- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Jibu la Swali
Hakuna Usalimishaji wa Gari ila Baada ya Kupokea Malipo Kamili
Kwa: Mahmoud Natour
(Imetafsiriwa)
Swali:
Assalamu alaykum wa rahmatullah wa barakatuhu,
Swali langu kwako, sheikh wangu, ni kuwa wauzaji magari na maonyesho ya magari wanapomuuzia mteja gari kwa malipo ya polepole, hawalisalimishi hadi hundi ya mwisho ya malipo. Je, inaruhusiwa kununua kwa njia hii?
Jibu:
Wa alaykum salaam wa rahmatullah wa barakatuhu,
Tayari tulishawahi kutoa jibu la ufafanuzi juu ya mada hii mnamo 24/5/2015, na inaonekana bado hujaliona, hivyo nalieleza tena kwako:
Suala hili linajulikana katika Fiqh kama "Kuizuia Bidhaa (kama Rehani) kwa Bei Yake" yaani kwamba bidhaa yenye kuuzwa itawekwa kama rehani na muuzaji hadi mnunuzi alipe bei yake. Hali hii haitokei endapo muuzaji na mnunuzi ni watu wenye sifa ambayo Mtume (saw) ameisifia katika Hadith iliyo pokewa na Bukhari kutoka kwa Jabir ibn Abdullah (ra):
«رَحِمَ اللَّهُ رَجُلًا سَمْحًا إِذَا بَاعَ، وَإِذَا اشْتَرَى، وَإِذَا اقْتَضَى»
“Mwenyezi Mungu anamrehemu mtu mwenye tabia nzuri anapouza, na anaponunua, na anapokopa”.
Huku wakati mwengine wakitofautiana kuhusu kupokea bidhaa kwanza au malipo kwanza, na muuzaji huenda akaizuia bidhaa kama rehani hadi apokee bei yake, hivyo kupelekea kutokea kwa hali hii. Wanazuoni wa kifiqh (Fuqaha) wametofautiana kuhusiana na suala hili, baadhi wanaliruhusu katika baadhi ya hali na kuharamisha katika hali nyenginezo… na kadhalika.
Baada ya kulitafiti suala hili mtazamo wangu umeegemea katika yafuatayo:
Kwanza: Aina ya bidhaa
1. Ile Bidhaa inayoweza kuhesabiwa, kupimwa, au kupandwa… nk, mithili ya mauzo ya mchele, pamba, nguo… nk.
2. Ile Bidhaa isiyoweza kuhesabiwa, kupimwa… nk, mithili ya kuuza gari, nyumba, au mnyama… nk.
Pili: Bei ya Mauzo
1. Malipo ya moja kwa moja yaani kwa pesa taslimu, kama kununua bidhaa kwa kwa elfu kumi pesa taslimu hapo kwa hapo.
2. Malipo ya mbeleni kwa muda maalumu, kama kununua bidhaa kwa elfu kumi lakini zitalipwa baada ya mwaka mmoja.
3. Kwamba baadhi ya malipo yatalipwa hapo hapo na sehemu iliyo bakia kulipwa mbeleni, kama kununua bidhaa kwa malipo ya kuanzia ya elfu tano, na elfu tano zilizo bakia kulipwa baada ya mwaka mmoja kwa mfano, au kulipwa kwa vigawanyo vya kila mwezi.
Tatu: Hukmu ya Shariah hutofautika kulingana na jinsi kadhia hizo za juu zinavyo tofautiana:
Hali ya kwanza: Bidhaa ambayo haihesabiki wala kupimika… kama kuuza nyumba au gari au mnyama:
1. Malipo ya moja kwa moja, kama kununua gari kwa elfu kumi pesa taslimu, na ambapo imenakiliwa katika mkataba
Katika hali hii, muuzaji aweza kuizuia bidhaa, ambayo itabakia naye kama rehani hadi malipo hayo ya moja kwa moja yalipwe kwa mujibu wa mkataba huo. Dalili ya hili ni Hadith iliyosimuliwa na Tirmidhi ambayo imeorodheshwa kama Hasan Sahih. Kutoka kwa Abi Umamah, amesema: Nilimsikia Mtume (saw) akisema katika hotuba katika Hijja ya Kuaga: «العَارِيَةُ مُؤَدَّاةٌ، وَالزَّعِيمُ غَارِمٌ، وَالدَّيْنُ مَقْضِيٌّ» “Kilicho azimwa hurudishwa, na mdhamini ni mwenye dhima, na deni hulipwa.”
Za'eem: mdhamini, Gharim: ana dhima, na dalili yake ni maneno yake (saw):
«وَالدَّيْنُ مَقْضِيٌّ» “na deni hulipwa”. Ikiwa mnunuzi atapokea bidhaa kabla ya kulipia thamani yake, itakuwa ni ununuzi wa mkopo. Na «وَالدَّيْنُ مَقْضِيٌّ» “na deni hulipwa” yaani kipaumbele ni kulipa deni maadamu ununuzi ni wa pesa taslimu, kwa maana nyengine ni kulipa bei kwanza maadamu bei hiyo katika mkataba huo ni pesa taslimu hapo kwa hapo. Al-Kasaani asema katika Bada'I As-San'I akisherehesha juu ya Hadith yake (saw) «وَالدَّيْنُ مَقْضِيٌّ» “na deni hulipwa”. Mtume (saw) alilisifu deni hulipwa kwa sifa jumla au Mutlaq, ikiwa deni hilo litalipwa mbeleni kwa ajili ya kukabidhi bidhaa basi deni hilo halijalipwa). Hii ni kinyume na andiko (nas).
Hivyo basi inaruhusiwa kwa muuzaji kuizuia bidhaa hadi mnunuzi alipe bei yake, na hivyo hakutakuwa na deni, na hili linakubaliana na mkataba kwa sababu uuzaji haukuwa wa deni bali wa pesa taslimu.
2. Bei itakayo lipwa mbeleni, katika hali ya kununua gari kwa elfu kumi ambazo zitalipwa baada ya mwaka mmoja, katika hali hii hairuhusiwi kuzuia bidhaa hadi malipo ya bei yakamilike kwa sababu bei ni ya mbeleni katika mkataba kupitia idhini ya muuzaji. Haruhusiwi kuizuia bidhaa ili kuhakikisha malipo ya bei maadamu tayari ashaiuza kwa malipo ya mbeleni, hivyo tayari ashabatilisha haki yake ya kuizuia bidhaa hiyo, na hivyo basi hairuhusiwi kwake kuizuia bidhaa hiyo, bali anapaswa kuikabidhi kwa mnunuzi.
3. Bei yaweza kuwa ya hapo kwa hapo na pia ya mbeleni, kama kununua gari kwa malipo ya kuanzia ya elfu tano yanayolipwa kwa pesa taslimu, na elfu tano nyingine zote zitalipwa baada ya mwaka mmoja, au zitalipwa baadaye kwa malipo ya kidogo kidogo.
Katika hali hii inaruhusiwa kwa muuzaji kuizuia bidhaa hadi malipo ya hapo kwa hapo yapokewe, baada ya hapo haruhusiwi kuizuia bidhaa hiyo, ili kukamilishwa kwa malipo ya mbeleni, hii ni kwa sababu ya nukta 1 na 2 tulizozitaja.
Kwa kutamatisha, inaruhusiwa kwa muuzaji kuizuia bidhaa kwa ajili ya malipo ya hapo kwa hapo, yaani ikiwa mkataba unaeleza kuwa malipo ni ya moja kwa moja na hapo kwa hapo, inaruhusiwa kwa muuzaji kuizuia bidhaa hadi mnunuzi alipe gharama ya hapo kwa hapo kwa mujibu mkataba.
Sio sahihi kuuliza vipi mnunuzi ataizuia bidhaa yake kabla ya kuipokea, yaani kabla aimiliki. Hii ni kwa sababu kuizuia bidhaa kama rehani hairuhusiwi isipokuwa ikiwa inaruhusiwa kuuzwa. Kwa kuwa bidhaa iliyo nunuliwa hairuhusiwi kuuzwa isipokuwa baada ya kuipokea kwa mujibu wa Hadith ya Mtume (saw) iliyo simuliwa na Al-Bayhaqi, kutoka kwa Ibn Abbas aliyesema:
Mtume (saw) alimwambia I'taab bin Usaid:
«إني قد بعثتك إلى أهل الله، وأهل مكة فانههم عن بيع ما لم يقبضوا»
“Hakika mimi nimekutuma kwa watu wa Mwenyezi Mungu, na watu wa Makkah, basi wakataze kutokana na uuzaji wa kile ambacho hawajakipokea”
Na Hadith ambayo imesimuliwa na At-Tabarani kutoka kwa Hakeem bin Hizam kuwa amesema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu mimi nauza kwa kutumia miamala tofauti tofauti, ni kipi ninacho ruhusiwa na kipi siruhusiwi? Yeye (saw) akasema:
«لَا تَبِيعَنَّ مَا لَمْ تَقْبِضْ»
“Usiuze kile ambacho hujakipokea”.
Hadith hizi zaeleza wazi wazi uharamu wa kuuza kile ambacho hakijapokelewa, ni vipi basi kwa bidhaa kuwekwa rehani kabla haijapokelewa?
Hii sio sahihi kwa sababu Hadith hizi mbili ni za bidhaa zinazo hesabika na kupimika… lakini ikiwa bidhaa ni aina nyinginezo kama mfano nyumba au mnyama, basi inaruhusiwa kuiuza kabla ya kuipokea kutokana na Hadith ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) iliyo simuliwa na Bukhari kutoka kwa Ibn Umar (ra), aliyesema,
فَكُنْتُ عَلَى بَكْرٍ صَعْبٍ لِعُمَرَ، فَكَانَ يَغْلِبُنِي، فَيَتَقَدَّمُ أَمَامَ القَوْمِ، فَيَزْجُرُهُ عُمَرُ وَيَرُدُّهُ، ثُمَّ يَتَقَدَّمُ، فَيَزْجُرُهُ عُمَرُ وَيَرُدُّهُ، فَقَالَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم لِعُمَرَ: «بِعْنِيهِ»، قَالَ: هُوَ لَكَ يَا رَسُولَ اللَّهِ، قَالَ: «بِعْنِيهِ» فَبَاعَهُ مِنْ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم، فَقَالَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم: «هُوَ لَكَ يَا عَبْدَ اللَّهِ بْنَ عُمَرَ، تَصْنَعُ بِهِ مَا شِئْتَ»
“Tulikuwa tunasafiri na Mtume (saw), mimi nilikuwa nikiendesha ngamia mkorofi wa Umar, sikuweza kumdhibiti, akawa akipita mbele ya watu, kisha Umar akawa anamkaripia na kumrudisha, kisha akawa anarudia tena, basi Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akamwambia Umar: 'Niuzie mimi'. Hivyo Umar akasema, 'Ni wako ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu', nikamwambia 'niuzie mimi' Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akamuuzia. Kisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akasema: 'Huyo ni wako ewe Abdullah bin Umar, mfanye unavyotaka."
Kitendo hiki katika bidhaa ilikuwa ni zawadi kabla ya kuipokea, kinaonyesha umilikaji kamili wa bidhaa kabla ya kuipokea, na kinaonyesha kuwa kuiuza inaruhusiwa kwa sababu ilimilikiwa na muuzaji wake.
Hivyo basi inaruhusiwa kuizuia bidhaa kama rehani kabla ya kuipokea (malipo ya thamani), maadamu inaruhusiwa kuuzwa kabla ya kupokelewa, lakini hili ni tu ikiwa bidhaa hiyo si katika zenye kuhesabika na kupimika kama nyumba, gari, mnyama, na kadhalika. Katika hali ya kutekeleza mkataba wa ununuzi wa malipo ya hapo kwa hapo au kuna kiwango fulani cha kulipwa hapo kwa hapo, basi inaruhusiwa kuizuia bidhaa kama rehani hadi bei ipokelewe, hadi malipo ya hapo kwa hapo au kiwango chote cha malipo ya hapo kwa hapo kilipwe.
Hali ya pili: bidhaa ni katika kile kigawanyo cha zinazo hesabika au kupimika, kama kununua viwango vya mchele, pamba, au nguo, katika hali hii, ni haramu kuizuia bidhaa kwa ajili ya bei yake, namna yatakavyo kuwa maumbile ya malipo ya bei iwe: malipo ya hapo kwa hapo au ya kuakhirishwa, au ya mbeleni kwa kiwango chote au kidogo kidogo:
Ikiwa bei ni malipo ya hapo kwa hapo, ni haramu kuizuia bidhaa kama tulivyo fafanua juu.
Ikiwa bei inapaswa kulipwa mapema, hairuhusiwi kuizuia bidhaa, yaani kuizuia kama rehani, kwa sababu hairuhusiwi kuzuia bidhaa zinazo hesabika au kupimika kama dhamana kabla ya kupokea bei, kwa mujibu wa Hadith za Mtume (saw) zilizo tajwa juu. Katika hali ya malipo ya hapo kwa hapo, muuzaji ni lazima akabiliane nayo katika njia mbili:
Ima aziuze bidhaa kwa malipo ya mapema na ampe mnunuzi na awe na subra na mnunuzi huyo, iwe atamlipa bei kwa haraka au baada ya muda pasi na kuzizuia bidhaa kama rehani… au kutoziuza bidhaa hizo, yaani pasi na rehani yoyote kwa bidhaa hizo.
Hivyo basi ikiwa bidhaa zinazoweza kuhesabika na kupimika zitauzwa kwa malipo ya hapo kwa hapo au kwa malipo ya mbeleni, hairuhusiwi kwa muuzaji kuzizuia bidhaa hizo kama rehani kwake hadi bei ilipwe.
Hili ndilo ambalo ninalo dhani kuwa lenye nguvu zaidi na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Zaidi Mwingi wa Hekima.
Ndugu yenu,
Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
01 Dhul Hijjah 1441 H
22/07/2020 M