Jumatatu, 21 Jumada al-thani 1446 | 2024/12/23
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Je, Inaweza Kusemwa Kuwa Zama za Ustawi wa Maendeleo ya Kisayansi Katika Ulimwengu wa Kiislamu ni Zao la Falsafa za Kigeni?

(Imetafsiriwa)

Waislamu lazima waibuke kutoka katika mporomoko. Hili angalau linakubalika kwa wote, waliberali na wanaharakati wa Kiislamu. Hata hivyo, tafauti inakuja katika fikra zinazopelekea katika uoni huu. Msukumo kwa msimamo wa waliberali ni maendeleo ya ajabu ya kisayansi na ya vitu ya Wamagharibi, ambayo yanaweka kipimo kwa waliberali.

Kwa kuwa Waislamu wako mbali sana katika mashindano haya, uoni wa kikundi kidogo lakini chenye kuathiri cha waliberali ni kuwa, lazima kwa Waislamu kuendelea katika nyanja za sayansi na teknolojia, kwa kuwafuata Wamagharibi. Inatiliwa nguvu na wao fikra ya kuwa hakuna dhara katika kufuata maadili na fikra za Wamagharibi, huku yakiachwa maadili ya Kiislamu.

Fikra za harakati za Kiislamu, zinazofanya kazi ya kubadilisha hali ya Ummah, ni tafauti na uoni wa kiliberali. Wanaamini kuwa Ummah wa Kiislamu ni wa mwisho ambao unafuata Wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu (swt), na Quran Tukufu ni Kitabu cha mwisho kutoka kwa Mwenyezi Mungu (swt), chenye kuongoza wanaadamu kwenye haki hadi Siku ya Kiyama. Wanatangaza kuwa Ummah wa Kiislamu ni mategemeo pekee kwa ustawi na ukombozi wa walimwengu. Hivyo Ummah wa Kiislamu lazima uongoze walimwengu, uing’arishe dunia, kwa Wahyi wa Mwenyezi Mungu (swt), kuondoa kiza cha ukafiri na dhulma, na kutoa afueni kwa walimwengu kupitia sheria za Mwenyezi Mungu (swt).

Kwa kweli, uongozi huu kwa walimwengu hauwezi kufikiwa huku tukijisalimisha kwa mfumo wa kirasilimali na kuchukua msimamo dhaifu dhidi ya mataifa makubwa ya dunia. Kwa hivyo, Ummah wa Kiislamu hivi leo lazima uwe na yote yenye kuleta uwezo na nguvu. Sayansi na teknolojia zina dori muhimu katika kujenga uwezo na nguvu. Hivyo, ni hitajio la muda kwa Waislamu kuzifuatilia.

Zama za teknolojia ya habari na mitandao ya kijamii imetoa fursa kwa watu wa dunia kutafiti zaidi kuhusu Uislamu na Waislamu, kinyume na taarifa zenye ukomo na upotoshaji, zinazotolewa na mitaala ya serikali. Taarifa nyingi zinasambaa katika mitandao ya kijamii katika kipindi cha miaka ya karibuni, juu ya maendeleo na vumbuzi za kushangaza za wanasayansi wa Kiislamu katika zama zilizopita. Nyoyo za Waislamu zinapata nguvu mpya kuhusiana na kuwa Waislamu walibaki kuwa na dola kiongozi kwa zaidi ya milenia moja, wakati wa zama za Khilafah yao.

Hii bila shaka, inazusha fikra katika nyoyo za Waislamu juu ya nini zilikuwa sababu za maendeleo na vumbuzi hizi muhimu. Je, ni kwa sababu ya Uislamu, au ilikuwa ni kwa sababu ya falsafa za Kigiriki, kama ilivyodaiwa na wataalamu wa mambo ya nchi za mashariki ambao waliathiri baadhi ya Waislamu? Je, maendeleo haya ni yao wenyewe, au yalitegemea wengine? Swali jengine hufuata, nalo ni kuwa kama dini pekee ndio msingi wa maendeleo, basi kwa nini Wamagharibi wameendelea baada ya kufungua pingu za dini? Kwa nini Waislamu hivi leo wamedorora zaidi na wapo chini kifikra hivi leo, licha ya kuwa wamejifunga zaidi na dini yao kuliko jamii za Kimagharibi? Je, hii ni kutokana na kujifunga Waislamu na Uislamu katika kushikilia jukumu muhimu la Uislamu katika ngazi zote za jamii kuwa ndio inayosababisha kuwa nyuma huku? Katika makala haya, tutapendekeza majibu kwa maswali hayo.

Zama za Uislamu kutokea Karne ya 9 hadi ya 13 inajulikana kuwa ni kipindi cha maendeleo ya teknolojia, sayansi na uvumbuzi wa Waislamu, japokuwa wanasayansi wengi, watafiti na wataalamu bingwa wameibuka baada yake. Ni jambo la ukweli kuwa mapinduzi ya kisayansi, yaliyotokea miongoni mwa Waislamu, yana mahusiano ya undani na Uislamu. Ilikuwa ni Uislamu pekee uliowapa Waislamu mnyanyuko wa kifikra, kuwafanya wawe wanafikra wabunifu. Hadhara iliyoibuka kutokea majangwa ya Arabuni imekuwa ni alama ya uvumbuzi na maendeleo kwa kiwango cha kilimwengu.

Kituo cha kilimwengu cha sayansi na sanaa kilitokea katika ulimwengu wa Kiislamu, huku Ulaya ikitangatanga katika giza la ujinga na ushirikina. Ama kwa mambo yaliyopelekea kwenye maendeleo haya ya kiajabu, katika fikra za Kiislamu yanapaswa kuchunguzwa:

1. Itikadi ya Kiislamu: Wakati Uislamu ulipoleta ujumbe wake wa kilimwengu, uabudiaji wa madhihirisho mbali mbali ya ulimwengu ulikuwa ni jambo la kawaida. Washirikina, Majusi, waabudu nyota na jua waliabudu viumbe tafauti vya ulimwengu. Uabudiaji huo ulikuwa ni jambo la heshima kuu. Hisia za ghariza ya kutukuza na heshima zilijitokeza kwa mwanaadamu wakati akiabudu. Inaweza kuwa hisia kama hizo zikashinda akili, na kupelekea kwenye msukumo, mihemko na shauku tafauti na ukweli.

Uislamu unatangaza kuwa ulimwengu wote ni viumbe. Dhihirisho la ulimwengu ni dalili ya uwepo wa Mwenyezi Mungu (swt). Sio wa kuchukuliwa kuwa ni vitu vya kupewa heshima kuu. Ulimwengu wote umefanywa uwe kwa ajili ya wanaadamu. Vitu vyake vya kushikika ni kwa manufaa ya wanaadamu. Mwenyezi Mungu (swt) amesema katika Quran Tukufu,

(وَسَخَّرَ لَكُمْ مَّا فِی السَّمٰوٰتِ وَ مَا فِی الْاَرْضِ جَمِیْعًا مِّنْه)  “Na amefanya vikutumikieni vilivyomo mbinguni na vilivyomo katika ardhi, vyote vimetoka kwake. Hakika katika hayo zimo ishara kwa watu wanao fikiri.” [45:13]

Hivyo, kinyume na dini nyengine, ugunduzi wa asili na hali ya vitu mbali mbali na kuvifanyia uchunguzi ilikuwa ni sawa kabisa kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu.

2. Hukmu za Uislamu kwenye Maisha na Sayansi: Uislamu umewapatia Waislamu njia sahihi ya kufikiri kuhusiana na dunia na masuala ya maisha. Imekuwa wazi kwa Waislamu kuwa lengo la Dini ni kutafsiri mahusiano ya mwanaadamu na Muumba na kuyaongoza masuala ya maisha. Kwa hiyo, utawala, siasa, jamii, masuala ya kiuchumi, uovu na adhabu ni mada zinazopaswa kubainishwa na Dini. Sio lengo la nususi za ki-Sharia kuweka maarifa ya kisayansi au nadharia zinazohusiana na vitu. Kutaja uumbaji mpana wa ulimwengu katika Quran Tukufu ni kuleta hisia za utukufu wa Muumbaji, ambaye ndiye pekee aliyeumba, kubuni na ni Mwenye Mamlaka makuu juu ya viumbe wote. Muelekeo wa Waislamu kwenye sayansi na sanaa unatafautiana na Wakristo. Wasomi wa Kikristo walizifanya taaluma za sayansi na nadharia kuwa ni sehemu ya masomo ya Biblia.

Hata hivyo, sayansi imetoa elimu yenye kikomo kuhusiana na sifa na tabia za vitu, ambapo huweza kutokea tafauti kila zama zinapobadilika. Hivyo nadharia za zamani ambazo Kanisa imeziweka kwenye dini, zilianza kuonekana sio sahihi kwa kupitiwa na muda, Kanisa liliwazuia watu kufuata fikra mpya za kisayansi. Ilifikia hata kutoa adhabu kali kwa wanasayansi kwa kuchukua hitimisho kinyume na mafundisho ya Biblia. Mfano mzuri ni ule wa Galileo Galilei. Kinyume chake, katika hadhara ya Kiislamu, wanasayansi walitukuzwa na Makhalifah wa Kiislamu kwa gunduzi na vumbuzi za kisayansi. Walisifiwa na kuzawadiwa, kwa vitabu vyao kupimwa kwa dhahabu, na kupewa ikiwa ni zawadi kwao.

3. Athari ya Fiqhi na Ijtihad ya Kisharia katika kutafiti masuala ya Kisayansi: Suala muhimu lililowasukuma Waislamu kuchunguza zaidi vitu vya kimada ilikuwa ni Fiqhi na njia ya Ijtihad. Waislamu walitafuta utatuzi wa masuala yao yote kutoka Quran Tukufu na Sunnah za Mtume. Uislamu umeonyesha kwa Waislamu njia maalum ya kuvua hukmu kutoka nususi za Kisharia kwa mambo yote ya maisha. Mbinu hii maalum haikuwa ikiegemea juu ya mantiki za Wagiriki, wala juu ya kubahatisha na dhana ziziso na mashiko.

Mchakato huu wa kufikia kwenye utatuzi uliegemea juu ya mazingatio ya ndani ya ukweli na uchambuzi juu ya kiwango cha mambo yanayohusiana nayo, ambayo huitwa ‘Tahqiiq al-Manaat’ (utambuzi wa uhalisia) katika istilahi ya Fiqh. Baada ya kufikia uoni wa ndani kuhusiana na uhalisia, Mujtahid huendelea kuangalia kwenye nususi za Kisharia kutafuta hukmu ya moja kwa moja kuhusiana na uhalisia na sio kuchukua njia ya mantiki ili kupata hukmu yoyote.  

Waislamu walijifunza kuwa mchakato wa Ijtihad hudhoofika pindi ufahamu wa wazi juu ya uhalisia usipofikiwa. Hivyo, uchunguzi wa ndani wa uhalisia, na tafakuri ya mambo yake madogo madogo, ikawa ndio tabia ya Waislamu. Tabia hii pia ikachukua jukumu muhimu katika kuchunguza dhihirisho pana la ulimwengu na kufikia hitimisho juu yake.

4. Uwazi wa Waislamu juu ya Kile Kinachopaswa na Kisichopaswa Kuchukuliwa kutoka Mataifa ya Kigeni: Baada ya maendeleo ya Wamagharibi na kuanguka kwa Waislamu, swali lililowakabili Waislamu ni juu ya nini tunachoweza kukichukua kutoka kwa Wamagharibi na nini tusichokiweza. Wakati hadhara ya Magharibi ilipoibuka kwenye ramani ya dunia ikiwa na maendeleo yake ya ki-mada, kukapatikana miongoni mwa Waislamu waliopumbazwa na hadhara ya Kimagharibi. Wakajadili kwa namna ya kuwapendelea Wamagharibi katika mambo yote ya maisha. Wachache miongoni mwa Maulamaa walihalalisha demokrasia ya Wamagharibi, japokuwa demokrasia ipo juu ya msingi wa ubwana kwa mwanaadamu. Walitoa hoja za kuchukua fikra za Kimagharibi, nidhamu na thaqafa zao. Kwa upande mwengine, kulipatikana wale waliopinga kila kitu kutoka kwa Wamagharibi. Walidiriki hata kutoa fatwa dhidi ya kuchapishwa Quran. Wakati mwanaadamu alipoingia kwenye anga, waliitangaza kuwa ni ushari na ufidhuli dhidi ya dini.       

Jamii za Waislamu ziligeukia katika mawanda ya mjadala na mabishano baina ya mapote mawili, kukiwa na baadhi ya Waislamu waliobaki kimya wakiwa katika mshangao. Kinyume chake, kwa Waislamu wa zama za mwanzo, ilikuwa wazi kwao juu ya kile kinachopaswa kuchukuliwa kutoka mataifa mengine na kile kisichopaswa. Hivyo, hawakuchukua kabisa kinachotokana na itikadi na sheria za mataifa mengine. Wakati Waislamu walipoyakomboa maeneo ya makafiri, hawakufasiri sheria na nidhamu za hadhara yao kwa Kiarabu. Waislamu, wakati huo, walitambua kuwa hukmu na nidhamu huweza kuchukuliwa tu kutokana na muongozo wa Wahyi. Kwa hivyo Waislamu walichambua kwa kuhakiki, kwa uoni wa Uislamu, utaratibu wa uongozi, elimu ya sayansi na sanaa za mataifa mengine. Walizitafsiri kwa Kiarabu na kunufaika nazo bila kusita.

5. Ufahamu wa Wazi wa Lengo la Maisha na Uwepo wa Makusudio ya Juu Zaidi: Waislamu walijifunza kutoka kwa Mtume (saw) jukumu lao wakiwa ni Ummah. Waislamu walifahamu ukweli wa kuwa wao ni Ummah bora, ulioletwa kwa watu kuwaangazia walimwengu kwa nuru ya Uislamu. Wakati taifa lolote likiwa na imani katika itikadi, ambayo inasimamisha lengo lake, basi taifa hilo halitosita kufikia kwenye lengo lake, huku likiongeza uwezo wake kukabiliana na vizuizi. Waislamu walijua kwamba njia ya ulinganizi kwenye Uislamu ni kwa kupitia Da’wah na Jihad. Da’wah ilitayarisha mazingira miongoni mwa mataifa hadi kizuizi pekee kikawa ni tabaka tawala na utawala wao. Nguvu inaondoshwa kwa nguvu, kupitia Jihad, na Uislamu unatekelezwa juu ya Makafiri. Hatimaye, wanashuhudia ukamilifu wa Uislamu katika kusimamia masuala ya maisha. Wanautambua Uislamu kuwa ni Dini inayolingana na maumbile ya mwanaadamu, ikiwashawishi kuwa Waislamu.

Hivyo, Waislamu waliendeleza yote hayo yaliyolazimu kuendesha Jihad kwa namna ya kuleta matarajio ya kufaa. Walikuwa mbele katika sanaa ya mishale na kufikia viwango vya juu. Chini ya Khilafah, mishale ya chuma cha Damascus ilikuwa yenye kuhitajika duniani kote. Ikiwa ni yenye ncha kali na imara lakini pia yenye kupindika, hivyo haikuvunjika katika mapambano. Waislamu walifanya uvumbuzi katika kutengeneza upinde, kiasi cha kuweza kulenga mshale kufikia futi 1500. Kabla ya ugunduzi wa baruti, ilikuwa ndio silaha kubwa zaidi duniani.

Kwa kutumia teknolojia, Waislamu waliunda mtambo wa kutupia mawe katika vita ulioweza kurusha mawe ya uzito wa pauni 500 kwenda hadi masafa ya futi 1000, ambapo kabla ya hapo umbali huu ulikuwa si zaidi ya futi 150. Vilevile, Waislamu walivumbua manuari kuwazidi nguvu Warumi, walivumbua mbinu mpya ya kuunda baruti, walipangilia mzinga kuivunja ngome imara ya Konstantinopoli na kuendeleza uundaji wa makombora. Sultani Tipu alifanya maendeleo makubwa katika teknolojia ya makombora na kuyatumia dhidi ya jeshi la Uingereza katika vita vya Mysore. Wakati huo, Uingereza walishindwa katika majaribio ya kutengeneza makombora yao. Baada ya kushindwa kwa Sultan Tipu, Uingereza waliyachukua makombora hadi Uingereza ambapo William Congreve, aliyaunda upya na kuwa makombora ya Congreve kupitia uhandisi wa ugeuzaji.

Matumizi ya teknolojia katika vita ilikuwa ni kulingana na mafunzo ya Mtume (saw). Wakati Mtume (saw) alipoizingira Taif, na watu wa Taif wamejiwekea ngome, Waislamu walihitaji zana aina ya vifaru na mtambo wa kurusha silaha. Hii ni aina ya teknolojia ya Warumi ambayo Waarabu hawakuwa nayo. Hata hivyo Jihad iliwahamasisha kujifunza matumizi yake. Waislamu waliiunda, kwa kutekeleza maagizo ya Mtume (saw) kutokana na ushauri wa Salman Farsi (ra). Hivyo, msingi wa kuendeleza teknolojia ya kivita iliwekwa na Mtume (saw).

6. Katazo la Kuchukua Mafunzo ya Wazee Waliopita bila Uchunguzi:

Ufuataji wa kibubusa wa wazee, au imani inayoegemea dhana, ni kizuizi kuelekea maendeleo katika elimu na uvumbuzi wa kiteknolojia. Tokea kuwepo kwake, Uislamu ulipiga vita imani za uongo ambazo Maqureshi walizichukua kupitia uigaji wa wazee wao waliopita. Kwa hiyo Uislamu ulifanya ni jambo la lazima kuifanya imani itegemee juu ya dalili isiyo na shaka. Waislamu waliacha kutegemea taarifa bila uchunguzi, uhakikisho na usahihi. Mafunzo hayo ya Waislamu yaliwasaidia Waislamu kwa kiasi kikubwa kwenye nyanja za sayansi na teknolojia. Hivyo, Waislamu walikuwa na hadhari katika kufasiri vitabu vya Kigiriki, Warumi au Wafursi, kuhusiana na hekima ya waliopita miongoni mwao.

7. Hitajio la Hukmu za Kiislamu Kuhusiana na Hesabu: Kuna hukmu za wazi za mirathi katika Uislamu, ambapo Quran Tukufu imeweka wazi mafungu mbali mbali ya warithi. Mtume (saw) amewashajiisha Waislamu juu ya kujifunza sheria za mirathi. Mtume (saw) amesema,

«تَعَلَّمُوا الْفَرَائِضَ وَعَلِّمُوهُ النَّاسَ فَإِنِّي امْرُؤٌ مَقْبُوضٌ، وَإِنَّ الْعِلْمَ سَيُقْبَضُ حَتَّى يَخْتَلِفَ الِاثْنَانِ فِي الْفَرِيضَةِ فَلَا يَجِدَانِ أَحَدًا يَفْصِلُ بَيْنَهُمَا»

“Jifunzeni elimu ya mirathi na wafunzeni watu kwani mimi nitaondoka karibuni. Kwani elimu hii itaondoka hadi kufikia watu wawili kuhitalifiana kuhusiana na urithi na wasimpate yeyote wa kuwapatia ufafanuzi” (Al-Mustadrak). Ili iwezekane kugawanya mali ya mirathi kwa mujibu wa hukmu za mirathi, ni lazima kusomwa somo la hesabu. Hivyo, Waislamu walijifunza hesabu na ilisomeshwa mashuleni. Wakati Khwarizmi alipovumbua algebra, pia ilitumika kukokotoa hesabu za mirathi.

8. Maamrisho ya Uislamu Yahusuyo Mahitaji ya Elimu ya Falaki: Katika Uislamu, hukmu za Swalah zimehusishwa na mwendo wa jua, wakati Ramadhan, Hajj na Idd zinahusiana na mzunguko wa mwezi. Hivyo hivyo, maarifa ya usahihi wa muelekeo wa Qibla ni jambo lenye umuhimu mkubwa katika kutekeleza Swalah. Kwa kipindi cha mwaka mzima, nyakati sahihi za Swalah huweza tu kujulikana pindi ufahamu sahihi juu ya mzunguko wa jua unapofahamika. Pia, maarifa ya hatua mbali mbali za mzunguko wa mwezi ni jambo msingi la utekelezaji wa kivitendo wa kalenda ya Kiislamu, pamoja na kusaidia kutambua kwa usahihi siku muhimu za ibadah kama Swaum na Hajj

Maendeleo katika elimu ya falaki iliwasaidia Waislamu katika kukamilisha majukumu yao. Waislamu walisahihisha sehemu kubwa ya uelewa mbaya juu ya elimu ya falaki. Waliweka mpangilio mpya wa falaki, kutambua vituo vya nyota angani, hatua za mwezi, kupatwa kwa jua na mwezi, nyakati za miongo, longitudo na latitudo, mawio na machweo ya jua, vituo vya sayari vya kila siku na vya mwezi na makisio ya kuanza kwa miezi katika kalenda ya Kiislamu.

9. Maamrisho ya Uislamu Yahusuyo Vumbuzi za Kitabibu:

Japokuwa Uislamu umeweka wazi kuwa suala la ugonjwa ni mtihani kama mitihani mengine, kuwa pia ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu (swt), Uislamu umeonya Waislamu dhidi ya kujiua na amewashajiisha kuhakikisha sababu kwa ajili ya tiba na kinga. Mtume (saw) amewaonyesha Waislamu kwa uwazi juu ya kutafuta tiba, na kuwa kitendo hiki ni jambo la kupata thawabu. Mtume (saw) amesema,

«تَدَاوَوْا فَإِنَّ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ لَمْ يَضَعْ دَاءً إِلاَّ وَضَعَ لَهُ دَوَاءً غَيْرَ دَاءٍ وَاحِدٍ الْهَرَمُ»

“Jitibuni kwani Mwenyezi Mungu (swt) hakuweka maradhi ambayo hayana dawa isipokuwa (maradhi ya) uzee” (Abu Dawuud). Pia, Mtume (saw) amesema,

«إِنَّ الله لم ينزل داء إلّا أنزل شِفَاءً، عَلِمَهُ مَنْ عَلِمَهُ وَجَهِلَهُ مَنْ جَهِلَهُ» “Mwenyezi Mungu (swt) hakuleta maradhi ila ameleta ponyo. Anaielewa yule mwenye kuielewa, na haielewi yule asiyeielewa”. (An-Nasai, Ibn Majah, Hakim na Ibn Hibban). Ndipo Waislamu wakavumbua maelfu ya dawa za miti shamba na madini kwa ajili ya tiba wakati wa zama za Khilafah. Hospitali zilijengwa katika miji ya Baghdad, Cairo, Qairawan na miji mingine, ambapo wagonjwa wakilazwa na kutibiwa. Vitabu kadhaa viliandikwa kuhusiana na tiba, miongoni mwao ni kitabu mashuhuri “Al-Tasriif” cha Abu-Al-Qasim Khalaf ibn al-Abbas Zahrawi, ambacho kinahusisha sehemu juu ya upasuaji, kilichotumika kusomeshea upasuaji katika miji ya Ulaya, kwa kipindi cha miaka takriban mia tano.

10. Fikra ya Wema: Mtume (saw) amesema,

«إِنَّ اللَّهَ كَتَبَ الْإِحْسَانَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ فَإِذَا قَتَلْتُمْ فَأَحْسِنُوا الْقِتْلَةَ وَإِذَا ذَبَحْتُمْ فَأَحْسِنُوا الذَّبْحَ»

“Mwenyezi Mungu ameandika ihsan juu ya kila kitu, basi mnapopigana (jihad) fanyeni uzuri kuuwa kwenu, na mnapochinja fanyeni uzuri kuchinja kwenu” (Muslim). Ni kutokana na mafundisho ya Uislamu kuwa mambo yanashughulikiwa kwa ufanisi, na kuwa kila juhudi hutumika kuyafikisha katika ukamilifu. Tunaweza kuona hili katika masuala mbali mbali ya sayansi na teknolojia wakati wa zama za Khilafah. Katika kila nyanja ambayo Waislamu wanaingia, wanaifanya kwa uzuri mno, ima iwe ni taaluma za kivita, sheria, lugha, utawala, ufanisi wa kiuchumi, uzalishaji wa kilimo, usanifu majengo, fasihi, ubunifu na sanaa ya uandishi, Waislamu walikuwa mbele ya mataifa mengine ya wakati huo. Katika utabibu, falaki, kemia, uhandisi, fizikia na jografia, hawakuwa na wapinzani, waliwatangulia kwa miongo kama sio karne kadhaa. 

11. Nafasi ya Uislamu katika Uhandisi na Ujenzi: Hivi leo, katika zama za urasilimali, katika majengo yao na uundaji wapo mbele yetu, kama katika maduka makubwa, vivutio vya utalii, hoteli za anasa, viwanja vya mipira na majumba ya maonyesho. Ni alama za sifa za hadhara ya ki-mada. Wakati katika zama za hadhara ya Kiislamu, majengo maarufu yalikuwa ni misikiti adhimu, ngome na majengo kwa ajili ya vistawishi vya ummah. Yote haya yanaungana na utekelezaji wa maagizo ya Uislamu. Misikiti ilikuwa ni sehemu za ibada kwa Waislamu. Ngome ni mahitaji ya Jihad. Bafu, masoko, hospitali, shule, vyuo vikuu, maktaba, nyumba za mapumziko, vistawishi vya umma, maeneo ya malisho na bustani ni maeneo ambayo mtawala analazimika kuyaweka. Mabaki ya ujenzi namna huo yanaonekana katika Bara Hindi hadi hivi leo. Hali hii ya sanaa ya ujenzi inaakisi uzoefu wa Waislamu katika nyanja tafauti za usanifu majengo na uhandisi wakati huo. Kwa wakati huo, miji ya Waislamu ilikuwa yenye ustawi zaidi duniani. Waislamu walijizatiti juu ya kujenga majengo, kuyabuni na kuyaendeleza kwa kutumia maarifa ya hesabati na kemia, na kujenga majengo ya kifahari.

12. Ulezi wa Dola katika Elimu: Dola ya Kiislamu sio kama dola ya Mongolia iliyokuwa dhidi ya sayansi na sanaa, iliyokuwa ikitupa rasilimali adhimu ya elimu, ikitumbukiza mtoni vitabu na thaqafa. Himaya kubwa zaidi duniani ya wakati wake, iliyo na eneo kubwa, ilipotea kutoka uso wa dunia bila kuwacha urithi wowote katika elimu au sanaa. Makhalifah wa dola ya Kiislamu wenyewe walikuwa wanachuoni na wasomi. Waliwakusanya pamoja nao wataalamu wa sayansi na sanaa. Khalifah al-Ma’mun alikuwa na shauku ya elimu kiasi cha kufanya mkataba na Warumi akiweka masharti ya kusoma na kufasiri vitabu ndani ya maktaba zao. Khilafah iliweka Bait ul-Hikmah, “Nyumba ya Elimu” jijini Baghdad, kwa gharama ya Dinari 200,000. Ilijumuisha maktaba, sehemu ya uchunguzi wa sayari, eneo la makaazi ya wanasayansi, zana za kisayansi na kituo cha kufasiri. Watu kutoka dini zote, kabila au rangi waliruhusiwa kusoma na kufanya tafiti humo. Vikao vya kitaaluma vilifanyika kila wiki katika Bayt ul-Hikmah. Mifano mengine kadhaa ya watawala wa Kiislamu inaweza kuonekana katika vitabu vya kihistoria kuonyesha ulezi wao katika elimu.

13. Kuyakusanya maeneo mapana chini ya Dola Moja: Mipaka ya dola ya Kiislamu ilienea kutoka China hadi Morocco, iliyojumuisha India, Fursi, Asia ya Kati, maeneo ya Arabuni na tawala za Roma. Yote haya yalikuwa na hadhara iliyotafautiana kabisa. Uunganishaji wa maeneo haya yalio na hadhara tafauti, kuwa chini ya dola moja, uliwezesha kuisafirisha sayansi na sanaa kutoka eneo moja hadi jengine kwa haraka. Uliweza kukuza mazingira ya kitaaluma katika maeneo ya Waislamu.

Waislamu si tu waliunganisha maeneo yote haya kuwa moja, bali pia waliifanya lugha yao moja yenye nguvu, ya Kiarabu. Kila wanapofungua eneo lolote, waliwafundisha Waislamu wapya lugha ya Kiarabu, pamoja na mafundisho ya Quran na Sunnah za Mtume (saw). Lugha rasmi ya dola pia ilikuwa ni Kiarabu. Hivyo Kiarabu, ambacho kikizungumzwa katika Bara Arabu pekee kabla ya Uislamu, hivi sasa kinazungumzwa na kufahamika kutoka Afrika hadi Ukanda wa Gaza ndani ya nchi 22. Katika eneo hili kubwa, lililopo katika muungano wa mabara matatu, utumiaji wa lugha moja umerahisisha usambazaji wa maarifa kutoka eneo moja hadi jengine. Ilijenga silsila na mawasiliano miongoni mwa watu wa maeneo tafauti kuwa rahisi na ya haraka. Hivyo, watu wa maeneo mengine waliweza kupata maarifa kutoka vitabu vya msomi au mwanasayansi Muislamu, kukuza maendeleo yao.

14. Kuamsha Fikra za Waislamu kutokana na changamoto za fikra na itikadi za waliotangulia: Wakati Waislamu walipoyakomboa maeneo ya Roma, falsafa za Wagiriki zilikuwa zimeenea. Badala ya hoja za kiakili, uchunguzi na majaribio, falsafa za Wagiriki ziliegemea dhana na kubahatisha pekee. Pia, wanafalsafa wachache wa Kigiriki waliamini kuwa maji ndio kiini cha ulimwengu, huku wengine wakiamini kuwa ulimwengu uliundwa kwa vitu vinne: maji, ardhi, upepo na moto. Hii iko kinyume na njia ya kufikiri ya Uislamu, inayosisitiza uchunguzi wa uhalisia, kusimamisha ushahidi kwa ajili ya hitimisho.

Kwa kuwa Uislamu umefundisha kwa Waislamu kuwa dai lolote lazima liwe na ushahidi, Waislamu wameichukua aqida kuwa ndio egemeo la dalili, kama walivyochukua hukmu za Shariah kuwa egemeo la dalili. Kufuata dhana, bila kuwa na uhusiano na uhalisia, haikubaliki kwa Waislamu. Katika sayansi na teknolojia vilevile, Waislamu wamechukua njia ya kufikiri ya msingi wa dalili. Kwa hivyo wanasayansi kama Jabir bin Hayan na Zahrawi wameweka wazi dhihirisho la vitu pamoja na uchunguzi na majaribio. Hata hivyo, Waislamu hawakuchukulia kuwa kila elimu lazima ipatikane kutoka kwenye uchunguzi. Hawakuzingatia kuwa hakuna haja ya elimu iliyotangulia. Bali, walizigawanya elimu kwa msingi wa kuwa baadhi hupatikana kutokana na uchunguzi, na nyengine zilisisitiza uongozi unaotokana na Wahyi.

Kupitia imani ya Dini hii ya mwisho, Waislamu waliona kuwa hadhara yao  ni ya juu zaidi ya hadhara nyengine zote. Thaqafa hii iliyo ya juu zaidi imekuza fikra miongoni mwa Waislamu kuzichunguza na kuzichambua falsafa nyengine na nadharia za kisayansi, kuzifanyia majaribio kwa ukaribu kabla ya kuhitimisha chochote kutoka humo. Hivyo tafiti za Waislamu zilifichua kasoro za falsafa na njia za kufikiri za mataifa mengine. Hata vitabu vya tafiti vilivyokuwa katika maeneo ya Waislamu vilikuwa chanzo cha elimu kwa wanafunzi wa falsafa za zamani.

Baada ya kufisidiwa na fikra za Kigiriki na hoja za kimantiki, wanafalsafa wachache Waislamu walifikia hitimisho la kupingana moja kwa moja na fikra zisizo na shaka za Uislamu. Hata hivyo, msimamo wao wa makosa ulipingwa na Ulamaa walioegemeza fikra zao juu ya aqida ya Kiislamu. Hivyo, uongozi wa itikadi ya Kiislamu ulibainisha ubatili wa fikra za Kigiriki kwa Waislamu. Waislamu walichambua njia ya kufikiri ya Wagiriki na kuonyesha makosa yake.

Maelezo ya Jumla ya Nukta Kumi na Nne Zilizotajwa: Uchunguzi umethibitisha kuwa kuibuka kwa hadhara ya Waislamu na maendeleo ya kisayansi ya Waislamu yalikuwa ni kwa sababu ya Uislamu pekee. Kulikuwa na vipengele kadhaa vya fikra ya Kiislamu, vilivyo waruhusu Mabedui wa Arabuni kutawala dunia, na kuwaweka kuwa viongozi wa dunia katika sayansi na sanaa. Kama Uislamu usingekuwepo, dunia ingenyimwa athari chanya za hadhara hii kubwa iliyoanzia Mashariki ya Kati. Mwangaza wenye kun’gaa wa Uislamu ulioangaza dunia yote kwa karne kadhaa, katika sheria, siasa, sanaa na sayansi.

Kwa vipi wanageuzwa wale wanaokataa dori ya Uislamu katika mripuko wa maendeleo miongoni mwa Waislamu. Wanachukua tu msimamo uliopinda kwa sababu ya chuki yao kwa Uislamu, wakiweka madai yasiyo na msingi kuyaunganisha maendeleo ya Waislamu kwa falsafa za Kigiriki na za Warumi. Wachache wao wamefikia hadi kudai kuwa hakukuwa na muibuko wa hadhara ya Uislamu mwanzoni. Fikra za hawa watu wa kisasa zimekosa uhalali wa kuukosoa Uislamu, ambao uliendelea kutabikishwa wakati wa Masahaba Watukufu (ra), Tabiina, Tabii Tabiina na Khilafah za zama za baadaye. Wao wameshikilia msimamo wao kuwa Waislamu lazima waachane na Uislamu na wafuate Wamagharibi ili waendelee. Sasa tugeukie kwenye baadhi ya mada zinazohusiana.

Kama Uislamu ulikuwa ndio Sababu ya maendeleo ya Kisayansi ya Waislamu, basi nini sababu ya maendeleo ya sasa katika nchi za Magharibi? Maendeleo jumla katika sayansi na teknolojia hayawezi kupatikana kwa kufungua taasisi chache tu za kisayansi. Hupatikana kwa kuwepo kwa hamasa na msukumo kwa ajili yake katika taifa zima. Taifa lolote linaweza tu kuhamasika katika kila nyanja ya maisha, wakati likichukua mtazamo mpana kuhusu masuala ya maisha. Mtazamo huu unaochukuliwa unaamua taswira ya taifa. Hivyo lengo la maisha huwa wazi kwa taifa hilo na huweka malengo, kwa mtazamo wa taswira zilizowekwa.

Pamoja na hayo, masuala ya taifa yanaongozwa juu ya msingi wa fikra hiyo pana inayofuatwa. Hivyo taifa linakakamaa kufikia malengo iliyojiwekea, yaliyotokana na itikadi yake. Maendeleo katika kila nyanja ya maisha ikiwemo sayansi na teknolojia hayaepukiki, ni matokeo ya kimaumbile. Kwa maana nyengine, hizi ni taswira za itikadi tu. Zinaipindua jamii yote. Ndipo jamii huenda kuelekea njia ya mwamko, huku ikiacha nyuma mporomoko.

Hivyo, mabadiliko ya kifikra na kisiasa yanatokea mwanzo, yakifuatiwa na maendeleo katika mawanda ya sayansi na teknolojia, yakiwa ni matunda ya mabadiliko hayo. Maendeleo ya Wamagharibi katika sayansi na teknolojia yapo kwa namna hiyo hiyo. Itikadi ya kiliberali ya kirasilimali ya Wamagharibi imezitia nguvu jamii za Kimagharibi kifikra. Jamii yote ikawa yenye harara, kutokana na mtazamo wa fikra ya maslahi, inayotokana na itikadi hii. Katika wakati huo huo, kutokana na matokeo ya vita vya msalaba, elimu ya sayansi ya Uislamu ilifikia Ulaya kupitia Uhispania. Hivyo, Ulaya ilichukua fursa ya maarifa haya makubwa kutoka kwa Waislamu. Ilinakili kwa usahihi vitu vingi kutoka kwa Waislamu. Vumbuzi nyingi za Waislamu walizidai kuwa ni zao. Wakazichukua, juu ya msingi wa fikra yao.

Kutokana na sura halisi ya uchoyo katika itikadi ya kirasilimali, mashindano ya kuvumbua yalianza na kuvipa vitu hati miliki. Watu wengi walitumia vumbuzi hizi kuwa ni njia ya kuongeza utajiri wao. Mataifa ya Magharibi yalitoa msaada, kwa kuwa mataifa haya yaliamini katika falsafa ya kirasilimali kuwa mashindano huleta utajiri. Pia waliamini katika kukuza anasa kunaongeza utajiri wa pamoja wa taifa, huleta ustawi wa kiuchumi kwa mataifa. Pamoja na hayo, dola za Kimagharibi zililenga kwenye sayansi na teknolojia kujikuza kijeshi. Juu ya msingi wa nguvu za kijeshi, walitawala dunia iliyobaki, na kupora utajiri wao.

Yote haya yalipelekea mapinduzi ya sayansi na teknolojia ya Ulaya. Ilikuwa hasa ni matokeo ya kuichukua fikra ya kirasilimali kuwa ni nembo ya maisha. Mapinduzi ya Wamagharibi pia hayakuwa juu ya msingi wa fikra au falsafa ya Wagiriki. Haya yalishuhudiwa katika nchi zao kwa karne nyingi, bila kusababisha mabadiliko yoyote. Kwa kweli, kama nchi za Magharibi zingechukua fikra na falsafa za Kigiriki, zisingeweza kuendelea.

Kwa hivyo, msingi muhimu unaohitajika kufahamika ni kuwa, wakati taifa lolote linapoichukua itikadi yake kuwa ni nembo ya taifa, hupelekea maendeleo kwenye kila nyanja ya maisha. Urusi iliendelea, ikiwa ni matokeo ya utekelezaji wa fikra ya kikomunisti. Nchi za Magharibi zimeendelea ikiwa ni matokeo ya fikra ya Kirasilimali. Dola ya Kiislamu ya Madinah iliendelea ikiwa ni matokeo ya fikra ya Kiislamu. Ziliendelea licha ya ukweli kuwa Ukomunisti na Urasilimali ni itikadi za batili kwa sababu ya ufahamu wake potofu unaotokana na akili finyu ya mwanaadamu, isiyoweza kutatua matatizo ya mwanaadamu katika namna bora. Utabikishaji wa mifumo hii, licha ya upotofu wake, ilileta manufaa ya vitu kwa taifa.

Mapinduzi ya Kisiasa au Mapinduzi ya Kisayansi: Mjadala unaoendelea umebakia miongoni mwa wanataaluma wa Kiislamu kuhusiana na mabadiliko, ima yaanzie chini kwenda juu au juu kwenda chini. Kwa hiyo kuna wanaosema kuwa maendeleo ya vitu hupatikana kwa elimu, sayansi na teknolojia ili kujiimarisha sisi wenyewe na kisha kuijenga dola kisiasa, na wengine wanasema kuwa mwanzo lazima kuwepo na mageuzi ya mapinduzi ya kisiasa, katika kiwango cha dola juu ya msingi wa Uislamu ili kuruhusu maendeleo katika nyanja zote, ikiwemo sayansi na teknolojia. Mtu yeyote anayejua juu ya mahusiano baina ya itikadi, mifumo na mabadiliko, huku akijua nguvu za Uislamu, atajua kwamba bila mabadiliko msingi yaliyojengwa juu ya Uislamu pekee, Waislamu hawataweza kuhuika na kuendelea katika njia inayoweza kumridhisha Mola wao (swt).

Kutokana na uoni halisi, maendeleo ya kisayansi na teknolojia hayatawezekana bila ya uwekezaji mkubwa. Yanahitaji uchumi imara na thabiti usiotegemea taasisi wala serikali yoyote. Hii inalazimisha kuwepo mfumo wa serikali inayotoa uthabiti wa ndani na nje.

Hivyo, maendeleo hayo hayawezekani bila uhuru wa kisiasa. Ukweli ni kuwa dola za kikoloni zinawaweka Waislamu nyuma kupitia watawala wa Ulimwengu wa Kiislamu. Wanawanyima maendeleo halisi katika nyanja za sayansi na teknolojia. Muendelezo wa kupoteza wataalamu kuelekea nchi za Magharibi unaonekana, kutokana na kukosekana uthabiti katika Pakistan (na nchi nyengine), lakini watawala hawa wasio na uoni hawahisi ukubwa wa hasara hii, wakilenga tu juu ya dolari zinazoingia nchini kutoka nje.

Je, Maendeleo ya Kisayansi ni Kigezo cha Mafanikio ya Nchi? Japokuwa uvumbuzi wa kisayansi ni muhimu, lakini huo sio kigezo cha ubora wa nchi. Kwa kuzingatia maendeleo ya kisayansi kuwa ni kipimo cha ubora, kwa kweli hiyo ni matokeo ya kuathiriwa na Wamagharibi. Baadhi hata hufikiria kuwa njia za kisayansi ni kigezo pekee cha fikra, na uendeleaji wa kisayansi ni dhihirisho la kukua kwa mwanadamu. Hata hivyo, ustawi bora ni ule ulio bora katika kusimamia mambo ya watu kwa ufanisi katika kuongoza mahusiano ya watu.

Licha ya kuwa wamekwenda mbele zaidi katika uvumbuzi wa kisayansi, Wamagharibi wanateseka na pengo linalokuwa baina ya matajiri na masikini, umiliki wa tabaka la warasilimali juu ya utawala, kuvunjika kwa maadili ya familia, kukithiri kwa ngono za aibu na kukosekana kwa furaha ya akili. Yote yanafichua kuwa maendeleo katika sayansi na teknolojia pekee sio hakikisho la utulivu na furaha. Hii licha ya kuwa vumbuzi za kisayansi zinawepesisha masuala ya kidunia, hufanya kazi kuwa nyepesi na pia kusaidia nchi katika kutoa huduma za umma kwa raia. Kwa kuhamasisha vumbuzi za kisayansi, Wamagharibi wanaficha kufeli kwao katika kusimamia vyema mambo ya raia. Wanajaribu kuleta hisia kwamba kwa vile wameendelea katika sayansi na teknolojia, dunia lazima ikubali kuwa wao ni wenye hadhara bora.

Kwa kutabikisha hukmu za Uislamu, baada ya kusimamishwa kwa Khilafah, uoni sahihi utaendelezwa katika sayansi na teknolojia. Kwa kipindi kirefu, Wamagharibi wamelimiliki tabaka la wasomi wa ummah walioathiriwa na Umagharibi. Kigezo chochote cha mabadiliko kinachoendelea hakiwezi kuwa kigezo cha mtindo wa maisha ulio bora.

Sayansi na teknolojia zinaendelea kubadilika. Wanaadamu wa kila zama wamenufaika na maendeleo ya kisayansi ya zama zao. Hata hivyo, falsafa ya Wamagharibi ya kuwa elimu inategemea uzoefu unaotokana na hisi wanavyodai kuwa wanaadamu waliopita walikuwa nyuma kimaendeleo kwa sababu hawakuwa na vitu vinavyowapa faraja na huduma za kileo. Pia, hakuna haja ya kutishika na sayansi na teknolojia ya Wamagharibi. Hili sio suala la kuwa Waislamu hawakulifikia kabla. Kwa hakika, kuna mchango mkubwa wa Waislamu kwa maendeleo ya Wamagharibi katika sayansi na teknolojia. Wamagharibi wamenufaika kutokana na maarifa na vumbuzi za Waislamu. Haya yalipatikana bure katika kujifunza bila kuhitajia hati miliki. Hivyo Wamagharibi waliendelea katika safari yao kwenye maendeleo ya kisayansi. Kwa kweli, mfumo wa Kikafiri, ulioijaza dunia kwa dhulma, njaa na machafuko, kuutia utumwani ulimwengu wa Kiislamu kupitia sera zake za kikoloni na watawala vibaraka, haustahiki shukrani au kutambuliwa.

Hivyo kila Muislamu mwenye ghera ya kuuhuisha Ummah wa Kiislamu lazima atie juhudi kubwa ya kuanzisha tena mfumo kamili wa maisha wa Kiislamu katika jamii za Kiislamu. Hili litawezekana tu kwa kuiregesha tena Khilafah. Hakuna zaidi ya utekelezaji wa mfumo wa Uislamu wa kiulimwengu uliokamilika, ukiwa ni dola, utakaohuisha ardhi za Waislamu, kuhuisha uwezo wa uvumbuzi wa Waislamu na kung’arisha nyoyo na akili za Ummah. Hakuna zaidi ya kuufanya Ummah huu kuwa kiongozi wa mataifa yote kwa mara nyengine tena. Mwenyezi Mungu (swt) amesema katika Quran Tukufu,

(كُنْتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنْكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ)

“Nyinyi mmekuwa bora ya Ummah waliotolewa kwa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu.” [Surah Aali Imran 3: 110].

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Hizb ut Tahrir na
Usman Adil – Wilayah Pakistan

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu