Alhamisi, 09 Rajab 1446 | 2025/01/09
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Siasa za Michezo

(Imetafsiriwa)

Uwekezaji wa mataifa ya Ghuba katika michezo umevutia hisia kubwa za kiulimwengu hivi karibuni kwa kuanzishwa ligi mpya ya mchezo wa gofu na Saudi Arabia inayoitwa ‘LIV Golf Invitational Series’. Vyombo vya habari vya Magharibi vimeishutumu Saudia, Imarati, Qatar na nchi nyengine za Ghuba juu ya ‘kasumba ya michezo,’ ambapo michezo hutumika kukuuza heshima iliyopotea, kupitia uandaaji wa hafla za michezo, kudhamini timu za michezo au kwa ushiriki michezoni. Mataifa ya Ghuba yamejibu kwa kuonyesha namna ambavyo uwekezaji wao kwenye michezo utakuwa ni sehemu ya mipango yao kuutanua uchumi wao kuwa zaidi ya mafuta.

Hafla za kimichezo zimetumika sana na mataifa kote duniani kama burudani ya kuwafanya watu washughulishwe na wajiweke mbali na matatizo ya ndani ya nchi zao. Hivi leo michezo ni sekta inayogharimu mabilioni ya dolari na imekuwa na athari kubwa za kiuchumi. Saudi Arabia imekuwa ni nchi ya mwanzo ya Waislamu kutumia michezo kwa lengo la kuyaweka mbali mazingatio ya watu wake. Hali ya baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia ilileta changamoto nyingi kwa watawala wa Kiarabu, ambao waliongoza mataifa yaliozaliwa upya, kutokea utaifa wa Kiarabu hadi kuibuka kwa Gamal Abdel Naseer, katika kupenyezwa kwa fikra za Kimagharibi kutokana na makampuni ya nishati ya Wamagharibi yaliokuwepo katika eneo ili kuweka msingi mpya katika eneo la masoko ya kiulimwengu ya mafuta na gesi. Mivutano baina ya Mfalme Saud na Mwana Mfalme Faisal ilishuhudia mahitaji yaliyoongezeka ya kuugeuza Ufalme kuwa ufalme wa kikatiba. Mnamo mwaka 1956, Saudia ilianzisha Shirikisho la Mpira wa miguu la Saudi Arabia, ambalo hivi sasa lina zaidi ya vilabu 150. Imeliweka hilo kwa lengo la kuhamisha mazingatio yawe mbali na siasa. Mashindano mawili ya mpira wa miguu kila mwaka: Kombe la Mwana Mfalme mnamo 1956 na Kombe la Mfalme mwaka mmoja baadaye yalianzishwa kwa ajili hii.

Hata hivyo, ilikuwa ni Mapinduzi ya Kiarabu mnamo 2011 ambayo hasa yaliushughulisha utawala wa Saudia. Machafuko nchini Yemen na Bahrain na uwezekano wa kuenea ndani ya Ufalme, yalishuhudia kuongezeka kwa kasi matumizi kwa ajili ya masuala ya michezo. Mfalme Salman na Mfalme Mtarajiwa Muhammad bin Salman (MBS) walianzisha Kombe la Ligi Kuu na Ligi ya Mfalme Mtarajiwa Muhammad bin Salman kuongezea orodha inayoongezeka ya mashindano ya mpira wa miguu katika Ufalme huo.

Washindani wa Kieneo  

Wakati Mataifa ya Ghuba yakitangaza vitega uchumi vyao kama fursa ya kutanua uchumi wao, ukweli usiopingika ni kuwa Mataifa yote ya Ghuba yamekuwa na ushindani wa muda mrefu na uliojikita miongoni mwao. Ushirikiano wa kieneo ulikuwa ni miongoni mwa malengo ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Ghuba (GCC) wakati ulipoundwa mnamo 1981. Lakini ushindani wa kihistoria uliwaacha wakiendelea kushindana baina yao. Wakati Saudi Arabia ilipowekeza katika viwanda vya kusafisha mafuta, mataifa mengine ya Ghuba yalijenga mfano wa hayo, japokuwa kiuchumi hayawezi kupata faida kutokana na idadi ndogo ya wakaazi wake. Ushindani huu katika eneo hatimaye ulienea katika kujenga bandari, mashirika ya ndege ya kifahari, viwanja vya ndege vya kimataifa, vyuo vikuu na hivi sasa michezo.

Mji wa michezo wa Qatar (Aspire Zone) wenye eneo la hekta 250 jijini Doha na ushindi wake wa 2010 kuandaa Kombe la Dunia la FIFA 2022, imechochea ushindani mkubwa kutoka Saudi Arabia na Imarati kwa kuwa Qatar imevutia macho ya walimwengu na mataifa yote mawili yameanza kuweka rasilimali kubwa zaidi katika ulimwengu wa michezo. Abu Dhabi kupitia hazina yake ya ‘Sovereign Wealth Fund’ na Dubai kupitia Shirika la ndege la Emirates, pamoja na lile la kitaifa Etihad, yamepata baadhi ya timu za mpira wa miguu zenye faida zaidi duniani. Saudi Arabia kwa upande mwengine imezindua sera ya michezo ya kujikuza kwa kupitia mradi wa jiji la NEOM, mradi mkubwa ulio katika ujenzi utaokuwa na jiji jipya la kisasa zaidi. Ni mwaka jana tu, Saudi Arabia iliichukua klabu ya Uingereza Newcastle United ambapo Waziri wa Michezo wa Saudia Abdulaziz Bin Turki alisema, “Mbingu ndio kikomo linapokuja suala la kuwa mwenyeji wa hafla za michezo.” [1] Maafisa wa Saudia pia wamependekeza kuandaa Kombe la Dunia la FIFA kila miaka miwili katika nchi hiyo ya Kifalme. [2]

Kasumba ya Michezo?

Vyombo vya upashaji habari vya Magharibi na makundi ya haki za binaadamu wameishutumu Saudi Arabia kwa kutumia michezo kupindisha sifa yake mbaya ya haki za binadamu. Mauwaji ya kutisha ya mwandishi habari Jamal Khashoggi yamemuaibisha Mfalme Mtarajiwa wa Saudia na hapana shaka kuwa yupo kwenye kampeni ya kuboresha sura yake kwa ummah. Lakini sifa ya Saudi Arabia imekuwa ya utatanishi hata kabla ya mauwaji ya Jamal Khashoggi. Saudi Arabia imekuwa kwa muda mrefu ikiangaliwa na dunia kuwa ipo nyuma, nchi ya wahafidhina, wakandamizaji wa wanawake, waungaji mkono wa ugaidi pamoja na kueneza Uwahabi duniani kote kwa miongo kadhaa. Shutma dhidi ya Saudi Arabia sio jambo jipya na madai mengi yao ni ya kipindi kirefu nyuma na ni zaidi ya haki za binaadamu.

Uwekezaji mwingi wa michezo wa Saudi Arabia, ikiwemo ligi ya mchezo wa Gofu (LIV Golf league), unagharamiwa kupitia Hazina ya Huru ya Uwekezaji (Sovereign Investment Fund), iliyoanzishwa mnamo 1971, na inamiliki rasilimali za dolari bilioni 480. Uwekezaji wake mkubwa sio michezo, bali unajumuisha Benki ya Taifa ya Saudia na Kampuni ya Simu ya Saudia. Hazina hii pia inasimamia mradi kubwa wa maendeleo wa Ruwaza ya 2030, ambapo katikati yake ni mradi wa NEOM. Uwekezaji wa Saudia katika LIV Golf, wenye thamani ya dolari bilioni 2 ni sehemu ya kampeni ya Ruwaza ya 2030. Makampuni ya Magharibi, jumuiya, wadhamini na ligi za michezo zingependa kuwa na rasilimali kama hizo. Ubishani unaozunguka LIV Golf zaidi unaegemea juu ya ukweli kuwa wana rasilimali kubwa sana ya kifedha inayowezesha kuwashinda wapinzani wao katika kuwavutia wachezaji bora zaidi duniani. Katika kuiweka LIV kwenye maono, Phil Mickelson alishinda dolari milioni 94 kama zawadi kwa jitihada zake za miongo miwili za PGA. Inaarifiwa kuwa analipwa hadi dolari milioni 200 kwa kujiunga na LIV! [3]

Wakati gofu ikiwa ni mchezo maarufu katika nchi zilizoendelea, kinyume na mpira wa miguu, unaoonekana kuwa ni mchezo wa anasa unaohusiana na matajiri. Kikwazo halisi cha LIV Golf ni katika uwezo wake wa kuvuruga hali ilivyo kwenye sekta ya mchezo huu. Katika kujaribu kuvutia wachezaji bora zaidi duniani pamoja na wapenzi wao na jamii, LIV Golf inahatarisha kuuhodhi mchezo huu. Huku Saudia na mataifa shindani ya Ghuba yakilenga mpira wa miguu, burudani na michezo mengine, yanahatarisha hali ya sasa ya ulimwengu wa michezo. Saudi Arabia, Qatar na Imarati wanaunda upya michezo ya kimataifa na wanaelekea kuhodhi hali ya ushindani wa wachezaji wa kulipwa.

Ubishani huu juu ya uwekezaji katika michezo unaonyesha kuwa mataifa ya Ghuba yana rasilimali za kutosha kuhodhi sekta za kilimwengu ili kujenga taswira zao na kuhifadhi tawala zao. Matumizi haya ya utawala, hata hivyo hayapo wakati yanapokuja masuala ya kisiasa au kuulinda Ummah kote duniani. Makampuni ya Magharibi yanalalamika wakati mataifa ya Ghuba yakitumia utajiri wao, kwa kuwa wao hawawezi kushindana na utajiri wao, lakini mkakati huu hautumiki dhidi ya Magharibi kwenye masuala mengine. Kile kinachooneshwa na kipindi hiki ni kuwa inapokuwa ni suala la kuhami falme na tawala zao, watatumia mali za ummah na kushindana na taasisi za Magharibi. Linapokuja suala la siasa na masuala kama ya Syria, Palestina na mengineyo, watawala wawa hawa watatumia mipango ya kisiasa ya Wamagharibi na kuwa kama vyombo vya kuwatumikia.  

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Adnan Khan

[1]See,https://twitter.com/danroan/status/1202698026906791936

[2] Saudi Arabia’s proposal for FIFA World Cup every two years gaining support in Asia | Arab News

[3] Phil Mickelson Just Took a $200 Million Gamble to Try and Revolutionize Golf (sportscasting.com)

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu