Jumamosi, 21 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/23
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 “Kuyeyuka kwa Familia” za Mujtamaa wa Kisekula wa Kimagharibi

SEHEMU 2: Sababu za Kuyeyuka kwa Familia Katika Dola za Kisekula za Kimagharibi

Serikali za Kimagharibi zimejaribu kuzindua miradi kadha wa kadha ili kuzuia wimbi la kuvunjika kwa familia ndani ya mujtamaa zao. Lakini, haya yameambulia patupu. Hii ni kwa sababu wameshindwa kutambua kwamba sababu msingi za kuyeyuka huku kwa familia ni maadili msingi ya kisekula na ukosefu jumla wa umuhimu unaopatiwa ndoa na maisha ya familia ndani mujtamaa huru za kirasilimali.

Uhuru Uso Mipaka wa Kibinafsi na Kingono:

“Uhuru wa kibinafsi na kingono” juu ya msingi wa mujtamaa huru umekuza dhana ya ubinafsi na kutojali chochote maishani kwa msingi wa utafutaji matamanio na matakwa ya kihayawani kuliko kukuza fikra ya kuhisabiwa katika vitendo vya mtu na uwajibikaji juu ya wengine. Imesababisha watu wengi kuchukia ndoa kutokana na hofu juu ya kujitolea, uaminifu na majukumu yanayohitajika – kuitazama ndoa kama “kizuizi cha uhuru wao” na badala yake kufadhilisha “uhuru na useja” na kuwa na mahusiano ya kijinsia na “yeyote, wakati wowote”. Imeibua utamaduni wa uzinzi unaopelekea viwango vya juu vya mimba za matineja nje ya ndoa, uavyaji mimba, kina mama wapweke na zinaa ambayo ni moja ya sababu kuu za talaka katika mujtamaa nyingi huru. Kwa mujibu wa utafiti ulionukuliwa na gazeti la ‘The Independent’, asilimia 50 hadi 60 ya wanaume waliooa na asilimia 45 hadi 55 ya wanawake walioolewa nchini Uingereza hufanya zinaa. Kwa mujibu wa tarakimu kutoka gazeti la ‘The Times’, zinaa inajumlisha asilimia 12 ya sababu za talaka nchini Uingereza. Abigail Lowther, wakili aliye na kampuni inayohusika na sheria ya familia, alisema kuwa ukosefu wa uaminifu nchini Uingereza ulikuwa “ukiongezeka kwa kasi” ikilinganishwa na aina nyenginezo ya tabia zinazohusishwa na talaka. Nchini Denmark, asilimia 46 ya wanandoa washawahi kuwa na uhusiano kwa mujibu wa idadi kutoka Statista. Na nchini Amerika, baadhi ya tafiti ziligundua kuwa 1 katika ya watu 3 alikiri kumdanganya mwanandoa mwenzake. Ukweli ni, ndani ya mujtamaa huru, utukufu wa ndoa na uaminifu umemomonyoka kiasi ya kuwa biashara zinazotoa ‘huduma za zinaa’ zinaendeshwa kihalali ndani ya dola! Lakini, falsafa ya kupata upeo wa juu wa uhuru wa kibinafsi haiwapi watu furaha ambayo kimsingi watu wanaihitaji. Ripoti ya shirika la Msalaba Mwekundu la Uingereza na Ushirika, iliyo chapishwa mnamo Disemba 2016, iligundua kuwa talaka na kuvunjika kwa familia imepelekea janga la upweke nchini Uingereza. Ukweli ni, imewaacha Waingereza milioni 9 na upweke.    

Utamaduni na muondoko huu wa uhuru wa kimaisha yamesababisha pia hali ambapo mtu huenda akawa na mahusiano nje ya ndoa na idadi kadhaa ya wanawake na kuwa baba wa watoto kutoka kwa kina mama tofauti tofauti, huku akikosa kuchukua jukumu lolote la kimwili au la kihisia la mtoto wake au mamake isipokuwa tu uwezekano wa malipo ya hundi moja tu kila mwezi. Hii imeyatishia maisha ya mamilioni ya watoto na wanawake. Hakimu Paul Coleridge, aliyekuwa jaji wa Mahakama Kuu ya Uingereza katika kitengo cha familia, alielezea kuwa hali hii ni kama, “mchezo uso kwisha wa ‘mahusiano ya kimuziki’ au ‘pitisha mpenzi’, ambao sehemu kubwa ya watu wanajihusisha nao … kiu iso mwisho na yenye kuambulia patupu ya kutafuta uhusiano imara.” Ni hali ambayo pia imesababisha ukosefu wa uaminifu katika watu wanaotafuta wenza katika ndoa, kwa kuwa hawana hakika kama uhusiano huo umejengwa juu ya utiifu, uaminifu na uangalifu au la, na wana wasiwasi kuhusiana na kuweza kudumu katika mazingira kama haya yaliyojaa uzinifu na kujistarehesha binafsi. Ni mojawapo ya sababu za kushuka kwa viwango vya ndoa kwa wamagharibi huru.   

Fauka ya hayo, fikra hatari iliyo kuzwa na maadili huru yanayo shajiisha watu kufuatilia na kutenda kwa mujibu wa matamanio na matakwa yao, sambamba na kuwadunisha wanawake ndani ya mujtamaa huru zinazo idhinisha ngono na kuiweka kama lengo katika sekta tofauti tofauti, ni jambo linalochangia pakubwa janga la ghasia za kinyumbani zinazo ziathiri mujtamaa za Kimagharibi. Mmoja kati ya wanawake watatu ashawahi kuripoti baadhi ya aina za dhulma za kimwili au kijinsia tangu umri wa miaka 15 (Shirika la Umoja wa Ulaya la Haki Msingi (European Union Agency for Fundamental Rights)). Nchini Uingereza, mmoja kati ya wanawake wanne amepitia ghasia za kinyumbani katika maisha yake, na wanawake 2 huuliwa kila wiki na mpenzi wa sasa au wa zamani (Afisi ya Uingereza ya Takwimu za Kitaifa (UK Office for National Statistics)). Nchini Amerika, mwanamke mmoja hupigwa na mumewe au mpenziwe kila sekunde 15 (Shirika la Kitaifa la Uchunguzi (Federal Bureau of Investigation)) na watatu huuliwa na wapenzi wao kila siku (Muungano wa Kiakili wa Marekani (American Psychology Association)). Na nchini Australia, kila masaa 3 mwanamke hupelekwa hospitali kutokana na ghasia za kinyumbani (Kitengo cha Utafiti cha Masomo ya Jeraha, Chuo Kikuu cha Flinders (Research Centre for Injury Studies, Flinders University, Australia)).  

Ubinafsi:

“Saratani” ya fikra ya ubinafsi ya “Mimi na nafsi yangu”, inayo kuzwa ndani ya mujtamaa za kirasilimali inayo tukuza kutafuta maslahi ya mtu binafsi juu ya kila kitu chengine imeila misingi ya muundo wa familia. Imesababisha watu binafsi kuangazia juu ya kile ambacho ni bora kwao kuliko kile ambacho ni bora kwa wanandoa wenza au ndoa, inayopelekea ongezeko la talaka. Imesababisha kuweka matamanio yao juu ya hali nzuri ya watoto wao na mujtamaa, na kutenganisha kujihusisha na vitendo vyao na miondoko yao ya kimaisha na athari angamivu iliyoko kwa wengine. Imechangia watu kuchelewesha au kukataa kuwa na watoto hadi baadaye maishani ili kuyatumia vilivyo maisha yao ya kijamii, fedha za kibinafsi na uhuru wa kibinafsi. Kwa mujibu wa Afisi ya Uingereza ya Takwimu za Kitaifa (ONS), kiwango cha watoto waliozaliwa na wanawake walio chini ya miaka 25 nchini Uingereza na Wales kilishuka kwa asilimia 47 mnamo 1971 hadi asilimia 25 mnamo 2008. Ripoti ya ONS 2010 ya Miondoko ya Kijamii arubaini ilieleza kuwa idadi ya watu wanaoishi katika nyumba za familia na watoto ilishuka kutoka asilimia 52 mnamo 1961 hadi asilimia 36 mnamo 2009, huku idadi ya familia zenye mzazi mmoja zikiongezeka kutoka milioni 1.7 hadi milioni 7 katika kipindi hicho hicho. Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, wanawake katika umri wa miaka ya arubaini nchini Uingereza ni takriban mara mbili ya wale ambao kuna uwezekano wa kutokuwa na mtoto kama katika rika la wazazi wao, huku mmoja kati ya wanawake watano waliozaliwa mnamo 1969 akikosa kuwa na mtoto leo. Clare McNeil, mwandishi wa ‘Generation Strain’ (ripoti ya hivi majuzi kutoka katika Taasisi ya Utafiti wa Sera ya Umma) anaonya kwamba, “Idadi ya watu wenye umri kati ya 65 hadi 74 wasiokuwa na watoto wa kuwahudumia wakati wa uzeeni itaongezeka takriban maradufu kabla ya kumalizika muongo ujao,” na kwamba, “Kufikia 2030, zaidi ya watu milioni moja katika rika la umri huu hawatakuwa na watoto, ikilinganishwa na 580,000 mnamo 2012.” Sensa ya Amerika ya Taasisi ya Utafiti wa Watu iliyo chapishwa mnamo 2015 iligundua kuwa takriban (aslimia 47.6) ya wanawake nchini Amerika kati ya umri wa miaka miaka 15 na 44 hawajawahi kuwa na watoto. Inawakilisha asilimia kubwa ya wanawake wasiokuwa na watoto tangu taasisi hiyo ilipoanza kufuatilia takwimu hiyo mnamo 1976. Katika utafiti wa Amerika juu ya wanaume na wanawake wasiokuwa na watoto, kwa anwani: “Wawili wanatosha: Muongozo wa wanandoa wa chaguo la kuishi bila ya watoto” (Scotts, 2009) ulionukuliwa na ‘Psychology Today’ asilimia 80 ya walio shirikishwa, hususan wale walio chini ya miaka 40, waliiorodhesha kama yenye lengo imara taarifa - ‘Nathamini uhuru na kujiamulia’.  

Ubinafsi umewasababisha wazazi kuwatelekeza watoto wao huku wakitafuta maslahi yao ya kibinafsi, na kuwasababisha watoto nao kuwatelekeza wazazi wao wakongwe, wakiwaona kama mizigo kwa wakati wao na fedha zao binafsi, wakiwaweka katika nyumba za wazee ili wengine wawahudumie. Na kujali kibinafsi juu ya familia ya mtu (mke na watoto wake) na kutowatilia maanani au kuwatelekeza jamaa zake wengine, imesababisha ukosefu wa nidhamu ya usaidizi kwa familia kuu jumla inayokabiliwa na matatizo ya kimwili, kifedha na kihisia, ikiwafanya wengi kuteseka peke yao kimya kimya.

Usawa wa Kijinsia:

Ndani ya mujtamaa za kisekula za kirasilimali, kumekuweko na kudunishwa thamani cheo cha mama na maisha ya familia dhidi ya maisha ya kiuchumi. Katika ngazi ya kihistoria, mvutano wa Kimagharibi wa usawa wa kijinsia na kuibuka kwa utetezi wa wanawake iliyaweka maisha ya umma na dori asili ya mwanamume kuwa mtafutaji riziki juu ya maisha ya kibinafsi, cheo cha mama na dori asili ya mwanamke kuwa mjenzi wa nyuma. Watetezi wengi wa wanawake wana hoja kuwa heshima ya wanawake na uhuru hauko sambamba na kumtegemea mumewe kiuchumi au majukumu kamili ya kinyumbani, na hivyo basi, sio jambo tu la mwanamke kuwa na haki ya kufanya kazi bali kukaribia kuwa ni lazima kwa mwanamke kufanya kazi. Christabel Pankhurst, mtetezi mkuu maarufu wa wanawake na mwanachama wa harakati ya (kuwapigania wanawake wapewe haki ya kupiga kura) mwanzoni mwa karne ya 20, alisema kuhusu majukumu ya maisha ya nyumba kuwa ni mzigo usiovumilika juu ya wanawake walioolewa, upotezaji wakati na nguvu za kiuchumi, na hauna ujira wala hutambuliwi.  

Leo, mojawapo ya natija za mtazamo huu wa maisha ya nyumba na fahamu ya “Usawa wa Kijinsia” ni kuundwa kwa mujtamaa ambazo wanawake sio tu wana haki ya kuajiriwa bali wanatarajiwa kufanya kazi hata kama ni kina mama wapweke walio na jukumu la kipekee la kuwachunga na kuwalea watoto wao. Fahamu ya usawa wa kijinsia ambayo nadharia yake ilikuwa kuzalisha “mwanamke mwenye kila kitu”, kiuhalisia ilizalisha “mwanamke mtendaji kila kitu” – aliye endelea kubeba mzigo wa majukumu ya mama na majukumu ya familia lakini sasa pia anang’ang’ana na mzigo zaidi wa kuimudu familia yake kifedha. Huku wazazi wote wawili wakiwa watafutaji riziki katika familia nyingi, kumekuweko na mvutano wa kudumu wa kutafuta muda kwa ajili ya watoto au muda wa kuziimarisha ndoa, aghalabu inayoleta mvutano katika uhusiano kati ya mume na mke. Hivyo basi, Usawa wa Kijinsia, ambapo mtu anaangalia kile ambacho ni bora kwa mwanamke kwa mkabala na kile ambacho ni bora kwa mwanamume kuliko kile ambacho ni bora kwa familia au jamii kupuuza kile ambacho ni bora kwa ajili ya kuimarisha ndoa kwa ajili ya watoto na kwa ajili ya mujtamaa kwa jumla. Fauka ya hayo, usawa wa kijinsia, unaomomonyoa kuridhia tofauti za kijinsia na dori, pia imeathiri utambuzi ndani makazini na katika mujtamaa wa umuhimu wa cheo cha mama, ikipelekea waajiri wengi kushindwa kuwajali vilivyo wale wanawake wenye watoto wadogo, kama kuwapa masaa muwafaka ya kazi au mahitaji mengineo yanayotakikana, wakipuuzilia mbali umuhimu wa majukumu yao katika familia zao.  

Fikra ya kimada:

Nidhamu ya kimada ya kirasilimali, iliyoweka mbele utafutaji wa mali kama lengo lake kuu la kimfumo imefadhilisha faida juu ya watu na fedha juu ya familia. Imeangazia kwa njia ya kudumu juu ya utafutaji rasilimali za serikali au mapato ya biashara juu ya uchungaji familia. Msukumo huu wa kudumu kwa ajili ya faida ya muda mfupi umedunisha cheo cha mama na maisha ya familia na kuwalazimisha hata kina mama wapweke kufanya kazi, ikiwaacha na muda mchache wa kulea watoto wao barabara. Hakika, aghalabu kuna vishajiisho vya kifedha vya kina mama kurudi kufanya kazi; vishajiisho vichache zaidi kwao kukaa nyumbani na kuhakikisha ulezi imara wa watoto wao. Kuthamini huku mada juu ya cheo cha mama kumepelekea hali ambapo mwanamke mja mzito au yule aliye na watoto wadogo aghalabu kuonekana kama mzigo kwa kampuni kuliko kuwa ni rasilimali kwa mujtamaa. Utafiti kwa mameneja 500 uliofanywa na kampuni ya sheria ya Kiingereza, Slater & Gordon ulio chapishwa mnamo 2014, unaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 40 walikiri kuwa kwa ujumla hofu ya kuajiri mwanamke aliyefikisha umri wa kuzaa, huku idadi kama hiyo hiyo wakiwa na hofu kuajiri mwanamke ambaye tayari ana mtoto au kuajiri mama katika cheo kikubwa. Thuluthi moja ya mameneja katika utafiti huu walisema kuwa ni heri waajiri mwanamume wa umri wa miaka ya ishirini au thalathini kuliko mwanamke wa umri huo huo kwa kuhofia wao kuchukua likizo ya uzazi. Utafiti wa 2005 kwa kampuni 98 nchini Uingereza wa Shirikisho la Uajiri uligundua kuwa 3/4 ya biashara ni heri zivunje sheria kuliko kumuajiri mwanamke mja mzito au aliyetimu umri wa kuzaa. Natija yake ni kuwa sio tu kuwa wanawake wanashinikizwa kuingia katika ajira na kutarajiwa kupokea mishahara kwa ajili ya familia zao, bali wanabaguliwa makazini kwa kuwa na uzao! Natija yake ni kuwa wanawake wengi wanafadhilisha kuchelewesha kupata watoto au kubaki bila ya watoto kuliko kukabiliana na “hukumu hii ya uwezo wa kuzaa” katika mapato yao au taaluma zao. Inaonekana kuwa, kwa wanawake wengi Magharibi, “kutiwa minyororo jikoni” kumebadilishwa kwa “kutiwa minyororo katika soko la kiuchumi”. Haya ni miongoni mwa mambo yanayochangia viwango vya chini vya uzazi na ‘mgogoro wa uwezo wa kuzaa’ yanayo athiri dola nyingi za kirasilimali za kimagharibi leo ambayo yana athari angamivu kwa mujtamaa, ikiwemo idadi chache ya watu wa kuwahudumia wazee.  Mtu pia asisahau janga la kihisia wanalopitia wale wanawake wanao lazimishwa kufanya matibabu ya IVF ili kuzaa kutokana na kupungua kwa uwezo wa kuzaa, kupoteza mimba na kuongezeka kwa matatizo ya ujauzito yanayo nasibishwa na kuchelewesha kuwa mama.  

Tamati:

Ni dhahiri kuwa ni maadili na sheria za nidhamu huru ya kisekula ya kirasilimali zinazotekelezwa ndani ya dola nyingi za kimagharibi ndiyo shina la tatizo la ghasia na kuangamia kwa muundo wa familia ndani ya mujtamaa zao. Hakika, nidhamu hii kimaumbile imeundwa kusababisha ukosefu wa utulivu katika familia na kuvunjika kwake, ikisababisha mateso ya kibinadamu yasiyo elezeka kwa watu wengi mno na watoto na matatizo yasio na idadi kwa dola.

Lakusikitisha, Ummah wa Kiislamu unaoishi Magharibi au katika ulimwengu wa Kiislamu haujakingwa kutokana na maadili haya ya kisekula au ya kirasilimali kutokana na kuzama ndani ya mazingira na kuishi chini ya nidhamu zinazopigia debe na kushabikia maadili haya yasiyokuwa ya Kiislamu. Natija yake ni kuwa fahamu ya “ndoa imara” na “viungo vya familia imara” ambazo daima zimefahamika na Waislamu kwa vizazi vyote kuwa ndio kitovu au msingi wa jamii imara leo pia zimemomonyoka ndani ya Ummah wa Kiislamu. Kama Waislamu, ni muhimu mno tuchukue mafunzo kwa makini kutokana na kuyeyuka huku kwa muundo wa familia ambao umejitokeza ndani ya mujtamaa za kimagharibi na kupinga itikadi, maadili na nidhamu zilizo sababisha ghasia hizi za kijamii, ili jamii zetu zisifuate njia hiyo hiyo ya maangamivu. Hii ni pamoja na kufahamu waziwazi na kukumbatia maadili, sheria za kijamii na nidhamu sahihi ya Uislamu ambayo pekee ndiyo yaliyojihami ili kutatua matatizo mengi yanayo athiri utulivu na umoja wa maisha ya familia katika Ummah wetu. 

“Katika miongo ijayo, mafanikio yatakusanyika tu kwa zile tamaduni zinazo hifadhi hadhi ya familia.” Joel Kotkin – Mwandishi wa ‘Watoto Wote Wamekwenda Wapi?’ na Msomi wa Masomo ya Mijini kutoka Chuo Kikuu cha Chapman eneo la Orange, California, Amerika.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Dkt. Nazreen Nawaz

Mkurugenzi wa Kitengo cha Wanawake Katika Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumatatu, 17 Agosti 2020 09:34

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu