Jumatano, 15 Rajab 1446 | 2025/01/15
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 “Kuyeyuka kwa Familia” za Mujtamaa wa Kisekula wa Kimagharibi

SEHEMU 1: Uhakika wa Kuyeyuka kwa Familia katika Dola za Kisekula za Kimagharibi

Mnamo Aprili 2008, Hakimu Paul Coleridge, jaji anaye husika na mahakama za kifamilia kote Kusini Magharibi mwa Uingereza, alitoa hotuba kwa mawakili wa familia kutoka katika shirika la “Resolution”, ambapo aliyasifu maisha ya familia nchini Uingereza kuwa ni “yenye kuyeyuka” yakidhihirisha janga la kuvunjika kwa familia. Alisema: “Idadi kubwa ya familia sasa zina watoto wanaolelewa na kina mama ambao wana watoto kutoka kwa mababa tofauti tofauti, hakuna yeyote kati yao anayechukua nafasi katika maisha yao au kuwasaidia au kuwalea… Hizi sio kesi kando, za kipekee. Ni sehemu ya shehena za kesi katika mahakama za kifamilia.” Aliendelea, “Takriban maovu yote ya kijamii yanaweza kunasibishwa moja kwa moja na mporomoko wa maisha ya familia. Sote twajua hili. Tathmini asili ya kila mtoto katika nidhamu ya uangalizi au nidhamu ya uadilifu wa vijana na utagundua familia iliyo vunjika. Ditto mraibu wa mihadarati. Ditto mlevi. Ditto wale watoto watoro au watundu shuleni. Chimba kesi hizi na utapata familia iliyo na matatizo, yaliyotokana na uhusiano wa wazazi ulio haribika na kuvunjika – au usio kuwako kamwe.”    

Wasifu huu mbaya wa maisha ya familia nchini Uingereza umejiri baada ya kutokea habari nyenginezo, ikiwemo kuanguka kwa viwango vya ndoa nchini Uingereza na Wales na kufikia kiwango cha chini kabisa tangu rekodi zianze kuwekwa mnamo 1862 (Afisi ya Takwimu za Kitaifa (ONS)) na ongezeko la viwango vya juu zaidi vya talaka tangu mnamo 1996. Maoni haya kuhusiana na kuyeyuka kwa muundo wa familia nchini Uingereza pia yalikaririwa na wengi wa wanasiasa, wasomi na walimu nchini humo. Robert Wheelan kutoka katika taasisi ya wachambuzi wakuu ya CIVITAS (Taasisi ya Utafiti wa Mujtamaa wa Kijamii), ambayo aghalabu huishauri serikali ya Uingereza juu ya maswala ya kijamii, ilielezea kuwa kuvunjika kwa familia ni tatizo kubwa mno kwa dola kusaidia kutatua. Alisema, “Dola huenda ingeweza kumwaga pesa na kuwapa watoto usaidizi kama ingekuwa kiwango cha familia zilizo vunjika ni kidogo, lakini haiwezi kulimudu tatizo lenye uzani mkubwa kiasi hiki.” Karen Woodall kutoka katika kituo cha familia zilizo tengana alitoa maoni, “Kutengana kwa familia hakika ndio ukweli wa maisha nchini Uingereza na katika mujtamaa zote. Ikiwa utaongezea mababu na nyanya wa watoto ambao wazazi wao wametengana na wa wazazi walio katika mahusiano na wazazi wengine waliotengana, ni wazi kuwa talaka na kutengana ndio kadhia inayo athiri nusu ya idadi hii.” Na walimu katika kongamano la 2008 la kila mwaka la Shirikisho la Walimu na Wahadhiri lilieleza kuwa “duara la sumu” la kuvunjika kwa familia ndilo linalo athiri uwezo wa watoto kusoma, afya yao ya akili na hali zao jumla.    

Kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita, mizani ya kuyeyuka kwa kiungo cha familia nchini Uingereza imeongezeka zaidi. Ukweli ni kuwa, kimekuwa katika mporomoko pasi kizuizi. Christian Guy, Mkurugenzi wa Kituo cha Haki cha Kijamii (CSJ), mchambuzi mkuu wa Kiingereza mwenye ushawishi anaye shauri juu ya maswala ya kijamii nchini Uingereza, alionya katika ripoti iliyo chapishwa mnamo 2013, kwa anwani, “Familia zilizo vunjika: Ni Kwa Nini Ustawi ni Muhimu”, kuhusu “‘tsunami’ ya kuvunjika kwa familia inayo ishambulia nchi hii’. Alitaja kuwa mwanadamu, jamii na gharama za kifedha ‘zina athari’ kwa watoto na vile vile watu wazima licha ya kukabiliwa na ‘dharura’ hii ya kitaifa, majibu kutoka kwa wanasiasa wa upande wa kushoto na kulia yamekuwa finyo.

Tsunami hii ya kuvunjika kwa familia inamulika dola zote katika ulimwengu wa magharibi. Nchini Uingereza, kiwango cha talaka kinasimama katika asilimia 42 (ONS). Mnamo 2012 kulikuweko na talaka 13 kila saa moja nchini Uingereza na Wales. Nchini Amerika asilimia 53 ya ndoa humalizikia kwa talaka, nchini Sweden ni asilimia 64, na nchini Belgium ni cha kushtua macho cha asilimia 70 (tarakimu kutoka Business Insider). Kwa mujibu wa shirika la Eurostat, kati ya 1965 hadi 2013 kiwango jumla cha talaka kiliongezeka katika nchi 28 za Umoja wa Ulaya (EU).

Ongezeko hili kubwa la talaka limefuatiwa na ongezeko kubwa la familia zenye mzazi mmoja – familia ambazo mtoto anaishi na mamake au babake pekee. Nchini Uingereza, kati ya 1996 na 2012 idadi ya familia zenye mzazi mmoja ziliongezeka kwa asilimia 25 hadi kufikia milioni 2 na sasa inawakilisha robo ya ‘familia’ zote zenye watoto wanaozitegemea (ONS). Ukweli ni, kwa mujibu wa tarakimu za serikali, takribani nusu ya watoto wote wenye umri wa miaka 15 nchini humo hawaishi na wazazi wao wote wawili wa kuwazaa. Katika jamii masikini zaidi, hii inaongezeka hadi 2/3 ya matineja hao. Idadi kubwa zaidi (aslimia 92) ya familia zenye mzazi mmoja zilizo na watoto wenye kuzitegemea zinaongozwa na kina mama; wengi waking’ang’ana kuwalea watoto wao peke yao, huku pia wakiwa watafutaji riziki peke yao wa familia zao. Kila mwaka kuna ongezeko la watu 20,000, wengi wao wakiwa wanawake, wanajiunga na wale wanaolea watoto peke yao. Natija yake ni idadi kubwa ya watoto nchini Uingereza, 1 kati ya 3, anakuwa pasi na baba nyumbani, huku ikikadiriwa kuwa milioni 1 hadi 2 yao wananyimwa mawasiliano ya maana na baba zao (ONS), na wengine wao wakiwa hawana mawasiliano kabisa. Tarakimu rasmi za usajili wa uzazi za 2015 zinaonyesha kuwa zaidi ya nusu ya kina mama wenye watoto matineja hawaishi na baba au jina la baba halikusajiliwa. Taasisi ya Mababa yaeleza kuwa kufikia wakati wanafika umri wa miaka 16, 1 kati ya 6 ya watoto wote nchini Uingereza huwa hajawahi kumuona baba yake kamwe. Davidi Cameron, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, alisema katika hotuba yake katika Kongamano la Chama cha Conservative kuwa, “Leo, tineja anayeketia mitihani ya GCSE kuna uwezekano zaidi wa kumiliki simu ya smartphone kuliko kuwa na baba anayeishi nao.”     

Hadithi hii hii ndiyo iliyoko katika dola nyenginezo za kisekula za Kimagharibi. Kwa mujibu wa zoezi la Usajili watu la Amerika ya 2010, 1 kati ya watoto 3 nchini Amerika (milioni 15) wanaishi pasi na baba na takriban milioni 5 wanaishi pasi na mama. Na katika baadhi ya sehemu za mijini, ni 1 kati ya watoto 10 pekee ambaye baba yuko.

Sambamba na janga hili la kuvunjika kwa familia ndani ya mujtamaa za Kimagharibi, kumekuweko na kushuka kwa viwango vya hali ya juu vya ndoa ndani ya nchi hizi kwa zaidi ya miongo michache iliyopita. Kwa mujibu wa Eurostat, kati ya 1965 na 2013, kiwango jumla cha ndoa katika nchi 28 za EU kimeporomoka kwa karibu asilimia 50 kwa tathmini ya juu juu. Nchini Uingereza, kwa zaidi ya miaka 40 iliyopita, kiwango cha idadi ya watu wazima ambao wamo ndani ya ndoa kimepungua kutoka asilimia 70 ya idadi ya watu hadi zaidi ya nusu (CSJ). Mwaka 2013 ulinakili kiwango cha chini zaidi cha ndoa. Kwa mujibu wa ONS, ni nusu ya matineja leo pekee nchini humo ambao wataoa. Katika nyingi ya nchi za Nordic kama vile Iceland, Denmark, na Norway, ni asilimia 30 pekee ya wanawake wameolewa, huku kiwango hicho kikishuka kuwa kichache zaidi ya asilimia 20 kwa wale wanawake walio na umri kati ya 25 na 29. (worldatlas.com)

Kinyume na kushuka huku kwa viwango vya ndoa, watu kuishi pamoja nje ya mafungamano ya ndoa ndani ya dola za Kimagharibi imeongezeka pakubwa mno huku ikitambuliwa ndani ya mujtamaa huru kama ‘muundo wa familia’ unaokubalika, na kuwa sambamba kimaadili mithili ya taasisi ya ndoa. Kwa hivyo, nchini Uingereza, huku wachache zaidi ya 1 kati ya watu wazima 100 chini ya umri wa miaka 50 waliishi pamoja nje ya ndoa katika miaka ya sitini, hii imeongezeka hadi 1 kati ya 5 leo (ONS), ikiwa ni familia milioni 3.3 (ONS). Ukweli ni, kuishi pamoja huku nje ya ndoa ni aina ya familia inayokuwa kwa kasi kwa zaidi ya miongo miwili nchini humo. Hii ni licha ya ukweli kuwa ripoti baada ya ripoti, utafiti baada ya utafiti zimefichua kuwa ndoa ndio njia imara zaidi pekee ya kulea watoto, huku kukiwa na uwezekano mkubwa wa familia zilioundwa kwa kuishi pamoja nje ya ndoa kushuhudia kutengana kwa wazazi wao kabla ya umri wa miaka 12 ikilinganishwa na watoto waliozaliwa na wazazi waliooana.    

Kama natija ya muondoko huu huru wa kimaisha katika Magharibi, hivyo basi haishangazi kuwa uzazi wa watoto nje ya ndoa umeongezeka pakubwa ndani ya dola hizi. Tarakimu za Eurostat zaeleza kuwa kiwango cha watoto waliozaliwa hai nje ya ndoa katika nchi 28 za EU mnamo 2014 ilikuwa ni asilimia 42. Mnamo 2015, idadi ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa iliipiku idadi ya watoto waliozaliwa ndani ya ndoa katika dola nyingi wanachama wa EU: Ufaransa – asilimia 59, Sweden – asilimia 55, Denmark – asilimia 56, Estonia na Slovenia (asilimia 58) (Eurostat). Nchini Uingereza, takriban nusu (asilimia 47) ya watoto huzaliwa nje ya ndoa (ONS), huku katika miaka ya arubaini ilikuwa karibu asilimia 6. Kwa mujibu wa utafiti wa wasomi katika Chuo Kikuu cha Amerika cha John Hopkins, uliochapishwa mnamo 2012, asilimia 57 ya wazazi nchini Amerika walio na umri kati ya miaka 26 na 31 wanapata watoto nje ya ndoa.    

Kuongezea tsunami hii ya kuvunjika kwa familia katika Magharibi, vile vile kuna matatizo mengine makubwa yanayoathiri maisha ya familia, kama vile wazazi kukosa muda wa kukaa na watoto kutokana na kuwa wazazi wote wawili baba na mama wamebanwa na matarajio ya kikazi ambapo pia yanadhuru ndoa; mateso ya “mwanamke bomba” kung’ang’ana ili kuweka mizani sawa kati ya majukumu ya kinyumbani na kudumisha taaluma au kazi; na kupunguza kiungo cha familia kwa wanandoa kuchagua kuwa na watoto wachache au hata kutokuwa na watoto kabisa imesababisha upungufu wa ‘watoto’ katika nchi kadhaa ikiwemo Ufaransa, Ujerumani na Uhispania, ikipelekea kuwepo kwa idadi kubwa ya wazee na vijana wachache wa kuwaangalia wazee hao. 

Kuporomoka kwa thamani ya maisha ya familia nchini Uingereza na mujtamaa nyengine nyingi za kisekula za Kimagharibi ni dhahiri kuona, kama zilivyo natija za familia kuvunjika au kukosa maelewano ambayo imeathiri vibaya maisha ya wengi, hususan watoto na kupanda mbegu za mrundo wa matatizo ya kijamii kwa dola hizi. Hakimu Paul Coleridge alielezea kuwa kuzidi kwa kiwango hiki cha juu cha kuvunjika kwa familia nchini Uingereza ni kama, “… tamasha lisilo na mwisho la mateso ya mwanadamu. Mto usio kauka wa machungu ya mwanadamu”.   

Sehemu ya 2 ya makala haya itatathmini sababu msingi za kuyeyuka kwa familia katika dola huru za kisekula za Kimagharibi.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Dkt Nazreen Nawaz
Mkurugenzi wa Kitengo cha Wanawake katika Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumapili, 12 Aprili 2020 07:18

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu