالَّذِي مَرَّ عَلَىٰ قَرْيَةٍ وَهِيَ خَاوِيَةٌ عَلَىٰ عُرُوشِهَا قَالَ أَنَّىٰ يُحْيِي هَـٰذِهِ اللَّهُ بَعْدَ مَوْتِهَا فَأَمَاتَهُ اللَّـهُ مِائَةَ عَامٍ ثُمَّ بَعَثَه

Au kama (mfano wa) yule aliye pita katika mji ulio kwisha kuwa magofu, akasema: Allah ataufufua vipi mji huu baada ya kufa kwake? Basi Allah akamfisha muda wa miaka mia.

[al-Baqara: 2: 259]

1. Kukita mizizi kwa Uislamu nyoyoni mwa Waislamu ni jambo lililo dhihirika licha ya majaribio makali kufanywa ili kuwaweka mbali Waislamu na Uislamu wao. Mifano yake inapatikana nchini Uzbekistan, Iraq, Tunisia na Syria ambako watawala wake wametawala kimabavu kuwaweka mbali Waislamu na Uislamu, lakini mbali na hayo wameshindwa katika majaribo yao.

2. Utekelezaji Uislamu kibinafsi ni jambo lililo enea leo, ambapo haikuwa hivyo miaka 70 na kitu iliyo pita. Kuswali, kusoma Qur'an, kutazama vituo vya runinga za kidini, na uvaaji hijab yote yanajitokeza leo duniani. Picha iliyo chapishwa na kituo cha Al-Jazeera ya barabara ya Misri iliyo pigwa katikati mwa karne iliyopita ikilinganishwa na picha ya barabara hiyo hiyo iliyo pigwa miaka michache iliyopita ni mfano mzuri wa kushikamana na Uislamu kibinafsi.

3. Fikra za ujamaa, ukomunisti na utaifa pamoja na al-Nasiriyah na fikra nyenginezo zimethibitika kuwa za kimakosa akilini mwa Waislamu. Na yeyote anaye endelea kuzibeba fikra hizi ni lazima sasa ajizibe kwa Uislamu ili akubalike. Mifano ya haya ni mapinduzi ya Iran, kufuga ndevu kwa mfalme Husain, kesi ya Erdogan, demokrasia kugeuzwa kuwa Shura na kampeni za uchaguzi katika biladi nyingi za ulimwengu wa Kiislamu nk.

Hata matukio nchini Algeria, Misri, Syria na biladi nyenginezo pia ni mifano mizuri ya Waislamu kutaka Uislamu pekee.

Mfano mwengine ni wa raia wa Libya aliyejeruhiwa (kwa sababu ya vita) katika hospitali za Jordan alipokataa kuisalimisha bendera ya Rayah (waliyo kabidhiwa na wanachama wa Hizb ut Tahrir wakati Hizb ilipowatembelea mahospitalini) kwa huduma za kijasusi za Jordan na kuwaambia kwamba Rayah hii ndio sisi (Walibya) tunayo pigana kwa ajili yake nchini Libya.

Zaidi ya hayo, tukiweka udadisi wa kisiasa kando kwa sasa, fikra ya kuweka amani na kidola cha kiyahudi ilitoweka wazi wazi wakati ulipo tokea moto mkubwa mnamo Novemba 2016. Hii yathibitisha kuwa kuweka amani na "Israel" ni wino tu katika karatasi lakini umma wangependa kuona kumalizika kwa kidola hiki.

4. Jihad kwa ajili ya Allah imekuwa ndio matakwa ya vijana wa Kiislamu baada ya kukanyagwa kwa Waislamu Palestina, Iraq, Afghanistan, Bosnia, Kashmir, Chechnya, Somalia, Libya na Syria. Vile vile, mama za mashuhadaa katika nchi zote hizi wamesimulia upya hadithi kubwa zinazo fanana na zile za wanawake wakongwe wa Kiislamu kama vile Al Khansa'. Na kadhia ya hivi majuzi ya milango ya Jerusalem (Al-Quds) ni mfano mzuri wa haya. Ni muhimu kuzingatia pia kuwa mashuhadaa hao walikuwa ni vijana na Waislamu wa "kawaida" ambao hawaonyeshi kushikamana na dini kwa mtazamo uliozoeleka na watu. Kwa hivyo, Waislamu wanapoa kutokana na maradhi aliyotuonya nayo Mtume (saw) alipo sema,

حُبُّ الدُّنْيَا وَكَرَاهِيَةُ الْمَوْتِ

Kupenda dunia na kuchukia mauti.

5. Huku tukizingatia kuwa nguvu za kijeshi za Amerika zimeharibiwa nchini Afghanistan na Iraq na kwamba nguvu za kijeshi za "Israel" ziliharibiwa mnamo 2006, Waislamu kwa jumla na haswa maafisa wa kijeshi wameanza kutambua kwamba wanaweza kuwashinda wamagharibi na washirika wao, awe ni Bashar au Iran au Urusi maadamu watamtegemea Allah (subhanahu wata’ala) peke yake.

6. Baadhi ya maafisa wa kijeshi na wanajeshi wa Kiislamu wamefanya vitendo murua kabisa kudhihirisha kheri iliyomo ndani yao. Nchini Misri, Sadat aliuwawa na Waislamu wenye imani. Nchini Jordan, mwanajeshi aliwapiga risasi na kuwaua watalii wa kiyahudi kwa sababu walikuwa wakimkejeli alipokuwa akiswali. Nchini Syria, huduma za kijasusi zilikuwa zikiwahoji maafisa wengi wa kijeshi kwa kutozijulisha kuwa walipokea simu kutoka kwa Hizb ut Tahrir mnamo 2005. Nchini Sudan, afisa wa jeshi wa ngazi ya juu aliangika bendera ya Rayah, aliyo kabidhiwa na ujumbe wa Hizb ut Tahrir, juu ya kambi yake ya kijeshi. Nchini Yemen, mmoja wa wanajeshi ilijipiga risasi mguuni mwake ili asiweze kushiriki katika mauaji ya raia wa Kiislamu, na kadhalika.

7. Wamagharibi walirudi kuja kuzikoloni biladi za Kiislamu kijeshi mnamo 2001 na 2003. Hili lenyewe ni ishara kuwa umma bado uko hai, na kama si hivyo ni kwa nini basi wamagharibi wapigane na taifa ambalo limekufa hususan ikiwa tayari wanatawala siasa, uchumi, vyombo vya habari na mitaala yetu ya elimu na kadhalika? Kwani wamagharibi watakuwa wanaogopa kitu gani? Wamagharibi wanaogopa kurudi kwa Khilafah. Ushahidi wa haya ni:

(a) Raisi Bush, mnamo Oktoba 11, 2006, alisema kuwa kuwepo kwa Amerika nchini Iraq kulikuwa ni kwa ajili ya kuzuia kusimama kwa Khilafah.

(b) Henry Kissinger, aliye kuwa Waziri wa Kigeni wa Amerika, aliandika Makala yaliyo chapishwa katika gazeti la 'International Herald Tribune Newspaper' mnamo 2 Aprili 2012, akifafanua kuwa sera ya Amerika kwa dini yetu imejengwa juu ya nguzo mbili: kudumisha (uporaji wa) mafuta na kuhifadhi "Israel". Lakini, akasema kwa sasa tunaongezea nguzo ya tatu nayo ni kuzuia kuibuka kwa dola yoyote katika eneo itakayo liunganisha eneo zima chini yake. 

(c) Lavrov, Waziri wa Kigeni wa Urusi, amesema kuwa kuporomoka kwa Assad itamaanisha kuibuka kwa serikali ya kisunni; bila shaka, hamaanishi serikali ya kisunni mfano wa Jordan na Saudi Arabia.

8. Mapinduzi ya Kiarabu yaliyofanyika katika baadhi ya sehemu za ulimwengu wa Waislamu yalikuwa na natija kadhaa nzuri:

(a) Yaliutia nishati Umma wa Kiislamu na kunyanyua hisia ya kujiamini kwake,

(b) Yalivunja kizingiti cha hofu,

(c) Yalidhihirisha umoja wa Umma huu,

(d) Yaliwatweza mashekhe-pesa pamoja na fikra ya kila mtu ajibadilishe kibinafsi,

(e) Yalimakinisha zaidi utambuzi kuwa tatizo la Umma liko katika viongozi (yaani ni vipi kivuli kitakuwa wima ikiwa kijiti hakiko wima),

(f) Yaliinua matakwa ya Waislamu kulingania Khilafah kama ilivyo kuwa nchini Yemen, kukusanyika mamilioni ya watu wakitaka sharia kama ilivyo kuwa nchini Misri, kupambana na viongozi wa kiilmani kama ilivyo kuwa nchini Tunisia, kupiga takbira "Allah Akbar" kama ilivyo kuwa nchini Libya, na kutoa kauli za "Peponi tutakwenda, tukiwa mamilioni ya mashuhadaa", "Ewe Allah hatuna mwengine isipokuwa Wewe", na "Tunamsujudia Allah peke yake" kama ilivyo kuwa nchini Syria.

(g) Mashekhe wengi nchini Misri, Saudi Arabia, Kuwait, Yemen, Jordan na nchi nyenginezo wakaanza kuhutubia kuhusu Khilafah Rashida ya pili.

Hivyo basi, uhalisia wa mapinduzi haya ya watu yaliobarikiwa ukajitokeza, licha ya kuwa vyombo vya habari vilijaribu kuuziba uhalisia huu. Na muamko wa Kiislamu unaendelea kukua.

9. Ripoti kadhaa zilitolewa na Wamagharibi zinazo onyesha uungaji mkono wa Waislamu kurudi tena kwa Khilafah, ripoti hizi ni kama:

(a) Ripoti iliyo tabiri kuwa kufikia mwaka wa 2020 Khilafah itakuwa imesimama tena.

(b) Kura ya maoni iliyo fanywa na shirika la Amerika la Gallup, zilizo onyesha kuwa idadi kubwa ya Wamisri wanaunga mkono kutawala kwa Sharia na kwamba thuluthi mbili ya Wamisri wanataka kuifanya Sharia iwe ndio chimbuko pekee la kanuni.

(c) Ripoti ya Maryland inaonyesha kuwa Waislamu nchini Pakistan, Indonesia, Morocco na Misri wanapendelea Sharia badala ya demokrasia.

Hii ndio maana Wamagharibi wakaitumia ISIS kama hatua ya mwisho kuwapotosha Waislamu kutokana na ulinganizi wa Khilafah. Lakini, kwa rehma za Allah (swt), siku baada ya siku, Khilafah ya ISIS imethibitika kuwa maneno matupu angani.

Ama kuhusu maendeleo ya Hizb ut Tahrir:

1. Kuna wabebaji da'wah wamakinifu wanaofanya kazi kwa hili. Na ulinganizi wowote, kujitokeza kwa uhakika wake, huwa ni suala la wakati tu maadamu wapo walinganizi wanao ufanyiakazi. Na Alhamdulillah da'wah ya Hizb ut Tahrir imeenea kutoka Australia upande wa mashariki mpaka Amerika upande wa magharibi. Zaidi ya hayo, Alhamdulillah, Hizb imeweza kuwaathiri wasomi, vyama, na watu wengi kiasi ya kuwa mamia ya kurasa hayatoshi kuwanakili.

Kuenea huku kukubwa kwa Hizb kumezighadhabisha nchi za kimagharibi, kufikia hatua ya, kwa mfano, kufanywa kongamano la siku mbili nchini Uturuki mnamo Septemba 2004 kwa anwani: "Changamoto ya Hizb ut Tahrir: Kuelewa na Kupambana na Mfumo Wenye Msimamo Mkali wa Kiislamu" lililodhaminiwa na kituo cha Kiamerika cha Nixon Center. Natija za kongamano hilo zilinakiliwa katika ripoti ya kurasa 157.

2. Hizb imefafanua fikra zote za Kiislamu zinazo husiana na Khilafah na ubebaji ulinganizi wake katika hali ambayo imewafanya Waislamu kurudisha imani yao kwa Uislamu, kufikia hatua kwamba Chama cha Kikomunisti katika Muungano wa Kisovieti kiliwaambia wafuasi wake nchini Palestina/Jordan kutofanya mazungumzo yoyote na Hizb kutoka na ufahamu wao mzito.

Hizb pia ilijitofautisha na vyama vyengine vya Kiislamu kupitia kutayarisha katiba kielelezo mpaka kufikia hatua kwamba mmoja wa viongozi wa chama cha 'Islamic Salvation Front' nchini Algeria wakati mmoja aliwahi kuulizwa: ikiwa mutapata mamlaka ya kutawala, je munayo katiba tayari kuitekeleza? Jibu lake lilikuwa, tunayo katiba ya ndugu zetu katika Hizb ut Tahrir. Kwa hivyo, Hizb iko tayari sana kwa Khilafah kiasi ya kuwa hata mitaala ya shule iko tayari.

3. Hizb imeshikamana barabara na fikra na njia yake, licha ya yale wanayo yapitia wanachama wake katika mateso ambayo wakati mwengine hupelekea mpaka kufikia daraja ya ushahidi, huku wanachama wa vyama vyengine wakiwa dhaifu mbele ya mmomonyoko wa kisiasa na kifikra au hata mbele ya fimbo na karoti. Zaidi ya hayo, fikra na njia ya Hizb zimethibitishwa kuwa sahihi wakati wa mapinduzi ya kiarabu, hususan kuhusiana na suala la kutafuta nusra kwa watu wenye nguvu, ambapo harakati nyengine ziliikejeli Hizb kwa hilo.

4. Hizb ilifaulu kuharibu uhusiano kati ya watawala na watu. Huku watu wengi wakiwatetea watawala hawa kama vile Arafat, Nasser, Saddam na wengineo, na huku baadhi ya harakati kubwa za Kiislamu zikikosa kuona madhara ya kuanzisha mahusiano ya kirafiki na watawala hawa, Hizb ilikuwa ikiwapiga vita watawala hawa kisiasa kufikia kiwango ambapo maraisi wa Uzbekistan na Pakistan, kwa mfano, walilalamika kuhusu Hizb ut Tahrir kwa Uingereza.

5. Hizb ilifanya makongamano kadhaa muhimu, kama kongamano la wasomi, la kiuchumi, la vyombo vya habari, na makongamano kadhaa ya wanawake, ambapo vyombo vya habari havikuwa na budi isipo kuyaangazia. Haya ni kuongezea maandamano ambayo Hizb ilifanya kabla ya harakati zote nyengine, yote yakidhihirisha historia ndefu ya Hizb, yakiwemo yale yaliyofanyika nchini Jordan kuunga mkono watu wa Syria na Libya na lile lililofanyika nchini Indonesia mnamo Machi 2017 ambapo watu milioni tatu walikusanyika dhidi ya gavana wa Jakarta aliye itusi Qur'an na Uislamu.

6. Hizb ut Tahrir imeomba na inazidi kuomba nusra kutoka kwa watu wenye nguvu walioko katika nchi kama Jordan, Syria, Misri, Iraq, Pakistan na kwengineko. Muitikio mzuri kwa Hizb kutoka kwa baadhi ya watu wenye nguvu unajulikana vyema na kutajwa wazi katika vyombo vya habari.                                                                                                                                 

Mwisho, matukio haya na hali hizi zinazotoa njia ya kuzaliwa kwa Khilafah hayapaswi kutufanya tuzubae na kusubiri, bali yanapasa kuwatia motisha, kuwashajiisha na kuwachangamsha wale ambao tayari wanafanya kazi au wale ambao wangependa kufanya kazi kusimamisha Khilafah Rashida ya pili. Hivi ndivyo walivyo kuwa maswahaba wa Mtume Muhammad (saw) wakizifanyia kazi bishara njema. Mtume (saw) alibashiri kufunguliwa kwa mji wa Kostantiniyya; maswahaba hawakusubiri tu kutimia kwa ahadi ya Mtume wa Allah pasi na kuifanyia kazi, bali walijaribu mara kadhaa ili kupata tunu ya kuufungua mji huu mpaka ulipoweza kufunguliwa na Mohammed Al Fateh (Mfunguzi).

Vile vile, Hizb ut Tahrir imeamua, kama walivyo fanya maswahaba wa Mtume (saw), kuendelea kufanya kazi na Ummah na kwa ajili ya Ummah, mpaka wakati ule ambao Allah ataamuru kusimama tena Khilafah katika njia ya Utume utakapo wadia.  

فَسَيُنْغِضُونَ إِلَيْكَ رُءُوسَهُمْ وَيَقُولُونَ مَتَىٰ هُوَ قُلْ عَسَىٰ أَن يَكُونَ قَرِيبًا

Watakutikisia vichwa vyao, na watasema: lini hayo? Sema: 'asaa yakawa karibuni! [Qur'an 17:51]

Imeandikwa na Ghassan Kaswani

Kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumapili, 26 Aprili 2020 11:01
Yaliyomo ndani ya kifungu hichi: Nidhamu ya Kuadhibu ya Kiislamu »

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu