Afisi ya Habari
Kenya
H. 18 Jumada II 1441 | Na: 1441 / 06 |
M. Jumatano, 12 Februari 2020 |
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Kifo cha Moi: Wasaa Makini wa Kutafakari Juu ya Muozo wa Nidhamu ya Kiutawala ya Kisekula
Aliyekuwa Raisi wa Kenya Daniel Arap Moi alifariki mnamo 4 Februari 2020 akiwa na umri wa miaka 95. Moi alikuwa ni Raisi wa pili na aliye tawala kwa muda mrefu wa miaka 24 hadi kustaafu kwake mnamo 2002. Viongozi wengi ulimwenguni wakiwemo viongozi wa serikali wa Afrika wameomboleza pamoja na Wakenya kufuatia kifo chake.
Kutokana na kufariki kwake, sisi Hizb ut Tahrir / Kenya tungependa kufafanua yafuatayo:
Kifo hakina budi na kila mmoja isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu pekee atakionja bila ya kujali cheo chake na wadhifa wake. Kutokana na hili, kifo kinapasa kuwa ukumbusho kamili kwa wanadamu wote kuwa maisha ya dunia ni ya muda tu na kuna haja ya kubadilisha mienendo yetu katika siasa, uchumi na jamii iwe sambamba na maamrisho ya Mwenyezi Mungu. Uislamu umefafanua waziwazi fungamano la viumbe yaani lengo la maisha haya ni kumuabudu Mwenyezi Mungu (swt) na fungamano la kufufuliwa ni kuwa matendo yanayo fanywa katika maisha haya yatahesabiwa Siku ya Kiyama.
Kuna riwaya mbili katika urithi wake, huku wengi katika tabaka la kisiasa wakionekana kuitakasa historia yake nyeusi kwa kumsifu huku ni wachache wao tu wakionekana kuikashifu enzi yake. Kwa kuwa kundi la wanasiasa walioko sasa baadhi yao walilelewa na Moi, haishangazi basi kuwaona wakiusafisha urithi wake. Ama kwa wale ambao wanaonekana wakiukashifu urithi wake hii ni kujaribu kuwahadaa wasio elewa kwani hawana nidhamu mbadala ya utawala isipokuwa usekula ambao umerithiwa na Moi kutoka kwa mtangulizi wake aliyeuchukua kutoka kwa mabwana wa kikoloni. Kwa kuwa usekula unatenganisha dini na siasa, kama serikali yoyote nyingine, idara ya Moi ilisifika kwa ufisadi miongoni mwa majanga mengineyo. Sakata kubwa kubwa kama vile Goldenberg ambayo inakadiriwa kugharimu 10% ya mapato ya nchi ya mwaka mzima ni mojawapo ya mfano dhahiri. Ni maarufu kuwa, Moi alikuwa ni mwalimu katika umri wake wa mwanzo wa ujana, hatimaye alikuja kuwa moja ya familia tajiri zaidi nchini Kenya. Jamii ya Waislamu katika sehemu za kaskazini mwa nchi wangali wanakumbuka kumbukumbu ovu ya Mauwaji ya Wagalla yaliyofanyika Februari 10, 1984. Kwa mujibu wa Tume ya Ukweli Haki na Maridhiano ya Kenya, mauwaji hayo ambayo idadi halisi ya waliokufa haijulikani ndio ukiukaji mbaya zaidi wa haki za kibinadamu katika historia ya Kenya. Kieneo, Moi pamoja na viongozi wengine wa Afrika Mashariki walikuwa ndio ala za kuendeleza njama za kikoloni za Kimagharibi kama vile kuigawanya Sudan.
Kinyume na usekula, uongozi katika Uislamu ni amana na kutokuwa na sera zenye madhara dhidi ya raia. Ni msimamo ambao hutatua matatizo ya wanadamu na kuwaongoza katika ufanisi. Kupitia nidhamu ya utawala iliyo amrishwa na Mwenyezi Mungu (swt), Mtume (saw) katika muda mfupi wa utawala wake, aliunda viongozi wengi pambizoni mwake akiweka mfano imara kwao kuiga. Tunaamini pasi na shaka kuwa kupitia kusimamisha tena Khilafah kwa njia ya Utume katika mojawapo ya nchi kubwa za Waislamu, ulimwengu utatawaliwa na viongozi wenye ikhlasi ambao hawatakuwa na ubinafsi bali watafanya kazi kwa ajili ya kuboresha raia wao na hivyo kuacha nyuma urithi mzuri.
Shabani Mwalimu
Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari wa Hizb ut Tahrir Kenya
Hizb-ut Tahrir: Afisi ya Habari Kenya |
Address & Website Tel: +254 707458907 |
E-Mail: mediarep@hizb.or.ke |