Ijumaa, 20 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Jibu la Swali
Waqf katika Ardhi ya Kharaj
Kwa: Yusuf Abu Islam
(Imetafsiriwa)

Swali:

Mwenyezi Mungu akubariki na atunufaishe kwa elimu yako. Kwa upole sheikh wetu nina maswali mawili: La kwanza: Ni ipi dalili ambayo katika waqf, inatakikana kwa mtu anayeweka Waqf awe ndiye mmiliki wa kitu chenyewe kinacho wekwa waqf? Pili: Je, kuna hukmu zozote za sheria kando na Waqf ambazo zinatofautisha maumbile ya ardhi ya 'Ushri na ardhi ya Kharaj? Mwenyezi Mungu atubariki na chama chetu kwa maisha yako na afya yako, na twamuomba Mwenyezi Mungu atupe ufunguzi mikononi mwako.  

Jibu:

Wa Alaikum Assalam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,

Kwanza: Ama kadhia ya Waqf katika ardhi ya Kharaj, kuna rai tofauti miongoni mwa wanazuoni:

1- Baadhi yao wanaruhusu Waqf uliofanywa juu ya ardhi katika majumba au mimea, hivyo ikiwa mtu atajenga shule juu ya ardhi ya Kharaj anayoimiliki, aweza kuifanya Waqf kwa wanafunzi, au ikiwa amepanda miti ya zaituni kwa mfano, aweza kuyafanya matunda yake Waqf kwa masikini na mafukara kwa sharti kuwa Waqf huu ni wa kudumu:

Jopo la Fiqh la Kuwait linaeleza:

[Ibn Abidin ameripoti kutoka kwa Al-Khassaf kuwa amesema: (Waqf wa maduka katika masoko unaruhusiwa ikiwa ardhi iko mikononi mwa wale walioyajenga kupitia kukodi, na kwamba Sultan (mtu aliye na mamlaka) hatawatoa kutoka kwayo, na tumeyaona mikononi mwa wamiliki walioyajenga na wakayarithi na kuyagawanya miongoni mwao wenyewe. Sultan hatawaingilia wala kuwasumbua, lakini yatakuwa na mapato ambayo atachukua kutoka kwao, na yalirithiwa kutoka kwa mababa na mababu, na miaka imepita na ingali mikononi mwao wakiuziana wao kwa wao, wakikodishiana wao kwa wao, na yalijumuishwa ndani ya wasia wao. Wanayavunja majengo hayo, na kuyajenga upya, na kujenga mengineyo, hivyo basi vilevile Waqf huu unaruhusiwa). Ibn Abidin asema: Ameupasisha katika Al-Fath na sababu ni kuendelea kwa muamala.   

Na ikiwa kile alichokiweka juu ya ardhi ni shamba, basi hukmu juu ya Waqf wake itakuwa ni hukmu ya jengo. Lakini ikiwa kile alicho nacho juu ya ardhi ni ukusanyaji mchanga tu au utengenezaji mbolea, basi si halali kuifanya kuwa Waqf.]   

2- Wengine wakaruhusu Waqf juu ya manufaa hata kama ni manufaa ya muda tu. Hivyo, ikiwa mtu atapangisha nyumba kwa muda wa mwaka mmoja, aweza kuifanya nyumba hii Waqf kwa wale wanaohitaji kwa muda huo wa mwaka mmoja uliotajwa katika mkataba wa upangaji, au aweza kukodisha shamba kwa muda hadi mavuno na kulifanya kuwa Waqf kwa mafukara kwa muda huo wa hiyo mimea kwa mujibu wa mkataba huo wa ukodishaji, ikimaanisha kuwa wanaruhusu Waqf juu ya manufaa pasi na sharti la daima bali yaweza kuwa maslahi ya muda.   

Kwa mujibu wa Jopo la Fiqh la Kuwait: rai ya jamhuri ya wanavyuoni wa Kihanafi, Shafi na Hanbali ni kuruhusiwa kwa Waqf juu ya manufaa kwa sababu wanaweka sharti kuwa mali iliyo tolewa kama Waqf inapaswa kuwa kitu ambacho kwacho manufaa yanaweza kuvuliwa huku dhati asili ya kitu hicho ikibakia vilevile wanaweka sharti la kuendelea kwa Waqf (1) rai ya wanavyuoni wa kifiqhi wa dhehebu la Malik ni kuruhusiwa kwa Waqf juu ya manufaa, hivyo ikiwa mtu atapangisha nyumba kwa muda fulani, inaruhusiwa kwake kuyafanya Waqf manufaa ya nyumba hiyo katika kipindi hicho, na Waqf huo utamalizika mwisho wa muda wa upangishaji, kwa sababu kwa mujibu wao kuendelea kwa Waqf sio sharti (2) (1) Mughni, Al-Muhtaj 2/377, Sharh muntaha al-irdat 2/492, Al-Bada'I 6/220, Hashiya ibn 'Abidin 3/359 ... (2) Hashiyat Al-Dusuqi 'ala Al-sharh Al-kabir 4/76, na Al-Sharh Al-Sagheer 2/298 T. Al-Halabi.] Mwisho  

Pili: Kuna rai nzito kuwa Waqf hauruhusiwi isipokuwa shingo (raqabah) ya ardhi iwe inamilikiwa kwa kudumu na huyo mtu anaye weka Waqf (Waqif). Na hii ndio tunayoiona kuwa na nguvu katika jambo hili kwa mujibu wa dalili sahihi katika jambo hili, na huu hapa ni ufafanuzi wake: 

1- Yafuatayo yameelezwa katika ufafanuzi wa Kipengee cha 133 cha Katiba Kielelezo, Sehemu ya 2; (Inawezekana kufanya biashara na kurithi ardhi ya 'Ushri na Kharaj kutoka kwa wamiliki wake, kwa sababu ni umilikaji sahihi kutoka kwa mmiliki wake, na hivyo kanuni zote kuhusiana na umilikaji hutekelezeka juu yake. Kuhusiana na ardhi ya 'Ushri hili liko wazi, na ama ardhi ya Kharaj, umilikaji wake ni mithili ya umilikaji wa ardhi ya 'Ushri pasi na tofauti yoyote kati yazo kutoka upande wa umilikaji isipokuwa katika kadhia mbili: ya kwanza ni kuhusiana na kile kinacho milikiwa na pili, kuhusiana na uwajibu juu ya ardhi hiyo.

Ama kadhia ya kile kinacho milikiwa, mmiliki wa ardhi ya 'Ushri awe anamiliki ardhi hiyo yeye mwenyewe na mazao yake, huku mmiliki wa ardhi ya Kharaj awe anamiliki mazao yake pekee. Hivyo basi, ikiwa mmiliki wa ardhi ya 'Ushri anataka kuitoa kama sadaka, anaruhusiwa kufanya hivyo wakati wowote anaotaka. Lakini, mmiliki wa ardhi ya Kharaj hawezi kufanya hivyo kwani ili kutoa kitu chochote kama Waqf, sharti ni kuwa mtu anayetoa awe anaimiliki yeye mwenyewe, na mmiliki wa ardhi ya Kharaj haimiliki ardhi hiyo yeye binafsi, bali anamiliki mazao yake, kwani shingo ya ardhi hiyo humilikiwa na Bait al-Mal.

Ama kadhia ya lile lililo wajibu juu ya ardhi, asilimia 10 au 5 hutekelezwa katika ardhi ya 'Ushri; kwa maana nyingine, Zakah juu ya kile ambacho kimezalishwa kihakika na ardhi hiyo ikiwa kinafika kiwango stahiki cha Nisab. Kodi ya Kharaj hutozwa juu ya ardhi ya Kharaj; kwa maana nyingine ni kuwa, ni kiwango cha kila mwaka kilicho fafanuliwa na dola…) Mwisho. Kama unavyoona, Waqf hauruhusiwi katika ardhi ya Kharaj kwa sababu Waqf unahitaji umiliki wa shingo yenyewe ya ardhi, na shingo (raqabah) ya ardhi ya Kharaj humilikiwa na Bait al-Mal, hivyo mmiliki haimiliki rasilimili yenyewe, bali humiliki tu mazao yake.

2- Nyuma tulitoa Jibu la Swali juu ya kadhia hii, mnamo 13/2/2019, ambalo huenda ukawa ndilo unalokusudia katika swali lako, linalosema: (… Kwa mfano, Waqf huhitaji umilikaji wa rasilimali inayotolewa Waqf, Kutokana na haya, ikiwa mmiliki wa ardhi ya 'Ushri anataka kuitoa kama sadaka, anaruhusiwa kufanya hivyo wakati wowote anaotaka. Lakini, mmiliki wa ardhi ya Kharaj hawezi kufanya hivyo, kwani ili kutoa chochote kama Waqf, ni sharti kuwa mtu anayetoa awe anakimiliki kitu chenyewe, na mmiliki wa ardhi ya Kharaj hamiliki ardhi yenyewe, bali humiliki mazao yake tu, kwani shingo ya ardhi hiyo humilikiwa na Bait al-Mal.) Mwisho.

3- Ama kuhusu dalili zinazo husiana na umilikaji wa shingo (raqabah) ya ardhi (mali asili ambayo kwayo manufaa huvuliwa) kama sharti la uhalali wa Waqf, inajumuisha yafuatayo:

- Al-Bukhari amesimulia katika Sahih yake kutoka kwa Ibn 'Umar: ('Umar alipata ardhi katika Khaybar. Akaja kwa Mtume (saw) na kutafuta ushauri wake kuhusiana nayo. 'Umar akamwambia Mtume (saw): "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, nimepata ardhi kutoka Khaybar, na sina chochote chenye thamani zaidi kwangu kuliko ardhi hiyo. Je, waniamrisha niifanye nini?" Mtume (saw) akasema: «إِنْ شِئْتَ حَبَسْتَ أَصْلَهَا وَتَصَدَّقْتَ بِهَا» "Ukipenda ifunge asili ya ardhi hiyo na uitoe sadaka" (kwa sharti kuwa ardhi hiyo asili haitauzwa wala kupeanwa kama zawadi, wala kama wasia, (na mazao yake) yatatumiwa kwa ajili ya masikini, jamaa wa karibu, ukombozi wa watumwa, Jihad, na kwa wageni na wasafiri, na msimamizi wake aweza kula mapato yake kwa njia stahiki inayohalisi, na pia aweza kuwalisha marafiki zake pasi na kulenga kujitajirisha kwayo. Nilimsimulia Hadith hii ibn Sireen na akasema: pasi na kuihifadhi mali hii kwa mtazamo wa kuwa tajiri"). 

- Na al-Bukhari amesimulia katika Sahih yake kutoka kwa Ibn 'Umar (Katika uhai wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), 'Umar alitoa sadaka baadhi ya mali yake, shamba la mitende linaloitwa Thamgh. 'Umar akasema, "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw)! Niko na baadhi ya mali ambayo naithamini sana na nataka kuitoa sadaka." Mtume akasema,

«تَصَدَّقْ بِأَصْلِهِ لَا يُبَاعُ وَلَا يُوهَبُ وَلَا يُورَثُ وَلَكِنْ يُنْفَقُ ثَمَرُهُ» “Itoe sadaka (yaani kama waqf) kwa sharti kuwa asili ya ardhi hiyo kamwe haitauzwa wala kupeanwa kama zawadi, wala wasia, bali matunda yake ndio yatatolewa sadaka.” Hivyo basi, 'Umar akaitoa sadaka, na ilikuwa kwa ajili ya njia ya Mwenyezi Mungu, ukombozi wa watumwa, masikini, wageni, wasafiri, na jamaa wa karibu. Mtu anaye kaimu kama msimamizi wake aweza kula kutokana nayo kwa ustahiki na uadilifu, na aweza kumlisha rafiki kutokana nayo maadamu tu hatakuwa na nia ya kujitajirisha kupitia mapato yake.)

- Vilevile Muslim amesimulia katika Sahih yake kutoka kwa Ibn 'Umar akisema: (Umar alipata ardhi katika Khaybar, akaja kwa Mtume (saw) na kutafuta ushauri wake kuhusiana nayo. 'Umar akamwambia Mtume (saw): "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, nimepata ardhi kutoka Khaybar, na sina chochote chenye thamani zaidi kwangu kuliko ardhi hiyo. Je, waniamrisha niifanye nini?" Mtume (saw) akasema: «إِنْ شِئْتَ حَبَسْتَ أَصْلَهَا وَتَصَدَّقْتَ بِهَا» “Ukipenda ifunge asili ya ardhi hiyo na uitoe sadaka.” 'Umar akaitoa sadaka lakini asili yake haikupaswa kuuzwa wala kupeanwa kama zawadi, wala wasia.” Asema, "akaipeana kwa masikini kama sadaka, kwa jamaa wa karibu, kwa watumwa huru, na kwa wageni. Hakuna dhambi kwa yule anayeisimamia endapo atakula chochote kutokana nayo kwa njia inayohalisi, au ikiwa atawalisha rafiki zake na hata ficha bidhaa (kwa ajili yake binafsi). Yeye (msimulizi) asema: nilimsimulia Hadith hii Muhammad, lakini pindi nilipofika (katika maneno) "pasi na kujifichia (yeye mwenyewe) chochote kutokana nayo." Yeye (Muhammad' asema: "pasi na kuhifadhi mali hiyo kwa mtazamo wa kujitajirisha." Ibn 'Aun asema: Yule aliye soma kitabu hiki (kuhusu Waqf) aliniarifu kuwa ndani yake (maneno yake ni) "pasi na kuhifadhi mali hiyo kwa mtazamo wa kujitajirisha…".) 

Hivyo basi, Hadith za Mtume (saw) ziko wazi katika kueleza kuwa Waqf ni ufungaji (utengaji kando) wa asili ya umilikaji huku ikitolewa nafasi kwa manufaa yake pekee, na ufungaji wake unahitaji kuwa shingo (raqabah) ya mali hiyo yenye kutolewa Waqf iwe inamilikiwa na mtu anayeitenga kando yaani mtoaji Waqf (Waqif) kabla hajaitenga na kuitoa waqf kwa sababu mtu hawezi kutoa waqf mali ambayo haimiliki. Hivyo basi utengaji kando mali ni haki ya mmiliki wake pekee kwa sababu ni tasarufu ya shingo (raqabah) ya ardhi ya kitu. Hivyo, ikiwa shingo (raqabah) ya mali haiko katika milki ya mtu, vipi anaweza kutasarufu nayo kupitia kuitoa waqf? 'Umar bin Al-Khattab (ra) alikuwa ndiye mmiliki wa shingo (raqabah) ya ardhi ile ambayo Mtume (saw) alimwagiza kuitenga kando kama ilivyo katika Hadith hizo za juu, kwa sababu yeye (ra): "alipata ardhi katika Khaybar. Akaja kwa Mtume (saw) kutafuta ushauri wake kuhusiana nayo. 'Umar akamwambia Mtume (saw): "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, nimepata ardhi kutoka Khaybar, na sina chochote chenye thamani zaidi kwangu kuliko ardhi hiyo. Je, waniamrisha niifanye nini?" Yaani, yeye (ra) aliimiliki ardhi hiyo na ikawa ni ardhi yake, yaani alimiliki shingo yenyewe ya ardhi hiyo, kisha akaja akamuuliza Mtume (saw) kuhusu jinsi ya kuifanya.

Hivyo basi, ni wazi kutokana na Hadith hii inayo ashiria uhalali wa Waqf kuwa mtoaji Waqf ni lazima awe ndiye mmiliki wa kitu hicho chenyewe. Mtume (saw) asema kama ilivyo katika Hadith hizo za juu:

«إِنْ شِئْتَ حَبَسْتَ أَصْلَهَا...»، «تَصَدَّقْ بِأَصْلِهِ...»، «إِنْ شِئْتَ حَبَسْتَ أَصْلَهَا...»

“Ukipenda ifunge asili ya ardhi hiyo...”, “Na uitoe sadaka...”, “Ukipenda ifunge asili ya ardhi hiyo...”, na shingo ya ardhi ya Kharaj humilikiwa na Bait al-Mal ya Waislamu, hivyo shingo yake haimilikiwi na mwenye ardhi kwani mwenye ardhi humiliki tu manufaa yake, na kwa kuwa mwenye ardhi hamiliki shingo yake kwa kuwa ni milki ya Bait al-Mal, vipi basi ataweza kuifunga shingo yake?

4- Hii ndio rai tunayoiona kuwa yenye nguvu na kujifunga kwayo kutokana na kutekelezeka juu yake dalili ya kisheria: yaani, haiwezekani kutoa Waqf ardhi ya Kharaj, lakini inaruhusiwa kuiuza, kuitoa kama mchango, na kuitoa sadaka yenyewe au thamani yake na shughuli zote ambazo zinaruhusiwa kwa mujibu wa sheria, isipokuwa kama tulivyo sema kuitoa Waqf, ambayo inahitaji umilikaji wa shingo (raqabah) yenyewe, na shingo ya ardhi ya Kharaj inamilikiwa na Bait al-Mal.

Tatu: Ama swali lako (Je, kuna hukmu zozote za sheria kando na Waqf ambazo zinatofautisha maumbile ya ardhi ya 'Ushri na ardhi ya Kharaj?). Jibu lake ni kuwa hatujaona tofauti nyingine yoyote inayohusiana na maumbile ya ardhi ya Kharaj na ardhi ya 'Ushri isipokuwa katika vitu hivyo viwili vilivyo tajwa juu yaani lile ambalo ni wajibu juu ya ardhi ya 'Ushri la Zakah na juu ya ardhi ya Kharaj la kodi ya Kharaj, na kadhia ya pili ni kuruhusiwa Waqf katika ardhi ya 'Ushri na kutoruhusiwa Waqf katika ardhi ya Kharaj.

Hili ndilo la sahihi zaidi kwetu na ambalo ndilo tunalo jifunga nalo, na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi na Mwingi wa hekima.

Ndugu yenu,

Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

21 Rabii’ II 1441 H

Jumatano, 18/12/2019 M

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoAlhamisi, 02 Aprili 2020 20:27

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu