Mnamo Agosti 4, 2018, shirika la habari la BBC liliripoti juu ya mwanamke wa kwanza wa Kiislamu kulipishwa faini nchini Denmark kwa ajili ya kuvaa niqab hadharani. “Bunge la Denmark liliidhinisha mswada mnamo Mei 2018 wa kumwadhibu yeyote anayevaa niqab kwa faini” (BBC, 31 Mei 2018). Kwa sasa sheria hiyo haitaji burka na niqab kwa majina, bali inaeleza, “Yeyote anayevaa nguo inayofinika uso hadharani ataadhibiwa kwa faini”. Marufuku hiyo ilipangwa kuanza utekelezwaji wake mnamo Agosti 2018. Mnamo Ijumaa 3 Agosti 2018 mwanamke wa Kiislamu mwenye umri wa miaka 28 aliyekuwa amevaa niqab katika soko kuu la hadhara mjini Horshom, km 25 (maili 15) kaskazini mwa Copenhagen, alishambuliwa kwa nguvu na mwanamke mwengine aliyepinga vazi lake na kuchukua hatua mikononi mwake kumvua kwa lazima vazi hilo la Kiislamu. Polisi waliitwa katika eneo hilo la “vita” na baada ya kuangalia kanda ya CCTV walimweleza mwanamke huyo wa Kiislamu kuwa angelipishwa faini ya kroner 1,000 ($155; £120) baada ya kukataa kuvua niqab hiyo kwa agizo la polisi. Kwa sasa faini hiyo imeongezeka mara kumi zaidi hadi kroner 10,000 ($1,500; £1,200) kwa wahalifu wanaorudia kosa.