- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Iran: Maendeleo Katika Haki Sawa au Maangamivu kwa Watu Wake?
Dola za kisekula huona fahamu za usawa wa kijinsia, utetezi wa wanawake, uwezeshaji wa wanawake na uhuru usio na mipaka kama mojawapo ya desturi muhimu mno za dola yenye kufaulu. Hivyo basi, dola za kirasilimali hudai kuwakilisha na kudhamini maadili haya, huku uhakika ukidhihirisha tofauti. Kwa mujibu wa taasisi ya Berggruen egregious ukosefu wa usawa wa kijinsia bado ungalipo duniani licha ya hatua kabambe za kitaifa na kimataifa kuchukuliwa kwa ajili ya usawa wa kijinsia.
Lakusikitisha, maadili haya yaliyo vumbuliwa na makafiri, pia wamezivamia biladi za Kiislamu na wengi wa Umma wameathirika na fikra hizi kutokana na kuugua ulemavu wa kifikra katika elimu ya Kiislamu. Sawia na kila sehemu nyengine duniani, Umma nchini Iran haujasalimika kutokana na maadili haya ya Kimagharibi ya dori za kijinsia. Mashirika mengi kama vile Wakfu wa Wanawake wa Iran na America, Shirika la Wanawake la Iran, UNICEF, UNDP, UN na mengine mengi yako katika harakati ya kupigia debe ugavi huru wa kisekula wa dori kati ya wanaume na wanawake.
Matokeo yake mabaya hayapaswi kupuuzwa. Wanaume na wanawake wameshindwa kupata nafasi yao wazi ndani ya muundo wa familia na katika mujtamaa na wanajaribu kuyakubali maadili ambayo yako dhidi ya umbile la mwanadamu. Natija yake, kimsingi maisha ya familia yameathirika pakubwa mno. Wanawake wanatafuta uhuru, kujitegemea wenyewe na ubwana. Dori msingi ya mwanamke kama mama na mjenzi wa nyumba limeorodheshwa kama lililopitwa na wakati na angazo liko juu ya taaluma, haki sawa na wanaume na utetezi wa mwanamke.
Takwimu zinaonyesha kuwa kiwango cha ukuaji wa idadi ya watu nchini Iran kimeshuka sio tu kwa asilimia 1.29 katika miezi 12 iliyopita, ikiifanya kuwa ya chini zaidi eneo hilo. Ukweli ni kwamba talaka zinaongezeka mno nchini Iran na hisa ya ndoa zinazoishia kwa talaka imeongezeka zaidi ya maradufu katika miongo iliyopita. Ikilinganishwa na kiwango wastani cha talaka duniani ambacho ni moja katika kila ndoa saba, nchini Iran kuna talaka 1 katika kila ndoa 4.8. Zaidi ya milioni 3 ya wanawake wasomi wa Kiirani walio na zaidi ya umri wa miaka 30 hawajaolewa, kwa mujibu wa Mirzan, shirika rasmi la habari la idara ya mahakama ya Iran. Kiwango cha familia kimedidimia kwa miaka kadhaa sasa. Katika sensa ya Iran ya 1976, kiwango cha familia kilikuwa ni 5.02 lakini majibu ya sensa ya Iran ya 2016 yanaonyesha kuwa idadi wastani ya familia ni 3.3. Ukweli mwengine kuhusu kiwango cha familia ni idadi ya familia zenye mzazi mmoja. Katika sensa ya 2016, asilimia 8.5 ya familia zilikuwa na mzazi mmoja. Idadi ya mahusiano nje ya ndoa pia imeongezeka katika miaka ya nyuma. Utafiti wa maoni uliofanywa na Shirika la Kitaifa la Vijana la Iran mwaka jana umeonyesha kuwa asilimia 55 ya vijana 7,000 wa kiume na kike walioulizwa walikuwa na wapenzi wa kike au wa kiume kabla ya ndoa. Wajuzi huru wanaamini kuwa asilimia halisi huenda hata ikawa ya juu zaidi. Pia haja ya ukahaba imeongezeka. Idadi halisi ya makahaba wanaofanya kazi nchini Iran haijulikani. Lakini, makahaba wanaonekana wazi katika baadhi ya vichochoro vya mitaa ya miji mikubwa. Mnamo 2012, gazeti la Iran, Entekhab, lilikadiria kuwa kulikuweko na takriban makahaba 85,000 jijini Tehran pekee.
Ni wazi kuwa desturi hizi na maadili haya ya Kimagharibi yenye madhara yamesababisha mvutano wa kijinsia leo, na mizozo katika mpangilio wa kifamilia na mgogoro katika uwepo jumla na kuishi baina ya wanaume na wanawake. Umma umesahau kuwa maoni na maadili haya ya Kimagharibi yanasimama dhidi ya mfumo wa Kiislamu na sheria yake sio kwa sababu Uislamu haudhamini haki za wanawake, bali kwa sababu maadili haya huru ya kuwatetea wanawake katika Magharibi na usawa wa kijinsia ni matunda ya kudhulumiwa wanawake katika Magharibi na batili ya kirongo ya Kikristo.
Watawala katika ardhi za Kiislamu pia wanauchanganya Umma. Raisi wa Iran, Bw. Rouhani, alisema katika Kikao cha Kitaifa cha Wanawake Kuunda Uchumi na Utamaduni nchini Iran: “Hatutakubali utamaduni wa ubaguzi wa kijinsia. Wanawake ni lazima wafurahie fursa sawa, ulinzi sawa na haki sawa za kijamii.”
Taarifa hizi na nyenginezo za Rouhani na wanasiasa wa Kiirani ni thibitisho zaidi kuwa Iran inawakilisha desturi na maadili ya Kimagharibi kuliko ya Kiislamu. Kutokana na kuchanganyikiwa kithaqafa kwa serikali hii, watu nchini Iran hawana njia ya kuyafikia maadili na desturi sahihi za Kiislamu. Usawa wa wanaume na wanawake, upunguzaji kiwango cha uzazi, kuangazia taaluma juu ya cheo cha mama, mahusiano nje ya ndoa, kuachana na vazi la Kiislamu, uhuru wa kibinafsi na uhuru wa kuzungumza kamwe siyo masuluhisho ya matatizo ya leo. Ukweli ni, kufeli kwake kunaonekana dhahiri duniani.
Kwa Allah (swt), wanaume na wanawake ni sawa kwa thamani yao, akili na maumbile kama wanadamu. Lakini, ni dhahiri kabisa kuwa kuna tofauti katika maumbile ya kimwili ya jinsia hizi. Hivyo, Allah (swt) amepanga dori zao ndani ya ulimwengu huu kwa mujibu wa maumbile ya jinsia hizi. Hivyo, Allah (swt) amewapa wanawake haki zilezile za kisiasa, kiuchumi, kielimu za kimahakama kama wanaume. Lakini, ili kuyapangilia maisha ya familia barabara, Uislamu ukaweka dori, majukumu na haki ndani ya ndoa na muundo wa familia ambayo yanatofautiana kati ya wanaume na wanawake. Dori na majukumu ya mwanamume si aula kuliko yale ya wanawake. Bali, kila jukumu ni muhimu katika kuhakikisha maisha ya familia yenye utulivu na uzalishaji ambayo haki za wanaume, wanawake, watoto, wazee na familia kuu jumla zinachungwa vilivyo. Hivyo basi, kuliko kufuata visigino vya mataifa ya Kimagharibi katika kuangamiza ndoa na muundo wa familia kupitia kutabanni maadili yao ya uhuru, usekula na utetezi wa wanawake, kama Umma wa Kiislamu tunahitaji kuyaangalia kwa kina na kuyakumbatia maadili, miondoko ya kimaisha, sheria na nidhamu uliyoekwa na Dini yetu ambayo pekee ndiyo yaweza kudhamini ndoa na viungo vya familia imara.
﴾إِنَّ الْمُسْلِمِينَ وَالْمُسْلِمَاتِ وَالْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ وَالْقَانِتِينَ وَالْقَانِتَاتِ وَالصَّادِقِينَ وَالصَّادِقَاتِ وَالصَّابِرِينَ وَالصَّابِرَاتِ وَالْخَاشِعِينَ وَالْخَاشِعَاتِ وَالْمُتَصَدِّقِينَ وَالْمُتَصَدِّقَاتِ وَالصَّائِمِينَ وَالصَّائِمَاتِ وَالْحَافِظِينَ فُرُوجَهُمْ وَالْحَافِظَاتِ وَالذَّاكِرِينَ اللَّهَ كَثِيرًا وَالذَّاكِرَاتِ أَعَدَّ اللَّهُ لَهُمْ مَغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا﴿
“Hakika, Waislamu wa kiume na Waislamu wa kike, na waumini wa kiume na waumini wa kike, na watiifu wa kiume na watiifu wa kike, na wakweli wa kiume na wakweli wa kike, na wenye kusubiri wanaume na wenye kusubiri wanawake, na wenye unyenyekevu wanaume na wenye unyenyekevu wanawake, na wenye kutoa sadaka wanaume na wenye kutoa sadaka wanawake, na wenye kufunga wanaume na wenye kufunga wanawake, na wenye kuhifadhi tupu zao wanaume na wenye kuhifadhi tupu zao wanawake, na wenye kumkumbuka Allah sana wanaume na wenye kumkumbuka Allah sana wanawake – Allah amewaahidi msamaha na ujira mkubwa.” [33:35]
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Amanah Abed