Alhamisi, 23 Rajab 1446 | 2025/01/23
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Uislamu na Ubaguzi wa Rangi

Uislamu ni Ujumbe kwa wanaadamu wote. Unawalingania watu wote, bila kuzingatia rangi. Uislamu haukuja kwa jamii, kabila, au taifa moja, au kwa watu maalum wanaoishi katika zama au eneo maalum. Hivyo, wakati Uislamu ulipoenea kutoka Uarabuni kuelekea sehemu nyengine za dunia, kutokea Uchina kuelekea Uhispania, uliweza kuyeyusha tofauti baina ya watu waliokuwapo kabla ya Uislamu. Uliwaleta watu pamoja kutoka asili zote kuwa ni taifa moja. Ulileta udugu baina ya watu kwa namna ambayo umeenea kwenye vipengele vyote vya maisha, kutoka kuabudu hadi kwenye ndoa na shughuli za kisiasa, Waislamu waliweza kukiuka mipaka ya kibaguzi iliyowekwa na mpango wa ulimwengu.

Njia ambazo Uislamu umeweza kuondosha nguvu ya dhulma ya ubaguzi kutoka katika jamii ni kwa kulielezea hili suala kupitia mafundisho yake ya kidini pamoja na nususi zake za kisharia. Kuhusiana na Itikadi ya Kiislamu, Muumba ndie Mwenye Mamlaka yote. Kwa hivyo, wanaadamu wote wanafungwa na kipimo kilichofunuliwa na Muumba, bila kuwekwa tofauti yoyote baina yao. Hii imepelekea kwa yule anaye beba Itikadi ya Kiislamu kuachana na tabia yake ya kujiweka yeye, kabila lake, au taifa lake kuwa na mamlaka juu ya wengine.

Mtume Muhammad (saw) amesema:

«أيها الناس، إن ربكم واحد، وإن أباكم واحد، كلكم لآدم، وآدم من تراب، إن أكرمكم عند الله أتقاكم، ليس لعربي فضل على أعجمي إلا بالتقوى»

“Enyi watu! Hakika Mola wenu ni mmoja, na baba yenu ni mmoja, nyote mnatokana na Adam, na Adam anatokana na mchanga. Aliye mbora wenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule anayemcha Mwenyezi Mungu zaidi. Muarabu hawi mbora juu ya Asiye Muarabu ila kwa ucha Mungu”

Pamoja na haya, nususi za kisheria za Kiislamu hazitofautishi baina ya wanaadamu kwa misingi ya kabila au utaifa. Uhifadhi wa maisha ya mtu, mali, heshima, nk. umeenezwa kwa raia wote wa Dola ya Kiislamu, Waislamu au wasio Waislamu. Hivyo, nidhamu ya kimahakama, kwa kuwa haikuweka suala la ukabila katika kesi zake za kisheria, huzuia kuibuka kwa ubaguzi wa rangi wa kitaasisi katika jamii.

Mwenyezi Mungu (swt) amesema:

[وَإِذَا حَكَمْتُم بَيْنَ النَّاسِ أَن تَحْكُمُوا بِالْعَدْلِ]

“Na mnapo hukumu baina ya watu, mhukumu kwa uadilifu.” [Surah Al-Nisa 4:58].

Haya ni maelezo jumla kwa watu wote, Waislamu na wasio Waislamu, Mweusi na Mweupe, Muarabu na asie Muarabu sawa sawa. 

Zaidi ya hayo, Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema:

«وَلَكِنَّ الْبَيِّنَةَ عَلَى الْمُدَّعِي وَالْيَمِينَ عَلَى مَنْ أَنْكَرَ»

“Lakini, dhima ya kuthibitisha ni juu ya mdai, na kiapo ni juu ya anayekanusha.” [Al-Bayhaqi]

Hii pia ni jumla na inahusu Waislamu na wasio Waislamu, Mweusi na Mweupe, Muarabu na asie Muarabu sawa sawa.

«أَنَّهُ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَضَى أَنْ يَجْلِسَ الْخَصْمَانِ بَيْنَ يَدَيْ الْقَاضِي»

“Mtume wa Mwenyezi Mungu amehukumu kuwa pande mbili zinazo zozana zikae mbele ya kadhi” [Al-Hakim].

Hii pia ni jumla na inajumuisha pande mbili zozote zinazo zozana, Waislamu na wasio Waislamu, Mweusi na Mweupe, Muarabu na asie Muarabu sawa sawa.

Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema:

«الإِمَامُ رَاعٍ وَمَسْئُولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ»

“Imamu ni mchunga na ataulizwa juu ya raia wake.” [Imewafikiwa na Muslim na Bukhari].

Neno “raia” ni jumla na linakusanya raia wote, Waislamu na wasio Waislamu, Mweusi na Mweupe, Muarabu na asie Muarabu sawa sawa. Hivyo hivyo, dalili zote jumla zinazo husiana na uraia katika Shariah ya Kiislamu zinaonyesha kuwa ni haram kutofautisha baina ya Muislamu na asie Muislamu, baina ya Muarabu na asie Muarabu au baina ya mweupe na mweusi. Bali, watu wote wenye uraia wa dola ya Kiislamu wanapaswa kuamiliwa kwa usawa, bila ya ubaguzi baina yao ima na mtawala, kwa upande wa kusimamia mambo yao na kuhifadhi maisha yao, heshima zao na mali zao, au na hakimu kwa upande wa usawa na haki.

Uislamu ni mfumo wa mwanzo kuwaleta watu pamoja kutoka makabila mbali mbali chini ya taifa moja. Kwa hakika, hadi hii leo, Uislamu ni mfumo pekee ambao umekamilisha mafanikio hayo makubwa. Ni hivi karibuni tu kutokana na kukoloniwa kithaqafa kwa ulimwengu wa Waislamu na Wamagharibi, Waislamu wameanza kuwa na muelekeo wa kikabila na utaifa.

Thaqafa ya Kimagharibi, kwa upande mwengine, imebeba fikra ya ukabila kutoka historia yao ya awali, kama ilivyokuwa wakati wa Wagiriki na Warumi. Wakati Wamagharibi walipouchukuwa mfumo wa Kirasilimali, hawakuweza kuiondoa fikra hii kutoka katika akili za waumini wake. Bali, thaqafa ya kiuchumi wa kirasilimali imechochea fikra ya ukabila kwa kuiruhusu kutumika kama ni sababu ya kunyonya nguvu za wageni, yaani taabu ya Waafrika katika mabara ya Amerika. Hivyo, sio ajabu kuwa Ubaguzi wa Rangi bado ni wenye kutapakaa katika nchi za Magharibi, hasa katika jamii zilizobobea kwenye urasilimali kama Amerika na Uingereza. Hata Thurgood Marshall, aliyefanikiwa kuchaguliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Amerika, alibaguliwa na hakukubaliwa na tabaka la wenye fursa. Ushahidi wake mwenyewe ni kuwa “Vilabu hapa katika mji huu [Washington D.C.], vinawaalika kila mtu isipokuwa mimi” (New York Yimes, 1/27/93), ni mfano wa wazi kwa mizizi iliokita ya ubaguzi wa rangi katika Magharibi.      

Pamoja na muelekeo wa kibaguzi katika fikra za Wamagharibi, Ubaguzi pia umerasimishwa katika nchi za Magharibi. Katiba ya Amerika imeweka misingi wa kisheria ya kibaguzi katika kifungu chake cha tatu ya tano, ambapo watu wa rangi (wasio wazungu) wanazingatiwa kuwa ni 3/5 ya mwanaadamu. Japokuwa maelezo hayo baadaye yalifanyiwa marekebisho, iliufanya ubaguzi wa rangi kuwa ni kitangulizi katika taasisi ya Amerika. Hata baada ya miaka ya mapambano, umwagaji damu, maandamano ya Haki za Binaadamu na matembezi, mauwaji, na majopo kazi kwa ajili ya kushughulikia ubaguzi wa rangi, jamii ya Amerika ingali inasumbuliwa na ubaguzi wa rangi. Hata wakati mgombea mweusi, kama Jesse Jackson, alipogombania uraisi, tunaona kuwa ilifanyika tu kwa sababu, mtu wa tabaka la juu Richard Nixon na chama chake, waligharamia kampeni yake ili kuzigawa kura za watu weusi kwa maslahi ya chama cha Republican.  Kesi za Rodney King na O.J. Simpson ni mifano ilioenea ya vipi ubaguzi wa rangi ulivyojikita ndani ya jamii. Suala muhimu zaidi katika kesi zote mbili hizi limekuwa ni kabila, na suala la kutoaminiana baina ya weupe na weusi limekuwa mbele wazi wazi. Mauwaji ya karibuni ya Ahmaud Arbery, Yasin Muhammad na George Floyd yameonyesha ukatili uliorasimishwa wa polisi dhidi ya raia Wamarekani weusi. Maisha ya Waafrika yamefungwa na makundi yaliojipanga ya wazungu wanaowatiisha kwa namna zote za kuwalazimisha kuvumilia matendo ya kudhalilisha na mazingira… kuyaongoza maisha yao ya jumla na ya kibinafsi kana kwamba hawakuwa wenye kuaminika na wasio na maadili ya uadilifu. Miaka mia moja iliopita haikuwa na mabadiliko katika mitazamo au viwango vya ukatili wa polisi, kuelekea sehemu hii ya jamii ya Waamerika… wala kutokea mabadiliko yoyote ya kudumu katika maadili ya kijamii katika upande wa ukabila na rangi, licha ya Amerika kupigia debe uhuru na haki za wachache, ndani ya nchi na hata kupitia mtutu wa bunduki.

Janga la ubaguzi wa rangi ambalo nchi za Magharibi inakabiliana nalo ni dhahiri kuwa linatokana na itikadi yake na katika taasisi zake. Ubaguzi wa rangi hauibuki kutokana na maumbile ya mwanaadamu bali unamea katika shakhsia ya mtu binafsi kutokana na thaqafa (utamaduni) anayoibeba. Hivyo, ili kujivua kutokana na ubaguzi wa rangi hatuna budi kutathmini upya thaqafa na mfumo ambao tunaubeba. Uislamu ndio mfumo pekee ambao umelielezea suala hili kwa namna ambayo hujenga shakhsia ambazo zinayayusha tofauti baina ya watu kuliko kujenga vizuizi. Ndio mbadala pekee uliopo kwetu.

    [يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُم مِّن ذَكَرٍ وَأُنثَى وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوبًا وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّهِ أَتْقَاكُمْ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ]

 “Enyi watu! Hakika sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mcha Mungu zaidi  katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari.”  [Surah Al-Hujurat: 13]

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Hameed Bin Ahmad

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu